Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata hii nafasi, nami niungane na wenzangu kwanza kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akifanya katika kutafuta rasilimali kwa ajili ya nchi yetu, pia katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maji. Ni kweli kabisa amefanya kazi kubwa sana na ndiyo maana tunaona miradi kila kona karibu kila Jimbo miradi mingi inaendelea. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na Watendaji wote wakiongozwa na Katibu Mkuu kwa kazi nzuri ambazo wamekuwa wakifanya, kwa kweli mnastahili kupewa sifa kwa sababu sote tunajua Wizara ya Maji tulikotoka, miradi ilikuwa ni miradi chechefu kweli kweli na ilikuwa ni miradi ambayo kwa kweli iliturudisha nyuma sana lakini sasa hivi kazi kubwa mmeifanya na sisi tunaona mwelekeo ni mzuri. Ninawapongeza sana kwa kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nimeona hata katika Jimbo langu mmenisaidia sana miradi. Kuna ule mradi mdogo ule wa Mlangali Mbewe pale unafanya vizuri, Mradi wa Itunga unafanya vizuri lakini kuna miradi mingine ya Msiya unaendelea kutekelezwa. Mheshimiwa Waziri nakubaliana na wewe kwamba maji ndiyo maisha. Maji ni uhai, maji ndiyo chakula chetu, maji ndiyo nishati, maji ndiyo usalama wa nchi na sote tunakubaliana na hayo. Kama hii ndiyo msingi kwamba maji ndiyo maisha yetu, ukiangalia nchi yetu ilivyo tumebahatika kuwa na mabonde, kuwa na mito, kuwa na maziwa makubwa, mpaka tunayo hata Bahari, sasa hatustahili kuendelea kulia kila siku kwamba tuna shida ya maji kwa ukubwa huu wa mambo yote haya ambayo tunayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachohitajika Mheshimiwa Waziri pamoja na kazi nzuri ambayo umeifanya, kilichobaki ni uje na mpango wa matumizi bora ya maji (water master plan) ya muda mrefu. Ukija na water master plan ya muda mrefu utakuwa umeacha legacy katika nchi hii. Sasa hivi tunatekeleza miradi mingi, kila mahali inatekelezwa lakini hatuwezi kuiendeleza nchi hii kwa kutekeleza hii miradi namna hii. Tuje na mpango ule wa maji namna ya kuyatumia yale maji, ili tutengeneze gridi za kuunganisha sasa kwamba hapa itatoka wapi, hapa itatoka wapi, hapa tutaunganishaje? Hiyo ndiyo itakuwa mpango wa muda mrefu wa kutatua tatizo la maji katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji yaliyoko katika nchi hii hatustahili kila Mkoa wala eneo lolote kukosekana kwa maji, kwa sababu tunayo mengi, tukiwa na gridi kubwa tukiwa na mpango huo wa matumizi basi kila kitu kitakwenda vizuri. Kwa hiyo, nadhani hili ni eneo ambalo unatakiwa uache legacy kubwa katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Waziri ulikuja kule Jimboni na wewe ni shahidi unaona Wilaya yetu ya Mbozi na Jimbo la Vwawa ambalo ni Makao Makuu ya Mkoa, upatikanaji wa maji ni chini ya asilimia 50. Sasa hivi maji katika eneo lile Mji wa Vwawa ni asilimia 49 wakati ndani ya nchi umesema upatikanaji wa maji umefikia asilimia 88.5 mijini. Mimi kwangu ni chini ya asilimia 50 Waziri na wewe ni shahidi ulikuja uliona. Kwa kweli hii haikubaliki!

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Wilaya inavyozalisha katika uchumi wa nchi hii, ukiangalia wananchi wanavyofanya kazi katika nchi hii, hatustahili kuwa na maji chini ya asilimia 50. Ulikuja tukazungumza miradi kadhaa tukaangalia mahali tutakakopata miradi miaka karibu mitatu tunazungumza hilo. Uliniambia tutachukua maji kutoka Ileje kwenye Mto Bupigu na mimi nikakwambia Mheshimiwa Waziri lazima tuwe na mkakati wa muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu na nikasema kule mnakosema uwe ni mkakati wa muda mrefu lakini nako inawezekana kuna changamoto na nikasema kuna maji yanapatikana kutoka kule Ilomba eneo la Mafumbo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni mengi yangeweza kuchukuliwa kule kwa mserereko yakaja mpaka Nyimbili, yakaja Idiwili, yakaja Nyimbili yakafika mpaka Vwawa kwa njia ya mserereko. Pale tunahitaji fedha kidogo tu. Mheshimiwa Waziri hebu hili liangalie. Nisingependa kwamba niwe Mbunge wa kulialia humu ndani. Pale maji unatega tu maji yanaserereka mpaka Vwawa pale Mjini. Kwa kweli hili naomba mliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmekuja na mpango sasa hivi ule wa maji ya Momba, mimi nakubaliana nalo lakini ule hauji Vwawa sasa hivi. Mmesema unaishia Tunduma, kwa nini uishie Tunduma? Halafu mseme utakuja kwenda Mbozi na mpaka Vwawa mpaka Mlowo baadaye? Kwa nini msingetafuta hizo fedha mkaunganisha huu mradi ukatufikia mpaka maeneo yote ili na sisi tuweze kutatua tatizo la maji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri, nakuomba nakuomba kama Kaka yako hebu lifikirie Jimbo la Vwawa. Hebu iangalie Wilaya ya Mbozi, hebu iangalie Wilaya ya Mbozi mtupatie maji katika maeneo hayo ili tuondokane na changamoto za maji. Ipo Kata ya Nanyara, Kijiji cha Songwe, Lusungo na Songwe vina shida kubwa ya maji. Vina mradi wa maji wa mwaka 1978. Mradi ule ulikuwa ni mdogo mpaka leo hii kuna shida ya maji unatakiwa upanuliwe ukarabatiwe ili uweze kutosheleza mahitaji ya maji. Tunaomba hilo mlifanyie kazi na muone namna mtakavyoweza kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Kijiji cha Ihowa, Kijiji cha Weru, Kijiji cha Shomora, Vijiji hivi vyote vinastahili kupata maji. Ije Igare kuna mradi mwingine ulikuwa mkubwa sana lakini maji hakuna. Mabomba yamepita maji hayajapatikana, maji hayapo. Sasa tunaomba mtufikirie muone namna mtakavyoweza kuboresha. Pale Vwawa, Ilolo tulichimba kisima, na wewe ulikuwa shahidi wakati ule ukiwa Naibu Waziri, tumechimba kisima. Kile kisima mmekuja kutuambia tena hakina maji mpaka leo. Sasa kama kisima tumewekeza tumechimba hakijapatikana maji, nini solution ya muda mrefu sasa? Sasa tunapataje maji maana tunahitaji haya maji. Kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri hebu jaribu kuangalia katika maeneo haya utusaidie hii miradi ya maji iweze kutatua matatizo yaliyoko katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Isango tunakushukuru sana mmeleta mradi wa kuchimba kisima ambacho kitasaidia sana kupunguza upatikanaji wa maji pale Kata ya Sanga lakini utakuja mpaka hapa Itengezya, nakushukuru kwa kazi hiyo inaendelea vizuri lakini tunaomba sasa itekelezwe mtuunganishe katika mradi mkubwa ili kusudi tatizo la maji la Wilaya ya Mbozi, Mji wa Vwawa, Jimbo la Vwawa mpaka hadi Mlowo liwe ni historia, utakuwa umeacha legacy kubwa nasi tutasema alikuwepo Waziri mdogo anaitwa Aweso akisaidiwa na Maryprisca walifanya kazi nzuri sana. Nakuomba Mheshimiwa Waziri tusaidie na sisi naamini tutakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia Mheshimiwa Waziri, maji ni uhai, maji ni usalama wa nchi, maji ni chakula, maji ni nishati. Tunahitaji uje na master plan ya matumizi ya maji. Uje na gridi, ikiunganisha nchi hii tuione miaka mitano, miaka 10, miaka 20, miaka 50 ijayo naamini utakuwa umefanya kazi nzuri na Mungu akubariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)