Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii adhimu kabisa kwa ajili ya kutoa mchango wangu muhimu katika Wizara hii ya Kilimo ambayo ndio maisha ya watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake, kwa kazi nzuri wanayoifanya, wanalengo na nia nzuri ya dhati na very serious kwa ajili ya kukomboa na kuleta revolution, kuleta mageuzi, mapinduzi ya dhati ya kilimo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu baadae utanipigia kengele kwa sababu nina mambo mengi ya kusema hapa. Sasa nataka nitoe sababu za kwa nini nataka kuunga mkono bajeti ya Wizara hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Singida Kaskazini, sababu yetu ya kwanza ya kuunga mkono bajeti hii, ni ruzuku ya mbegu ambayo tumepata latika jimbo langu. Tulipata tani 67,000 na wananchi wametumia mbegu ya alizeti iliyo bora na mwaka huu mavuno yatakuwa mengi kuliko miaka yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata ruzuku ya mbolea ambayo katika jimbo langu tumepata tani 239. Pia tukapata pikipiki 13 za Maafisa ugani kwenye kila kata, kata13 out of 21. Hii ni sababu moja wapo kubwa ya sisi kuunga mkono hoja hii. Pia, pikipiki zile kwa Maafisa Ugani zilikuja pamoja na vitendea kazi vingine ambavyo vilisaidia kupima afya ya udongo n.k.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine kubwa la muhimu katika wilaya yangu kwa nini tunaunga mkono hoja hii, nina miradi mikubwa miwili ya umwagiliaji katika Jimbo la Singida Kaskazini. Mradi wa Musange na Mradi wa Mohamo, ambayo katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, imeonekana katika ukurasa wa 228. Nashukuru hotuba ya Mheshimiwa Wizari, nimeipitia vizuri, nimeona amevitaja katika ukurasa wa 228 kwamba kazi inakwenda kukamilika na wanachi wataanza kunufaika. Kazi ya upembuzi yakinifu inakwenda kukamilika na mabwawa yale yanategemea kuanzia mwaka 2023 sasa yatakwenda kuanza kazi. Hizi ni sababu kuu nne za kuja kusema hapa kwa niaba ya wananchi wa Singida Kaskazini, kwa nini tunaunga Mkono bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kidogo kutoa maoni ama mapendekezo na changamoto ambazo zipo kwenye eneo hili. Kwanza, kwenye mbolea. Mheshimiwa Waziri, ile mbolea naomba wafanye packaging ya kuanzia kilo tano, kumi, ishirini hadi hamsini ili na wakulima wadogo nao wanufaike. Kwa sababu tunapoweka ile packaging kubwa inawalenga wakulima wakubwa tu lakini wale wakulma wadogo wadogo wa bustani na nini wanakosa fursa hii. Hivyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri, alichukue hili na alifanyie kazi mwakani tumletee majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa mbolea na mbegu ninaomba vile vituo vya kugawa hizi mbegu visiwe tu sehemu moja, viende mpaka kwenye kata zetu, viwafikie wananchi kuwapunguzia gharama na usumbufu mwingine usiokuwa wa lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la muhimu ni kwenye hizi irrigation schemes. Kwenye Jimbo langu la Singida Kaskazini, tunayo maeneo mengine ambayo ni ya muhimu yana maji na ni mazuri kwa kilimo. Ninamshukuru Mheshimiwa Waziri, nilipouliza swali langu hivi karibuni katika Bunge hili, kwenye eneo la Mradi wa Mgori tayari Maafisa wa Wizara ya umwagiliaji wamekwisha fika ninampongeza na ninashukuru sana kwa hatua hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kweli wakati wa utambulishpo pale asubuhi, nimeona wanatambulishwa Maprofesa, ni kweli nimeona these people are serious na kweli ni wasikivu na wanatekeleza kile wanachoahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, bado kuna maeneo mengine ya maji katika jimbo langu ambayo yanahitaji scheme kama hizi. Kuna Bwa la Kisisi, Bwawa la Masogweda, kuna Bwawa la Ntambuko, kuna Bwawa la Mikuyu maeneo haya tunaomba Mheshimiwa Waziri, uyachukue tena hawa ni jirani zako, Nzega na Singida Kaskazini ni majirani na ni ndugu. Nikuombe na maeneo haya uyatazame tupate miradi katika maeneo haya ili na wenyewe wanufaike na kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni eneo la bei ya alizeti. Alizeti imelimwa sana mwaka huu kwa sababu ya hamasa nzuri ya Waziri na hata Waziri Mkuu alipokuja Singida, lakini cha ajabu na cha kusikitisha leo hii bei ya alizeti imeshuka. Leo hii bei ya gunia la alizeti ni 30,000, 40,000, kilo moja shilingi 600.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuhakikishia nataka nikuambie hapa leo, sasa hivi wakulima wataenda kuihama alizeti, watahamia mazao mengine kwa sababu ya changamoto ya bei. Bei ya alizeti ni mbaya, wananchi wanaomba tuache kuagiza mafuta kutoka nje. Kama tumeshindwa kuacha kuagiza basi tuweke kodi, tuweke VAT ili mafuta yale yanapoingia yasiwe na fursa kubwa kuliko mazao tunayozalisha sisi hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumeitikia wito, tumeitikia agenda hii ya kuhakikisha alizeti inatoa mafuta na tunazalisha mafuta katika nchi yetu lakini tunaomba mtupokee msituache peke yetu tuanze kuteseka. Lakini hilo la masoko na bei liende hata kwenye eneo la kitunguu. Sisi Mkoa wa Singida tunalima sana Kitunguu, ndio uti wa mgongo wa maisha ya watu wa Singida. Shida inakwenda kwenye mnyororo ule wa soko, kuna msemaji amezungumza hapa kuhusu tatizo la madalali. Kuna madalali, sijui kuna ushuru, sijui kuna vitu gani, vitu vingi, bei yenyewe hamna, gharama ni kubwa, tumuokoe mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jimbo langu tuna eneo zuri kwa ajili ya kujenga soko pale njia panda ya Merya. Mheshimiwa Waziri, ninaomba na Serikali inanisikia katika hili, sio tu Waziri wa kilimo, Serikali inisikie kuanzia TAMISEMI, Viwanda na Biashara, njooni mtujengee soko pale kwa ajili ya kuhakikisha Mkoa wa Singida tunaendelea kuimarisha na kuboresha kipato cha nchi yetu katika eneo la zao la Kitunguu ambalo zao hili kwa Singida ni zao la Kimataifa. Kwa sababu Singida wanakuja watu kutoka Kenya, Uganda, Ethiopia, Sudani mpaka Rwanda wanakuja Singida kwa ajili ya kufuata kitunguu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Waziri pamoja Serikali kwa ujumla walichukue hili. Tuboresheeni yale mazingira ya uuzaji na ufanyaji wa biashara katika zao hili la kitunguu. Lakini eneo hilo hilo bado tatizo la rumbesa lipo, tuendelee kuikomesha tatizo la rumbesa ya kitunguu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni eneo la matreka, niombe sana tu–modernize kilimo chetu. Ni kweli kabisa wananchi sasa wameitikia kulima na wako tayari kufanya kazi. Shida kubwa tunayokutana nayo ni mazingira, hivi tutalima kwa mkono mpaka lini? Hebu tuhurumieni, niombe sana pembejeo za kilimo hasa matrekta tuyalete vijijini na yawe na masharti nafuu wananchi waweze kukopa. Mwenyewe nilienda hapo Mfuko wa pembejeo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Abeid, ahsante sana. Malizia muda wako umekwisha.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana mengine mengi nitawasilisha kwa njia ya maandishi. Ninaunga mkono hoja, Waziri achape kazi tunaimani nae. Ahsante sana. (Makofi)