Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Martha Nehemia Gwau

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii uliyonipa ya kuchangia Wizara hii muhimu sana ya Kilimo, ambayo kwa wananchi wetu tunaowawakilisha ndio shughuli kubwa wanazozifanya kwa kujipatia kipato, nimshukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kabla sijaendelea nisiwe mchoyo wa fadhila kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuishika Wizara hii, lakini pia kwa kuona umuhimu wa Wizara hii na kuiongezea bajeti mwaka hadi mwaka wa fedha. Kwa hiyo nimpongeze sana. Pili, niipongeze Wizara chini ya kaka yangu Mheshimiwa Bashe na Naibu Waziri Mheshimiwa Mavunde, lakini na watendaji wote wa Wizara kwa juhudi kubwa na mikakati mingi wanayokuja nayo kwa ajili ya kumkwamua mkulima wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu leo utakua kwenye mambo mawili; suala zima la kilimo cha alizeti na suala zima la mbolea. Tanzania tuna wakulima nadhani wa aina tatu. Kuna wale ambao ni small scale farmers ambao ni majority ya watu wetu, ndio hao wanajishughulisha na kilimo kidogo kidogo. Pia tuna wale middle ambaye Kaka yangu Bashe amekuja na hii program ya BBT, mimi naweza nikasema kama hao ndio middle farmers. Vile vile tuna wale large farmers ambao wao wanakuja na mitaji yao na teknolojia yao. Sasa leo nijikite kuwaelezea au kuwatetea hawa small scale farmers ambao ndio mama zetu, baba zetu, wajomba zetu na watu wetu wote waliopo mikoani mwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nielezee zao la alizeti. Zao la alizeti ni kati ya mazao ya kibiashara yanayolimwa katika Mkoa wangu wa Singida. Pamoja na mazao mengine ya kibiashara lakini zao la alizeti ni zao letu moja la kibiashara. Tulipata heshima ya Waziri Mkuu kuja kuzindua mikoa ya kimkakati ambayo Singida ilikuwa kati ya hiyo mikoa ya kimkakati itakayolima zao la alizeti. Nimshukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna uongozi wa mkoa chini ya Mkuu wetu wa Mkoa Mheshimiwa Peter Serukamba na Wakuu wa Wilaya zote tano wakihamasisha na wakisaidia wananchi kuhamasisha kulima zao hili la alizeti, kwa sababu Serikali imetusaidia mbolea, ruzuku pamoja na mbegu. Kwa hiyo wao wanafanya uhamasishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetoka kwenye kulima hekari laki nne na sasa tumelima laki sita na projection ya mwakani tutalima mpaka hekari milioni moja na tutakuwa na uwezo wa kulisha zaidi ya asilimia 40 ya mafuta kwa Nchi hii ya Tanzania katika Mkoa wetu mmoja wa Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri kwa Mheshimiwa Waziri, pamoja na juhudi nyingi wanazofanya na mikakati mingi, zao hili la alizeti sasa wakulima wetu wa Singida wanakata tamaa kulima. Wanakata tamaa kwa sababu bei ya mafuta ya alizeti imeshuka na zao la alizeti limeshuka kwa sababu Serikali haijaweka kodi kwa mafuta yanayotoka nje. Sasa how can you compete na Mheshimiwa Waziri kaka yangu slogan yake ni kumkomboa mkulima wa Tanzania. Ukombozi wa mkulima wa Tanzania, moja lazima iwe kulinda bei ya zao lake analolilima kwa sababu, nimesikiliza hotuba yake mwanzo mwisho kaongelea masoko ya ndani, ya nje na mambo mengi mazuri. Bahati mbaya sijasikia Mheshimiwa Waziri kaka yangu akiongea jinsi gani atalinda bei za mkulima huyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapowahamasisha watu, Serikali wanapoweka mikakati mizuri ya kupata mbolea za ruzuku wananunua, lakini mbegu bora, sasa zao kama halina soko hawa watu wanakata tamaa, wanavunjika moyo. Kwa hiyo kabla Waziri hajaruhusu kodi kutowekwa kwenye mafuta ya nje, kutoa au kutokutoa, je, hivi wanawaza implication kwa hawa wakulima itakuwaje? Kwa hiyo nadhani ni mikakati ambayo Wizara inabidi ifanye kabla haijaruhusu kwa wakulima hawa kuvunjika moyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, Mheshimiwa Waziri aje na mikakati, atueleze na hawezi kushindwa kwa sababu he is the one of the best Ministers, ataweza kuwalinda wakulima wetu na kulinda bei za wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine cha pili hapo hapo, ni ushauri kuwa, wakulima wetu wauze final product badala ya kuuza mbegu. Kwa sababu Mheshimiwa Waziri amekuja na wazo la BBT, hawezi kushindwa kwa wakulima hawa kutengeneza au kujenga kiwanda labda kila halmashauri ili wakulima hawa wauze final product, badala ya sasa hivi wananuza magunia ya lumbesa ambayo wanalaliwa tu au wanalanguliwa na watu ambao wanaenda kufaidika zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kama kuna kiwanda wakakamua mafuta watauza mafuta, lakini watauza mashudu nao watapata kipato kizuri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nashauri tu katika hili zao la alizeti naomba aliangalie kwa sababu Mkoa wa Singida kiuchumi kwa kweli zao la alizeti ndio zao ambalo wanalitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa mwisho ni suala zima la mbolea. Tuna mbolea na Serikali waliweka ruzuku kwa mbolea, lakini nashauri kwa nini hii ruzuku isitolewe kwa mbolea ya viwanda vyetu vya ndani? Nasema hivi kwa sababu viwanda vya ndani vina economic benefit ya kupewa ruzuku. Mbolea zote zinazoagizwa sisi tunafanya kama tuna export job, kwa sababu ukitoa ruzuku kwa mbolea za nje ni kama una-export job badala ya kufanya job creation. Tukiweka ruzuku kwa mbolea za viwanda vyetu vya ndani, ina maana tunaruhusu hivi viwanda viajiri watu wengi, lakini tunaruhusu uchumi u-circulate kwa sisi kwa sisi hapa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna faida ya kuweka ruzuku kwa viwanda vyetu vya ndani, mojawapo ni accountability. Mheshimiwa Waziri amekuja na ule mfumo wa zile namba za kugawa mbolea. Sasa kama viwanda vyetu vya ndani vitapelekwa ruzuku moja kwa moja kiwandani, ina maana tutakuwa na uwezo wa kusema Mkoa wa Singida peleka tani kadhaa na tutafanya accountability, kwamba hizo tani zimepelekwa na kweli zimewafikia wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine tutaweza kufikisha mbolea kwa wakati. Mbolea nyingi wananchi wanalalamika hazifiki kwa wakati. Ule msimu wanataka kulima, mbolea inakuwa haijafika, lakini tukitoa ruzuku kwa viwanda vyetu vya ndani kuanzia mwezi Julai wanaanza kusambaza hizo mbolea kwa wakulima wetu wa vijijini. Kwa hiyo itafika mahali mwezi Desemba mbolea zishawafikia wakulima. Tofauti na sasa, wakulima hawapati mbolea kwa muda muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine tutapata kodi kwa Serikali kwa sababu uzalishaji wa viwanda vyetu vya ndani utakuwa mkubwa na wakulima watakuwa na choices. Wataambiwa bei hii ya mbolea ya nje, lakini bei hii ni mbolea ya ndani ambayo tayari ina ruzuku. Kwa hiyo, nashauri hayo kwa Waziri ayachukulie kama chachu, lakini ayachukue kama atatengeneza ajira na atakuza uchumi. Kiwanda cha Dodoma mfano, wakiajiri watu 3,000 na uchumi wa Dodoma utabadilika na wananchi maisha yao yatabadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)