Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Daniel Awack Tlemai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia katika Wizara hii ya Maji. Namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia fedha nyingi Jimbo la Karatu kupitia TAMISEMI mwezi huu wa Mei tumepokea zaidi ya shilingi bilioni mbili ya kuendelea kujenga madarasa, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Karatu tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na pia namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwa kutupatia Jimbo la Karatu fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Maji na Watendaji wa Wizara ya Maji na leo nachangia nikiwa na furaha kwamba kuna majukumu makubwa sana kwenye hii Wizara imefanyika katika Jimbo la Karatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miaka miwili iliyopita nilikuwa nachangia bei kubwa ya maji katika Jimbo la Karatu, ilikuwa maji kwa Jimbo la Karatu upatikanaji wake kwa unit ni shilingi 3,500, sasa upatikanaji kwa unit katika Jimbo la Karatu inapatikana kwa shilingi 1,300, kwa maana hiyo namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kutoka shilingi 3,500 na leo wananchi wa Jimbo la Karatu katika Mji wa Karatu wanapata maji kwa shilingi 1,300 kwa unit. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuunganisha. Karatu kulikuwa na Bodi mbili, kulikuwa na Bodi ya KAFIWASU ambayo ilikuwa inauza maji kwa shilingi 3,500. Kulikuwa na Bodi ya KARUWASA ambayo wanauza maji kwa shilingi 1,750 baada ya kuungana sasa maji yanapatikana kwa shilingi 1,300. Tunakushukuru sana na ninaamini kwamba ni sera ya Wizara kuunganishwa ili wananchi wale wasiendelee kuwa na mwingiliano katika hizi bodi mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri pia nakushukuru baada ya kuunganisha wafanyakazi wale wote wa KAFIWASU na wale wa KARUWASA wakaunganishwa hakuna aliyekosa kazi wote sahizi wanaendelea kufanya kazi. Pia ulipendekeza aliyekuwa Manager wa KAFIWASU sasa kuwa Mkurugenzi wa Maji katika Mji wa Karatu na anafanya kazi nzuri sana katika Mji wa Karatu na wananchi wanapata maji. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile jana Mheshimiwa Paresso amechangia akisema kwamba wananachi wa Karatu wanalalamika. Nikuhakikishie nimetoka Jumapili Jimbo la Karatu, wananchi wa Karatu hawalalamiki. Wananchi wa Karatu walipata shida kutoka mwaka 2002 kununua maji kwa shilingi 3,500 lakini niweke kumbukumbu sawa, siyo kwamba Karatu baada ya 2002 ndiyo kwamba mradi wa maji ulianza. Mradi ulikuwepo kabla ya 2002 na ulirithi miradi ya Serikali ambayo ni matenki na ma-lane na wakaendelea kuhudumia kwa bei ghali ya shilingi 3,500. Kwa hiyo, nikuambie Mheshimiwa Waziri hakuna Wananchi wa Karatu wanaolalamika, mimi ndiyo Mbunge wa Jimbo la Karatu, wananchi wamefurahia kuunganishwa kwa ile vyombo, kwa sababu hitaji letu ni maji, sisi hatuna shida na majina ya KAFIWASU na KARUWASA, shida ya wananchi wa Karatu ni wapate maji ili maendeleo yawepo katika Jimbo la Karatu, hatuna shida na KAFIWASU na KARUWASA, lengo letu kubwa ni mwananchi apate huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo nikushukuru sana kwa hilo ila nina lalamiko la Wanakaratu, uliwaahidi utawapatia shilingi bilioni 4.5. Hili ndilo lalamiko la Wanankaratu isipopatikana shilingi bilioni 4.5, na nikushukuru kwa sasa mmetoa shilingi milioni 865 kati shilingi bilioni 4.5. Tunachoomba Wanakaratu sasa hizo fedha zingine zilizobaki katika shilingi bilioni 4.5 zipatikane ili wananchi wa Jimbo la Karatu waendelee kupata neema ya maji katika Mji wa Karatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukipata shilingi bilioni 4.5 upatikanaji wa maji katika Mji wa Karatu utakuwa zaidi ya asilimia 100 katika Mji wa Karatu. Kwa maana hiyo nikuombe Mheshimiwa Waziri tuweze kupatiwa shilingi bilioni 4.5 katika Mji wa Karatu maji yatapatikana kwa zaidi ya asilimia 100. Hii shilingi milioni 865 mliyotoa, inaweza kupeleka maji kutoka asilimia 70 mpaka asilimia 78, tukipata hizo fedha zingine zilizobaki ina maana tunakwenda kumaliza tatizo la maji katika Mji wa Karatu. Nikuombe sana hii shilingi bilioni 4.5 ambayo umeahidi Wananchi wa Jimbo la Karatu na tulikuwepo Wabunge wote wawili, tulikuwepo Baraza la Madiwani, walikuwepo Wenyeviti wote wa Mitaa katika Mji wa Karatu. Ulituahidi utatupatia shilingi bilioni 4.5. Ombi langu kwako tuweze kupta hiyo shilingi bilioni 4.5 ili wananchi wa Karatu waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri kuna maeneo mengine hela chache chache zimebaki siyo hela nyingi sana ili mradi ukamilike. Kwa mfano, katika Mji wa Karatu kuna mradi ambao unatekelezwa eneo la Bwawani Mangaki ambao Serikali imeleta shilingi milioni 375 na mradi ule ulikua unahitaji shilingi milioni 640. Tulikuwa tunaomba hiyo hela nyingine kidogo iliyobaki mtupatie kama Wizara, lakini lingine ni shilingi milioni 640 eneo la Kata ya Mang’ola. Tunaomba mtupatie hizo fedha shilingi milioni 640.

Mheshimiwa Spika, lingine ni mradi ambao unatekelezwa katika eneo la Laja ambao unagharimu, umebaki shilingi milioni 136. Tukipata hiyo shilingi milioni 136 inamaana suala la maji katika eneo la Laja linaisha kabisa, vilevile kuna eneo la Chemchem, Mkandarasi pale anahitaji shilingi milioni 192 ili aweze kumaliza majukumu yale ya maji katika eneo la Chemchem. Tukipata hii shilingi milioni 192 kazi pale Chemchem itakuwa imeisha eneo la Kata ya Rotia.

Mheshimiwa Spika, vilevile tukipata fedha shilingi milioni 64 kumalizia mradi ambao unatekelezwa katika eneo la Mang’ola Juu Kijiji cha Mang’ola Juu Kata ya Daa. Vilevile niseme Mheshimiwa Waziri tunakushukuru sana, wananchi wa Jimbo la Karatu tunakuomba utupatie hizo fedha na mimi naamini ukitupatia hizi fedha nilizotaja hapa ni kwamba katika eneo la Mjini maji yanakwenda asilimia 100, maji katika eneo la vijijini inakwenda asilimia zaidi ya 75. Nikuombe tupatie hizi fedha ili wananachi wa Jimbo la Karatu waendelee kupata neema ya maji ambayo imekosekana kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri mimi nikuombe katika Jimbo la Karatu maeneo ya vijijini hitaji letu sisi maji yanapatikana, huwezi kuchimba zaidi mita 100. Kwa hiyo, tunachoomba ni kwamba sasa utaratibu ule wa gari zile za Mkoa ambayo sasa imeletwa kwa Mkoa wetu wa Arusha Mheshimiwa Zaytun amechangia hapa kwamba tayari tuna gari, ombi letu ni kwamba sasa katika eneo la Karatu uweze kutupatia visima vichache katika maeneo ya vijijini ili wananchi wetu waendelee kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana na nikutoe hofu wananchi wa Jimbo la Karatu wanakusubiri kwa hamu kubwa sana ili wakushukuru, kwa niaba yao nimkuja kuleta shukrani kwako kwa watu walinyonywa miaka 20 iliyopita kwa shilingi 3,500 na leo tunaendelea kula neema ya shilingi 1,300 kwa unit. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye DP maji leo zinapatikana kwa shilingi 1,000 kwa unit. Nikushukuru sana Mungu akutangulie uendelee kutuletea mambo mengine mengi katika Jimbo la Karatu sana, nikushukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)