Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii kutoa mchango wangu juu ya hotuba hii ya bajeti ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambae ameniwezesha jioni ya leo kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza sana wakulima wa Jimbo langu la Nanyumbu. Natambua changamoto kubwa ambazo wanakumbana nazo katika kuhakikisha kwamba kilimo hasa kilimo cha korosho kinakwenda mbele. Kwa hiyo naomba nichukue nafasi hii kumjulisha Mheshimiwa Waziri changamoto ambazo wakulima wangu wa Jimbo la Nanyumbu wanakumbana nazo katika kuhakikisha kwamba kilimo chetu cha korosho kinakwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka huu uliokwisha kilimo cha korosho ndani ya taifa letu kimeshuka sana, kutoka tani 240,000 hadi tani 182,000. Hii yote kulingana na maelezo ya Mheshimiwa Waziri ni kwamba imesababishwa na hali ya hewa. Lakini naomba nichukue nafasi hii kulijulisha Bunge lako Tukufu pamoja na kwamba kilimo cha korosho kimeshuka lakini ndani ya Wilaya yangu ya Nanyumbu kilimo cha korosho kimepanda katika uzalishaji wake. Kwa hiyo basi nachukua nafasi hii kuwashukuru sana na kuwapongeza wananchi wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wananchi wangu wanavyo changamoto zifuatazo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni bei isiyoeleweka ya korosho. Jambo hili ni changamoto kubwa sana kwa wakulima wetu. Nimewahi kushauri ndani ya Bunge lako, kwamba kwa nini Serikali yetu, kwa nini Wizara isitoe bei elekezi ya zao la korosho ili mkulima akajipanga na akajua kwamba gharama zangu za uendeshaji ni shilingi ngapi na nitapata faida kiasi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wetu wanakwenda kama maisha ya kubahatisha, hawajui mwaka huu bei ya korosho itakuwa kiasi gani; na hii inadhorotesha uzalishaji wa bei ya korosho. Kwa hiyo namuomba sana Mheshimiwa Bashe ajaribu kuliangalia jambo hili, atoe bei dira, bei ambayo itawawezesha hata wanunuzi wanaokuja kuanza kuanzia katika eneo lile. Kukiwa na bei dira wale wanunuzi uchwara wanunuzi wadogowadogo hawatakuja katika mnada, watawaacha wanunuzi ambao wako serious na kuhakikisha kwamba bei ya mkulima inakuwa nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, wakulima wetu, hasa wa korosho, wana changamoto na mikopo, benki zetu haziwasaidii wakulima wetu. Jambo hili nimelizungumzia sana, na Mheshimiwa Bashe analifahamu. Kwa wale wasiojua korosho, korosho si pembejeo tu. Niishukuru sana Serikali imetoa pembejeo kwa wakulima, jambo hili mimi nalipongeza sana. Lakini kumpa tu pembejeo hakusaidii, korosho unahitaji kupalilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu mwenye ekari kumi ana mikorosho 240 huwezi ukapalilia wewe na mkeo, ni lazima utahitaji vibarua, na ndiyo maana tunakwenda kwenye taasisi za benki kuomba mkopo ili fedha zile tutumie kwenye kupalilia mikorosho. Tunahitaji mikopo ili kuweza kununua mafuta na kuweza kupulizia mikorosho; na mikorosho huwezi ukaipulizia peke yako, hekari kumi unahitaji kuwa na watu wa kuwakodisha ili wakusaidie kupulizia. Tunahitaji vibarua wa kuokota korosho, ndoo moja tunaokota kwa shilingi 2000, ukiwa na mikorosho 2400 huwezi ukaokota wewe na mkeo inahitaji vibarua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana tunaomba taasisi za benki ziwakopeshe hawa wananchi ili waweze kutumia mikopo hiyo katika uzalishaji na kuinua pato la taifa. Sasa ndugu yangu Bashe Waziri msikivu, jambo hili la mikopo benki zetu wanashindwa vipi kuwapatia wakulima wetu? Leo ni mwezi wa tano, mwezi wa sita maandalizi ya zao la korosho yanaanza huku benki ikiwa bado hawatoi mikopo kwa wananchi wananchi wanahangaika kule. Kwa hiyo namuomba Mheshimiwa Bashe hili jambo aliangalie sana katika mstakabali mzima wa kuinua zao letu la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kwenye bajeti yake Mheshimiwa Bashe amazungumza suala zima la umwagiliaji, mimi nampongeza sana. Hata hivyo nina masikitiko makubwa. Sisi tumepitiwa na Mto Ruvuma. Mto Ruvuma ukianzia Mtwara Vijijini kwa Bwana Chikota kule hadi jimboni kwangu mpaka Tunduru; mimi ndani ya jimbo langu nimepata mradi mmoja tu wa kuchimba bwawa katika Mto Ruvuma, hili jambo linasikitisha sana. Tuna maeneo makubwa ya umwagiliaji kuna watu wamezungumza hapa, naishukuru Serikali kwa kuapta miradi ya skimu ya umwagiliaji miradi 11 miradi 15 mimi mradi mmoja na sijui kama utafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Bashe next time awe mwangalifu na miradi ya namna hii. Haiwezekani sehemu moja inapata mradi mmoja wengine wanapata miradi kumi, kumi na tano, hili jambo si sawa. Wote tunatambua mabadiliko ya hali ya hewa, jambo hili linaathiri nchi nzima, na suluhisho la mabadiliko ya hali ya hewa ni kwenda kwenye kilimo cha umwagiliaji. Sasa inakuwaje leo katika eneo kama lile ambalo ndio wazalishaji wakubwa unatoa mradi mmoja wa bwawa? Hili jambo si sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namuomba sana Mheshimiwa Bashe hili jambo aliangalie ili tutakapokuja mwakani tuhakikishe miradi hiyo ya umwagiliaji inakwenda sambamba nchi nzima. Hata hivyo naishukuru sana Serikali tunao mradi mmoja wa uchimbaji bwawa ukachimbwe bwawa. Tutatarajia mwakani tuje hapa tujue lile bwawa ambalo lilienda kuchimbwa katika Kata ya Masuguru likachimbwe ili wasaidie shughuli za umwagiliaji kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba kuchangia kuhusu suala zima la bei ya pembejeo, mbolea. Ndani ya wilaya yangu pembejeo, hasa mbolea, mwaka huu haikuwepo. Muuzaji wa pembejeo alikuwa napatikana kilimeta 54 kutoka wilayani. Jambo hili kwa kweli lilinihuzunisha sana, na niliwasiliana na Mheshimiwa Waziri, na Mheshimiwa Waziri akaahidi kwamba atafanya mabadiliko. Lakini naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri, kwa nini tusivitumie vyama vyetu vya msingi kuwa mawakala wa kuuza pembejeo hizi? Kwa sababu vyama vyetu vya msingi kule kwetu wako karibu kila kata, kwa hiyo mbolea hii itakuwa rahisi kuigawa na kuisimamia marejesho yake kama itahitajika kurejeshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hivyo kwa sababu wakulima haiwezekani akasafiri kilometa 54 kwenda kuifuata mifuko miwili kule halafu akarudi kilmeta 54, ni mbali sana. Kwa hiyo kama mbolea inakuwa ni shilingi 70,000 haitakuwa tena 70,000, itafika 90,000 mpaka 100,000; kwa hiyo itakuwa haujamsaidia mkulima. Ninaomba sana Serikali kwa hili la pembejeo nalo litiliwe mkazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba pia kuzungumzia masuala ya ujenzi wa mabwawa, nimezungumza kwamba tumepangiwa bwawa moja pale Masuguru, lakini sisi katika wilaya yetu tunayo mabwawa ambayo sasa hivi endapo yangeendelezwa yale yaliyopo yangesaidia sana kutatua kero hii. Mfano Nangomba mimi ninalo bwawa, pale Chipweputa kwenye Kijiji cha Lomasogo ninalo bwawa na sehemu nyinhine nazo kuna mabwawa. Yale mabwawa nilitegemea sasa yangekuja kuboreshwa ili yaweze kuinua suala zima la umwagiliaji

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni suala la kuongeza thamani mazo yetu. Ninatambua kwamba Wizara ina mkakati mkubwa wa kujenga kiwanda kikubwa katika Mkoa wa Mtwara. Naomba nishauri, tunayo majengo katika Mkoa mzima wa Mtwara. Tunayo majengo maeneo ya Newala, Mtwara Mjini na Masasi. Sasa, kwa nini tusitumie majengo yale kuweka mashine ili kuweza kubangua korosho zetu badala ya kutumia nguvu nyingi….(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache naunga mkono hoja hii, nashukuru sana. Natambua kwamba mwakani Wizara itafanya mambo makubwa sana katika Wilaya yangu. Ahsante sana. (Makofi)