Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii niweze kutoa mchango wangu kwenye sekta hii muhimu ya Kilimo. Ndugu yangu Mheshimiwa Bashe, nikupongeze umetoa hotuba nzuri ya bajeti ya kilimo na mwelekeo kwa ajili ya bajeti inayogusa watanzania walio wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa namna ambavyo amekuwa akitupia jicho kwenye Wizara hii. Kwa kweli kwa jinsi tulivyokuwa tukipitia bajeti ya Kilimo kwa miaka ya nyuma na kuanzia mwaka 2022/2023 wa bajeti Mheshimiwa Bashe, huna kisingizio chochote, imebaki tu sisi kukupigia kelele Wizara ya Fedha ikuletee fedha na mwaka huu pia naona bajeti imeongezeka kwa asilimia hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nikupongeze ulifanya ziara ndani ya Mkoa wa Rukwa na hususani ndani ya Jimbo langu la Kwela, kwa mara mbili mfululizo. Leo, nilijua unakuja ku–table bajeti yako hapa, kuna mambo uliahidi kule jimboni katika ziara zako zote mbili. Kwa hiyo, nilitumia wikiendi hii kufanya ziara maeneo yale uliyoahidi ndani ya Jimbo la Kwela. Nikupongeze kweli mambo yote uliyoniahidi, uliahidi utaanza upembuzi yakinifu kwenye scheme 11 ndani ya zaidi ya kata 20 ndani ya Jimbo la Kwela, ambazo ni hekta 67,800. Nimekwenda jana nimezungukia Kote nikakuta Vijana wako wapo site. Nakushukuru Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili, ulituahidi Mkandarasi kuanza kazi Scheme ya Ilemba bilioni 21. Tayari tarehe 18 nimekuta anafanya mobilization, nimekwenda nikaongea nae tumekubaliana tarehe 18 Mei,2023 itakuwa ni official launch ya mradi wa scheme ya bilioni 21 pale Ilemba. Hilo Mheshimiwa Waziri, nakushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia kwenye suala la mbolea lakini nataka nizungumzie mambo ya financing model kwenye sekta ya kilimo. Nimeona Waheshimiwa wengi wanaongelea mambo ya Tanzania Agricultural Development Bank lakini ngoja nianze na suala la mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumpongeze Mheshimiwa Rais, kwa kutoa ruzuku kwenye hii sekta ya mbolea, lakini mbolea ilikuwa na changamoto kubwa sana hii mbolea ya ruzuku. Nadhani ni kwa sababu ya maandalizi yalikuwa hafifu. Kwenye Mkoa wetu wa Rukwa, kwanza registration tu wakulima ili waweze ku–qualify kupewe mbolea ya ruzuku, ulikuwa ni mchakato wenye shida kubwa sana. Ulichukua muda mrefu na ilifanyika mwisho mwezi wa 11 mvua zimeanza kunyesha na wakala, kwa mfano ndani ya Jimbo langu la Kwela, tulikuwa na wakala mmoja tu wa ku–supply mbolea kwa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe wito, sasa tuko mapema tunakwenda kukupitishia bajeti yako, naomba ufanye approval na kufanya vetting ya mawakala walau karibia kila kata. Kata zangu ziko 21 tuwe na wakala wakuwa–supply wakulima mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo muhimu sana Mheshimiwa Bashe. La sivyo, jimbo langu liko so controversial, wewe unalijua umezunguka kule bondeni, kufika Makao Makuu ya Halmashauri Lahela unasafiri zaidi ya kilomita 250. Kwa hiyo, huyu mkulima kwenda kufuata mbolea Lahela, inamgharimu zaidi ya 70,000 na kuendelea. Kwa hiyo, nikuombe tuweke center kila kata ndani ya Jimbo la Kwela, ili wananchi waweze kupata mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia suala la mbegu, kuna mbegu ambazo zimekuwa user friend kwa wakulima ndani ya jimbo langu. Kwa mfano; zao la mahindi tumekuwa tunalima Seed Co 647, Chapa Tembo na Pannar 715 ndio mbegu ambazo wakulima wamezizoea. Sisi TOSC ambao wana certify mbegu hawajatoa kibali kwenye hizi mbegu. Kwa hiyo, wakulima wamekuwa wakitegemea kutoka Zambia. Hiyo sasa imepelekea kuwe na magendo. Smuggling ni kubwa kwenye mipaka, tunachukua mbegu hiyo Zambia na baade tunanufaisha nchi jirani wakati ni jambo dogo sio rocket science.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbegu ambazo tunajua zinawafaa wakulima tunategema nchi jirani. Kwa kweli Mheshimiwa Bashe, kwa umakini wako hii hapana ni aibu kubwa sana. Nikuombe sana hili lifanyie research hizi mbegu zinazokubali za mahindi, zinazotoa uzalishaji mkubwa wa mazao tukazifanyie utafiti, TOSC isiwe na ukiritimba i–certify hizo mbegu wakulima waweze kuwa–supplied mbegu ndani ya Mkoa wa Rukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la mikopo na hiyo ndio Financing mode ya sekta ya kilimo ndani ya nchi hii ina changamoto kubwa. Nakubaliana, kwenye Mkoa wa Rukwa, wakulima walikwenda kuomba mikopo kwenye benki CRDB, NMB na benki zote hizi, walipofika pale wao walitoa masharti kwamba tunakopesha zao la ngano, mahindi hatukopeshi. Hata hivyo, nakubalaiana nao na sababu yao kubwa ni kwamba flexibility yaani sera zetu zimekuwa zikiyumba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wakulima wa alizeti walikuwa wanakopesheka kwa miaka minne mitano iliyopita lakini leo hii hakuna benki itakayotoa mkopo kwenye zao la alizeti kwa sababu limeanguka, haliwezi kulipa. Kwa hiyo, benki zimekuwa ziki–divert, zinakuwa zina-hesitate kutoa mikopo kwenye mazao haya. Mahindi wana–hesitate, miaka minne nyuma ilikuwa zao la mahindi halitabiriki. kwa hiyo, mkulima wa mahindi hakopesheki. Serikali mnaisaidiaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wameongelea Benki ya kilimo iwe na tawi kila Mkoa, ile kwanza sio commercial bank, ni development bank ambayo kwa nature ya benki ilivyo sio ya kuwa na tawi kila Mkoa, wilaya wala kila kata. Ni benki ambayo inatakiwa ifanye kazi na mawakala na hilo mmelifanya. Benki ya Kilimo inafanya kazi na CRDB, NMB, TCB shida ni kwamba benki iko undercapitalized. Ina mtaji wa bilioni 267 kwenda 300 lakini mtaji unaohitajika ni trilioni moja. Sasa, trilioni moja mna deficit ya bilioni 700. Pia, Waziri wa Fedha uko hapa, pelekeni bilioni 700 halafu mpeleke kwenye hizi commercial bank ambazo ni mawakala wetu ili wakopeshe wakulima. Hatuhitaji kuwa na physical buildings za mabenki kwenye kila kata ama kila wilaya, tunahitaji fedha zipelekwe wakulima wapate mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tunajua kwamba mna–hesitate kuwapa fedha kwenye mfuko mkubwa wa hazina, sawa tuna vipaumbele vingi, basi wapeni approval. Kuna financing kwenye multination financial institution kama World Bank, African Development Bank, BADEA, wako ladhi kukopesha benki zetu ku–boost mitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazuia kwa sababu tunasema tunakwenda kukuza deni la Taifa. Basi deni la Taifa likue kwenye kukuza kilimo kwa sababu hizi hela zinaenda ku–boost kilimo. Kwa hiyo, Waziri wa Fedha na Waziri wa Kilimo, hili jambo ni la kwenu nendeni mkai–boost Tanzania Agricultural Development Bank la sivyo Waheshimiwa Wabunge, mtapiga kele miaka mingi. Kwa mtaji wa bilioni 268 namshukuru Mama Samia, aliyoongeza kwa miaka mingi benki ilikuwa haipewi mtaji. Kwa hili tumpongeze Mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jinsi tunavyokwenda, portfolio ile unaijua Mheshimiwa Bashe, ni ya wakulima wakubwa wachache Bagamoyo Sugar na wachache hawafiki 20 portfolio yote ya Benki ya Kilimo imekwisha. Mkulima mdogo kamwe hatokuja ku–access mkopo wowote kwenye benki yetu ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sasa twende kama tumedhamiria. Haiwezekani uende Tume ya umwagiliaji ukachukua financing moja kwa moja. Kwa nini usipitishie kwenye benki ya Kilimo halafu ili tuweze kukuza balance sheet ya benki ile iweze kukopesheka na mabenki makubwa ya kimataifa na tuikuze iwe ni benki ambayo ni potential itakayokuza sekta ya kilimo ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Bashe nakwambia na haya yote unayajua ndio maana tumesema kwa uwazi na Waziri wa Fedha yupo humu ndani na wewe umo, msaidieni Waziri tukai–boost ile benki, ikifanya vizuri wala hatuhitaji kuwa na physical branches. Wakala tu wa benki kama CRDB, TCB, NMB wana ma–branch nchi nzima. Wanahitaji window zile zifanye kazi isiwe tu ni mapambo ambayo tunawambia wakulima benki ya kilimo, model hivi, no, no. Twendeni tukawe serious, tukakuze kilimo cha Watanzania ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)