Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja iliyoko Mezani inayohusu maji.

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii. Pia nawashukuru wananchi wa Urambo kwa kuendelea kufanya kazi pamoja nami. Vile vile kipekee nitoe shukrani kwa upande wa Waziri, Mheshimiwa Jumaa Aweso na msaidizi wake wa karibu, Naibu Waziri Mheshimiwa Engineer Mahundi na Katibu Mkuu, Engineer Kemikimba; na Naibu Katibu Mkuu, Engineer Luhemeja; na wakati huo Engineer Kapufi wa Mkoa wa Tabora na Engineer wa kwetu Urambo ambaye tunafanya naye kazi sana katika sekta ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli anatujali, hasa kwenye suala la maji, tangu ameingia kazini akiwa Rais, fedha nyingi na juhudi kubwa zake yeye binafsi na kupitia pia Wizara yake tumeziona, kwa kutupatia fedha shilingi 5,085,000,000 kwa eneo hili ikiwemo shilingi milioni 220 kwa ajili ya bwawa litakalojengwa Kalemela Urambo.

Mheshimiwa Spika, ninapokuwa kwenye mikutano yangu ya hadhara huwa naendelea kuwakumbusha wananchi wa Urambo kwamba najua changamoto za Urambo, na ya kwanza kabisa ni maji. Mengine huko yanafuata, upatikanaji wa mbolea kwa wakati, umeme na kadhalika, lakini ya kwanza huwa ni changamoto ya maji.

Mheshimiwa Spika, changamoto ya maji imekuja kutokana na aina ya miamba tuliyonayo. Pamoja na jitihada nyingi za Serikali za kuchimba visima, kwa kweli ilifikia wakati hata fedha, Shilingi milioni 500 zilirudi Wizarani baada ya Mkandarasi kushindwa kuzitumia kutokana na ugumu wa upatikanaji wa maji Wilayani Urambo. Hata hivyo, naishukuru Serikali hii, na hasa alipopata Wizara hii Mheshimiwa Jumaa Aweso, ametambua kwamba kweli Urambo kuna matatizo ya maji. Nakushukuru sana Waziri. Ndiyo maana akatuingiza kwenye miji 28. Mwenyezi Mungu akubariki sana baba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa Mheshimiwa Waziri nakuheshimu, nakupenda, mwanangu, tangu tulikwenda Chamwino tukashuhudia kusaini, maji yale bado. Nakuomba leo kwa heshima na taadhima, utakapokwenda pale mbele, hebu tamka kwa uwazi kabisa mwanangu Mheshimiwa Jumaa Aweso. Lini maji yanafika Urambo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulikwenda kushuhudia maji yalipofika Tabora, ni kilomita 90 tu, halafu kwenda Kaliua kule ni kilomita 30 tu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri utamke leo wananchi wa Urambo wapate imani na Serikali yao, wajue sasa ukombozi wa maji umefika. Hilo tu ndilo nakuomba mimi, na siendelei kukuhutubia zaidi, kwa sababu ninachokitegemea ni hicho, kwamba leo Mheshimiwa Waziri Jumaa Aweso atatamka lini maji yanafika Urambo? Nakuomba pia, siku wanaanza ile kazi, nawe uwepo, au ukishindwa kabisa, mtume Mheshimiwa Engineer Mahundi ili tuzindue, na wananchi wawe na imani na Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kwa kuwa nategemea leo atatamka pale mbele kwamba lini maji yanafika Urambo, kazi inaanza lini? Sina haja ya kuendelea.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja hii. Ahsante. (Makofi)