Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwanza nianze kwa kutangaza maslahi kwenye Wizara hii siyo maslahi yale ya kikanuni maslahi ya kifedha ni ukweli kwamba nilipata bahati ya kutumikia Wizara hii kama Katibu Mkuu kwa miaka mitatu na nusu na kwa nafasi hiyo nilifanya kazi kwa karibu sana na Mheshimiwa Jumaa Aweso. Kwanza aitwi Juma anaitwa Jumaa Hamidu Aweso nilimpokea pale nataka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nithibitishe kwamba Waziri huyu ni mtu makini, ni mzalendo sana, ni mchapakazi, ni mnyenyekevu lakini muhimu sifa za ziada ambazo siyo lazima uziseme na kazi yake ni mcheshi, ni mchangamfu sana na watu waliyofanya kazi Wizara ya Maji wanafahamu kwamba anafahamu kiswahili vizuri ndiyo maana katika hotuba yake zimejaa methali za kiswahili jambo jema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Mamlaka ya Maji Jijini Dar es salaam DAWASA kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya Mkoa wa Dar es salaam, hususani Jimboni kwangu mimi nina kata 8, mitaa 46 zile 86 ambazo amezisema sisi tulishazivuka siku nyingi. Kwa hiyo, tuna bahati, tunashukuru kwa hilo. Lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri alikuja mtaa ulikuwa umebaki Mtaa wa Golani tulikwenda nae mpaka kule mlimani sana, wale wananchi wamenituma asubuhi hii nikushukuru sana wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Engineer Edison Meneja wetu wa Ubungo na Engineer Julieth John Meneja wa Magomeni wanafanya kazi kubwa. Nichukue nafasi hii pia kumponeza mdogo wangu Cyprian Luhemeja kwa uteuzi ambao ameupata, amefanya kazi kubwa Dar es Salaam tunarajia kwamba atasaidia katika nchi na tumtakie Engineer Kiula na wengine wote waendelee kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka niombe Engineer Julieth tumeisha ongea, Engineer Lidya ile tumetengeneza mradi mzuri wa maji taka, Mtaa wa Manzese, National Housing na Sinza na sehemu zingine lakini mitaa ni critical kwa sababu ina shida kubwa sana ya maji taka tumeisha zungumza hili niwaombee mlitekeleze vizuri ili wananchi wetu waweze kukaa vizuri pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya maji hakuna shaka, katika miaka ya hivi karibuni imepata mafanikio makubwa ambayo Mheshimiwa Waziri ameyaeleza. Nataka nitumie dakika ambazo zimebaki kueleza mafunzo ambayo tunayapata yanayotokana na mafanikio katika sekta ya maji na wale ambao wapo humu ndani muda mrefu wanafahamu ni nikiwa Katibu Mkuu tukija hapa Mwaka 2017 palikuwa hapakaliki. Tukikaa pale mlikuwa mnatupiga nyundo za kutisha, ukitoka hapo unamuomba waziri likizo ya wiki nzima baada ya bajeti kupita lakini hii kazi ilikuwa ni kubwa lakini baada ya muda mfupi kazi kubwa imefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mafunzo matano kama muda ukiruhusu moja; ni umuhimu wa kuwa na taasisi imara katika usimamizi wa shughuli za Serikali. Sekta ya maji inasimamiwa na taasisi kubwa tatu tunayo mabonde ya maji, mamlaka za maji ambazo zipo kwenye mijini na miji midogo na tuna RUWASA hii ambayo mmeipigia makofi mengi. Hizi ni Taasisi ambazo zinafanya kazi kubwa, kwa hiyo, nikusii Mheshimiwa Waziri uendelee kuzipa nguvu taasisi hizi kwa sababu kwakweli ndiyo miguu yako.

Mheshimiwa Naibu Spika, funzo la pili; ni umuhimu wa kuwa na mipango ya muda mrefu na kuishikilia. Sekta ya maji inaongozwa amesema Mheshimiwa Waziri na Program ya Maendeleo ya Sekta ya Maji water sector development program. Sekta hii imekuwepo kwa takribani miaka 20 na kila Waziri akija anakabidhiwa nyaraka hii na anatembea nayo, tofauti tu ni kasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekaa pale Mawaziri kadhaa alikuwepo Mheshimiwa Jumanne Maghembe, akaja Mzee wangu Kamwelwe akaja Profesa Mbarawa na wengine tofauti ni kwamba, wanatekeleza program hii hii hawabadilisha hata nukta. Tofauti kubwa ni kasi, kijana anakasi kubwa huyu, anakimbia zaidi, na kwa sababu yeye amevunja rekodi ya Jakaya Kikwete, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, amevunja rekodi, kwa sababu yeye ndiye mdogo kuliko wote sasa hivi katika Mawaziri wote wa Wizara ya Maji tangu Wizara hii iundwe. Alikuwa anashikilia rekodi Mheshimiwa Jakaya ameishapitwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, funzo la tatu; muhimu ni muhimu wa kuheshimu, kuwajali na kuwapenda watalamu wetu. Sekta ya maji ni moja ya sekta ambazo zina heshimu sana watalamu wake. Kwa hiyo, ni jambo muhimu tuwape nafasi, tuwaheshimu, kwa sababu ukweli ni kwamba mkono mmoja hauchinji ngo’mbe. Mheshimiwa Waziri, yuko hapa ana ng’ara lakini nyuma yake kuna vijana wakakamavu, waliyosoma vizuri, wanafanya kazi yeye anawapa nafasi. Hili ni jambo la msingi ambalo lazima aliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la nne; ni umuhimu wa uwekezaji. Sekta ya Maji inapata fedha kutoka mfuko wa maji jambo hili ni jambo zuri la kushukuru kwa kweli liendelee, kwa sababu hii ndiyo hasa nguzo ambayo inafanya miradi wa maji itekelezwa kwa ukubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tano; sekta ya maji na sekta za huduma zingine zinahitaji utulivu na tumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kuipa sekta hii maji utulivu mkubwa sana kwa kiwango ambacho watalam wanafanya kazi yao kwa kutulia, kwa kutumia utaalam wake, sekta hizi ni ngumu. Katika hilo tatizo la sekta ya maji ni kwamba inapambana ni kama kila mara goli linapanuka kwa sababu leo anazungumzia asilimia 86
lakini kesho inaweza ikashuka kwa sababu ya ukuaji wa idadi ya watu hiyo ndiyo changamoto kubwa. Kwa hiyo, ni muhimu sana tuendelee kuwekeza fedha katika sekta hiii ili tuendelee kushughulikia miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la miwisho nichukue nafasi hii kuiba muda wako kama Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Elimu, Utamaduni na Michezo moja kuwapongeza vijana wetu wa yanga kwa mechi yao ya leo. Kwa sababu wamefanya kazi kubwa, wapo nusu fainali na la pili kuwatakia kila kheri katika mechi yao ya leo, leo ni siku kubwa katika… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Zungumzia hoja iliyoko mbele yako. (Vicheko)

MHE. PROF. KITILA M. MKUMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo najua hilo utakuwa umelizingatia hata wewe mwenyewe tunawapongeza vijana wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)