Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Rehema Juma Migilla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kukushukuru kwa nafasi ili niweze nami kuchangia Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na afya. Pia niwashukuru Mawaziri wote wawili, Kaka yangu mzee wa ukinizingua nakuzingua, na dada yangu pale Mheshimiwa Maryprisca, mnafanya kazi nzuri, bila kuwasahau viongozi wetu, hasa wa RUWASA, Engineer wangu makini sana Kapufi, Engineer wangu wa Wilaya, Engineer Mapambano na kwa ushirikiano mkubwa kabisa wa Mkuu wetu wa Wilaya, Kaka yangu Rashid Chuachua.

Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo nataka nianze kuchangia Wizara hii kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri yetu ya Kaliua yenye Kata 28, vijiji 99 na idadi ya watu 700,000 mpaka leo upatikanaji wa maji ni asilimia 45, very shameful. Miaka 62 ya uhuru sasa, karne ya 21 bado tuna asilimia 45 tu ya usambaaji wa maji, hii hali haikubaliki! Mheshimiwa Aweso, nikuulize, hivi ninyi Wizara yenu haina ile sera ya Wizara ya Afya kwamba mgonjwa aliye mahututi ndiye anapewa huduma haraka? Kama Kaliua tuna asilimia 45 hamtuongezei miradi mnapeleka maeneo mengine, Kaka yangu safari hii ukinizingua tunakuzingua Wanakaliua. Tunaomba miradi ya maji iende Kaliua na maji yapatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ninapenda nichangie leo ni kuhusu mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria. Kwanza tuanze kushukuru kwamba katika mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria wa miji 28 na Kaliua tumo, ambao utakwenda ku-save Kaliua na Jimbo la Ulyankulu.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuwekwa kwenye huu mradi, tukiwa Tabora pale kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kulikuwa kuna nyomi ya hatari, Rais wetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, aliongea kwamba wakati anazindua mradi wa maji wa Tabora, Igunga na Nzega kuna fedha ilibaki shilingi bilioni 25, na akasema zile fedha zitakwenda kusambaza maji Kaliua, Urambo na Sikonge, lakini mpaka leo zile hela hatujui zimeyeyukia wapi. Kaka yangu, Mheshimiwa Aweso, leo nimesema nakuzingua kwa kushika shilingi yako, nataka nipate majibu, hizi shilingi bilioni 25 ambazo tulitengewa zimekwenda wapi, hatuoni mradi umeanza, hatuoni ma-caterpillar huko au wakandarasi. Kaka yangu tunaomba utupe maelezo ya kutoka hizi fedha zimekwenda wapi, kwa sababu watu bado wanapata shida ya maji, tunaendelea ku-share maji na wanyama, karne ya 21 hii ni aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndoa nyingi zinakufa huko vijijini kwetu kwa sababu ya watu kwenda kutafuta maji, bado wananchi wangu hasa akina mama kule watu wanasema siyo pisi kali kwa sababu hata kusuka nywele hawasuki vizuri. Atasuka nywele aende kufuata maji mbali? Naomba Kaka yangu Mheshimiwa Aweso, leo kitaumana hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kutoa shukrani, nimeona Bwawa langu la Ichemba tumelitengea shilingi milioni 750 kwa ajili ya kuanza utekelezaji. Sasa hivi hatutaki mbambamba, yale masuala ya ukinizingua nakuzingua au ubwabwa unaonekana kwenye sahani hatutaki, tunataka kwamba tumetenga hizi fedha tuone wakandarasi wamekwenda site kule na hawa wakandarasi wawe ni wakandarasi wasio makanjanja, tumeteseka kwa kutosha Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni katika gharama za uunganishaji wa maji na bei ya maji. Mheshimiwa Waziri, maji tunayotumia ni ya RUWASA, hatuna chanzo kingine. Kama inavyofahamika utafiti umeonesha Wilaya za Kaliua na Urambo vyanzo vya maji haviko karibu. Kwa hiyo, chanzo kikubwa cha maji ni kutumia sources nyingine. Urambo na Kaliua maji yaliyo karibu ni kutoka kwenye Mto Ugalla au Mto Malagarasi, lakini mpaka leo hatuoni mchakato wowote wa kuchukua maji kutoka Mto Ugalla au Mto Malagarasi.

Mheshimiwa Spika, sasa tunauliza hivi kuna agenda gani juu ya maji ya Ziwa Victoria? Why maji kutoka Ziwa Victoria? Why hatuoni mpango wa kutoa maji Ziwa Tanganyika au Mto Ugalla ambapo ndiyo karibu na kwetu Kaliua na Ulyankulu? Why hatuoni kuna mpango wa kuyatoa maji kutoka Malagarasi kuyaleta Kaliua lakini tunataka tuyatoe Ziwa Victoria? Kuna utafiti gani ambao mmefanya mkaona maji yanayofaa kwa matumizi ya binadamu ni ya Ziwa Victoria na siyo ya Ugalla wala siyo majiya mto Malagarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali hii kwa sababu mnayatoa mbali mnasababisha hata gharama za uunganishaji kuwa kubwa lakini bado hata hakuna bei elekezi, leo mtu anatamani aunganishe maji lakini kwa sababu hakuna bei elekezi maji yanachacha. Tunashukuru kuna miradi ya maji pale lakini yale maji yanachacha, watu wanaunganishiwa kwa bei kubwa lakini bado hata ndoo shilingi 50. Shilingi 50 kwa mwanakijiji jamani ni kubwa sana. Leo hana uwezo wa shilingi 50 kwenda kununua maji, matokeo yake wanasafiri umbali mrefu kwenda kuchukua maji kwenye vile visima walivyovizoea. Hebu tu-regulate hii bei ya maji ili wananchi wengi waweze kuunganishwa na kuendana na kasi ya Mama Samia ya kutua ndoo kichwani.

Mheshimiwa Spika, tumekalia tu kusema RUWASA, maji bombani, maji bombani hayatoki. Hatujawahi kufungua maji. Niombe sana huu mpango wa kuunganisha itoke bei elekezi ili hawa wananchi wetu waweze kupata maji, waweze kuingiza majumbani kwao kama inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala hilohilo la maji, tunaona kwamba bado kuna migogoro mingi sana na ushirikishwaji kwenye miradi ya maji watu wetu hawashirikishwi. Hali hii inasababisha miradi iweze kukwama au isifanyike kwa wakati. Unakuta hata Wabunge tupo huku mambo kule yanaendelea. Matokeo yake wale wananchi wanazua migogoro, hawalipwi fidia zao, tunaomba sasa tunapopeleka hii miradi tuhakikishe kuna suala la ushirikishwaji wa wananchi kwenye hii miradi, waione kwamba ni ya kwao sasa ili hata uvunjifu wa mikataba au uharibifu mwngine usiweze kutokea. Kwa hiyo, ninaomba sana wananchi washirikishwe, kama ni fidia walipwe kwa wakati wasiwe na kinyongo. Mwananchi akiwa na kinyongo ukipeleka mradi usiku kwa usiku atauhujumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kaka yangu Mheshimiwa Aweso, naamini wewe ni kijana na ninaamini utendaji wako wa kazi na Watendaji wako mnafanya kazi vizuri sana na nina- appreciate, lakini leo suala la kusema ubwabwa wa kushiba unaonekana kwenye sahani Kaka yangu leo nitakamata shilingi yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, siungi mkono hoja mpaka maelezo yangu na mahitaji yetu ya Wanaulyankulu na Kaliua yatakapokamilika. (Makofi)