Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Jeremiah Mrimi Amsabi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote nimshukuru sana sana Rais Dkt. Samia kwa kazi kubwa ambayo ametufanyia pale Serengeti. Kwa muda mrefu kabisa barabara zetu zilikuwa ni changamoto, lakini Rais ametoa fedha nyingi, iko barabara sasa inajengwa kutoka Tarime mpaka Serengeti, lakini ipo nyingine kutoka kule Bunda mpaka katika Mji wetu wa Serengeti. Tunamshukuru Rais bado katika miradi mingi katika afya, katika elimu na kadhalika, lakini katika miradi ya maji tumeona akifanya mapinduzi makubwa sana. Katika miaka yake miwili iko miradi mingi ambayo inaendelea kutekelezwa, iko Miradi ya Kibanchabancha, Nyiberekera, Rigicha, Gesarya, Motukeri, Nyamitita, Kenyana na Nyamakobiti, iko mingine mingi kwa sababu ya muda siwezi kuitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa nishukuru kwa jitihada hizi za Rais za kutafuta fedha, miradi ambayo nimeipendekeza, nimewasilisha pia imeweza kuingizwa katika bajeti ya mwaka 2023/2024. Upo Mradi wa Nyamisingisi, Nyamihuru, Gantamome, Bwitengi, Nyichoka, Iharara, Kuitete, Iseresere, Mesaga, Masinki, Ketembere, Misarara, Nyansurura, Tamkeri na Manyata, lakini pia viko visima 20 ambavyo vinachimbwa katika sehemu tofauti. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Aweso, Naibu wake na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa ya usimamizi na utekelezaji wa shughuli hii kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa muda huu mfupi niseme changamoto chache ambazo tunaziona na tunashauri zifanyiwe kazi katika Mradi wetu mkubwa wa Maji katika Mji wa Mugumu pale Makao Makuu ya Wilaya ya Serengeti. Tunamshukuru Rais kipekee, mradi huu ulikuwa umeshindikana katika miji yote 28, lakini Rais kipekee kabisa amepata fedha. Sasa bilioni 11.5 zinazokuja pale Mugumu kwa utekelezaji wa mradi huu naishauri sana Wizara iangalie namna ya kuupitia tena ule mradi. Ule mradi unakutana na changamoto ya scope, una-cover maeneo machache. Wakati mradi huu unakuwa designed miaka iliyopita huko wali-focus population ndogo.

Mheshimiwa Spika, Mji wetu wa Mugumu ulikuwa na watu takribani 30,000 na hata mji ulikuwa hujapanuka kiasi ambacho umepanuka sasa hivi. Sasa Mji wetu wa Mugumu una wakazi 59,348, ukiona ni karibu mara mbili ya ongezeko la watu ambao walikuwepo. Kwa hiyo, tunaomba, kwa mfano specific ukienda Kata ya Matare maji yanafika kwenye Eneo la Senza pale. Ukienda maeneo ya mbele Igina mpaka Shule ya Sekondari Kambarage, kuna zahanati imejengwa kule maji katika mradi huu hayatafika. Kwa hiyo, ombi letu na ushauri kwa Mheshimiwa Waziri, mradi huu sasa uongezewe ile scope uweze kukutana na watu wengi kulingana na population ya watu ambao imeongezeka katika mji wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto ya pili ni chanzo cha maji; katika chanzo cha maji cha mradi huu wa bilioni 11 iko changamoto kubwa. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri nilimwandikia barua, nimezungumza naye mara kadhaa na Waziri ameonekana kuwa msikivu. Waziri Aweso namfahamu ni mtu msikivu, ni mtu wa mabadiliko, ni mtu anayeweza kubadilisha vitu na akavifanya kuwa bora zaidi. Mradi huu najua kwa uwezo wako, kwa umahiri wako angekuwa ni yeye ndiyo ameu–design kwa wakati huu angeufanya kuwa wa tofauti, lakini nimwombe sana Mheshimiwa Aweso, bado hatujachelewa. Alituma wataalam baada ya ombi langu wakaja, wakafanya tathmini, kwa maana ya chanzo kile sasa ambacho ni kidogo. Wakati bwawa hili linajengwa lilikuwa na uwezo wa kuwa na maji lita milioni 23, sasa hivi limeweza kupungua mpaka lita milioni 14. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati linajengwa lilikuwa ni kwa ajili ya mji ule mdogo ambao ulikuwa bado kijiji, population yake ilikuwa ni around watu 7,000 tu. Sasa population imekuwa kiasi hiki, lakini pia mahitaji yamebadilika kwa maana ya namna ambavyo ule mji sasa unaendelea kubadilika na nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, timu ile ilijielekeza sana kumshauri kuhusu kuchukua maji kwenye chanzo cha maji ya Mugango, Kiabakari, Butiama na wakamwambia kwamba haiwezekani. Ni kweli kwa sababu tayari Mradi wa Mugango – Kiabakari - Butiama ulikuwa umeshafika mbali, lakini bado hawakuwa na option nyingine.

Mheshimiwa Spika, tunamwomba Mheshimiwa Waziri, watu wa Serengeti tunaona shida hii inaweza ikawa kubwa baadaye na upo ushauri wa wataalam wengi, Profesa James Scott wa University of Yale kule Marekani. Huyu ni Profesa wa Political Economy katika kitabu chake cha Weapons of the Weak, anasema long term solutions is the function of proper planning. Kwa hiyo, sisi katika hali yetu hii, uchumi wetu huu bado tunapambana hivi, tunapaswa kuwa na mpango ambayo ni sahihi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana sasa tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri Aweso aangalie, ilipangwa miradi mingi ya muda mfupi kutafuta solution ya muda mfupi mpaka leo tumepoteza fedha nyingi kwa ajili ya Taifa hili. Pale Serengeti ipo miradi ya HESAWA ilijengwa mingi sana, almost kila kijiji leo ukienda vijiji vingi vinaonekana havina maji, kwa sababu vile visima vilikuwa ni temporary solution. Iko pia miradi mingine ya mabwawa mengi katika sehemu mbalimbali za nchi ambazo yote mpaka leo inaonekana siyo kitu, miradi ile imeisha na tumefikiri tena miradi mingine.

Mheshimiwa Spika, unapofikiria long term solution lazima uangalie scope kwa upana kabisa, population ya watu inaongezekaje, mahitaji na vyanzo vyenyewe. Ukiona kama chanzo cha Bwawa la Manchira wakati ule kilikuwa kina vijito takribani nane vilivyokuwa vinaingiza maji. Kutokana na population pressure, wakati ule Serengeti ilikuwa na watu takribani 180,000, sasa kwa sensa ya 2022 tuna watu 340,349, watu wameongezeka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya pressure hii, vyanzo vingi vya maji vilivyokuwa vinapeleka katika bwawa hili vimeharibika. Kutokana pia na mabadiliko ya tabianchi hatupati mvua za kutosha. Kwa hiyo, ni dhahiri chanzo hiki cha maji ya Bwawa la Manchira hakiwezi kuwa cha kudumu ni cha muda mfupi. Kwa hiyo, hatutaki tena baada ya muda mfupi tuliingize Taifa katika shida ya kutafuta namna tena ya kujenga miradi mingine.

Mheshimiwa Spika, leo tumeshuhudia mahali pengi miradi ilijengwa baadae tena wanaacha yale mabomba wanaweka mengine, wanaweka mabomba makubwa. Huu ni uharibifu wa fedha ya Taifa hili. Kwa hiyo, tunamuomba ndiyo maana tumekuja na ushauri mkubwa kabisa kwa Mheshimiwa Waziri lazima tuwe na integrated water systems kwenye nchi. Kama kwenye nchi nzima ni shughuli kubwa basi walau iwe katika regional. Lazima tuwe na mpango ambao ni unganishi na shirikishi wa kupata maji katika Mkoa.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano Mkoa wa Mara, Mkoa wa Mara leo tungeweza tukawa na vyanzo vikubwa vitatu tu, vikubwa sana. Watu wengi hapa kila wakati wameshauri nchi hii ni vizuri tukawa na mipango ya miaka 50, miaka 60 kwa maana gani? Tunapofikiri kuwa na maji, tusi-focus kuwa na maji ndani ya miaka mitano au 10, tufikirie miaka 50 kwa maana hiyo tunaweza tukajenga mradi mkubwa wa maji kule Mugango ambao unge-fucus population ya watu zaidi ya milioni 10 kwa wakati unaokuja. Sasa leo tutaweka milioni moja, milioni mbili baada ya muda watu wameongezeka, maji yale hayatoshi tena tunaanza upya, tunatafuta fedha upya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri tunakuomba sana Mji wa Mugumu utakapokuja katika ground bricking ceremony ya mradi huu mkubwa wa maji, tunaomba uje na taarifa ambayo wananchi wa Serengeti wanaitamani. Tunatamani kusikia tunao mradi mkubwa wa maji sasa unaanzia kule Rorya - Tarime na unakuja mpaka mji wa Nyamongo. Kutoka Nyamongo mpaka Mugumu ni takribani kilometa 57, ni rahisi sana kuleta maji katika Mji wa Serengeti.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo rai yetu ni kwamba ule mradi tunauhitaji…

SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili imeshagonga.

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, tunamuomba sasa Mheshimiwa Aweso aweze kufikiria mradi ule uendelee lakini ujengwe katika scope ya kuchukua maji Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)