Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri wa Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ya pekee ambavyo anaisimamia Serikali, kwa namna ambavyo Bunge linapitisha bajeti na yeye anaendelea kuleta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Waziri wa Maji na Naibu wake. Sina shaka na vijana hawa kwa sababu ya kazi wanazozifanya ni kielelezo kwa Umma; kwa kweli mnafanya kazi nzuri. Nimpongeze Katibu na Naibu Katibu wake kwa namna ya pekee ambavyo kwa kweli tunashirikana nao vizuri, unapohitaji ufafanuzi mara moja wanakusikiliza. Nimpongeze sana Mkurugenzi wa RUWASA, Engineer Clement Kivegalo, kwa kweli huyu amekuwa ni mtu wa mfano, wakati wote ukimpigia simu Engineer Clement anakupokea, wakati wowote ukitaka kwenda ofisini anakuruhusu kwenda. Kwa kweli nakupongeza sana kwa kazi nzuri unayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na Miji ya Kisesa, Bujora, Bukandwe pamoja na Bujashi. Kwa kweli hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais. Nikushukuru sana Waziri wa Maji, alipokuja Makamu wa Rais kwa kweli ulisimama kidete kusema kwamba sasa kazi zinaanza. Naomba nikutaarifu kwamba tenki ambalo ulisema linaanza mwezi huu wa tano bado halijaanza. Ninayo matumaini kwamba labda litaanza baadaye kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, hili nikuombe tu kama mradi huu hautakwenda haraka mwaka kesho kitaumana humu ndani ya Bunge. Lazima kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilika. Hili nasema kwa sababu nina uhakika kwamba wananchi wale wameteseka siku nyingi na idadi ya watu tayari ni 100,000 kwenye miji hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nikuombe, nimeona miradi hii kwenye Kata ya Lutale, huu mradi umesanifiwa na unaweza kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 19. Huu mradi ukikamilika unakwenda kutatua changamoto ya vijiji vinane katika kata tatu. Kwa hiyo, niombe sana kwa kweli kama ambavyo umesanifiwa uweze kutekelezwa ili yasiwepo mabadiliko ya usanifu kwa sababu tunapochelewesha miradi hii baadaye kunakuwa na mabadiliko ya usanifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa Lugeye, Kigangama ambao umeanza kutekelezwa, kwa kweli huu unakwenda kutatua changamoto kubwa ya Kata za Kitongosima, Nyanguge, Mwamanga pamoja na sehemu ya Kata ya Kahangala. Kwa hiyo niombe sana mkandarasi ameanza, asimamiwe vizuri ili aweze kukamilisha miradi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, tunao mradi ambao umekamilika Magu Mjini, lakini hamjaufungua. Nikuombe umlete Rais ili aweze kuufungua huu mradi. Umekamilika vizuri, una mapungufu machache. Mwaka jana mamlaka ya maji iliomba shilingi bilioni moja mkapitisha hapa Bungeni na ipo kwenye bajeti. Tunaomba sasa hiyo shilingi bilioni moja ipelekwe Magu ili vifaa na namna ya kutekeleza vifaa ambayo imebaki iweze kutekelezwa. Kwa sababu akija Mheshimiwa Rais kufungua siyo vizuri wananchi ambao hawajapata maji wakasimama na mabango. Niombe sana jambo hili liweze kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Waziri, tunayo Tarafa ya Ndagalu yenye Kata tano, vijiji 18 ambayo ina ukame kila mwaka wananchi wanapata shida. Mto Simiyu unapokamilika wananchi wanapata shida kubwa sana ya kuchota maji. Niombe mwaka huu sasa, Engineer Clement kwa sababu nakuamini, bahati nzuri Mkurugenzi huyu Engineer Clement, hataki miradi midogomidogo, ukienda kwake anakushauri mradi mkubwa ambao unaweza kutatua changamoto ya wananchi wengi, sasa Tarafa hii ya Ndagalu yenye vijiji 18 nikuombe sana Waziri umruhusu Mkurugenzi ili aweze kufanya usanifu na vijiji hivi viweze kupata maji ndipo tutakapo kuwa tumewasaidia wananchi watanzania, ndipo tutakapokuwa tumepunguza magonjwa kwa wananchi wetu lakini pia tutampa heshima Mheshimiwa Rais kwa sababu kazi kubwa anayofanya ni kuhakikisha kwamba na wakina mama anawatua ndoo kichwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna miradi inayoendelea katika Kata ya Mwamabanza, Kata ya Sukuma na Kata ya Uhumbi, miradi hii imebakiza fedha kidogo sana na kwa kweli miradi hii ikikamilika, Tarafa yote ya Itumbili itakuwa na maji ya bomba kwenye kila Kijiji. Kwa hiyo, naomba fedha ambazo zimebaki Wizarani, na wakandarasi wapo asilimia 80, ziweze kuja ili waweze kuikamilisha miradi hii, ikiwezekana kabla ya kuanza mwaka mpya wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja hii. Kwa kweli nawapongeza sana Wizara hii. (Makofi)