Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Prof. Shukrani Elisha Manya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Waziri wa Maji, ambayo anataka Bunge limuidhinishie bilioni 756.21 kwa ajili ya kuendelea kuwapelekea huduma ya maji watanzania. Nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, moja ya sekta ambazo zimeiheshimisha Serikali ya Awamu ya Sita ni sekta ya maji. Hii ni kwa sababu ya miradi mingi ambayo imekwenda moja kwa moja kwa wananchi na haya hayawezekani isipokuwa kwa utendaji mzuri wa watendaji wa Wizara, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote. Kwa msingi huo kwa kweli pongezi wanzozipokea wanastahili. Kwa mtindo wanaokwenda wanaitekeleza kabisa azma ya Mheshimiwa Rais, kuwatua wanawake ndoo kichwani na tunawaombea baraka zote za Mwenyezi Mungu juu ya hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitangulie kuunga hoja mkono kwamba Wabunge wote tuweze kukubali bajeti hii ya bilioni 756.21 iweze kwenda kuwasaidia wizara kutekeleza majukumu yao katika mwaka fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, ninazo hoja tatu za kuchangia katika hotuba ya Waziri asubuhi ya leo.

Mheshimiwa Spika, moja ni ambayo imezoeleka kwa lugha rahisi ya local content lakini kiswahili chake ni uwezeshaji watanzania kushiriki ujenzi wa miradi mikubwa ya maji. Katika hoja hii mara nyingi sana tunazo hoja mbili muhimu kwa nini watanzania au kampuni za kitanzania huwa hazipewi kandarasi katika ujenzi wa miradi mikubwa ya maji.

Mheshimiwa Spika, moja ni uwezo wa kitaalamu; pili, ni mtaji. Lakini kama nitakavyoongea haya mambo mawili yametuchelewesha na kwa misingi hiyo fedha nyngi imeendelea kupelekwa kwa kampuni za nje kumbe tunaweza. Kwa sababu gani ninasema hivi? Ukweli si kwmba hawana uwezo. Je, wamepewa nafasi kuonesha uwezo wao? Kamati yetu ya Maji na Mazingira ilitembelea mradi wa Dareda – Sigino – Singu – Bagala ambao pia unaleta maji katika Mji wa Babati. Tulichokiona Mradi huu ulisanifiwa na wazawa, wale wa BAWASA, wataalam wazawa lakini mradi huu pia umejengwa na wazawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi huu pia ukaokoa bilioni 15 ukatumia bilioni 12.7 badala ya bilioni 27 na unatekelezeka kwa ubora uleule. Hoja hapa ni kwamba kumbe wataalam wetu wanaweza. Tujifunze kupenda cha kwetu, kwa sababu mara nyingi sana tukikaa hapa tuna dhana ya kwamba watanzania hawawezi kumbe watanzania wanaweza kama watapewa nafasi, kama watawezeshwa hilo limedhihirika wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nampongeza Mheshimiwa Waziri, pomoja na menejimenti yake kwa kuwaamini watalamu hawa ambao wameweza kutekeleza mradi kwa uwezo mkubwa sawasawa na miradi mingine ambayo tumeitembelea. Na kwa jinsi hiyo liwe ni funzo ndani ya Serikali yetu, kwamba wazawa wapewe nafasi na pia wapewe mitaji. Na wakati mwingine, kama tumeona uwezo wao ni mzuri wahamasishwe kufungua kampuni zao ili waweze kuchukua kandarasi kubwa badala ya kusubiri mtu astaafu miaka sitini halafu ndipo atumie utaalamu wake kwa kufungua kampuni. Wahamasishwe kufanya hivyo ili huko mbele katika miradi mikubwa hii inayoendelea kujengwa hapa nchini tupate kampuni za Kitanzania ambazo zitashindana ndani pamoja na nje ya nchi. Kwa hiyo hilo ni jambo zuri la kujifunza kutoka Ofisi ya Babati jinsi ambavyo wanatekeleza mradi wao wenyewe.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu nyingine inatokana na ziara hiyohiyo ya Kamati tulipotembelea katika maeneo ya Nzega. Kumekuwa na uzoefu wa wananchi ambao wanaamua kuanzisha makazi mbali kidogo na wenzano; wanakaa kwenye mashamba huenda ya babu zao. Sasa mradi unatekelezwa halafu wao wako mbali kidogo, kwa hiyo Serikali inatumia gharama kubwa kuwapelekea watu wachache mradi wakati ni kwa sababu wao waliamua kujitenga; na nadhani hili pia ndio limeleteleza hizi shule shikizi kwa sababu watu wachache wapo mahali walikoamua kwenda lakini Serikali inalazimika kuwapelekea huduma.

Mheshimiwa Spika, hoja hapa ni kwamba nadhani kuna sababu ya sisi kupanga makazi na namna ya kurahisisha Serikali kutotumia gharama kubwa kwa ajili ya kuwapelekea watu huduma, la sivyo watu wata detach, wataenda mbali halafu wanahitaji huduma. Hivyo nilitamani kwamba Serikali iangalie, kwamba tuweze kupanga makazi kwa ajili ya kurahisisha kuwapelekea watu huduma bila kutumia gharama kubwa.

Mheshimiwa Spika, hoja ambayo pia Wabunge wengine wameiongelea, mafanikio haya tunayoyashuhudia katika Sekta ya Maji yametokana mara nyingi kwa kutumia vyanzo ambavyo ukiacha mradi wa Ziwa Victoria yanayoweza kuathirika na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi na katika ukurasa wa 81 wa hotuba ya Waziri amedokeza juu ya mpango kabambe wa kitaifa wa uendelezaji wa maji ameuita National Water Master Plan upo katika mpangokazi wake wa kutekeleza katika mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri anayo bajeti moja tu ya mwakani kuelekea 2025. Ningemsihi Mheshimiwa Waziri, katika mpango wake huu hebu ile tunayoiongelea kama gridi ya taifa ya maji hebu iweke, itakupa mileage, itakupa cha kuzungumza baada ya wewe kumaliza uwaziri wako.

Mheshimiwa Spika, ni kwa sababu gani nasema hivi, hii itatusaidia pia kuanza kutumia maji kutoka katika vyanzo ambavyo havikauki. Yaani Misri wanatumia maji ya chanzo kikubwa kutoka Ziwa Victoria, wanakunywa wanamwagilia wanapata faida lakini sisi tunavyanzo vikubwa vya maji lakini hatuja vitumia vizuri. Kwa hiyo katika ule mpango kabambe wake ninamsihi sana Mheshimiwa Waziri; kwamba haina maana watu kama wa Kisiwa cha Ukerewe ambao wao wanazungukwa na maji lakini leo hii bado upatikanaji wa maji ni asilimia 57, siyo sawa.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri watu wa Katavi, Rukwa watu wa Mbeya watu wa Kigoma wanazungukwa na ziwa ambalo lina kina kirefu sana lakini bado hawatumii maji ya kutosha. Mheshimiwa Waziri mcheza kwao hutunzwa, kwenye National Water Master Plan wayaingize haya na atakwa amefanya vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana nakuksukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)