Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye bajeti hii ya kilimo. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa jambo hili zuri la kuona kilimo na kuipandishia bajeti yake kila mara. Pili naomba kumpa pongezi Mheshimiwa Bashe ambaye ndiye Waziri wetu wa kilimo pamoja na Mheshimiwa Mavunde ambaye ndiye makamu wake na Wizara nzima yote ya Kilimo, nasema hongereni sana mnafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nikianza kwa upande wa bajeti, ndiyo bajeti inaongezeka na sasa hivi imeongezeka mpaka bilioni 970, lakini lazima na ni vizuri tuendane pamoja na Makubaliano ya Malabo na Maputo ya asilimia 10 ile yote ni ya kilimo kutokana na bajeti yote ya taifa; kwamba asilimia 10 iwe ya kilimo. Kwa hiyo ninashauri kuwa, licha ya kuongeza bajeti mara kwa mara naomba bajeti iendelee kuongezwa kadiri bajeti inavyokwenda mwaka kila mwaka tuweze kuwa na kilimo chanye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi kwenda mbali bila ya kumpongeza Mheshimiwa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Bashe kwa upande wa BBT ambayo wameianzisha, hasa kwa upande wa vijana pamoja na wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inasaidia sana kwa upande wa kulima mashamba makubwa (block farming) ambayo tunaweza kupata mazao kwa wingi tunaweza kupata maafisa ugani ambao wanatoa service mara moja kwa watu hao wote; kwa hiyo ni kitu kizuri sana; na inatoa ajira kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalizo ni moja tu; ninaomba kuwa wale vijana muwaangalie kwa undani kabisa kuwa ni kweli wanakwenda wana interest ya kilimo kweli? Au wanakwenda kwa sababu hawana ajira? Hiyo tuiangalie kusudi BBT iweze kuendelea, na iweze kuendelea hata kwa kanda, kama ulivyosema Mheshimiwa Waziri pia kwa mikoa. Naamini mkuu wangu wa Mkoa wa Morogoro Mheshimiwa Waziri Bashe mmeshaongea tayari. Kwamba Mkoa wa Morogoro tumeshatenga eneo la kuendeleza BBT kusudi vijana wetu waweze kulima kilimo chenye tija kwenye sehemu hiyo. kwa hiyo naomba hiyo uikumbuke, kuwa mkoa wa Morogoro, inawa hukuutaja kwenye mikoa ambayo ina kipaumbele, lakini mkoa wa Morogoro ni mkoa wenye mikakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwa upande wa kilimo lazima tukumbuke kuwa kuna kanuni bora za kilimo na hasa ukitaka kuwa na kilimo chenye tija. Kanuni ya kwanza hasa ni kuwa na mbegu bora. Mbegu bora hizi ambazo sana sana zinazalishwa na ASA, ASA kazi yake ni kuzalisha mbegu hizo bora pamoja na wakulima wengine ambao wanaratibiwa pamoja na TOSCI ambayo inaangalia ubora wa mbegu, pamoja na TARI ambayo inafanya utafiti. Vitu hivi vitatu, ASA, TARI, TOSCI wakiungana kwa pamoja wanzalisha mbegu bora ambayo ikitumika kwa mkulima anaweza akapata mazao bora na mazao yenye uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo muhimu ni kuwaongezea fedha, naamini wamewaongezea fedha inakwenda inapanda, kuna wakati walipata bilioni 11.6, wakaja bilioni 43 na kitu na sasa hivi imepanda. Kwa hiyo tujaribu kuwaongezea kwa sababu hizi ni taasisi ambazo ni muhimu kwenye upande wa mbegu bora. Nikija kwenye mbegu bora pia tusisahau mbegu za asili au mbegu za mkulima. Mbegu za mkulima hizi unaweza ukazitumia kila wakati, mwaka hadi mwaka. Cha msingi wapate elimu ya kuzichambua hizi mbegu kuona ni mbegu zipi atatumia kwa mwaka ujao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni mbolea; tunashukuru Mheshimiwa Rais tumepata mbolea ya ruzuku, lakini hii mbolea ya ruzuku imesambaa kwenye mikoa mingine vizuri, lakini kwenye mikoa mingine haijafanya vizuri kwa sababu ya usambazaji. Naomba safari ijayo waangalie kwa umakini kuhusu usambazaji. Ni kweli kwenye ushirika imesambazwa vizuri lakini kwa wakulima wengine haikwenda na kwa madukani, maduka ya kilimo wengine walikataa kabisa kuwa na hii mbolea kwa sababu ya milolongo mirefu ambayo ilikuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mbolea, nashauri kuwa kwa kuungana pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara tuweze kuanzisha viwanda vyetu vingine vya mbolea kusudi kupunguza makali ya bei. Hapa mpaka sasa hivi tuna Kiwanda cha Minjingu pamoja na kiwanda hiki kilicho hapa Dodoma ambavyo ndivyo vinazalisha mbolea ambayo haitoshi. Mpaka sasa hivi mbolea nyingine inatoka nje, kwa hiyo tungeliomba tuweze kuwekeza kwenye uzalishaji na kujenga viwanda vya mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuongelea ni maji. Lazima mbegu ipate maji, ikipata maji na hapa naongelea kilimo cha umwagiliaji. Kilimo cha umwagiliaji ni muhimu sana na kilimo cha umwagiliaji ni muhimu sana kwa sababu kuna mabadiliko ya tabianchi, ukame hasa. Kwa hiyo tukimwagilia tunaweza kupata mazao yenye tija na mazao ambayo, kwa mfano upande wa mpunga, unaweza ukavuna magunia 40 mpaka 80 kwenye hekta moja. Kwa hiyo kama ndio hivyo kwa nini tusilime kilimo cha umwagiliaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namshukuru Mheshimiwa Waziri, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuleta mitambo 33 ambayo itaweza kuchimba mabwawa na magari 53 ya ufuatiliaji. Jambo la msingi kwenye ufuatiliaji sio magari, kwenye ufuatiliaji ni wafanyakazi. Kwa hiyo lazima tuwe na wataalam wa kutosha na nashauri kuwa kadri fedha zinavyotolewa, kadri bajeti inavyokuja kila mwaka magari yaweze kuongezwa kusudi tuweze kuchimba na kufuatilia hawa watu kwa ujumla. Hiyo inaendana pamoja na kilimo cha umwagiliagi Mkoa wa Morogoro. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mkoa wa Morogoro ni mkoa uliojaliwa mito mingi, ni mkoa wenye skimu mpaka sasa hivi tuna Dakawa, tuna Mkula tuna na skimu nyingine nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ila ningeliomba kuwa tupate skimu nyingine…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Christine.

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: …ili tuweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na Maafisa Ugani…

MWENYEKITI: Muda wako umeisha Mheshimiwa.

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari bado?

MWENYEKITI: Muda wako umeisha Mheshimiwa.

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Ugani waangaliwe vizuri. Ahsante na Mwenyezi Mungu ambariki Bashe, Mwenyezi Mungu ambariki Mheshimiwa Rais, tuweze kuendeleza kilimo chetu. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)