Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. STANSALUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi naomba nitumie fursa hii kwanza kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi. Vilevile nimshukuru sana Mungu wetu wa Mbinguni anayeishi kwa kuendela kutupa uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitazungumza maneno machache sana. Nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, na katika ile hesabu ambayo Mheshimiwa Waziri ameitaja ya maika miwili ya mafanikio kwenye sekta ya maji ya Mheshimiwa Rais, sisi watu wa Nyamagana Pamoja na Jimbo la Ilemela kwa mama yangu pale Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula tunayo kila sababu ya kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa sababu katika mafanikio ya miaka miwili Nyamagana tunaenda kuopata chanzo kingine kipya cha maji baada ya miaka 43.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tupigie mstari baada ya miaka 43 iliyopita ndipo tunaenda kupata chanzo kingine cha maji. Lakini pale Ilemela tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu pale Kabangaja tunategemea kuwa na chanzo kingine cha maji, tangu Ilemela imeanza, tangu Mwanza imekuwepo. Tafsiri ya vyanzo hivi viwili ni kwenda kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la maji kwenye Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela. Kwa hiyo tunamshukuru sana Rais na namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu, yeye ndiye anayelala na mgonjwa na kwa sababu yeye ndiye anayelala na mgonjwa anajua matatizo mengi. Nimpongeze yeye na timu yake kwa sababu, ya kuokoa muda. Kila aliyeko kwenye Wizara ya Maji atambue kwamba, nimempongeza kutokana na kazi kubwa wanayofanya, wakiongozwa na Waziri mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivi? Nasema hivi kwa sababu nchi hii, wamesema pale Mheshimiwa Hokororo na Mheshimiwa Engineer Ulenge, tumekuwa na matatizo ya maji toka miaka mingi iliyopita. Nikizungumza leo Nyamagana hapa, miaka 43 iliyopita tulikuwa tunategemea chanzo kimoja peke yake kilichojengwa miaka ya 80 kikiwa na uwezo wa kuhudumia watu laki moja peke yake. Leo, miaka 43 baadaye tunazungumza chanzo kipya kinachojengwa kitakuwa na uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 48 kwa siku na kitahudumia ongezeko la watu zaidi ya 105,000. Hapa nataka kusema nini Mheshimiwa Aweso? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika pamoja na changamoto nyingi tulizonazo, safari aliyoianza Waziri toka amekuwa kwenye Wizara hii, sisi wenzake inatupa matumaini na faraja ya kwamba, iko kazi kubwa anayoifanya na Wizara yake. Nina hakika ni lazima tumuunge mkono na kumtia moyo kwamba, miradi ya maji siyo sawa na ujenzi wa nyumba, unaweza kufikiri asubuhi, ukajenga jioni, kesho umekamilisha na matokeo yakaonekana. Kazi kubwa anayoifanya ndio itakayotupa sisi dira ya kule tunakokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Nyamagana kama nilivyosema, chanzo chetu cha kwanza kimejengwa miaka ya 80. Leo tunaongeza lita milioni 48 kwenye chanzo kipya, naishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita, mpaka hivi tunavyozungumza Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake umesema mwenyewe tuko takribani asilimia 71. Ukweli usiopingika, kukamilika kwa chanzo hiki itakapofika Julai, tarehe 30, tutakuwa tumefanikisha kupata lita zipatazo jumla yake Kapri Point na Butimba zitakazofikia milioni 148 peke yake. Bado tunahitaji lita milioni 22 ili kuwahudumia wananchi wa Jimbo la Nyamagana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoutaja mradi huu Mheshimiwa Waziri akumbuke ndio utakaowasaidia watu wa Magu na Misungwi, lakini maeneo yetu yote kwa sasa ambayo yanapata changamoto ya maji, ukienda kule Buhongwa, Rwanima, Kishiri, Igoma, Nyegezi, Mkolani, Luchelele, kote huko changamoto hii inategemea kukamilika kwa chanzo hiki. Sasa ushauri wangu Mheshimiwa Waziri; tunafahamu, Ilemela nimetaja chanzo cha Kabangaja, Nyamagana tunacho chanzo cha Capri Point, ili tuweze kuwa na uhakika wa maji kwa wakazi wetu wote kwa maeneo haya, tunahitaji uzalishaji wa chanzo cha Kabangaja pale kwenye Manispaa ya Ilemela, lakini tunahitaji uboreshwaji wa chanzo cha Butimba kitoke kuzalisha lita milioni 48 kwa siku mpaka lita milioni 160 ili tuweze kufikia malengo ambayo tumekubaliana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu na kila mmoja anajua Serikali yetu bado ni himilivu sana kwenye ukopaji na bado inazo sifa za kuendelea kukopa. Kama tuna uwezo wa kukopa au kushawishi na kushirikisha mashirika mbalimbali, kama tulivyofanya kwenye huu mradi ulioko Nyamagana leo, tuendelee kuchukua fedha kwa sababu, tukikamilisha miradi hii tutakuwa tumeliokoa Taifa hili, tumewasaidia wanawake wa Taifa hili, tumeimarisha ndoa kama wanavyosema akinamama za Taifa hili na tumejenga umoja kwenye Taifa hili kwa sababu, tutakuwa na uhakika wa maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine kadri tunavyofanya nusunusu tafsiri yake ni kwamba, leo tumelaza bomba kilometa 17 kutoka Butimba kwenda Sahwa ambapo maji yatakuwa yanapokelewa kutoka kule Butimba, lakini kutoka Sahwa kwenda Igoma kwenye tenki linalozalisha lita milioni tano. Maana yake ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukilazimika kuja kuongeza miaka miwili baadaye itatulazimu kuweka mfumo mpya wa ulazaji bomba, ili liweze kuendana na chanzo tutakachokuwa tumekijenga. Tukikamilisha vyanzo hivi sio mbaya, tunahitaji takribani bilioni 400 kwa mujibu wa wataalamu walivyofanya na bilioni 400 sio nyingi kwenye kuzalisha maji kwa sababu, Mamlaka ya Maji ya MWAWASA inao uwezo mkubwa wa kujiendesha yenyewe kama itakuwa na uhakika wa kusambaza maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri, watendaji wake wote wa Mamlaka ya Maji ya MWAWASA, nafahamu wananchi wa Nyamagana wanazo changamoto, lakini hakuna safari tunayoweza kufika bila kutembea. Hakuna safari tunayoweza kufika bila kuchukuliana. Kazi hii ni kubwa, haijaanza leo na ndio maana nimesema, Waziri Mheshimiwa Aweso chini ya Serikali ya Awamu ya Sita anaingia kwenye rekodi ya Jimbo la Nyamagana na Wilaya na Jiji la Mwanza kwa kuwa wa kwanza kuhakikisha chanzo cha lita milioni 48 kinajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina shaka kazi hii aliyoianza kwa muda mrefu itawasaidia sana, lakini hatuwezi kukamilisha chanzo peke yake bila kukamilisha maeneo yatakayopokelewa maji na usambazaji. Nafahamu tunatarajia au tunakusudia kujenga tanki moja kule Rwanima, Mtaa wa Kagera, litakalobeba lita milioni 10, lakini kule Rwanima yenyewe lita milioni tano, Mtaa wa Kasese kule Mkolani lita milioni tano, ili tuweze kuwahudumia watu wa Luchelele. Pale tuna Chuo cha SAUT peke yake kinahitaji maji yasiyopungua lita milioni 10 kwa siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri alitazame Jiji la Mwanza ambalo ni kilometa zisizopungua saba kutoka kwenye maji mpaka kwenye chanzo na usambazaji wake, ukichukua eneo lote la Nyamagana, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri ni eneo ambalo linawezza likatushangaza na likatuletea mapato mengi kupitia Mamlaka ya Waziri ya Maji na akafanya kazi nyingine na mamlaka hii inaweza kusaidia kuzalisha fedha zitakazotoa huduma kwenye maeneo mengine. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeupiga mwingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie kusema nampongeza sana Mheshimiwa Aweso. Miradi ya maji ni safari na safari hii ameianza vizuri na anaenda nayo vizuri, ni wajibu wetu kumuunga mkono, ni wajibu wetu kumuunga mkono sana Mheshimiwa Rais kwa sababu, malengo na mafanikio yanaonekana. Mabadiliko tunayoyaona kwenye bajeti ya kila mwaka ndio tafsiri ya utekelezaji na matokeo yake. Nimshukuru sana na nimpongeze, watu wa Nyamagana wanamsubiri Waziri kwenye uzinduzi wa chanzo hiki cha maji pamoja na Mheshimiwa Rais, ili waje waone faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe babu, unajua Waziri Mheshimiwa Aweso ni babu yetu, unajua Waziri ni mjukuu wa Wasukuma, kwa hiyo, kila analolifanya ahakikishe babu zake wasimtie laana mzee na safari hii umepata Naibu Katibu Mkuu hapo na yeye ni mjukuu wake, kwa hiyo, ahakikishe kazi hii inakwenda vizuri sana. Mungu awabariki sana, nawashukuru sana, ahsanteni. (Makofi)