Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kuunga mkono hoja hii ya Wizara ya Kilimo, lakini vile vile nataka kwa dhati kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nia njema aliyonayo katika kukuza kilimo cha nchi yetu. Kama tunavyofahamu mwaka juzi uliopita bajeti ya kilimo ilikuwa karibu bilioni 300, lakini mwaka huu ambao unaisha bajaeti ya kilimo ikaongezeka kuwa bilioni 751, lakini mwaka huu bajeti ya kilimo imekuwa bilioni 970. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio hilo tu ukiangalia utekelezaji wa bajeti hii unaona kabisa kwamba fedha inatoka na utekelezaji hadi sasa ni asilimia 73.2 na huko nyuma ilikuwa ni asilimia 51, 49, 50, ni hapo hapo, lakini safari hii inaenda hadi asilimia 73. Kwa hiyo kwa kiasi kikubwa nataka niseme Wizara hii kazi kubwa inafanyika nampongeza sana Mheshimiwa Waziri amekaa kimkakati lakini vile vile nimpongeze sana na Naibu Waziri Mheshimiwa Mavunde lakini vilevile nataka nitoe pongezi za dhati kabisa kwa Mkurugenzi wa Umwagiliaji. Tunaona kabisa lengo kubwa la kutaka kuendeleza kilimo cha umwagiliaji na kuinua kilimo katika nchi yetul inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la umwagiliaji katika nchi yetu ni takribani milioni moja na laki mbili. Hadi sasa tunamwagilia kiasi cha hekta 727,000. Kwa hiyo bado tuna kazi kubwa na bado Wizara hii ipewe fedha za kutosha ili tuweze kufikisha lengo la Watanzania la kuwa na chakula cha uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue nafasi hii vilevile kuishukuru sana Serikali, Wilaya yangu ya Bahi ilikuwa imeathirika sana na upungufu wa chakula, lakini kupitia NFRA tumeweza kupata chakula karibu kata zote na jumla ya tani 1,530 zimegaiwa katika kata zote. Jambo hili kwa dhati naishukuru Serikali. Kupitia hapo nataka nimkumbushe Mheshimiwa Waziri nimeangalia katika mpango ule wa kugawa mbegu, ipo alizeti lakini mtama mfupi haupo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri kwa dhati kabisa atuangalie hasa kanda ya kati na jambo hili nimekuwa nalisema sana kwamba, bado tunahitaji mtama mfupi ambao ndio mkombozi katika eneo letu. Hatupati mvua za kutosha. Kwa hiyo, pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri ametupatia alizeti naomba sana Mkoa wa Dodoma uwe na special treatment tuweze kupata mbegu ya mtama mfupi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye suala zima la BBT; jambo hili ni zuri, lakini yapo mambo ambayo naona lazima tuyarekebishe. Kwanza eneo hili tumewapa vijana ambao hawana ajira, tunataka kuwakomboa, lakini tunataka walime mazao ya muda mrefu. Zabibu inachukua miaka mitatu ili aweze kuvuna, hali kadhalika na korosho nayo nasikia inaenda miaka mitano. Sasa Mheshimiwa Waziri hapa tunafanya kama ni rescue plan. Sasa kijana huyu ambaye atasuburia miaka mitatu wakati hana ajira, mkakati huu nauona kama hauendi sawa sawa. Vile vile kwenye umilikishaji tulisema kwamba vijana hawa watamiliki kwa miaka 66. Sasa kijana ambaye ana miaka 30 leo unataka amiliki kile kieneo kwa miaka 66 atakuwa babu tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni lengo la kuhamasisha na kutoa ajira kwa vijana, nashauri iwe miaka 10 hadi 15. Ili kwamba ikishapita miaka 15 amesha-graduate ili tuchukue vijana wengine na ikiwezekana Mheshimiwa Waziri yasiwe mazao ya muda mrefu, yawe mazao ya muda mfupi. Kwa sababu kwanza ukiangalia katika nchi yetu hatujapata uwekezaji kwenye nafaka, sasa tukiweka katika suala hilo ina maana tutaweza kupata watu wa nafaka lakini vile vile vijana wetu wakapata fedha kwa muda mfupi na iwe ni program ya miaka 15 ili akisha-graduate na wengine waweze kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nije kwenye suala la zabibu; mkoa wetu ndio pekee ambao unastawisha zabibu kwa kiasi kikubwa. Nimesema suala la Bodi ya Zabibu, naomba sana na namhakikishia Mheshimiwa Waziri nitashika shilingi, nataka aje na majibu ya kuanzisha Bodi ya Zabibu. Nasema hilo kwa nia njema tu, Wizara ya Kilimo ina mambo mengi, zao la zabibu kuwa chini ya Wizara ya Kilimo, kidogo kuna kuwa na mambo mengi. Sasa tunakosa umadhubuti wa kuweza kulikuza zao hili. Kama mwaka huu ukiangalia uuzaji wa zao la zabibu bado haueleweki. Viwanda vingi vinasema havitanunua na havitanunua kwa sababu kwanza bado wana mchuzi ule kwenye maghala yao, lakini vile vile bado uhakika wa soko hauko kwa wakulima. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba majibu ya kutosha akija kwenye suala hili la zabibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, amenipa Mradi wa Umwagiliaji pale Kongogo wa bilioni tano na milioni 600. Haijawahi kutokea katika Wilaya ya Bahi kupata fedha hizi kwa pamoja, nakushukuru sana na naipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba, tuna skimu yetu kubwa sana ya umwagiliaji ya Bahi na tumeunganika na Kintinku. Mwaka jana Wizara ilisema wanafanya upembuzi yakinifu na mwaka huu tena naona upembuzi yakinifu. Namwomba Mheshimiwa Waziri, watu wa Bahi wanasubiri ukarabati wa skimu ile na kama anavyofahamu, kama nilivyosema Bahi na Kintinku, tunategemea zaidi mabonde haya kwa maisha ya watu wetu. Mji wa Bahi unategemea zaidi suala zima la kilimo cha mpunga. Kwa hiyo naomba badala ya upembuzi yakinifu, twende kwa haraka ili kwamba ikiwezekana mwaka huu unaokuja tuanze ukarabati ambavyo mwanzo nilikuwa najua itaweza kufanyika hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri ametaja kukarabati Skimu ya Chikopelo, Skimu ya Mtitaa, Skimu ya Mkakatika, lakini jambo kubwa zaidi nataka niseme kwenye suala zima la skimu zetu. Maeneo mengi ambayo maji tunatenga kwa mfano Skimu ya Kongogo ile tutalima mwaka mzima. Kwa hiyo na skimu nyingine hizi tukiweka utaratibu kwamba tuwe na uhakika wa kulima mwaka mzima tutakuwa tumewaokoa wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda tena nichukue nafasi hii kuiunga mkono hoja na nampongeza Mheshimiwa Waziri. Ahsante sana. (Makofi)