Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Robert Chacha Maboto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kupata nafasi hii ili niweze kuchangia Wizara ya Maji, lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa hii kwa kunipa pumzi mchana huu wa leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo ameendelea kutusaidia katika Halmashauri ya Mji Bunda katika kuhakikisha kwamba, Mradi mkubwa wa Maji wa Nyabehu umekamilika, ambapo mpaka sasa Mradi wa Nyabehu umekamilika kwa asilimia 99, ulikuwa una thamani ya karibia shilingi bilioni 10 na sehemu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia wananchi ambao wananufaika na mradi huu ni zaidi ya wakati 178,000. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa sababu, wakati anaingia kwenye nafasi hii, mradi huu bado ulikuwa hautoi matokeo ambayo wananchi wa Bunda Mjini wanayategemea. Kwa sasa tumeshapata matumaini kwa sababu, mradi huu unatoa maji safi na salama kwa kiwango kikubwa. Sasa ombi letu kwa Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii ya Maji, ndugu yangu Mheshimiwa Aweso, ni kuhakikisha kwamba, atusaidie mambo madogo madogo yale yaliyobaki ya usambazaji maji kwenye maeneo yale ambayo bado maji hayajafika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuna Mradi wa Ujenzi wa Tanki la Maji Misisi-Zanzibar ambapo tenki hili litahakikisha kwamba, wananchi wote wa Kata ya Sazira na wengine wa Kata hii ya Kabasa watapata maji mara baada ya kuwa tenki hili limekamilika. Mpaka sasa tumepata zaidi ya shilingi milioni 733 ambazo naamini Mheshimiwa Waziri tumeshapokea kwako fedha milioini 583 kwa ajili ya utekelezaji wa tenki hili ambalo litabeba maji zaidi ya lita laki moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba, jambo hili likishakamilika maeneo hayo tutapunguza uhaba mkubwa wa maji na malalamiko kwa wananchi wetu ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiona mradi mkubwa wa maji kwao na maji yako karibu kilometa tatu, tano hivi kuingia Ziwa Victoria, halafu wakawa wanashangaa maji hawayaoni, lakini sasa wananchi wa Bunda Mjini wameanza kunufaika na mradi huu mkubwa ambao unatekelezwa pale Bunda. Mradi huu nakumbuka mwaka jana Mheshimiwa Rais alikuja kuuzindua na baada ya kuuzindua umeleta matokeo makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, ni ujenzi wa tenki la maji ambalo litasambaza Manyamanyama na Mugaja. Lenyewe hili lina thamani ya shilingi bilioni moja na milioni 65 ambazo sasa mchakato unaendelea. Ombi langu ni kwamba, Waziri aweze kutuwezesha sisi ili tuweze kupata fedha hizo Halmashauri ya Mji wa Bunda, ili mradi huu uweze kutekelezwa na wananchi wetu waendelee kunufaika na maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni ujenzi wa tenki la maji ambalo litasambaza maji Kata ya Balili, Rubana na Kunzugu. Maeneo haya tukishawatengenezea tenki la maji, mradi ambao utakuwa unagharimu karibu zaidi ya milioni 759, naamini Mheshimiwa Waziri anafuatilia jambo hili vizuri, tunamwomba tuendelee kupata fedha ili tenki likamilike na wananchi wetu wale wapate maji vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa jiografia ya Mji wa Bunda ilivyo na jinsi ambavyo tuko karibu na ziwa, lilikuwa ni jambo la kushangaza kwamba, sisi ndio tulikuwa tunakuwa walalamikaji wa kwanza kukosa maji, lakini sasa namhakikishia kwamba, atakapokuja Bunda kwa mara nyingine ataona furaha iliyopo kwa wananchi wake kutokana na kwamba, wamepata huduma nzuri ya maji wanapata maji safi na maji salama kwa wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, muhimu ni kuhakikisha kwamba, jambo hili…

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumpa mzungumzaji Taarifa kwamba, anapozungumza Bunda azungumzie Jimbo la Bunda Mjini. Jimbo la Bunda la kwangu bado lina ukame mkubwa sana wa maji. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Robert, Taarifa hiyo.

MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naamini Mheshimiwa Getere anafahamu jimbo lake na mimi nafahamu jimbo langu. Mimi Jimbo langu ni la Bunda Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la upotevu wa maji na jambo hili nimeona tatizo kubwa liko kwenye ile mipira ya kuvutia maji. Hawa ndugu zetu wenye viwanda vya kusambaza mipira hii naamini mipira hii haiko katika viwango vile ambavyo vinatakiwa. Yale mabomba yale ya maji wananchi wanayanunua, wakiyatumia kwa muda mfupi, ndani ya miezi mitatu mabomba yalishapasuka ambayo yanawaingiza wananchi kwenye gharama nyingine tena ya kununua mabomba mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naamini jambo hili na kwa sababu, wale ni wadau wa maji ni vizuri Waziri akawawekea mkazo kwenye mabomba haya ya maji. Yawe mabomba ambayo yanalingana na thamani halisi ya fedha ambazo wananchi wetu wanazitoa. Kwa sasa jambo ambalo litakuja kujitokeza pale kubwa ambalo ni baya ni hilo la mabomba ya maji kupasukapasuka kwa sababu, tumekuwa tukipata malalamiko mengi sana kwa wananchi wetu kwamba, mabomba wanayoyatumia kwa muda mfupi yanakuwa yalishapasuka, halafu wanaingia tena gharama za kununua mabomba yale kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, nimwombe Mheshimiwa Waziri, tuna mradi pale wa kutibu majitaka na maji safi, pale Bunda, lakini tulishapata eneo pale karibu eka 100, kule Butakare, kilichobakia tu ni kupata fedha za fidia ili kwamba, eneo lile na kutokana na mwingiliano wa wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini, ni vizuri tukapata fedha hizi za kulipa fidia maeneo haya, ili mradi ule uweze kutekelezeka ili uweze kuleta manufaa makubwa katika Mji wa Bunda. Kwa sababu jiografia ya Mji wa Bunda ndio picha halisi ya Mkoa wa Mara kwa mtu yeyote anayekwenda Mkoa wa Mara, picha nzuri ya Mkoa wa Mara anaianzia kwa kuona Bunda. Kwa hiyo, akikuta jiografia ya Bunda imekaa vizuri hasa kwenye miundombinu ya maji anajua hata huko anakokwenda lazima atakuta hali halisi ni nzuri zaidi. Kwa hiyo, ombi langu ni kuhakikisha kwamba, jambo hili linafanyika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia jambo lingine nimwombe Mheshimiwa Waziri kwamba, yule Mkurugenzi wetu wa BUWASA aliyeko pale Bunda…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)