Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Ahmed Ally Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Solwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Mimi binafsi naunga hoja mkono kwenye Wizara hii ya Maji. kama kuna siku ambayo mimi binafsi Mbunge wa Jimbo la Solwa sina changamoto nyingi kwenye Jimbo la Solwa kwenye suala zima la maji kama awamu hii awamu ya sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu ni kubwa na ninajua kabisa Mama yetu Rais wetu mpendwa kubwa anaifanya sana; anaitendea haki Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania. Ninajua sana chini ya Wizara ya Maji chini ya Waziri Mheshimiwa Aweso, Naibu wake na timu nzima ya Wizara ya Maji mnaitendea haki Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Solwa mwaka 2005 tulikuwa tuna vijiji 16 tu vyenye maji ya Ziwa Victoria. Lakini tulikwenda awamu baada ya awamu uvumilivu na ustahimilivu chini ya Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi miradi ambayo inatekelezwa sasa hivi katika Jimbo la Solwa ni mingi.

Mheshimiwa Spika, Ukianza na mradi wa Masengwa package vijiji vinane awamu ya pili wenye gharama ya bilioni 4.7 wakandarasi wako kazini wanafanya kazi. Mradi huu una awamu tatu. Mpaka tunamaliza awamu tatu tutakuwa tuna vijiji 12. Katika Masengwa Package tuna Kijiji cha Ishnabulandi, Bubale, Idodoma, Isela, Ibingo, Mharanga, Mwamara na Nalibanza katika kata ya Mhamara. Tumeshajenga tenki Ishnabulandi na sasa hivi inajengwa tenki Mwamara kwenye kata ya Mwamara.

Mheshimiwa Spika, Ndugu zanguni katika Jimbo la la Solwa tuna vijiji vingine sita ambao unagharimu zaidi ya bilioni tatu Jimbo la Solwa tu hilo Mwandutu, Mwabageu, Maemiru, Mwasenge, Mwongozo, na Mwenge vijiji sita tayari wanakunywa maji ya Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Spika, katika Tinde package kuna vijiji 22 hata Makamu wa Rais alipokuja kuzindua ule mradi pale tinde walikuja pamoja na Mheshimiwa Waziri sasa hivi mabomba yanalazwa kwenda kwenye Kijiji cha Jomu kwenye Kata ya Tinde. Kata ya Tinde nadhani Waheshimiwa Wabunge wengi mnaifahamu, ni junction kubwa sana ambayo kila mtu lazima aipite kwa maana ya kwamba kama anakwenda nchi jirani.

Mheshimiwa Spika, vijiji 22 lakini katika Kijiji cha Jomu sasa hivi mabomba yanalazwa. Kwa hiyo mwezi wa sita wataanza kunywa maji ya Ziwa Victoria. Mradi huu una-cost bilioni sita. Kata za Mwamara, Didia, Tinde, Osanga pamoja na Nsalala katika Tinde package hii ambayo sasa hivi nafikiri na nina Imani kabisa Wizara wanafanya mchakato wa kuleta fedha ili tukamilishe. Hoja yangu na ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri, tunapoomba fedha kwa ajili ya kukamilishaji kwa ajili ya Tinde package nikuombe sana ije kwa wakati ili miradi hii yote ikamilike kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mwalukwa kuna miradi pia sasa hivi inatekelezwa katika vijiji vitatu, kwa kushirikiana na life water, tunawashukuru sana. Tunaendelea, na mradi utaisha baada ya miezi mitatu minne na wenyewe watakunywa maji ya Ziwa Victoria, lakini pia Kilimawe bilioni 304. Kilimawe kijiji kiko ndani sana lakini tunapeleka maji kwa kuwashirikiana na life water, RUWASA wanasimamia pale. Pia Mwashagi katika zile fedha za COVID tumepeleka maji. Vilevile kwenye Kata ya Mwakitorio, nafikiri hata Mheshimiwa Waziri amekuwa akiitolea mfano sana kwenye mikutano yake yote; ule mradi ulitusumbua sana. Sasa hivi kwenye Mwakitorio wenyewe kijiji hicho wanakunywa maji.

Mheshimiwa Spika, vilevile Mheshimiwa Waziri alitoa maelekezo ya kujenga tenki, tenki limeisha, linachukua lita laiki tano, ambalo litahudumia vijiji vitatu, ambavyo ni Mwakitorio, Nyarigongo, na Nyang’ombe. Hivi ninavyoongea kwa faida ya wananchi wa Nyerigongo na Nyang’ombe niwaambie tu mabomba yameshashushwa pale Ofisi ya RUWASA, wiki hii hii na wiki ijayo tutapeleka mabomba kulaza ili wananchi wa Kijiji cha Nyerigongo na Nyang’ombe wapate maji ya Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunaomba fedha kwa ajili ya usanifu wa vijiji 22 vingine. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, vijiji 22 vingine vya Kata za Ryabukande, Iryamidati, Ilola, Bukene, Usule pamoja na Puni, tulikuomba fedha hizi utuletee ili tukamilishe vijiji 22. Tunajipanga kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi asilimia 85 kupeleka maji vijijini, yaani tuwe tumekamilisha kufikia 2025. Miradi hii yote ikikamilika sasa sisi kwenye Jimbo la Solwa tutafika asilimia 87 kufika 2025, na tutakuwa na vijiji 105 ndani ya vijiji 126.

Mheshimiwa Spika, ni miujiza. Yaani wakati mimi nasoma shule nilikuwa nikitoka Kijiji cha Mhangu ninakwenda, kuna wakati kama kuna ukame, mnachukua gari kwenda kuchukua maji kilomita 30 ambako Serikali ilichimba bwawa moja kubwa sana kwenye Kata ya Nindo pale Selamagazi. Unatoka kule unaenda kuchukua maji wengine walikuwa wanakwenda kwenye Malambo kule.

Mheshimiwa Spika, ukikumbuka enzi hizo wakati nasoma mpaka sasa hivi nimekuwa Mbunge wa Jimbo la Solwa, kwa kushirikiana na chama changu utekelezaji wa ilani chini ya awamu ya sita leo tumefanya maajabu na miujiza mikubwa mno katika Wizara hii ya Maji

Mheshimiwa Spika, mimi niseme tu ndugu zanguni tumpe Mama moyo mkubwa sana katika awamu ambayo mimi nimefanya kazi kwenye Jimbo la Solwa hakuna fedha nyingi zimekuja kama awamu hii ya sita yenye miradi yote ikiwemo miradi ya maji. Vilevile nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Aweso, Aweso chapa kazi wewe mdogo wangu uko vizuri sana. Sina tu cha kusema. Sisi tukuiingia Mskikitini kuswali tunakuombea dua. Zaidi ya kuombea dua ufanye kazi yako vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine niombe tu Engineer wangu Meneja Eng. Nkopi, anakaimu, hebu ichukue hii tumthibitishe, mthibitisheni huyu. Mimi nimefanya kazi na ma-engineer wengi sana hakuna engineer ambaye unafanya naye kazi unamuelewa anasimamia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Haya, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Spika, naomba tu athibitishwe na alatewe gari ili kazi tufanye vizuri na nawashukuru sana katibu mkuu meneja wa maji vijijini, wote kwa pamoja Mungu awabariki sana nawashukuru sana ahsante sana.