Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili mimi niweze kuchangia hoja iliyoko mezani kwetu. Naomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza na pongezi kwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kwa kweli amefanya kazi nzuri sana katika kuhakikisha kwamba mwanamke anatuliwa ndoo kichwani. Zamani tulifikiri siasa lakini tunaona kabisa ana nia na anadhamira ya kweli kuhakikisha kwamba wanawake sasa tunatuliwa ndoo kichwani, na amejua kutuheshimisha sisi wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niungane na Waheshimiwa Wabunge wote kumpongeza Waziri wetu, Mheshimiwa Jumaa Aweso, amefanya kazi nzuri sana Pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Prisca Mahundi. Ana misemo yake usione vinaelea vimeundwa. Mheshimiwa Aweso anafanya kazi nzuri kwa sababu kuna mchango wa akina mama wale wawili ambao leo alitutambulisha pale juu, tena akina mama shupavu; wamemfanya atulie na kuzingatia kazi na Wizara inaenda vizuri. Tunawapongeza sana, utupelekee salamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona kobe yuko juu ya mti ujue amepandishwa. Niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kumpandisha Engineer Kemikimba kuwa Katibu Mkuu, lakini vilevile kumpa unaibu Katibu Mkuu Cyprian Luhemeja. Tuseme sasa upele umepata wakunaji na Wizara itaendelea vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sijawatendea haki kama sitampongeza Mkurugenzi Mkuu wa IRUWASA Eng. Kidegalu, lakini pia Meneja wetu wa Iringa Eng. Joyce, wanafanya kazi nzuri sana ya kuhakikisha kwamba vijiji vyetu vya Iringa vinapata maji na wanatekeleza miradi yao vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze sana Mkurugenzi wa IRUWASA Engineer Kalanje wameubeba Mkoa wetu wa Iringa.

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

TAARIFA

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa tu mzungumzaji, na nimuongezee tu taarifa yake kwamba ni sehemu ya Mawaziri wa ukituma message wanajibu, ukipiga simu wanapokea. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hata usiku wa manane tukimtumia message anapokea. Mkoa wa Iringa umekuwa wa kwanza katika utoaji huduma za maji safi na mazingira kati ya mikoa 26, ndiyo maana nimewapongeza sana viongozi wetu wa Mkoa wa Iringa. Tunashukuru Wizara kwa kuipatia IRUWASA miradi mikubwa ya kuboresha huduma za maji katika Manispaa ya Iringa, katika Miji ya Kilolo na Ilula kupitia chanzo cha Mto Mtitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wametoa kibali cha kutekeleza miradi ya kuongeza chanzo cha maji kata ambazo zilikuwa hazijapatiwa maji, nawapongeza sana Wizara ya Maji. Kwa mfano mji wa Ilula tumeweza kupata milioni 445.7, Mji wa Kilolo milioni 413.8. Tunaomba sasa tupatiwe sasa hiyo advance payment ya milioni 413.3 ili sasa mabomba yanunuliwe ili kazi ya usambazaji iweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee na suala la upotevu wa maji. Nimeona Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamezungumzia upotevu wa rasilimali ya maji. Pamoja na rasilimali za maji kuwa adimu lakini kuna upotevu kati ya asilimia 30 na 40. Hii itaweza kudhibitiwa endapo kutafanyika matengenezo, kwa sababu kumekuwa na matengenezo ya mara kwa mara. Mabomba mengi yamekuwa chakavu sana na miradi mingi imekuwa ya muda mrefu, haikarabatiwi. Sasa, kama itakarabatiwa basi angalau tutapunguza upotevu wa maji mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini changamoto nyingine ni pamoja na upungufu wa watumishi, hasa fani ya ufundi sanifu na wahandisi. Lakini tunacho Chuo cha Maji, tena sasa hivi vijana wengi sana wanakwenda kusoma pale. Tunaomba sasa Serikali iwatumie wale vijana ili wapunguze upungufu ambao uko katika mikoa yetu ikiwepo hata na Mkoa wa Iringa. Pia kuna wafanyakazi wengi sana wana vibali tu, hawaajiriwi. Siku nyingi sana tumekuwa tukisema, kwamba saa ifike sehemu Serikali itoe vibali, kwa sababu hizi mamlaka zina uwezo wa kuwalipa mishahara, ili vijana hawa wasiendelee tu kuwa kwenye zile mamlaka miaka miwili mikataba miaka mitatu; na hasa Dar es Saalam ulikotoka Naibu Katibu Mkuu, na wewe unajua. Sasa waajirini wale vijana basi sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pia kuna tatizo la changamoto ya vitendea kazi zikiwepo gari, hasa Mkoa wetu wa Iringa pia kuna tatizo kabisa la ukosefu wa magari katika wilaya zetu zote. Tunaomba sasa Mheshimiwa Aweso awe na mkakati wa kuhakikisha kwamba vitendea kazi vinapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze pia Wizara kwa kuanza mradi wa maji katika miji 28, hongera sana. Mradi huu ni wa siku nyingi, tumeuliza maswali mpaka tumechoka; lakini sasa hivi tunaona sasa umeanza kutekelezeka. Tumeona mkandarasi ameanza kazi hata pale katika Mji wa Mafinga tumepata tank la lita 2,000,000 pale Changarawe, kwa hiyo tunaapongeza sana. Vilevile kuna mradi wa Matanana na Itimbo, visima vimeshachimbwa bado fedha ya usambazaji. Sasa, tunaomba basi Wizara ituletee ili wanawake waendelee kufaidika na maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye Jimbo letu la Isimani kwa Mheshimiwa Lukuvi tunaeona kuna mradi ule wa Kilolo – Isimani, tayari asilimia 90 umetekelezeka, na ule mradi unaanzia katika Kata ya Lugalo tunaomba pale kata zote au vijiji vyote vipatiwe maji sasa fedha ya usambazaji ndiyo inahitajika pia. Kuna mradi wa Pawaga unahitaji treatment plant, wananchi wanakunywa maji machafu sana. Hiyo yote ni fedha tunaihitaji Mkoa wa Iringa. Tuna miradi mingine tena bado kama mradi wa Kilolo. Mradi wa Kimara tunashukuru kwamba angalau umeshakamilika na wenyewe bado usambazaji. Mradi wa Uwambingeto unaendelea, na sasa uko asilimia 51, mradi wa Ifuwa tulipata bilioni 2.2 mkandarasi kalipwa asilimia 20 tu na maradi umesimama. Tunaomba pesa ende pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Kihesa – Mgagao – Masege wananchi wanapata shida mno, lakini bado uko kwenye uzabuni kila siku wanarudia tunaomba kazi ifanyike. Mradi wa Kata ya Kalenga kwa Mwenyekiti wetu. Kuna mradi wa Tanangozi – Tosamaganga mpaka Lupalama unahitaji ukarabati tu, tunaomba fedha ipatikane. Kata ya Nzii ma – tank mawili tayari tunaomba kazi ya usambazi maji. Lakini pia tunayo kata Mufindi Kusini, Ihoanza Malangali, Igunda. Mradi wa vijiji tisa, mradi wa Mtambula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nielezee sasa kuhusu upungufu wa rasilimali maji. Takwimu zinaonesha upatikanaji wa maji kwa Mtanzania tangu tumepata uhuru hadi sasa. Wakati wa upatikanaji wa uhuru maji yalikuwa wastani wa lita za ujazo 10,000 kwa mtu mmoja kwa mwaka, lakini wastani huo umepungua sasa hivi ni lita za ujazo huo huo 2,250, ambao ni sawa sawa na upungufu wa lita 7,750 sawa sawa na asilimia 77.5. Upungufu huo umechangiwa na sababu zifuatazo; ongezeko la watu na mifugo, uharibifu wa mazingira, uchafuzi wa vyanzo vya maji, shughuli za binadamu, kilimo, ufugaji na mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwaka 2022 Serikali ilifanya mabadiliko ya sheria, lakini sasa tunaomba Serikali ione umuhimu wa kuzingatia zile sheria ili wananchi tuweze kupatiwa. Haya maji bila kufanya hizi sheria zikawa zinafanyika kazi; maana tunaona sheria zinatungwa lakini utekelezaji wake unakuwa sio mzuri sana. Kwa hiyo tunajitahidi vyanzo vingi vinakuwa vinaharibiwa. Tunaomba sasa Serikali isimamie kikamilifu ili tuweze kulinda vyanzo vya maji na mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nampongeza Mkurugenzi wa Dodoma wa Maji (DUWASA) amejitahidi sana, kuna population kubwa sana hapa Dodoma. Lakini juzi tulienda pale Mtera tulienda na Waziri wa Maji, Waziri wa Fedha, Waziri wa Mazingira na Waziri wa Nishati. Tumeona kabisa mambo ni mazuri pale tunaweza tukachukua maji kuyaleta Dodoma, kuliko kwenda kuchukua maji kule Mwanza kuyaleta hapa Dodoma gharama itakuwa kubwa sana. Mimi naona tuangalie huu mradi, kwanza hapa Jirani, kutoka Mtera kuja hapa. Sisi zamani tulikuwa tunafikiri labda itakuwa tatizo kubwa sana kuchukua yale maji ya Mtera, lakini jinsi tulivyoelezewa, alivyoelezea Waziri wa Nishati, wa Mazingira na wa Maji tumeona kumbe inawezekana. Kuna maji mengi sana yanafunguliwa yanapotea pale. Sasa basi yaletwe hapa Dodoma ili yaweze kusaidia wananchi, ili wananchi wa Dodoma waweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba sasa Serikali iangalie hizi mita za maji, tuwekewe mita za maji kama ilivyo TANESCO, kwa sababu wananchi wengi wanalalamikia kwamba prepaid meter…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa…

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja mkono asilimia 200.