Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Emmanuel Lekishon Shangai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia bajeti ya Wizara ya Maji. Nitangulize kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa upendo mkubwa pamoja pia na kumpongeza Waziri wa Maji, Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu na Wasaidizi wote pamoja na watumishi wa RUWASA Wilaya ya Ngorongoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi binafsi nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri. Nimemfuata sana kuhusiana na suala la mradi wa maji wa vijiji nane, mradi wa Mageri. Mradi huo umeanza toka mwaka 2016, mradi huu ungetakiwa kuwasaidia zaidi ya wananchi 80,000 lakini mpaka leo bado una suasua. Nashukuru kwamba nilikuona toka wiki iliyopita umeweza kutusaidia tumepata zaidi ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya mradi huo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru pia kwenye mradi wa Lopolu umetupatia shilingi milioni 100 ambayo itaenda kumaliza tatizo la maji kwenye Kijiji cha Lopolu pamoja Oldonyouwas, nashukuru kwa hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye Wilaya yetu ya Ngorongoro tuna miradi zaidi ya 14 ambayo inaendelea, miradi hiyo yote inahitaji zaidi ya shilingi bilioni 10 ili iweze kuwahudumia wananchi, lakini mpaka sasa kwenye bajeti ya mwaka jana tumepta fedha 40% tu kwa miradi yote inayoendelea. Kwa hali hiyo ni kwamba hatuwezi kwenda kutatua shida ya maji tunakuwa na miradi mingi inayoendelea lakini fedha hazitoki. Mimi nikusihi Mheshimiwa Waziri tunaomba tunapotenga fedha hasa katika maeneo ambayo yana shida ya maji kama Wilaya ya Ngorongoro tujitahidi kuwapa kipaumbele, tuwaletee fedha kwa wakati ili wananchi wanufaike na juhudi za Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala lingine, kwa mfano leo kati ya miradi inayoendelea kwenye Wilaya ya Ngorongoro kuna mradi wa maji Digodigo. Inahitaji shilingi milioni 42 na imefika 90%, tukipata hizo fedha mradi huu utaisha. Tuna mradi wa maji wa Oldonyosambu Masusu. Mradi huu umeanza toka mwaka 2018 lakini mpaka leo mradi huo umefikia 85%, mkandarasi hajalipwa, fedha zinadaiwa shilingi milioni 270 kwenye mradi huo.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni uchimbaji wa visima viwili katika Vijiji vya Loswas na Soitsambu. Inahitajika shilingi milioni 112 na mradi umefikia 100% lakini fedha hazijafika. Wananchi wanahitaji kutumia yale maji lakini bado fedha hazijalipwa, maana yake kuna vitu bado vinahitajika kwa ajili ya kumalizia. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri utupe kipaumbele kwenye miradi hii ili wananchi waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi mwingine ni mradi wa ukarabati Oldonyosambu, Kisangiro, Olaika imefikia 95% lakini fedha shilingi milioni 117 bado hamjapeleka. Nikuombe wewe binafsi Mheshimiwa Waziri unafanya kazi nzuri lakini tukichelewesha fedha maana yake wananchi hawatapata maji. Nikuombe mpeleke fedha huko.

Mheshimiwa Spika, mradi wa Olemishiri nashukuru kwamba hilo umeshatatua tumepata shilingi milioni 100 kwa ajili ya kumalizia mradi ule lakin mradi wa Mbuke awamu ya kwanza na awamu ya pili bado wanadai shilingi milioni 550 hamjapeleka mpaka leo. Wananchi wale wanafuata maji zaidi ya kilometa 40. Tunatakiwa kuwasaidia mradi wa Mbuke phase one and two. Kwa sababu baada ya wataalamu kuanza kufanyia marekebisho kwa sababu ni existing project sasa hivi wananchi hawapati maji. Niwapongeze wataalamu kwa sababu juzi wamefunga solar lakini bado haiwafikii wananchi imefika Shule ya Msingi Arash lakini haifiki kule ambako kuna wananchi kwenye DP zile tisa zingine.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri suala lingine ambalo nataka tuone ni kwamba kwenye Wilaya ya Ngorongoro kuna zile Kata ambazo zimefuatana na eneo la Pori Tengefu. Wananchi wale walikuwa wanategemea maji kutoka yale maeneo yaliyotengwa lakini sasa hivi hawana maji. Ukienda Kata ya Ololosokwan wananchi wanategemea kwenda kuchukua maji kule kwenye eneo la Pori Tengefu lakini hakuna na kule pia hakuna vyanzo vingine vya maji. Mlichimba visima lakini mpaka leo tunasikia tu procurement ya pump bado zinafanyika ngazi ya Wizara. Tunaomba mfanyie kazi hilo kwa sababu wananchi hawapati maji na ndiyo maana bado unasikia kwamba bado kuna vurugu kati ya wananchi na wahifadhi kwa sababu hawapati maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine kwenye Kata za Arash pamoja na Piaya inaonekana kwamba kuna uhaba wa vyanzo vya maji. Kwa hiyo, tunahitaji visima zaidi. Suala lingine ni suala la Kata ya Piaya. Mheshimiwa Waziri nikuombe ombi special kabisa. Kwenye Kata hiyo ya Piaya wananchi wanakunywa maji ya chumvi ambayo ina fluoride ambayo ukiwakuta watoto wadogo wanadhurika. Kwa hiyo, nikuombe ututafutie mtambo wa kusafisha maji kwenye Kata ya Piaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la bei ya maji na hii nitaondoka na mshahara wako leo usipotuambia. Ukija kuhitimisha hapa, mwaka jana nilichangia kwenye Mji wa Waso na Loliondo bei ya maji ni kubwa sana ambayo wananchi wanashindwa kumudu. Nikuombe tena utakapokuja kuhitimisha utuambie kwamba kwa sababu ulishawatuma wataalam wa EWURA kuja kushughulikia jambo hilo tujue kwamba limefika wapi ili wananchi wapate ahueni. Wananchi wengine wameamua badala sasa ya kuchota maji kwenye bomba kama anavyodhamiria Mheshimiwa Rasi, kuna wakina mama wamerudi mtoni kwa sababu hawawezi kumudu bei ya maji kwenye Mji wa Waso na Loliondo. Kwa hiyo nikuombe sana uweze kushughulikia hilo.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la vitendeakazi. Unajua jiografia ya Wilaya ya Ngorongoro Mheshimiwa Waziri kwa sababu wewe umefika. Ukitoka Makao Makuu uende mpaka Pinyinyi kwenye mradi uliopo ambao unatekelezwa ambao pia bado inahitaji fedha na gari lenyewe iliyopo kwenye Wilaya yetu ambayo RUWASA wanayo ni gari bovu. Wanaweza wakakaa zaidi ya wiki mbili hawawezi kwenda kwenye mradi kwa sababu ya tatizo la gari. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri kama nilivyowasilisha mwaka jana nikuombe tena uweze kutusaidia kupata gari kwa ajili ya wataalam wa RUWASA ili wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro wanufaike na matunda ya Serikali ya Awamu ya Sita. Kwa hiyo, nikuombe sana hayo uweze kufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo mimi nishauri, naomba nishauri urasimu mkubwa uliopo kwenye Wizara yako. Tujaribu kuangalia namna ya kuweza kutatua tatizo hilo kwenye utekelezaji wa miradi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)