Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi ya kuchangia katika Wizara yetu ya Maji. Niungane na Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri ambayo inafanyika ndani ya Wilaya ya Misenyi, Jimbo la Nkenge na hasa kwa huduma ya maji ambayo tukiangalia historia ya miaka miwili iliyopita na sasa, tuko sehemu nzuri sana kwa miradi iliyotekelezwa.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze sana Waziri Mheshimiwa Aweso, Naibu Waziri Mheshimiwa Maryprisca Mahundi, kwa kazi nzuri wanayoifanya, lakini nyuma yao wapo watu ambao wanawapa support. Kwa nafasi ya pekee pia, nimpongeze dada yangu Katibu Mkuu, Nadhifa Kemikimba, lakini na Ndugu yetu Bwana Cyprian Luhemeja, ambao na wenyewe wanashiriki kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kwamba, wanasogea.

Mheshimiwa Spika, Wizara inafanya kazi nzuri, lakini na katika mikoa yetu wapo watendaji ndani ya Wizara hii ambao wanafanya kazi vizuri. Nichukue fursa hii pia kumpongeza Regional Manager wa Mkoa wa Kagera, ndugu yangu Warioba Sanya. Pia na Meneja wangu wa Wilaya ya Misenyi, bwana Andrew Kiembe, pamoja na timu zao zote kwa sababu, wanafanya kazi kwa ushirika. Mheshimiwa Waziri kama anavyojua anao watoto wengi, lakini anao wa BUWASA. Ninaye ndugu yangu pale John Silati naye, Mtendaji Mkuu wa BUWASA pamoja na wasaidizi wake wanafanya kazi nzuri, wanamwakilisha vizuri Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijachangia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, kulikuwa kuna mfumo ambao kidogo ulikuwa unachelewesha utendaji kazi wa manunuzi wa kikanda, sasa hivi ameupiga chini, ameuweka ngazi ya Mkoa. Nimpongeze sana kwa sababu ni hatua kubwa ambayo inarahisisha kazi kwa wasaidizi wake na kazi ikaenda kwa speed kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasimama hapa nikiwa nina furaha kubwa kwa niaba ya wananchi wa Misenyi. Kazi imefanyika kubwa, kata 20 zote leo tunapoongea nyingine tumemaliza suala la maji katika kata nzima, lakini sehemu nyingine tuko katika mkakati wa kupeleka maji pale. Tukiangalia Kata ya Gera maji yameenda katika vijiji vyote wananchi wanapata maji safi na salama. Ukiangalia Kata ya Ishozi mradi mkubwa wa maji uko pale, sasa hivi maji yanawekwa kwenye tenki ili ku-test mifumo, ili kuona maji sehemu ambapo yanaenda vizuri na sehemu ya kurekebisha.

Mheshimiwa Spika, pia tukiangalia Kata ya Buyangu, Serikali imetuletea fedha, mradi umekamilika, wananchi wa Rutunga, wananchi wa Rwamachi wanapata maji na eneo la Buyangu lililobaki tunaona tunapata maji kutoka mradi mkubwa wa Kata ya Kitobo ambapo vijiji vitano vyote vya Kata ya Kitobo, lakini na huku Vijiji vya Kishoju, Rushasha na Kikono watapata maji kutoka kwenye mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaona Kata ya Nsunga mradi umekamilika na Kijiji cha pembeni cha Ngando sasa hivi kisima kinachimbwa ili kiweze kupelekewa maji. Nimwombe Mheshimiwa Waziri ambacho, wakandarasi wetu pale katika maeneo hayo miradi hii wakati mwingine malipo yanachelewa. Jana ametuambia mahususi kwamba, pochi la mama limefunguka, tuombe basi wakandarasi hawa wapate fedha zao kulingana na maombi yao na kazi waliyofanya ili sasa waweze kukamilisha hizo kazi kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunao Mradi mkubwa wa Kyaka - Bunazi. Mheshimiwa Waziri mradi huu ni mkubwa sana na amefanya juhudi yeye pamoja na Wizara yake kuhakikisha kwamba unakamilika na ulikamilika. Mheshimiwa Rais amekuja ameuzindua mwaka jana, lakini kuna kazi kubwa ambayo wameifanya kwa kutumia akili ya kuhakikisha wanavusha maji kutoka upande wa Kyaka kwenda upande wa Kasambya kupitia katikati ya Mto Kagera. Ilisumbua sana kitaaluma kupitisha chini ya daraja, ikaonekana sio kweli, lakini wamezama ndani ya maji, maji yakavuka, lakini mwuombe Mheshimiwa Waziri thamani ya kuvusha maji yale kule mbele kwa wananchi bado haijaonekana vizuri kwa sababu, bado kuna maeneo ambayo wananchi hawajapata maji.

Mheshimiwa Spika, tukiangalia katika Kijiji cha Gablanga maji hayajafika, lakini ukiangalia Kakindo maji hayapo. Ukiangalia Mabuye sehemu imepata maji, lakini sehemu nyingine maji bado hayajafika, lakini pia ukiangalia Nyabiyanga maji yamepita baadhi ya maeneo. Tungependa kwamba, Mheshimiwa Waziri akipeleka maji katika Kijiji fulani, vitongoji vyake vyote amemaliza na hiyo kazi inakuwa imeisha.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Kyaka tunaona katika Vitongoji vya Nyakashaga, Doga, lakini pia na Bungabo bado maji hayajafika. Kwa hiyo, nimwombe Waziri kwa kazi kubwa iliyofanyika katika eneo hilo, basi aweze kukamilisha mradi huo ili uweze kuwa mradi wenye thamani kwa wananchi ambao wako katika Makao Makuu ya Wilaya ya Misenyi.

Mheshimiwa Spika, niipongeze Serikali, wakati naingia hapa kilio changu kilikuwa ni kuhakikisha kwamba, tunapata maji kutoka Ziwa Victoria na Mheshimiwa Waziri ninaposema Ziwa Victoria sisi kwetu ni hatua kumi kwenda ziwani, sio kama hizi kilometa nyingine ambazo zinaombwa kwa sababu, Ziwa Victoria liko hapo kandokando ya kata zetu. Sasa kilio changu ni Kata ya Kashenye, Mradi kutoka Ziwa Victoria sasa hivi ni mwaka wa pili, lakini nimshukuru Mheshimiwa Waziri, nimewasiliana na wataalam wangu kwamba, sasa hivi Mradi mkubwa wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika Kata ya Kashenye katika Vijiji vyote vya Kashenye, Bukwali na Bushago, sasa hivi unaanza na taratibu za manunuzi zimeshafanyika.

Mheshimiwa Spika, mradi huu hauishii Kashenye unaenda mpaka Kata ya Kanyigo yote ili watu wapate maji safi na salama ya uhakika, unaenda Kata ya Bwanja. Nimwombe Mheshimiwa Waziri kuna kata jirani za pale ambazo zina shida ya upatikanaji wa vyanzo vya maji, kwa mfano, nikisema Kata ya Bugandika; nimwombe mradi huo ukishakuja kwa phase hizo jinsi walivyojipanga kibajeti, basi hata hizo kata ambazo ziko jirani zina shida ya kupata vyanzo tuziangalie ili mradi huo sasa uweze ku-extend mpaka Kata ya Bugandika ili wananchi waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naangalia maeneo mengine ambayo sasa katika bajeti ya 2023/2024 tumeweka kwenye bajeti, Kata ya Bugorora hakuna maji, lakini tunaona Kata ya Minziro. Niombe Mheshimiwa Waziri fedha hizo kinapofika kipindi cha bajeti basi tupate fedha hizo ili wananchi hawa wa kata hizo na wenyewe wasijione wapweke kwa sababu, katika kata nyingine kama nilivyosema miradi ya maji kwa kweli, ni mizuri, ni ya uhakika na mingine inaendelea. Ni pongezi sana kwa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna kata nyingine ambazo zinahitaji maboresho, bado tunatafuta vyanzo vya maji. Kata ya Ruzinga bado mpaka sasa hivi suala la maji halijawa la uhakika, lakini tunaona Kata ya Ishunju, Mabali na Kirimilile na eneo la Mutukula, niombe sana. Tumeomba fedha milioni 450 Mheshimiwa Waziri ni kidogo kwa Kata ya Mutukula kupeleka maji katika vitongoji vyake ambavyo ni vitatu, ambavyo havina maji.

Mheshimiwa Spika, kwa kusema maneno hayo, nikushukuru kwa nafasi. Naamini sasa bajeti ya Misenyi itakamilika ili wananchi waweze kupata maji. Ahsante sana. (Makofi)