Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon Ally Juma Makoa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu lakini pia nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna anavyowatendea wananchi wa Jimbo la Kondoa, especially kwenye hii sekta ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Kaka yangu Mheshimiwa Aweso Waziri wa Maji, Naibu Waziri, nawashukuru wizara kwa ujumla Katibu Mkuu na watendaji kwa sababu wote hawa ni watu wema sana na ni msaada mkubwa sana katika muda ule ambao tunahitaji huduma kwa ajili ya wananchi wetu. Mungu awabariki awape nguvu waendelee kuchapa kazi na waendelee kuiheshimisha nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru Serikali kwanza kwa kukubali maombi yetu wana kondoa mjini kuweza kutenga fedha kwa ajili ya miradi yetu ambayo inaendelea. Mradi wa Hachwi, Murua na Mradi wa Bicha pamoja na Mradi mkubwa wa Kondoa Mjini. Pia naishukuru Serikali kwa kuweza kutukamilishia uchimbaji wa visima nane kwenye mitaa nane ambayo kwa kweli natoa pongezi nyingi sana kwa miradi hii na kwa kweli imekamilika, ispokuwa kisima kimoja na ambapo si tatizo la wizara ni tatizo la kule kwetu nadhani tutalifanya vizuri, mkandarasi alipata changamoto kidogo Kisima cha Itiso. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niishukuru Serikali yangu kwa kukubali maombi yetu wana kondoa Mjini, kupanua mradi wetu wa maji Kondoa Mjini kwa ajili ya Mitaa yetu ya Kwapakacha, Mtaa wa Bicha, Tura pamoja na Mitaa ya kichangani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru sana Serikali kwa kukubali kutenga fedha kwa ajili ya kutuchimibia visima kwenye maeneo matatu, mitaa ambayo kwa kweli ilikuwa haina mradi wa maji ambao ni Mtaa wa Chang’ombe ambao uko Kondoa Mjini maarufu Serengenyi, lakini Mulua pamoja na Mtaa wa Damai. Ninaishukuru na kuipongeza Serikali kwa kutukubalia maombi yetu sasa wametenga fedha kwa ajili ya kwenda kutoa huduma hiyo kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani ni nyingi kwa sababu miradi ni mikubwa sana. Hapa sasa baada ya kuipongeza Serikali ninaushauri wa mambo kama matatu ambayo kwa kweli yakifanyiwa kazi haya yataleta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri namba moja; tumekuwa tukichimba hivi visima kama alivyotangulia kusema mwenzangu halafu vinachukua muda mrefu sana. Kwa sababu tunachimba kisima mwaka huu, mwaka ujao tunafanya designing lakini mwaka mwingine pengine ndio tunaweza kuanza kuwasambazia wanachi. tumechimba vizima vinane ambavyo kwa kweli wananchi wamepata matumaini kubwa sana lakini mpaka leo hatujaanza kuvisambazia. Visima hivi vipo Chora, Ausia, kwamtwara, Tamkori, Chemchem, Hurumbi, Dumi pamoja na Seria, Munguli na Msoi. Nimeona hapa kuna baadhi ya visima ambavyo tayari vimetengewa fedha kwa ajili ya usambazaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa nashauri hapa Serikali, kwa sababu wananchi wana kiu ya maji na wananchi wanapata shida na wanakwenda mbali, Serikali inapopanga kwenda kuchimba visima basi japo wakati tunasubiria kufanya usambazaji mkubwa ule wa fedha, fedha nyingi kwa ajili ya usambazaji, basi watuwekee japo sehemu moja kwa ajili ya wanachi kuchota maji wakati tukisubiria kuja kusambaziwa, lakini na sehemu moja kwa ajili wananchi kuweza kunywesha mifugo yao. Itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuwe na miradi ambayo tunafanya designing and building kwa wakati mmoja japo tuwe na eneo dogo la wananchi kupata maji. Natolea mfano, kuna huu Mtaa wa Chora, huu wanapakana na hifadhi, wanapokosa maji hasa kipindi cha kiangazi inawalazimu kuingiza ng’ombe kwenye hifadhi. Sasa tunaleta mgogoro kati ya wananchi na hifadhi na wananchi wetu wanaonewa kwa kupigwa faini kubwa hali ya kuwa wanatafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hawa watu wa Hurumbi, wanapakana na Pori hili la Swagaswaga. Kipindi cha kiangazi wanapata sana shida ya maji matokeo yake wanaingiza ng’ombe kwenye hifadhi. Hata hivyo, ni hekima za watu wa pale Swagaswaga wanawaruhusu wakati mwingine kwenda kunywesha kwenye hifadhi lakini hii pia ni mgogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili kuwasaidia watu hawa inabidi basi kisima tumechima basi watolewe maji japo wapewe DP moja pamoja na eneo la kunywesha mifugo litakuwa linawasaisia, huo ni ushauri wa kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa pili; tuna mfuko wa maji ambao unafanya vizuri. Nikushukuru Mheshimiwa Waziri, juzi wakati tunafuatilia fedha kwa ajili ya mkandarasi wetu wa Kondoa Mjini, tulizungumza mambo mengi na tulikubaliana na nimeona matumaini ndani ya wiki hii. Mungu awabariki sana, maana yake mkandarasio wetu atapata fedha zake na ataendelea na mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuna mfuko huu wa maji, ambao kwa kweli kwa nini mfuko huu usingekuwa unapeleka fedha kwa wasimamizi wa huduma moja kwa moja kama wanavyofanya watu wa barabara? Ili kuepuka kuchelewa kuwalipa wakandarasi ambapo sasa hivi mpaka wa-arise certificate itembee kwenye ofisi nyingi inachukua muda mrefu wakandarasi wasio na uwezo wanashindwa kumalizia miradi. Tukifanya kama wanavyofanya watu wa barabara, fedha hizi za mfuko wa maji zikaenda kwa wale wasimamizi wa huduma mikoani au wilayani inaweza ikasababisha wakandarasi wakawa wanalipwa kwa wakati na miradi ikakamilika kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu; ambalo nataka nitoe ushauri kwa Serikali. Kuna changamoto kwenye vile vyombo vya watumiaji wa huduma za maji wanaita CBWCO. Unakuta vyombo hivi vinatumia gharama kubwa kuliko makusanyo ambayo yanafanywa na watumiaji wa maji vijijini. Kwa sababu wachangiaji wa vijiji vingi sio wengi sana kitendo ambacho kinafanya mapato yanakuwa madogo matumizi yanakuwa makubwa, tunawalipa mafundi na wanalipa pia wahasibu. Kwa nini Serikali isingeajiri watu hawa ili kupunguza burden (mzigo) kwa wananchi ambapo kweli maeneo mengi ambayo wanatumia hiki chombo cha maji wanalipwa, wamekuwa wakishindwa kuendesha miradi kwa sababu makusanyo ni kidogo matumizi ni makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ninaombi ambalo Mheshimiwa Waziri, unapaswa ulichukue na ulifanyie kazi. Tunafanya Mradi mkubwa pale Kondoa Mjini na tumeuongezea ukubwa wa takribani bilioni Nne. Kwa sababu Mkandarasi wetu yule ambae tunashukuru mlitupatia mkandarasi mzuri pamoja na changamoto lakini mpaka sasa ameweza kufikia zaidi ya asilimia 72. Sasa kwa sbabu ukame na hali mbaya ya maji ilikuwa kwenye Jimbo la kondoa Mjini… ilifikia Waziri Mkuu alikuja…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ally Makoa, ahsante sana.

MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa tu na ombi dogo kwamba Mradi huu ukikamilika basi Mheshimiwa Aweso, amlete Waziri Mkuu, auzindue ule Mradi kwa sababu wananchi walipata shida na sasa wana neema kubwa. Ni hilo tu na baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)