Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na nikushukuru wewe na Bunge lako Tukufu kutoa fursa kwa Wabunge wengi kuchangia na pale ilipohitaji hata ratiba ilibadilishwa ili Wabunge waweze kuchangia hoja hii ambayo ni kwa maslahi ya Watanzania wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wamechangia Wabunge 88 kwa ujumla. Kwanza nitumie nafasi hii kuwashukuru Wabunge na niwaambie mwaka jana tulivyo-submit bajeti yetu hapa mawazo na ushauri wenu ni sehemu ya kuandaa mpango wetu wa mwaka ujao kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu sisi hatuishi in isolation, kwenye Kijiji tunaishi na watu na tunathamini sana michango yenu. Nataka niwaambie tu kwamba maoni na ushauri na critics zote mnazozitoa kwetu sisi ni sehemu ya lesson na niwahakikishie tunazichukua tunaenda kuzifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zipo hoja zilizotolewa na Wabunge nyingi, inawezekana nisizijibu zote. Hoja ya kwanza ambayo nilitaka niseme ni je, tuna uhitaji ushirika? Jibu ni ndiyo. Je, tunahitaji ushirika wa namna gani? Tunahitaji ushirika unaoenda kumsaidia mkulima na wala siyo ushirika utakaomnyonya mkulima. Je, ushirika tulionao ni mtakatifu? Jibu ni kwamba ushirika tulionao una changamoto na ndiyo maana kuna Waziri wa Kilimo, kuna Tume ya Ushirika tuna wajibu wa kwenda kusimamia changamoto hizo. Je, upo ushirika unaowatendea haki wakulima kwenye nchi hii? Jibu ni ndiyo upo. Upo ushirika unaowaibia wakulima? Jibu ni ndiyo upo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hatuwezi kwenda kuua mfumo wa ushirika katika nchi kwa sababu tu tunao washirika ambao siyo waaminifu. Tutachukua hatua na nimhakikishie Ndugu yangu Mbunge wa Mbozi na Wabunge wa Kahawa wa arabica, ilituchukua miaka miwili kujadiliana na kuelewana na wenzetu wa robusta, leo changamoto zilizoko kwenye robusta zimepungua, ushirika una compete na sekta binafsi, wanashindana sokoni, tunawapa mitaji, wanaingia kununua na mkulima analipwa fedha yake on time. Tutakuja kwenu Mbozi na nimwambie Mwenisongole kwa macho yangu nimeona viongozi wa ushirika wa Mbozi walivyowaibia wakulima wa kahawa na mimi nilimkamata, nikamuweka ndani na timu ya Wizara ya Kilimo imeenda, imetuletea takataka zilizoko. Nikuhakikishie tunaenda kufanyia kazi, wakulima wa Songwe, Mbozi mpaka Mbinga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika yuko hapa, ni marufuku Chama cha Ushirika kwenda kukopa fedha kabla ya msimu na kusema tunalipa malipo ya awali, halafu mzigo wa riba na gharama za uendeshaji mnaenda kumbebesha mkulima. Hii tabia ife na tutaenda na watu wetu kwenda kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ushirika ni lazima tuuwezeshe. Tunafanya sasa hivi feasibility study ya TANICA. Tutaenda kuipa TANICA shilingi bilioni nane ili kui-capitalize iweze ku-compete na kuweza kufanya value addition, hili linawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni irrigation. Je, kuna matatizo kwenye Tume ya Umwagiliaji? Mwenyekiti wa PAC ametoka. Nataka nimwambie, taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imekuwa ni sehemu ambayo sisi ni kama instrument ya kufanyiakazi. Hatutaki kuwa hostage wa matatizo ya mwaka 2017 na 2018, ingekuwa hivyo leo hii kwenye hii nchi kwani TRC haikuanguka? ATCL haikuanguka? Si zilianguka? Hakukuwepo na ubadhirifu au mambo matatizo yaliyokuwepo? Ni jukumu letu sisi kufanyia, kuchukua hatua juu ya matatizo yaliyopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, irrigation kwenye nchi yetu as a country toka mwaka 2000 hatukuwahi kuweka emphasis kwenye mifumo ya umwagiliaji na usimamiaji wa umwagiliaji katika nchi hii. Ndiyo ukweli! Tulitenga shilingi bilioni 20 na mimi nilikuwa Mbunge nakaa pale alipokaa Mheshimiwa Tabasam. Fedha haziendi, tunataraji kwamba zaidi ya Halmashauri mia moja na kitu, tunatenga fedha za usimamizi za umwagiliaji shilingi milioni 20. Hakuwezi kutokea muujiza! Ndiyo maana kuna hayo matatizo tuliyoyaona. Aliyaona Mkaguzi wa Hesabu za Serikali.

Mheshimiwa Spika, tumechukua hatua gani? Hatua ya kwanza Tume ya Umwagiliaji sasa imeenda kuwa na ofisi kila Wilaya. Pili, Mheshimiwa Rais katupa kibali tumeajiri ma- engineer sasa hivi wana mwezi mmoja tumewapeleka katika Wilaya. Tatu, tumewanunulia vitendeakazi tumenunua gari 53 tunapeleka katika kila Wilaya. Nne, tumeongeza bajeti na sasa hivi hakuna mradi wa umwagiliaji unaofanyika bila feasibility study. Nchi yetu Mwenyezi Mungu kaijalia hekta milioni zaidi ya 29 kwa miaka 60 tume-invest only 2.7 per cent ni aibu! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mama Samia kafanya nini? Kasema wekeni emphasis kwenye irrigation. Kwanza hauwezi kuweka fedha za umwagiliaji bila kutambua maeneo ya umwagiliaji, Naibu Waziri amesema. Tuna maji Ziwa Victoria mita 300 wakulima wanasubiri mvua. Tumefanya nini? Tunafanya feasibility study kuanzia Mara mpaka Kagera. Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu hata asipojenga Samia, atakuja kujenga mtu kwa sababu leo tunajenga Stigler’s waliofikiri juu ya Stigler’s na kufanya feasibility study na detailed design leo hawapo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sisi plan zetu kama Wizara siyo za kesho, niwaambie Wabunge kama mnafikiri tunawekeza kwenye umwagiliaji kujenga mifereji ya mita mia mia siyo Wizara hii, siyo Waziri huyu. Tunafikiri kufanya miradi ya umwagiliaji ili tumwagilie kiangazi na masika. Tuna mradi wa 55 billion hapo kwa Mheshimiwa Lukuvi. Ule mradi tunaujenga kwa miaka miwili. Mradi ule tu barabara za mashamba ni kilometa 98. Mradi ule mifereji ni zaidi ya kilometa 100. Halafu mnataraji eti kuna hoja hapa kwamba imetengwa shilingi bilioni 300 fedha kwa nini hazijatoka zote? Labda tubadilishe utaratibu tuleteeni pale Wizarani zikae shilingi bilioni 300 na nyie ndiyo mna mamlaka badilisheni Sheria ya Manunuzi hapa, kila kitu iwe force account. Haina shida mimi nitaziweka ofisini, bwana eeh, chukua in advance. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utaratibu ni kwamba miradi yote tuliyoiahidi mwaka jana mpaka kufikia mwezi Aprili, asilimia 70 tumeshasaini na leo ninavyowaambia miradi ya mwisho tumeipandisha kwenye mfumo. Tunaenda Juni 30 hatutakuwa tunadaiwa mradi mmoja. Wakandarasi wote watakuwa site na miradi hii inajengwa kwa miezi 18 mpaka 24, mwaka kesho ndiyo ina kamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, phase two tumesema miradi yote katika haya mabwawa 100 kwa kuwa tunajenga irrigation scheme sasa phase two kwenye fedha za mwaka kesho tunaanza kujenga mabwawa ili tulime mwaka mzima. Huu ndiyo mwelekeo wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, hapa ameongea Dada yangu Mheshimiwa Halima kasema tunafanya kilimo cha iPad na mimi namheshimu. It is a very good statement, ni kweli! Tunataka siku moja nchi hii na dunia hii watu waingie google wajifunze kilimo kilichofanywa Tanzania. Mimi nashangaa watu wanashindwa kuota, this is the country na mimi nataka niwaambie, sisi ndiyo purity ya nchi, kama sisi tunawaza kimaskini we are in trouble. Niwaambie ukweli! Kama sisi tunawaza kimaskini tena tuna tatizo kubwa mno ambalo linatukabili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna hoja ya BBT. Kwanza naomba ni-clarify. BBT ina-compete na wakulima wadogo waliopo? Jibu ni hapana. BBT imesababisha wakulima wadogo tuwaweke pembeni? Jibu ni Hapana. BBT imesababisha wakulima wadogo wasihudumiwe? Ruzuku ya mbolea ina- target wakulima wadogo. Tunavyopeleka Maafisa Ugani, tuna-target wakulima wadogo.

Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti hii tumeweka fedha kwa ili kila Halmashauri tuchukue wakulima au mashamba 150, tutawachimbia kisima bure, tutawawekea pampu kwa kutumia solar technology, tutawawekea tank la kuanzia lita 5,000 na tutawawekea irrigation kit ya ekari 2.5. Huyu ni nani? Mkulima mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nataka niwaambie Wabunge wenzangu, ukiona Taifa lolote asilimia 70 ya population wako shambani, ni Taifa masikini. Ndiyo principle za economics. Haiwezekani the bigger population iko shambani ina-contribute asilimia 25 tu ya pato la Taifa. Ni sign of poverty. Kwa nini? Kwa sababu productivity ni ndogo.

Mheshimiwa Spika, tunachotakiwa sisi leo, kwa kuwa sisi tuko shambani, watoto wetu wasiende kulima hekta moja moja. Tujenge uwezo wa-graduate kutoka kwenye agriculture, waende kwenye service industry na maeneo mengine. Economy zote zilizokuwa duniani, watu wachache wako shambani, wengi wameondoka. Sasa kipato cha mkulima mdogo ni Shilingi ngapi? Haizidi 1.2 million Shillings kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa nini tumeenda kwenye program ya BBT? Kwanza nataka niwaambie Watanzania wenzangu, ni aibu kuhoji kwamba kwa nini tumemmilikisha kijana ardhi? Leo anakuja Mzungu kutoka Ulaya; juzi ofisini kwangu ilikuja kampuni moja kutoka China, inataka kuwekeza. Condition ya kwanza nimpe ekari 20,000; condition ya pili, nimpe subleasing title ya miaka 60; condition ya tatu, anataka barabara; condition ya nne, anataka umeme.

Mheshimiwa Spika, sasa nikimpa Mtanzania hekta 10, nimemwandalia shamba, nimemwekea irrigation scheme, nimempelekea umeme, nimempimia afya ya udongo, mnasema, kwa nini tumemilikisha? Wawekezaji wangapi katika nchi hii tumewamilikisha ardhi na hawaitumii? What is wrong kummilikisha mtoto wa Kitanzania ardhi? Nauliza hili swali, kuna dhambi gani? Mheshimiwa Halima usiingie kwenye historia ya kuhoji kijana wa Kitanzania ambaye kaenda kurithishwa ardhi…

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

WAZIRI WA KILIMO: Umechangia, give me space.

MHE. HALIMA J. MDEE: Usiniwekee maneno.

WAZIRI WA KILIMO: Nimesema hivi…

SPIKA: Ngoja, ngoja, Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Halima, naomba ukae. Waheshimiwa Wabunge, kwenye ngazi hii, Waziri akiwa amesimama anahitimisha hoja, huwa hakuna taarifa. Kinachoweza kutokea, ukiona kilichojibiwa ni tofauti na ulichokuwa umesema wewe, utatumia kanuni nyingine, lakini kanuni ya taarifa haiwezi kutumika katika ngazi hii.

Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, out of respect, hoja imekuwepo tunawatoa Dar es Salaam. Hivi nimuulize graduate yeyote aliyemo humu ndani, alipomaliza Chuo Kikuu, destination ya kwanza ilikuwa wapi? Nawaulizeni! Mimi nimemaliza Mzumbe, nimeenda Dar es Salaam, sikurudi kwetu kijijini, Nzega. Nimeenda Dar es Salaam, nazunguka na bahasha ya kaki, na kula wali wa shilingi 700 IFM. Leo tunahoji, eti kijana aliyeko Dar es Salaam hawezi kulima! Nani kasema kwamba kijana aliyekwenda Dar es Salaam hawezi kulima? Nani? Tumemjaribu wapi? Hawawezi kulima kwa sababu tunataka kuwa-subject walime kwa teknolojia za 1960, 1970, 1980, it is impossible. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini vijana hawalimi? Halafu tunasema sisi viongozi mbele ya Mungu, nami niko honest, I will push BBT, aidha nifanikiwe mimi na wenzangu, ama nikaanguke. Siwezi kusubiri, siwezi kuwa mmoja wa viongozi wanaowanyooshea vidole vijana wa nchi hii kwamba kwa nini hawataki kujiajiri? Tunao wajibu. Tuna moral responsibility ya kuwatengenezea vijana wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mazingira ya kujiajiri, na ndicho kinachofanywa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii nani anaweza kwenda kununua ardhi ya shilingi milioni mbili, milioni tatu hekta moja? Nani, kijana aliyetoka chuo kikuu? Nani anaweza kutumia Shilingi milioni mbili au milioni moja na nusu au milioni tatu kuweka drip irrigation? Yuko wapi huyo kijana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nimpe mfano, nami na- focus kwenye hoja ya Mheshimiwa Halima kwa sababu, let me say, nasema ukweli.

MBUNGE FULANI: Unachagua hoja!

WAZIRI WA KILIMO: Yes, nimechagua hoja.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, hebu tusikilizane. Unapozungumza Waziri akiwa amesimama hapa mbele, unataka aongelee hoja anazojibu au muanze kujibizana? Tafadhali naomba utulivu, Waziri anajibu hoja za Wabunge. Yeye wakati ninyi mnachangia aliwasikiliza, mpeni nafasi na yeye ya kumsikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nataka nitoe hii takwimu. asilimia 74 ya Watanzania walioko mashambani, wana wastani wa ekari mbili. Asilimia 25 tunaowaita medium size, wana ekari tano mpaka 20. Tunaowaita large scale, wana ekari 20 mpaka 100. Hii ndiyo taswira. Wote hawa wanavuna mara moja kwa mwaka, wanasubiri kudra ya Mungu. Lazima tuondokane na hii hali. Hii hali hatuwezi kuondokana nayo kwa msimu mmoja, au miwili, au mitatu, is a long-term process. Lazima tufanye hii kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine niongelee suala la ruzuku ya mbolea. Nakiri kulikuwepo na changamoto za distribution network. Tunachukua hatua. Hatua ya kwanza, tunawekeza kwenye TFC, kampuni yetu wa Serikali. Kwenye bajeti tumeipa shilingi bilioni 40, mwaka jana 2022 tuliipa shilingi bilioni sita, mwaka huu tumeiongezea shilingi bilioni 40, na sasa hivi tuko kwenye negotiation na funding kutoka JICA ambazo zilikuwa ziende ku-support hiyo ruzuku, tutawapa dola milioni 25, itakuwa capitalized.

Mheshimiwa Spika, kwa nini tunai-facilitate kampuni hii? Tunai-facilitate ili tuwe na jicho la Serikali ambalo linaweza kutusaidia kwenye price discovery huko nje. Wata-import mbolea kutoka huko nje na watanunua kutoka huko nje, lakini capacity ya ndani tunaendelea kuijenga.

Mheshimiwa Spika, leo tuna hiki kiwanda chetu cha INTRACOM ambacho kinaendelea kufanya kazi, tunatarajia mpaka mwezi wa Kumi kitafika tani milioni moja. Kwa kuwa program ya ugawaji wa ruzuku ya mbolea; na kwa nini tunafanya hivyo? Hapa nitaijibu hoja ya Mheshimiwa Mpina.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mpina kahoji kachukua idadi ya wakulima tuliowasajili, kagawa kwa mbolea tulizotoa; nadhani ni katika kuelewa. Kwanza wakulima milioni saba wa nchi hii sio wote wanaotumia mbolea. Matumizi ya mbolea katika nchi hii kwa hekta moja sasa hivi, wastani ni kilo 19. SADC minimum standard ni 50 kg.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa nini kuna tatizo la matumizi ya mbolea? Elimu, hilo la kwanza; la pili, taarifa ya afya ya udongo; la tatu, ni availability na affordability. Kwa hiyo, Serikali inaweka ruzuku ili bei iweze kushuka. Siyo sahihi katika hoja yake, nami nimeichukua hoja yake hapa, ninayo, kanipa yeye mwenyewe kwa maandishi. Kuna mambo kama manne kayataja. La kwanza, kasema mfumo wa usajili na mfumo wa ruzuku haukupata approval ya Serikali, umeenda kinyume na utaratibu. Nataka nimwambie, tumepata approval ya Katibu Mkuu Kiongozi, tunayo approval ya e-GA; tarehe 26 Juni, tulipata approval ya e-GA, na tarehe 16 Julai vilevile Katibu Mkuu Kiongozi aliwaandikia e-GA kuwasiliana na Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kutengeneza mfumo wa ruzuku ya mbolea. Barua hii hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni vizuri, nami nataka nimshauri, na ninajua ameenda hadi e-GA. Namwomba kwamba kwa mila zetu hasa sisi tunaotoka huko maeneo ya wafugaji, ni vibaya sana mtu ambaye umefika katika level ya uongozi, kuongea mbele ya Baraza ku-accuse mambo ambayo huna facts. Nataka nimwombe, next time akiwa na jambo linalohusu Wizara ya Kilimo, mlango wangu uko wazi sana. Saa yoyote njoo, tutakusikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yake ya pili ni kwamba, mfumo wetu ulikuwa haufai, kuna double scanning. Sasa tumegunduaje mfumo kwamba huyu mtu ka-double scan kama mfumo wetu hautoi taarifa? Mfumo wetu unatupatia taarifa, mtu yeyote atakaye-temper na system; na wizi uliokuwa unafanyika, na Bunge hili litumike, uko wa aina nyingi. Mkulima alikuwa akifika dukani, akichukiliwa namba yake ya kusajili na Agro-dealer, leo allocation yake ni mifuko kumi, akilipa mitatu, akiondoka, kwa kuwa Agro-dealer kabaki na ile namba, anaitumia tena ile namba, meseji inaenda kwa mkulima, mkulima anapiga call center ya Wizara ya Kilimo. Sisi tunafanya tracing.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi wanaendelea kuhojiwa. Kuna wengine wamefika, tumewakamata walikuwa wame- double scan mbolea za zaidi ya shilingi milioni 100, wanasema naomba nisamehewe, hiyo shilingi milioni 100 ifutwe, tuendelee. Nataka niwaambie, tulianza tukiwa hatuna mfumo wa kumtambua mkulima nchi hii. Tumeanza safari, sasa tumefika wakulima milioni tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie Bunge lako tukufu kuwaambia wakulima, tarehe 01 mwezi huu wa Tano, TFRA ilitangaza wakulima kwenda kujisajili na ku-update data zao. Nendeni mkajisajili, mwendelee kutoa taarifa zenu sahihi, mfumo utaendelea kuwa updated, na process ya kusajili wakulima ni ya mpaka mwaka 2025. Tutakamilisha kumjua mkulima jina, GPS ya shamba lake, afya ya udongo wa eneo lake, na kujua mazao anayolima, na kuwa na taarifa sahihi. Kwa muda mrefu tumehudumia wakulima tusiowatambua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, gharama za mradi wa BBT. Wastani wa shilingi milioni 16 kwa hekta. Kwanza, nilitaka niseme jambo moja. Hekta moja ni ekari 2.5, nasi hatuchukui mashamba yaliyoandaliwa, tunachukua mapori, ambapo tunaenda kusafisha. Kusafisha hekta moja ya pori, ni wastani wa 1.5 million shillings. Gharama hizi za shilingi milioni 16, zinahusisha kusafisha, kupima afya ya udongo, gharama ya kupima shamba, ni wastani wa shilingi milioni mbili. Huyo anayekuja, hawezi kuzilipa hizo gharama. Sisi ndiyo tunaolipa gharama za upimaji wa haya mashamba. Tuna-include gharama za kupanda, tuna-include gharama za kupima afya ya udongo, tuna-include gharama za teknolojia itakayotumika, whether ni sprinkler ama ni drip irrigation kama kwenye maeneo ya mabonde kama kule Membe, tunakotumia canal technology.

Mheshimiwa Spika, siku ya mwisho tunapomkabidhi huyu kijana gharama ya hekta moja ambayo ni ekari mbili na nusu, ni karibu Shilingi 16,700,000. Ukigawa, haizidi Shilingi milioni saba kwa ekari. Ni muujiza gani? Mheshimiwa Halima analima pale panaitwa Ihanga, ndiyo mfano wangu leo. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, yeye mwenyewe ameshindwa kuweka the best technology za irrigation, anatumia zile za vijungu, zile traditional. Mmenielewa! This tells the costs ya investment. Mmenielewa lakini? This tells the costs of investment kwamba shilingi milioni 16 is nothing. Shilingi trilioni moja, tukichukua hekta milioni moja kwa ekari milioni 2.5; shilingi trilioni 16 tukiajiri vijana 250,000 na scientifically imedhibitika kwamba ajira moja ya shambani inatengeneza ajira sita kwenye value ya addition; gharama ya kutengeneza hizi ajira, ni shilingi milioni nane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii jamani ni simple economics siyo muujiza, ni namba. Je, tunatarajia kunaweza kukatokea changamoto? Inawezekana kabisa. Sasa hivi tunafanya mikoa mingapi? Dodoma, tunafanya Njombe ekari 80,000, tunafanya Singida, tunaenda Geita, tunaenda Shinyanga, kote huko tunaenda. Tumepokea maoni yenu kuhusu namna ya kuwapata vijana. Tutaenda kuyafanyia kazi. Hili tutaenda kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine la mabadiliko kwenye Tume ya Umwagiliaji, tunakuja na sheria, inaitwa Tanzania Irrigation and Extension Development Authority. Kwa sababu tunapeleka vitendea kazi, tunapeleka watu, lazima tuwe na mamlaka yenye kuwajibika kusimamia shughuli hizi.

Mheshimiwa Spika, kulitolewa wazo la kuwepo na mfuko wa umwagiliaji. Sheria ipo. Tumeanzisha Irrigation Development Fund, tumepata shida kwenye ukusanyaji wa maduhuli, na ziko sababu. Tumeamua kwenda kuzifanyia kazi hizo sababu, kwa sababu hatukuwa na mfumo wa registration wa scheme za nchi. Sasa hivi tunafanya registration ya scheme zote za nchi. Hatukuwa na mfumo wa kuwasajili wakulima walioko kwenye scheme, sasa hivi tunafanya shughuli ya kusajili wakulima walioko kwenye scheme.

Mheshimiwa Spika, niliombe Bunge lako Tukufu kwamba tusi-condemn vijana wa nchi hii. Tusiumie kwa nini mtu amemiliki ekari 10. Nchi hii ina jumla ya hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo. Tulizotumia hazizidi hata milioni 15, bado ardhi ipo. Tuhangaike kuongeza tija ya uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, suala la mbegu, ni kweli, kama nchi tuna tatizo la mbegu. Mahitaji yetu ya mbegu ni jumla ya tani 670,000. Tunazalisha asilimia 10, Serikali inachukua hatua gani? Kwanza, tumeanza kuweka miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba yetu yote ya mbegu.

Mheshimiwa Spika, pili, tunaihusisha sekta binafsi ya nchi yetu kwenye uzalishaji wa mbegu na tumeanza kuwapa mashamba. Tumewapa pale Mbozi, na mwaka huu wamezalisha tani 7,000. Tatu, tuna-acquire land kama Serikali ili tuweze kuwa na ardhi tunayoihitaji ili tujitosheleze kwa mbegu. Nchi yetu inahitaji jumla ya hekta 360,000 za kuzalishia mbegu.

Mheshimiwa Spika, lingine, tunawekeza kwenye utafiti, naongelea issue ya kuwepo kwa maabara za tissue culture, kwa watu wa Kagera kwenye eneo la kahawa. Tunapeleka pale maabara Maruku, tunaenda kuweka maabara kwa ajili ya tissue culture ya migomba na tissue culture kwa ajili ya kahawa.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine, tunapima afya ya udongo wa nchi. Niseme tu jambo moja. Hapa ndani, niwaambieni, hili ndiyo Bunge na sisi ndio Watanzania, na Watanzania wote wajue. Taifa letu toka tunapata uhuru, suala la kupima afya ya udongo, tulikuwa tunategemea makampuni ya mbolea na donors, haiwezekani. Serikali imechukua hatua gani?

Mheshimiwa Spika, kwanza, tumetengeneza mfumo wetu, tumeshaanza na sasa hivi kupima ramani kwa ajili ya kuangalia acidity level kwenye nchi yetu. Hiyo ni ramani ya nchi yetu na hali ya afya yetu ya udongo, lakini database hiyo tunaimiliki wenyewe, tunatengeneza mfumo wa kuhifadhi taarifa za upimaji wa afya ya udongo ili tuweze kujua mbolea sahihi unayoipeleka Nzega is a process siyo jambo la usiku mmoja.

Mheshimiwa Spika, la tatu; uwekezaji kwenye infrastructure za umwagiliaji tutatumia maji ya Ziwa Victoria wala siyo aibu, tutatumia maji ya Lake Tanganyika wala siyo aibu tutatumia na tumeisha tangaza. Sasa hivi feasibility study zinaanza kufanyika na mwaka huu unaokuja katika mabonde yenye jumla ya hekta 306,000. Mwaka huu unaokuja kwa sababu feasibility study zinafanyika ndani ya mwaka huu wa fedha wa 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka kesho tutaanza kujenga hekta 300,000 katika kila bonde ndiyo muelekeo wa Serikali. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge, transformation ya agriculture naweza nikasema with confidence baada ya Mwalimu Nyerere mimi nakuwa mkweli. Baada ya Mwalimu Nyerere ni Serikali ya Awamu ya Sita ndiyo imeamua kwenda kuwekeza kwenye maeneo ya msingi ya kilimo ndiyo ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mwalimu kaondoka kaacha mashamba 17 ya mbegu ni yaleyale sixty years Mwalimu kaondoka kaziacha maabara zilezile. Leo ndiyo tunawekeza kwenye maaabara za utafiti, leo ndiyo tuna expand tunaanza kufungua mashamba kwa ajili ya kuweka miundombinu ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho program ya BBT inahusisha kwenda shambani, inahusisha kutoa financing kwa vijana walioko kwenye mashamba ambao hawamo ndani madarasa sasa hivi. Mwezi uliyopita tumewapa vijana two hundred million walioko mashambani ambao hawawezi kwenda kukopeshwa na taasisi za fedha. Tumeweka eighty hundred million katika mfuko wa pembejeo tutawapatia hawa vijana ambao wanafanya shughuli za kilimo mashambani na wanaofanya value addition. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee issue ya ngano na alizeti. Eneo la alizeti tumesambaza mbegu na nataka niipongeze taasisi yetu ya ASA mbegu walizosambaza safari hii satisfied seed zimeweza kuleta matokeo mazuri na uvunaji umeanza.

Mheshimiwa Spika, ninajua wakulima wa alizeti kuna anguko la bei, nataka niwaambie hivi tunampelekea Mheshimiwa Rais barua ombi la kututeulia Mwenyekiti wa COPRA Mamlaka inayosimamia cereals na other produce. Ambayo kwa mujibu wa sheria hii ndiyo itatoa masuala ya bei elekezi, tutatoa bei elekezi ya alizeti clearly. Hatua ya pili tunawasilia na wenzetu Wizara ya Fedha tumewaomba tuongeze kodi ya mafuta yanayotoka nje ya refine kutoka asilimia 25 kwenda asilimia 35 na wachajiwe VAT ya asilimia 18. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la ngano sisi tuna import ngano tani milioni moja kwa mwaka. Ili tujitosheleze ngano tunahitaji tani 50,000 za mbegu za kwenda kumpa mkulima alime tumechukua hatua gani? Tumeanza kuzalisha mbegu mama, sasa tunazalisha mbegu za pre basic, tunaenda kuzalisha basic seed 2025/2026 tutazalisha mbegu kwa ajili ya wakuwapelekea wakulima. Tumewaandikia makampni ya ngano yote kwamba waingie MOU na Serikali kwamba kabla ya ku–import watanunua ngabo ya ndani kwanza, wamekataa mpaka sasa.

Mheshimiwa Spika, nataka niseme mbele ya Bunge lako Tukufu, niseme mbele ya Wabunge na mbele ya watanzania kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu 2025/2026 tunaenda kuzalisha ngano mwenye mamlaka ya kuwapa cheti cha ku– import ngano ndani ya nchi ni Waziri wa Kilimo. Kama takuwa kwenye kiti viwanda vitageuka chuma chakavu
hawatoingiza hata kilo moja kama hawajanunua ngano ya ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watanzania hawatokufa kwa kukosa ngano, haiwezekani unambembeleza mmefanya nao trial, tumewapa mbegu wao wenyewe kwenye maabara zao. Wamesema inafaa alafu wakati wa kusaini MOU wanasema hatutaki over my dead body watasaini mkataba, wasipo saini hatutowapa phytol-sanitary kuingiza ngano watajua watakachofanya na viwanda vyao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani 1970, 1980 asilimia 80 ya ngano ya nchini, hii ilikuwa inapatikana ndani tulifungua mipaka. Kwa hiyo, hili walifahamu tutaufunga Mkoa wa Manyara, tunafanya pilot Njombe, tumeona matokeo ni mazuri, tutaweka cluster na sasa tumeishaamua kuwa na korido za mazao. Kuna mazao tutazalisha maeneo maalum maeneo mengine hatutoyaruhusu kuzalishwa ili tuweze economies of scale. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, dakika mbili malizia.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa kusema kitu kimoja, bila kuongeza tija kila siku tutakutana hapa bei ya mkulima mbaya, bei ya mkulima juu bei ya nini. Lazima tuongeze tija, lazima tumiliki mbegu zetu wenyewe, lazima tuwekeze kwenye umwagiliaji na ni lazima tuwekeze kwenye skimu za umwagiliaji siyo mifereji ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili tuweze kufanya hivi tunahitaji kuwekeza kwa muda mrefu na huu ndiyo muelekeo sahihi kokote kule duniani. Lazima tufungue mashamba ya kuzalisha mbegu, lazima tuhakikishe tunaiwezesha sekta yetu binafsi ya ndani na kwenye bajeti tumeweka bilioni 10 ambayo tutawapatia wafanyabiashara wa kitanzania wanaobangua korosho, wanaoongeza value addition kwenye zabibu, kuwanunulia vifaa kwa ajili ya kununua mazao ya wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, nataka niwaambie vijana wa kitanzania Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuwafanya wamiliki nyenzo za uzalishaji na kuwamilikisha ardhi. Tutawekeza kwenye eneo la kuwamilikisha ardhi, tutawasapoti waweze kufanya shughuli zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho niwaambie Waheshimiwa Wabunge maoni yenu tutaendelea kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsanteni, natoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naafiki.