Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja iliyo mbele yetu ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kunipa uhai kuweza kusimama hapa kwa siku nyingine. Pili, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Jumaa Aweso, kwa kutuletea bajeti nzuri na kwa kazi yake nzuri. Niwapongeze vilevile Naibu Waziri, Dada yangu Mheshimiwa Mahundi na Watendaji wote ndani ya Wizara wakiongozwa na Katibu Mkuu Injinia Kemikimba, Naibu Katibu Mkuu. Kwa namna ya pekee, Jimbo la Njombe, mimi ndiye Mwakilishi wao, naongea kwa niaba ya wananchi wa Njombe, ninawapongeza sana Maafisa wa RUWASA ambao nimekuwa nikifanya nao kazi kwa karibu sana katika siku zote hizi. Resident Manager Ndugu Shaka na Injinia Malisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Njombe lina mjini na vijijini na nitaiongelea hiyo kama moja ya sehemu yangu kubwa ya mchango wangu wa leo. Kwa hiyo nimpongeze Injinia Kyauri ambaye ni MD wa NJUWASA kwa maana ya kwamba yeye ana-cover eneo la mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya matatizo makubwa sana ya Mji wa Njombe toka nimeingia hapa Bungeni ilikuwa ni ukosefu wa maji katika Mji wa Njombe na katika vijiji vyake, jambo hili lilikua linaleta sintofahamu kubwa kwa sababu Njombe tuna vyanzo vingi vya maji, nami ninapenda toka ndani ya roho yangu kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mtu wa kwanza kutukomboa kwenye matatizo ya maji. Maji bado hayajaanza kutoka lakini tuna miradi ambayo inaleta matumaini makubwa sana kwa Mji wa Njombe kwa mara ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miradi mikubwa mitatu pale Njombe Mjini ambayo italeta maji kwenye eneo la mji, pia tuna mradi mkubwa sana, naishukuru sana Serikali, mradi wa Benki ya Exim - India, mradi huu tumeungojea kwa hamu, sasa tunajua Wakandarasi wameanza kazi, kwa hiyo tuna uhakika sasa ahadi ambayo Chama cha Mapinduzi kilitoa kupitia Ilani, mimi Mbunge niliitoa na Mheshimiwa Rais akitembelea Njombe aliitoa kwa wananchi, kwamba utakapofika wakati wa uchaguzi tutakuwa na maji yanayomwagika, kwa lugha ya kwetu tunaita maji bwerere pale Njombe. Nafurahi sana kwamba mambo haya tutakwenda kuyatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna mradi mwingine nimeuona kwenye bajeti ya Mheshimiwa Aweso wa majitaka. Mji wa Njombe unakua kwa haraka sana na sasa tuko katika maandalizi ya kuomba kuwa manispaa. Kwa hiyo kwetu mradi wa majitaka ni mradi muhimu sana, tunakushukuru sana Mheshimiwa Aweso na timu yako nzima kwa kuona umuhimu wa kuipa Njombe mradi huu kwa wakati huu, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye jambo la pili ambalo ni kubwa sana kwangu. Nashukuru sana nina ushirikishwaji mzuri sana katika kupanga miradi hasa ya vijijini, katika kufuatilia nikagundua kwamba baadhi ya miradi ambayo tulitegemea tungeipata mwaka huu katika vijiji vyetu haijaingizwa kwenye mpango, nilivyozidi kudodosa na kuuliza nikakuta kwamba tuna mradi mkubwa wa Benki ya Dunia unaitwa P4R (Utaratibu wa Malipo kwa Matokeo) bilioni 350. Nilikuwa na matumaini makubwa sana kwamba vijiji vyetu vitaingia katika mradi huo, lakini kwa bahati mbaya sana havimo, maelezo yanaonekana kama yana-make sense lakini nilipenda nieleze na Mheshimiwa Aweso anisikilize kwa makini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tumeondolewa kwenye mradi huu ambao ni muhimu sana kwa wananchi wa Njombe. Njombe ni Njombe Mjini lakini asilimia 40 ya Njombe Mjini iko mjini, asilimia 60 iliyobaki yote ni vijijini, vijiji zaidi ya 40. Sasa complication hiyo na mradi huo mkubwa ambao una-cover maeneo ya vijijini, Njombe Mjini haimo kwa sababu ina jina linaitwa mjini, lakini Njombe actually asilimia kubwa ni vijiji. Inayo Kata 13, lakini Kata 10 zote ni maeneo ya vijijini, Kata tatu ndiyo za mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, umbali wa vijiji vya Njombe vijijini, niite sasa vijijini ili ieleweke vizuri, unakwenda kilometa 120 nje ya Mji wa Njombe, lakini siyo hilo tu katika Halmashauri zote za mji katika Tanzania, Njombe ndiyo Halmashauri ya mji iliyo kubwa kuliko zote, ina square kilometers 3,210.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika mazingira hayo ni kwamba lengo la kupeleka maji vijijini kwa asilimia 85, Mheshimiwa Aweso kwa ku-exclude Halmashauri ya Mji Njombe na Jimbo la Njombe Mjini, unakwenda ku-distort hiyo figure kwa sababu unabakia na vijiji vingi unavyoviona kwamba viko mjini lakini vyenyewe viko vijijini. Kwa hiyo ni vizuri sana jambo hili likaangaliwa upya tukawa realistic. Kuna majina hapa mimi nimeyakuta tu yako kisiasa, kuita Jimbo la Vijijini Mjini na hili jambo nimeshalifikisha TAMISEMI, tutaangalia huko mbele ili tusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana, hili ni ombi mahsusi kutoka kwa wananchi wa Njombe, kwamba tunaomba sana tufikirie upya kwenye ule mradi mkubwa ambao una- cover maeneo ya vijijini. Tulikuwa na vijiji kama vitatu au vinne ambavyo tayari vilikuwa vinaingia kwenye hiyo program, kuna Kijiji cha Lilombwi, Kijiji cha Ihanga hakina maji ni kijiji kikubwa na kina uwekezaji mkubwa, hivi vijiji vyote vina wawekezaji wakubwa wa parachichi, mahindi, viazi ni watu wanajiweza, hata ukiweka mradi pale kulipia wala siyo tatizo. Kwa hiyo tuwaangalie kwa jicho tofauti, nimelisema hili kwa nguvu sana kwa sababu nina uhakika Wananchi wa Njombe wananitegemea na wanategemea majibu kutoka kwa Mheshimiwa Aweso.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kulisema hilo, ninamshukuru sana Mheshimiwa Aweso, tuna mradi mwingine ambao nilipoingia hapa Bungeni ulikuwa mradi chechefu, mradi wa Igongwi. Maji ya mserereko ambayo yanakwenda kwenye Kata Nne, vijiji zaidi ya Kumi. Mradi huu tunaishukuru sana Wizara imeweza kutoa fedha kwa kiasi fulani mpaka hapo ulipofika. Mradi huu umefika hatua za mwisho, mradi huu bado una lot moja ambayo naishukuru tena Serikali kwamba imeingizwa kwenye bajeti hii, lot five kwa ajili ya kufanya mtawanyiko wa maji kwenye kijiji cha mwisho kabisa katika vijiji zaidi ya nane. Vijiji hivyo ni Kitulila, Kona, Denseland, Madobole, Luponde, Njomlole, Majengo, Uwemba na Ikisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso bado tuna tatizo, nina uhakika kwamba mradi huu unapata fedha kutoka kwenye Mfuko wa Maji. Mfuko wa Maji kwa mwaka jana tunaambiwa kwamba ulipokea karibu bilioni 105, na ilikuwa ni kati ya mwezi Aprili mwaka huu ulikua ni asilimia 60. Kwa hiyo, ni wazi miradi ni mingi sana na mahitaji ni makubwa na Mfuko wa Maji hauwezi ku-cover miradi yote. Ndiyo maana umesema kwenye hotuba yako na mimi naungana mkono na wewe kwamba ni lazima tutoe vipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapanga vipi vipaumbele, umetuambia utapanga vipaumbele kukamilisha miradi ambayo imefikia hatua za mwisho ili wananchi waanze kupata maji. Nami napenda kusema mradi wa Igongwi umefikia hatua za mwisho kabisa, naomba sana kwamba mradi huu upewe kipaumbele katika kupewa fedha hizi za mwisho ili wananchi wa Njombe wa vijijini, vile vijiji vingine ambavyo vyenyewe viko vijijini kabisa, waweze na wenyewe kuanza kupata maji haraka iwezekanvyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukumbusha kwamba Mheshimiwa Rais akiwa Makamu wa Rais, akiwa kwenye kampeni alisimamishwa na wananchi wa vijiji hivi walikusanyika na walimwomba sana vitu viwili, kimojawapo ilikuwa barabara hicho kimeshatekelezwa mkandarasi yuko site, pili ilikua ni kukamilisha mradi wa Igongwi. Kwa hiyo, ni matumaini yangu ukiongezea na nguvu na ahadi ya Rais mwenyewe kwenye mradi huu, tutaukamilisha kwa hizi hatua chache za mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme wazi kabisa, tumshukuru sana Mkandarasi ambaye alisimamia mradi huu, mradi huu

ulikuwa chechefu, tuliutoa ulikuwa mradi wa 2017 ulikuwa umekufa kabisa, 2020/2021 tumeuanza upya. Niendelee kusema kwamba Mkandarasi aliyesimamia mradi huu baada ya kuufufua amefanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba yako na Kamati wamesema kwa kweli tutoe motisha kwa wafanyakazi na makandarasi ambao wanafanya kazi vizuri. Kutoa pongezi ni moja ya motisha nzuri sana, tusiogope kusema kama mkandarasi ametufanyia kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi huyu ana madai bado, ninaomba sana mkandarasi aliyefanya kazi nzuri kwa kujitoa kizalendo kama huyu Jobea General Construction kwa kweli tumfikirie tumkamilishie malipo yake maana yake ni miezi sita toka ame-raise certificate yake na kazi karibu ameimaliza, naishukuru sana Kampuni hii ya Jobea kwa kazi nzuri sana iliyotufanyia Wananjombe.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)