Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Esther Lukago Midimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Rais kwa dhamira yake ya dhati ya kumtua mama ndoo kichwani. Pili, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu; Waheshimiwa Wabunge ni ukweli usiopingika Waziri Mkuu anazunguka nchi nzima kukagua miradi ya maendeleo. Nampongeza sana Mungu ambariki. Tatu, nampongeza Waziri Mheshimiwa Aweso pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanazozifanya. Wizara ya Maji wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali yangu kwa kutuletea miradi mingi midogo midogo ya maji, nashukuru sana. Wilaya ya Maswa kuna Mradi wa Chujio, Kata ya Zanzui umegharimu bilioni tatu. Naishukuru sana Serikali, lakini pia naishukuru Serikali kwa kutuletea tenki la maji Maswa Mjini. Watu wa Maswa Mjini wanakunywa maji mazuri, safi na salama sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Maswa, kuna Vijiji vya Mwamashindike, Budekwa, Mwabalaturu na Busilili, kuna changamoto sana ya maji. Naiomba Serikali ituchimbie visima. Nasema hivyo kwa sababu gani, juzi tu Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mkoa wa Simiyu amezindua gari la kuchimba visima, hicho ni kishindo cha Mama Samia Suluhu. Naomba hilo gari liweze kutuchimbia visima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Busega naipongeza Serikali, Kata ya Mukura kuna mradi mkubwa wa bilioni 2.7, naipongeza sana. Kata ya Kabita kuna mradi unaendelea kujengwa na Serikali, tumeanzia bilioni sita naipongeza sana Serikali. Ombi langu kwa Busega, naomba Kata ya Shigala na Igalukilo kuna shida kubwa sana ya maji, naomba Serikali iweze kutuchimbia visima virefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naenda Kata ya Bariadi. Naipongeza sana Serikali kwa Mradi mkubwa wa Maji wa Ngulyati, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameuzindua juzi, umegharimu bilioni 1.3, naipongeza sana Serikali kwa hilo. Watu wa Kata ya Ngulyati wanaishukuru sana Serikali, wamenituma, sasa hivi hawana shida ya maji tena, wenyewe sasa hivi wanatafuta pesa tu hawana shida na maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi kwa Bariadi, naomba kuna changamoto kubwa Kata ya Sapiwi, Kata ya Sakwe, Kata ya Lukindwabiye, Kata ya Mwasuguya na Kata ya Likungulyabashashi. Tunaomba waweze kuchimbiwa visima kwa sababu, muda mwingi wanaupoteza kutafuta maji kuliko kufanya kazi za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Itilima, naipongeza sana Serikali kwa Mradi wa Gangabiriri, ni mradi mkubwa na ni mradi mzuri, lakini Wilaya ya Itilima, Gangabiriri ni Makao Makuu, Wilaya inaendelea kupanuka, naiomba Serikali ituongezee tenki, lakini vilevile naomba Serikali ichimbe kisima kirefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali iweze kufanya ukarabati katika mabwawa; la kwanza, Noghbora, Mwamapalala, Sawida, Habia na Nkoma. Nikija Wilaya ya Meatu, kuna Bwawa la Mwanjoro limepasuka na halijaanza kufanya kazi, naiomba Serikali iweze kukarabati. Bwawa hilo likikamilika litahudumia vijiji vitano. Mheshimiwa Aweso ananisikia, Meatu kuna ukame mkubwa sana, naomba ajitahidi ikiwezekana Meatu kila tarafa wachimbe bwawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuipongeza Serikali yangu kwa mradi mkubwa wa maji. Mheshimiwa Waziri ametupa matumaini na namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kwa kutoa zaidi ya bilioni 444 kwa ajili ya Mradi wa Ziwa Victoria, ahsante sana mama kuwajali wanawake. Wanawake wa Mkoa wa Simiyu muda mwingi walikuwa wanaupoteza kutafuta maji kuliko kufanya kazi za maendeleo. Mama suluhisho la ukame Mkoa wa Simiyu ni Mradi wa Ziwa Viktoria, hongera sana mama yangu. Hicho ndio kishindo cha Mama Samia Suluhu, nani kama mama? (Makofi)

WABUNGE FULANI: Hakuna.

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sasa Mheshimiwa Waziri, akija hapa kutoa majibu, aniambie mradi huo unaanza lini? Kwa sababu, maeneo ambayo mradi unapita tayari fidia zimeshalipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wananchi wa Mkoa wa Simiyu sio wavivu, ni wakulima wazuri na ni wachapakazi. Maji yale yakifika tutalima kilimo cha umwagiliaji, tutalima mbogamboga, tutalima michicha, tutalima kabichi, tutalima bilinganya, tutalima nyanya, tutalima vitunguu. Tutalima mazao ya chakula na tutalima mazao ya biashara, lakini vilevile tutasaidia na mikoa ya jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Serikali sasa hivi ni kuwa na uwanja wa ndege kila Mkoa. Nina imani na Simiyu utajengwa na eneo tayari tumeshatenga, tutauza mbogamboga zetu na nje ya nchi. Tutauza mbogamboga zetu Dar-es-Salaam, Mbeya na kila sehemu watakula mboga za kutoka Simiyu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)