Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Silvestry Fransis Koka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. SILYVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa nafasi uliyonipangia ya kuchangia. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta zote za kuwahudumia wananchi wa Tanzania. Pamoja na kazi nzuri sana inayofanywa na Serikali katika usambazaji wa maji, bado tuna matatizo madogo madogo ambayo hakika wananchi wangu na hususan wa Kibaha Mjini wanakumbana nayo ambapo inawaondolea nafasi ya kufurahia matunda haya ya usambazaji wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Kibaha Mjini, Kata ya Pangani na hususan Mtaa wa Pangani, lakini vilevile Mtaa wa Lumumba, Mtakuja na Miwale wao hawajafaidika na usambazaji wa maji, licha ya bomba kubwa la maji kupita, ambapo linapopita ni chini ya kilometa tatu hadi nne kufikia maeneo hayo. Jambo hili tumelijadili sana na Wizara na kuna mpango wa ujenzi wa tenki la lita 6,000 ambalo litaondoa tatizo katika ule Mtaa wa Pangani na hii mingine kiasi kwamba, hata machinjio yetu ya kisasa yatapata maji. Huu ni mwaka wa tatu kwenda wa nne, kila mwaka mkandarasi anakuja, kila mwaka tenda inatangazwa, jambo hili bado halijafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ni rafiki yangu na ni mchapa kazi, lakini wananchi wa Pangani wanasema bado zile cheche zake za kuchapa kazi hawajaziona. Nimwombe sana, ili tunapofunga bajeti hii tusigombane kwa kushika mshahara wake, basi namwomba atoe majibu sahihi ni lini tenki hili linajengwa, ili wananchi hawa waondokane na adha hiyo kubwa ambayo wamekuwa nayo kwa takribani miaka mitatu minne sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na Kata ya Pangani, lakini tuna maeneo mengine ambayo nayo yana changamoto ya maji ukizingatia Kibaha Mji ni Makao Makuu ya Mkoa wa Pwani. Kata ya Viziwaziwa kuna uchakavu na kuna msukumo mdogo wa maji. Kwa hiyo, maeneo ya Mitasa, Gare, Viziwaziwa na Mikongeni hawapati maji kwa sababu ya msukumo mdogo, lakini vilevile Kata ya Msangani usambazaji wa maji na hususan, Mitaa ya Kumba, Miembeni na Garagaza nako kuna tatizo kubwa wananchi hawajafikiwa na maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Maili Moja usukumaji wa maji ni mdogo kwa hiyo, wananchi hawapati maji ya kutosha, lakini Visiga, tuna Mitaa ya Saheni, Yerusalemu, Gaza pamoja na Bwawa la Chumvi na kwenyewe bado hawajapata maji licha ya kwamba, hizi ni kata zilizoko katika mji ambao ni Makao Makuu ya Mkoa wa Pwani. Ombi langu kwa Serikali na kwa Mheshimiwa Waziri, ahakikishe kwamba, pamoja na kazi nzuri ambayo imeshafanyika ya kupeleka mabomba makubwa na kwamba, bomba kubwa linalokwenda Dar-es-Salaam vilevile linapita maeneo haya, sasa basi mgawanyo wa maji haya kwenda katika maeneo haya na msukumo wa maji uzingatiwe, ili wananchi wafurahie matunda ya Mradi mkubwa wa Ruvu Juu na Ruvu Chini kwa ajili ya wananchi wa Pwani na Dar-es- Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kuhusu mita za maji. Wananchi wengi wanapata adha kubwa kwa sababu ya kupata bili ambazo sio sahihi. Hili limekuwa ni tatizo kubwa kwa muda mrefu katika maeneo mbalimbali. Napenda niishauri Wizara kwamba, kama itachukua hatua zifuatazo nina imani tutaondokana na tatizo hili na hatimaye bili za maji zitakuwa sahihi, hatutakuwa na malalamiko na wananchi watakuwa wanalipa bila kuwa na foleni kubwa ya malalamiko na marekebisho ya bili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tujikite katika teknolojia, kwamba, twende kwenye mita ambazo ni za LUKU. Vilevile ununuzi wa mita na wenyewe una changamoto. Kwa hiyo, ningeishauri Wizara ifanye consolidation kama ni mita ambazo tutakubaliana kwamba, ni kweli zinafaa na ni sahihi, basi zinunuliwe kwa pamoja ili kila mamlaka iweze kupata mita zile na kila mahali katika nchi yetu ambako wanasambaza maji kusiwe na mita ambazo ziko tofauti, hizi zinasoma vizuri, zile zinasoma vibaya, angalau tuwe na mita ambazo zinakubalika na zitakuwa zinatoa usahihi wa ujazo wa maji ambayo yanakwenda kwa wateja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo, kwanza tutaondoa tatizo la upotevu wa maji, lakini pili tutaondoa tatizo la malalamiko na kuwaonea wananchi kwa kuwapelekea bili ambazo hakika hawajatumia maji kiasi kikubwa hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, itafanya hizi mamlaka zetu za maji ziweze kupata fedha bila kutumia gharama kubwa ya kusambaza maji kwamba, kuna watu wanapita kwenda kusoma mita na kutoa makadirio saa nyingine kwa utashi wa mtu kulingana na alivyoona. Kwa hiyo, ningeomba sana hili litiliwe mkazo ili sasa na upande wa maji na yenyewe yasambazwe katika utaratibu wa teknolojia kama tunavyofanya kwenye umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ya kwangu yalikuwa ni hayo machache na naomba nichukue nafasi hii kuunga mkono hoja. Tuko bega kwa bega na Wizara kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata maji. Ahsante. (Makofi)