Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii nyeti. Nawapongeza watani zetu Yanga, kwa jitihada kubwa walizozionesha kwa kuliwakilisha Taifa vizuri. Hongereni sana. Hicho wana Simba ndicho tulichokuwa tunakitaka, msiwe mnadandala dandala tu, pigeni mzigo, boli litembee, mlete ushindi na heshima ya Taifa. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo. Maji ni afya, maji ni biashara, maji ni chakula, maji ni dawa, maji ni kila kitu. Nianze na Jiji la Dodoma. Nitambue jitihada zinazoendelea za kwenda kupata maji safi na salama yenye uhakika kwa jiji la Dodoma. Jitihada hizi bado hazileti matumaini kwa wanajiji wa Dodoma kulingana na miradi iliyowekwa ambapo miradi hiyo ni mikubwa na itatekelezwa kwa muda mrefu. Kwa hiyo, maana yake nini? Wanajiji la Dodoma bado tutaendelea kuteseka na ukosefu wa maji ya uhakika ndani ya jiji hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jiji la Dodoma lina mradi unaotarajiwa kuja kumaliza changamoto ya maji Dodoma ni Farkwa. Pia tuna mradi wa Ziwa Victoria. Miradi hii yote haiishi leo wala kesho, ni zaidi ya miaka sita. Nikawa najaribu kufikiria, kama miradi hii inatupeleka miaka sita, hiyo ni michache, labda mpaka nane, kumi, jitihada gani za Serikali kwa Wizara yako inayokwenda kuzifanya kwa ajili ya kuhakikisha tunapata maji safi na salama na yenye uhakika kwa kipindi hiki ambacho ninyi mnaendelea na michakato hiyo kwa ajili ya Ziwa Victoria pamoja na Farkwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba kuna visima Nzuguni mmechimba. Vile visima mbona navyo vinachukua mchakato wa muda mrefu? Tangu tumekwenda kutembelea mwaka 2022 mpaka leo kuko kimya. Tunaomba hiyo miradi ikamilike mpunguze hiyo jam kwenye Kata ya Nzuguni, Kata ya Ipagala na Kata ya Kisasa ili yale maji yaliyokuwa yanatoka Mzakwe kuja kwenye hizi kata yaweze kugawanyika yaende kwenye maeneo mengine. Wizara toeni fedha, mpeni Mkandarasi asambaze maji kwenye vile visima ili tupunguze hiyo adha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, mchakato wa Ziwa Victoria, upembuzi wa awali umekamilka, Farkwa, halikadharika, hivi ni nini kinachosuasua mpaka leo? Naomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja utawaambia wana Dodoma changamoto ambayo bado ipo inayosababisha kutokuendelea na miradi hii miwili ni nini? Nitaomba uje uwaambie wanajiji la Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri, miji 28, Waheshimiwa Wabunge wamesema; Chemba Mkandarasi ameripoti, amefika, lakini Mheshimiwa Waziri Mkandarasi huyu karipoti. Jimbo la Chemba lina vijiji 114, kata 26, na vitongoji 436. Jimbo hili kati ya vijiji 114 lina vijiji 47 tu vyenye maji. Vingine vilivyobaki havina maji. Tunatarajia na tunaendelea kutarajia na kuiomba Serikali kubadilisha mtazamo wa maji ya Farkwa kutokuja Chemba, kwa sababu mtakuwa hamtutendei haki. Mradi huu wa miji 28 unakwenda kutekelezwa Chemba na viunga vyake. Ina maana tutatekeleza kwenye vijiji visivyozidi vitano. Kwa hiyo, jumlisha 47, tutakuwa na vijiji 52. Angalia huo upungufu wa maji kwa Wilaya ya Chemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunatamani na tunawaomba sana, mradi wa Farkwa, maji tupate na sisi wana Chemba, ndiyo suluhisho letu, badala ya kutuambia, mnatoa maji Farkwa, Wilaya ya Chemba ambako ndiko maji yanakozalishwa, mje myapitishe yaende Bahi, yaje Chamwino, yaje Dodoma Mjini, Chemba tubaki tunatazama tunapiga picha. Hatutakubali hicho kitu mkifanya kwa namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali ya kuondokana na changamoto ya maji kwenye Wilaya ya Chemba, ulitupatia mabwawa matatu; mabwawa mawili yamekamilika. Tuna suala la bwawa la Kiboka, Mkandarasi alileta certificate tangu mwaka 2022 mwezi wa Kumi na Moja, hamjampa advance payment. Tunaomba huyu Mkandarasi apewe advance payment aweze kwenda site aanze mradi ule ili nasi tuondokane na hiyo adha ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitambue jitihada kubwa za mamlaka zetu za maji zinazofanya huko kwenye Mikoa yetu na kwenye Wilaya zetu. Katika jitihada hizo zote mamlaka za maji wanazozifanya, bado wana changamoto kubwa ya ukusanyaji wa madeni kwa watumiaji wa maji. Kwenye hili Waziri nitakuomba, Mamlaka zako naomba uzisimamie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi sana naomba nizitaje chache kuhusiana na madeni haya. Naomba nianze na mamlaka RUWASA, imeshindwa kukusanya Shilingi milioni 119, ziko huko, hawajakusanya wao; DUWASA Shilingi bilioni 207; SUWASA Shilingi milioni 532; KUWASA, Shilingi bilioni 1.7; MUWASA Shilingi bilioni nne; DUWASA Shilingi bilioni 6.7; MWAUWASA Shilingi bilioni 6.9 na DAWASA Shilingi bilioni 11. Hizo chache! Jumla kwa haya madeni yote ukijumlisha ni Shilingi bilioni 31.6. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hii laiti ingekusanywa vizuri, ingetusaidia kuwasaidia na wenzetu wengine wa vijijini kuhakikisha nao tunawaboreshea mazingira bora ya upatikanaji wa maji safi na salama ya kunywa. Wanafanya kazi kubwa, tunaitambua, lakini tunaomba uwasimamie waongeze jitihada ya ukusanyaji wa madeni kwa watumiaji maji kwenye maeneo yao waliyosambaza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, tasisi za Serikali zinazodaiwa na mamlaka ya maji pia tuziombe zilipe madeni yao zimalize ili taasisi hizi ama mamlaka zetu hizi, ziweze kujiendesha na ziendelee kutoa huduma za maji kwa watumiaji wengine wa maji ambao mpaka sasa bado hawajapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la majitaka kwa Jiji la Dodoma na majiji mengine. Bado tuna changamoto ya majitaka katika nchi yetu na hususan Jiji la Dodoma. Niliona jana Mheshimiwa Waziri ukisaini mikataba kwa ajili ya mchakato sasa wa kwenda kuhakikisha tunaanza miundombinu ya uondoaji wa majitaka ndani ya Jiji la Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, speed ni ndogo, kutoka asilimia 20 mpaka kufikia asilimia 40, Mheshimiwa Waziri tunaomba mpambane. Hizi fedha ambazo leo DUWASA wameshindwa kukusanya Shilingi bilioni sita, na pia kuna upotevu wa maji yanapotea huko barabarani kutokana na miundombinu mibovu; hizi fedha wangekusanya wangeweza kusaidia pia kwenye suala la uwekezaji kwenye miundombinu ya majitaka na hatimaye Jiji hili likaendelea kuwa safi na watu tukaepukana na maradhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, speed wanayokwenda nayo ya kwenye suala zima la majitaka tunaomba waiongeze, ni eneo ambalo wamelisahau sana. Kwa hiyo, tunawaomba sasa twendeni kwenye suala zima la uwekezaji wa majitaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ambalo nilitamani kulisemea ni suala zima la upandishaji wa bill za maji. Kumekuwa na utaratibu wa mamlaka zetu kwamba wanakwenda, wanaona gharama za uendeshaji zimekuwa kubwa na kuamua kupandisha bili za maji. Wamekuwa wakitumia mfumo wa kutuma ujumbe kwenye simu za wateja ili kwenda kushiriki kwenye vikao vya kupandisha maji, lakini taarifa zile, na huu ni mkanganyiko wa hizi taasisi; anayetaka kupandisha bili ya maji, tuseme ni DUWASA, lakini kibali anatakiwa apewe na EWURA, Wizara ya Nishati. Sasa huyu anayetakiwa kupewa kibali ili aweze kupandisha gharama ya bili za maji, yeye ndiye anayealika wajumbe ama wadau wa watumiaji maji kwenye huo mkutano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mfano mmoja. Mwezi uliopita, mimi binafsi na baadhi ya Wabunge tulipata message.

MBUNGE FULANI: Mmh!

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Saa 7.00 mchana ndiyo tunatumiwa message za kwenda kwenye kikao kesho, lakini ukiangalia hata hizo jumbe zenyewe namna zilivyotumwa, siyo rafiki sana. Nikawaza kwamba aidha, kuna mbinu inayochezwa baina ya EWURA pamoja na DUWASA ili watumiaji wa maji wasiende wengi ili wao wapitishe kile wanachokihitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Wizara ya Nishati na Wizara ya Maji, suala la kupata maoni kwa ajili ya kupandishwa bili za maji, wasiwe wanaalika mkutano wa hadhara wa kuja kukaa JK pale, waende chini kwa watumiaji wetu wa maji kule walikopeleka mita. Tuwaitishe mikutano; tuna taasisi zetu, tuna mifumo ya kitawala. Tuna Mwenyekiti wa Mtaa, Mwenyekiti wa Kijiji, tuna watendaji wako kule, wawape taarifa, waweke kipaza sauti, wawatangazie wadau wa maji, ili waende wakatoe maoni yao kuhusiana na sula zima la kupandisha bili za maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naitolea mfano Dodoma kwa sababu ndilo eneo ambalo nina uzoefu nalo. Dodoma leo tunapandishiwa maji, lakini kutokana na hali halisi tuliyonayo ya mgao wa maji, kwa mwezi tunapata maji siku nane. Siku nane ndizo tunazopata maji, sasa unataka unipandishie bili tena, kwa hiyo, unajikuta unaanza kuwaza, kama maji siyapati, kwa nini unataka kupandisha bili? Kwa hiyo, kwenye hili, nawaomba sana Wizara ya Maji pamoja na Wizara ya Nishati, angalieni namna bora na msiwe mnaona tu, wakati mwingine Mheshimiwa Aweso, haya madeni mamlaka zikusanye, ziache kukimbilia tu kwenda kupandisha bili, kuwaongezea wananchi mzigo. Wakusanye madeni yao, waboreshe mabomba yao ili upotevu wa maji usiwepo, maji yapatikane vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kwa Mheshimiwa Waziri, ili kuondokana na hizo gharama za madeni, tulikuomba hapa pre-paid meter. Lete pre-paid meter. Mmefunga kwenye baadhi ya taasisi, tunaomba na Watanzania wengine tupeni. Zipe mamlaka ziagize pre-paid meter wafungiwe watu. Moja utapunguza hata watumishi ndani ya Wizara, kwa sababu umeme leo tunalipa ndiyo tunatumia, kwa nini maji tusilipe ndiyo tutumie? Tutaondokana na migogoro, na kusuguana na kunyoosheana vidole kusikokuwa na tija. Utaondokana na malalamiko ya ubambikizaji wa bili, utaondokana na malalamiko ya kila aina. Tutafutie pre-paid meter zitazoenda kutuletea ukombozi katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ndani ya Wizara yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi. Nakutakila kila la heri Mheshimiwa Aweso katika utekelezaji wa majukumu yake pamoja na watendaji wake wote, Mungu awabariki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)