Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana ya maji ambayo tunasema maji ni uhai. Nasi watu wa Chunya tunaitegemea sana Wizara hii kuhakikisha kwamba mji wetu unakuwa na maji ya kutosha. Tuna imani kubwa sana na Mheshimiwa Waziri pamoja na wasaidizi wake wote wa Wizarani, wakiongozwa na Naibu Waziri. Pia tumpongeze Mheshimiwa Rais, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba anatoa fedha ya kutosha ili waweze kufanya kazi yao vizuri sana. Tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Spika, kwenye Wilaya yetu ya Chunya, katika Mkoa wa Mbeya sisi ndio tunapata wastani wa maji ya chini sana. Sisi tunapata maji kwa wastani wa asilimia 40, ambayo ni kiasi kidogo sana ukilinganisha na mikoa mingine na ndani ya Mkoa wetu wa Mbeya. Kwa hiyo, hili jambo ambalo linafanyika hapa lazima tuliseme ili kuhakikisha kwamba maji yanapatikana ndani ya Wilaya ya Chunya. Tuwapongeze kwa kweli kwenye upande wa RUWASA, wanafanya kazi yao vizuri sana. Kuna miradi Chunya inaendelea ambapo pesa zinaletwa pale, na miradi mingine imeweza kufanyiwa kazi. Kwa hiyo, tunapongeza kwa kazi bora inayofanywa. Tunampongeza Engineer Hans pamoja na Engineer Ismail kwa ushirikiano wao, juhudi zao zinaonekana na wananchi wanaona kazi ambayo inafanyika.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi hiyo ambayo inaendelea kufanyika, tunashukuru pia Serikali kwa kutuletea mtambo wa kuchimba maji kwenye Mkoa wetu wa Mbeya, na gari hili limeweza kufanya kazi kwenye Wilaya ya Chunya. Tayari katika vijiji 14, vijiji vinne vimeshafanyiwa kazi. Kijiji cha Itumbi wameshachimba maji, kikiwemo na Kijiji cha Matondo, Kijiji cha Igundu na Kijiji cha Shoga. Tunapozungumza sasa hivi, tayari fedha zote zilishalipwa, zaidi ya takribani Shilingi milioni 250, lakini wale watu wa mamlaka ya kuchimba maji, DCCIA hawapo eneo la site. Kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri uwasisitize, pesa wameshalipwa, warudi site ili waweze kuchimba vijiji kumi ambavyo vimebaki.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri kama anakumbuka wakati anasaini mradi wa maji wa Kiwira alituahidi kutuletea Shilingi milioni 250 kwa ajili ya mradi wa maji wa Itumbi. Kisima kimeshakamilika tayari, na tayari Engineer wa Maji Wilaya alishakuandikia barua ya kukukumbusha, naomba nami nikukumbushe kwa niaba ya wananchi wa Chunya na wananchi wa Itumbi utuletee hizi pesa ili mradi huo uweze kukamilika.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi nzuri ambayo inaendelea, naishukuru tena Wizara, imetuletea pesa kwa ajili ya mradi wa maji wa extension ya Makongorosi zaidi ya Shilingi milioni 200, kazi inaendelea, na mradi wa Matwiga pia wametuletea pesa ya kumalizia. Naomba kupitia Wizara yako, wasisitize mradi huu wa Matwiga uweze kukamilka kwa wakati. Fedha ipo, na mradi huu kutokana na kuwa ni wa muda mrefu sana, naomba sana uwasisitize mradi huu uweze kwisha ili vile vijiji vya mwanzo viwili; Kijiji cha Matwiga pamoja na Kijiji cha Isangawana, viweze kutumia maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumze kuhusu mradi wa maji wa miji 28. Sisi watu wa Chunya ni moja kati ya wanufaika wa mradi wa maji huu katika miji 28, na mradi huu wa maji, tuna imani ukikamilika utakuwa mkombozi mkubwa sana kwa wananchi wa Chunya hasa Chunya Mjini.

Mheshimiwa Spika, Sera ya Maji ya mwaka 2022 inasema kwamba, ushirikishaji wa wadau ambao ni wanufaika wa maji, lazima uzingatiwe. Kwenye Wilaya yetu ya Chunya, ukiwaza kuwashirikisha wadau, utamshirikisha Mbunge, Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkurugenzi, Mabaraza ya Madiwani pamoja na wananchi kwa ujumla. Kwa huu mradi wa maji ambao unaenda kwenye miji 28, tunasikitika sana kwamba ushirikishaji wake ni mdogo sana kwa sisi wadau wa Wilaya yetu ya Chunya. Katika mradi huu wa maji, sisi tuna maoni yetu namna ambavyo tunataka kushirikishwa.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Chunya ni moja kati ya Wilaya kame, na uchimbaji wa Visima umeweza kuchimbwa kwa muda mrefu na matunda yake yameonekana ni madogo sana. Mwaka 2017/2018 uliletwa mradi wa maji wa Nyatura. Kilichimbwa kisima cha maji na lilijengwa tenki la lita karibu 500,000, lakini mpaka leo tunapozungumza, maji hayapo kwenye ule mradi. Kwa hiyo, tuna experience ya kutosha kuhakikisha kwamba miradi ya maji kwa kutumia visima kwa Wilaya ya Chunya sasa hivi haifai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi watu wa Chunya tulishauri na tukapendekeza kwamba ili kutatua changamoto ya maji ndani ya Wilaya ya Chunya, tuweze kutumia maji ya Mto Bwaziva na Wizara ilifanya kazi hiyo. Mheshimiwa Naibu Waziri ni shahidi, ametembelea mara kadhaa kile chanzo cha maji na mwaka huu pia aliweza kutembelea pamoja na wataalam wake wa maji kuonesha kwamba kile chanzo cha maji kitaweza kutufaa kwa muda mrefu zaidi.

Mheshimiwa Spika, matumizi ya maji ya Chunya kwa sasa hivi ni takribani lita milioni mbili na nusu, na kile chanzo kina maji zaidi ya lita milioni saba na nusu kwa siku. Kwa hiyo, ni chanzo cha uhakika kwa miaka mingi zaidi. Masikitiko yetu, kupitia Mradi wa Maji wa Miji 28, wataalam wa Wizara wanataka wautekeleze mradi huu kupitia visima, kitu ambacho tayari huko nyuma kimeshaonesha kimefeli.

Mheshimiwa Spika, watu wa Chunya wamenituma tuwaambie Wizara, sisi watu wa Chunya hatuko tayari kuona mradi huu unatekelezwa kwa takribani zaidi ya Shilingi bilioni 11 kuchimba visima vya maji ambavyo tuna uhakika kwamba havitakuwa na tija kwa muda mrefu. Nawaomba sana Wataalam wako, wiki iliyopita nilikuja Wizarani nikaonana nawe, nikaonana na Katibu Mkuu, tunashukuru wameweza kulifanyia kazi, amewatuma kule wataalam, wameshaenda kule, naomba mlifanyie kazi.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Chunya wamesema hawako tayari kuona kwamba mradi huu unatekelezwa kwa visima hivi vinavyoenda kuchimbwa kwa sababu wanajua hautaweza kuwanufaisha. Wataalam wa maji wanaishi Dar es Salaam, wanaishi Dodoma, sisi kule ndio wahanga wakubwa wa maji. Watatekeleza wanavyoona wao, lakini wakiondoka sisi ndio tutakaopata shida.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana, sisi watu wa Chunya ndio tunaojua adha. Mheshimiwa Waziri ana usemi wake mmoja unaosema kwamba, anayelala na mgonjwa, ndiye anayejua mihemo yake. Sisi ambao tuko Chunya, ndio tunaojua hii adha. Hao wataalam ambao wako Dodoma na Dar es Salaam, hii adha hawaijui. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, unapokuja ku-wind up hapa utupe jibu la swali hili ili wananchi wa Chunya kule nao waweze kuwa tayari kupokea mradi huu.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)