Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Boniphace Nyangindu Butondo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kishapu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nami naanza kuungana na wenzangu kwanza kukupongeza wewe Spika wetu wa viwango kabisa kwa namna ambavyo Bunge letu hili tukufu ambavyo umekuwa ukiliendesha kwa umahiri na busara ya hali ya juu sana. Hongera sana Mheshimiwa Spika, Dkt. Tulia Ackson. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo Rais huyu ameendelea kukonga nyoyo za Watanzania na hasa kwa kuhakikisha kwamba anaendelea kuwatua ndoo akina mama ambao wamehangaika kwa muda mrefu sana na tatizo kubwa la maji. Kwa kweli sisi Watanzania tunamtakia kila la heri na afya njema Rais wetu aendelee kutuletea maendeleo katika Taifa letu hili la Tanzania.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Aweso pamoja na Mheshimiwa Mahundi, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na DG wa RUWASA kwa namna ambavyo kwa kweli wamekuwa wakitusimamia vizuri sana katika eneo hili la sekta ya maji. Watanzania wote wanaiona kasi yenu, utendaji wenu na kwa kweli sisi kama Wabunge, tunaridhishwa sana kwa namna ambavyo mmekuwa mkishirikiana na watendaji wa ngazi za chini, na pia kwa namna ambavyo mnashirikiana nasi Wabunge katika maeneo yetu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kumpongeza Engineer wetu wa Mkoa wa Shinyanga, Dada Juliet Kayovela, na pia nimshukuru sana Engineer wangu Dickson Mazima, huyu ni Meneja wa TARURA wa Wilaya ya Kishapu. Hawa wote kwa kweli wamekuwa na ushirikiano mkubwa nasi Wabunge na hasa mimi mwenyewe katika eneo la jimbo langu na watendaji wa Halmashauri na viongozi wengine katika Wilaya yangu ya Kishapu.

Mheshimiwa Spika, na hiyo unaweza kuona kwamba miradi katika Wilaya ya Kishapu imekuwa ikienda vizuri sana, lakini kwa sababu ya ushirikiano mkubwa wa RM pamoja na DM katika eneo langu hili la Kishapu.

Mheshimiwa Spika, nataka tu niseme kwamba mpaka sasa Kishapu tangu mwaka 2020 mpaka hii 2023, hali halisi ya upatikanaji wa maji ilikuwa ni asilimia 39 katika kipindi cha mwaka 2020, lakini kwa sasa tuko asilimia 76. Ni hatua kubwa sana. Hili ni jambo ambalo wengi wa wanaKishapu wanaona ni ndoto, ni jambo ambalo hawaliamini katika macho yao. Pongezi zote tunaomba tumrudishie Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwa kweli Mama anaona umuhimu wa kuweza kuwasaidia na kuwashusha ndoo akina mama wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tuna miji kama Maganzo inapata maji ya Ziwa Victoria, kuna Mbiu, Kata ya Mwadui Lohumbo, kuna Uchunga, kuna Wela, Ukenyenge na Mji wetu ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Kishapu, haya maeneo tunapata maji ya Ziwa Victoria, lakini haitoshi. Ipo miradi ambayo sasa hivi inaendelea kutekelezwa. Naomba tu nitaje baadhi ya miradi. Upo mradi wa Nyenze – Mwang’oro hadi Kabila; na Idukilo - Igumandobo ambayo ina thamani ya Shilingi bilioni 2.5. Mradi huu unaendelea mpaka sasa, na huu ni mradi wa maji ya Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Spika, upo Mradi wa Ipeje – Itilima - Ikonopyelo, Ikoma na Ipeja. Huu ni mradi mkubwa wa thamani kubwa ya Shilingi bilioni 3.1, ni mradi ambao sasa hivi unaendelea pia kutekelezwa. Upo mradi wa Mwashohohela, huu ni uchimbaji wa visima; na Dulisi. Hii ni miradi ambayo inatekelezwa kwa sasa, japokuwa kuna changamoto ya upatikanaji wa maji, lakini naamini kwamba tutawasiliana na Mheshimiwa Aweso ili katika usanifu utakaokuwa unaendelea, tuone namna ambayo tunaweza kuwaokoa hawa watu wa Kata ya Sekebugoro, na ikiwezekana tuongezewe bomba pengine kutoka Old Shinyanga, ilimradi tuongezewe uwezo wa kuweza kusambaza maji katika maeneo hayo, kwa sababu maeneo hayo yako karibu sana na Old Shinyanga.

Mheshimiwa Spika, vile vile upo Mradi wa Wela, Wila, Mataga na Mwanulu, ni mradi ambao unaendelea mpaka sasa hivi, na huu ni mradi mpya. Hii ni miradi ambayo inakwenda. Upo Mradi mkubwa wa Igaga - Mwamashele unakwenda Mwamanota unakwenda Lagana, ni mradi mkubwa wa shilingi bilioni 6.5. Kampuni ya Emirates mpaka sasa ninavyozungumza iko site inaendelea na kazi. Ni mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Spika, uko mradi wa Ndoleleji wa Malasa, Mwakipoya wa bilioni 1.6 mradi wa maji, usambazaji wa maji katika Mji wa Maganzo milioni 250 unaendelea. Lakini mradi wa usambazaji wa maji Mwamalasa, Mwamashimba mradi 101, pia kuna mradi wa Ngundangali – Seseko, mradi wa Mangu, Kiloleli, Ng’oloshinong’ela na Bulekela milioni 156 hizi tumeomba fedha za usanifu. Mheshimiwa Aweso tunaomba utupatie hizi fedha ili mradi tuone namna ambavyo tunaweza tukaamua ni mradi gani tutapeleka maeneo hayo. Kwa sababu uchimbaji wa visima virefu inaonekana kama unashindikana, ikiwezekana tutaomba tuchimbiwe mabwawa katika maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, kuna mradi wa Momolasa, Somagedi, Mwagalankulu ambao huu na wenyewe nimeuzungumzia lakini mradi wa Nobora, Jijongo milioni 510 unaendelea. Mradi wa kutoka Mhunze kwenye Mwabusiga na wenyewe unaendelea. Kwa sababu muda hautoshi naomba nizizungumzie baadhi ya changamoto, miradi wa Maji ambayo inafadhiliwa na Mfuko wa Maji wa Taifa imekuwa na changamoto kubwa, fedha zimekuwa hazifiki kwa wakati na hii imesababisha kuchelewesha miradi mingi ambayo iko chini ya mfuko wa fedha hizi. Mheshimiwa Waziri nakuomba sana hili jambo waone umuhimu wa kuweza kufatilia ili mradi mfuko huu utoe fedha kwa wakati na miradi iweze kutekelezeka kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna tatizo kubwa, kuna changamoto pia ya gari juzi nimepewa na Eng. Julieth gari moja kukuu nina gari moja lililochoka sana. Kwa hiyo, hili ni tatizo kubwa. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri kwa Wilaya ya Kishapu tupatie gari jipya ili mradi kazi ziweze kutembea sawasawa.

Mheshimiwa Spika, kuna suala zima la certificate zinapokuwa zimekuwa–raised na ziko tayari tatizo kutokutoa, kutokulipa fedha kwa wakati. Kwa fedha ya miradi yote hili limekuwa ni tatizo sugu nakuomba Mheshimiwa Waziri hili lisimamie hili certificate zinapokuwa raised na zilipwe kwa wakati ili mradi miradi iweze kutekelezeka kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, jambo jingine ni maeneo ambayo…

SPIKA: Mheshimiwa Kengele ya pili imeishagonga, dakika moja malizia.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Maeneo mengine ambayo nilikuwa nataka kuzungumzia ni maeneo ambayo hasa ya miradi ambayo ni ya zaidi ya bilioni moja. Kumekuwepo na tatizo kubwa sana kwenye msamaha wa kodi VAT exemption. Ninaomba Mheshimiwa Waziri miradi mingi sana imekuwa ikichelewa kutekelezwa kwa sababu ya ucheleweshwaji wa upitishaji wa hii VAT exemption. Ninaomba sana hili lizangatiwe na hii itasaidia sana miradi kukamilika kwa wakati lakini hata wakandarasi hawa tuwahurumie wakati mwingine tunaingiza katika mufilisi pasipo kuwepo na sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo baada ya kuzungumza hayo ninaunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.