Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuisimamia vizuri Wizara hii na kuhakikisha kwamba inapata fedha za kutosha ili kuendeleza uchumi wa nchi hii unaotokana na kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Mheshimiwa Antony Mavunde; Katibu Mkuu, Gerard na Naibu Katibu Mkuu Hussein Mohamed kwa kazi nzuri na timu nzima ya Wizara wanayoifanya katika Wizara hii. Naomba ni-quote aya ya 29 ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri leo ambayo inasema, “Taifa lolote ambalo liko huru, lenye kulinda heshima na utu wa watu wake ni lile ambalo linajitosheleza kwa chakula na uchumi imara. Ili uwe na uhakika wa chakula ni lazima kuimarisha uzalishaji, tija na kuwa na umiliki wa mbegu zetu, kwani atakayetawala dunia hii, ni yule ambaye ana umiliki wa mbegu bora na utoshelevu wa chakula. Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kwa hali ya mtetereko wa uchumi duniani ilivyo sasa hivi, uzalishaji wa chakula cha kutosha na mazao ya biashara ya kutosha ni nyenzo muhimu sana kwa mustakabali wa nchi yetu na uchumi wake. Tumeshuhudia hapa Waheshimiwa Wabunge wengi wamekuwa wakimshukuru Waziri na Wizara kwa kuwapelekea chakula kwenye maeneo yao yale ambayo yalikuwa na upungufu wa chakula. Kama tusingekuwa tumejitosheleza kwa chakula, hasa mahindi, tungebabaika sana na uchumi wetu ungeyumba sana. Kwa hiyo, naipongeza sana Wizara hii, napongeza sana kwa utaratibu wenu mnaousimamia na kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa na chakula cha kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nirudi kwenye eneo la mazao. Nitaanza na zao la soya. Tanzania tunakadiria kwamba tuna mahitaji ya soya zaidi ya tani 250,000 kwa mwaka, kwani kuna mahitaji mengi ambayo yanahitajika kwa ajili ya chakula, lishe bora lakini pia kwa ajili ya kutengeneza chakula cha mifugo. Vile vile tuna upungufu mkubwa wa uzalishaji wa soya nchini. Kuna makampuni pia yanayotengeneza vyakula vya binadamu, yanahitaji soya hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nchi ya wenzetu ya Zambia, takwimu zinaonesha kwamba wanazalisjha kati ya tani laki tatu na nusu mpaka tani laki nne kwa mwaka na inaongoza kwa uzalishaji kusini mwa Bara la Afrika ikifuatiwa na Malawi ambao wanazalisha tani 250,000. Sisi tunakadiriwa, na haifiki tani 20,000 kwa mwaka, na asilimia 50 mpaka 70 ya Soya hii inazalishwa Jimbo la Namtumbo. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri, sisi tuna uhitaji wa hizo tani 250,000 ndani, lakini tuna trade agreement ya Soya na China ambayo inahitaji zaidi ya 500,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, naiomba sana Wizara na timu ya Wizara ya Kilimo tushirikiane kuweka mkakati wa kulisimamia zao hili kwa karibu, uzalishaji wake, uzalishaji wa mbegu, utalaam katika kulima, uvunaji, uhifadhi, masoko yake pia yawe huru na ya ushindani ili kuwapa nguvu wakulima na kuongeza uzalishaji. Pia tuwe na viwanda ambavyo vitakuwa vinasafisha na ku-standardize quality kwa ajili ya kuuza nje hiyo soya. Tulisikia juzi Balozi wetu wa China alikuwa akilalamika kwa baadhi ya wanaopeleka soya China, walipeleka Soya chafu. Hii inaweza ikafanya tukaondolewa kwenye soko kama hatuangalii quality ya mazao yetu. Kwa hiyo, nilitaka kuanza na hilo la soya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni tumbaku. Msimu huu tumbaku tunakwenda vizuri. Nasi tunaishukuru sana Wizara kwa usimamizi mzuri chini ya Mheshimiwa Bashe. Pia tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu alilisimamia sana zao hili na kujenga confidence kwa makampuni kurudi. Kwetu Namtumbo tulikuwa tunazalisha tani 500, lakini leo tuna mkataba wa tani 9,600 ambao ni mkataba mkubwa sana wa uzalishaji wa tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu kwenye hili, naungana na wenzangu, kwamba hawa Classifier, wateuzi wa tumbaku wawezeshwe waende wafike kwa wakati ili zao hili lisitumie muda mrefu kuuzwa sokoni, kwa sababu hawa ndio wateuzi wa tumbaku, sasa lazima wawezeshwe, wawe na usafiri wa kutosha, gharama zao; Wizara na Serikali ihakikishe inafanya zoezi la biashara hii au soko hili, likamilike kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naungana na wenzangu, mbolea hii 101824NPK ambayo inatumika kwa wingi kwenye tumbaku ya mvuke na tumbaku ya hewa, tunaomba sana msimu wa mwakani 2024 basi iingizwe kwenye ruzuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wengi wanolima tumbaku ya mvuke na tumbaku ya hewa wanatumia mbolea hii. Kwa hiyo, tunaomba sana hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuwa sisi nchi yetu Mungu ametujalia. Narudia kusema hili, kijiografia sisi kule Namtumbo kiasili ni wakulima na wahifadhi. Sisi haya mahindi ambayo yamechukuliwa na yakahifadhiwa na tumewagawia wenzetu, asilimia fulani yametoka Namtumbo na Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana, tunachoomba sisi, ili maeneo haya ya kilimo yasiingiliane na mifugo, narudia tena yasiingiliane na mifugo. Leo hii sisi mifugo imekuja bila hata taarifa, bila vibali, hii leo naomba nirudie pia ni-quote hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ambayo aya ya 30 ilisema; “Tathimini ya kina ya hali ya chakula na lishe imebaini kuwa upungufu wa uzalishaji katika baadhi ya maeneo kwa msimu wa 2021/2022, ulitokana na athari ya mabadiliko ya tabia ya nchi.” Nasema sio tabia ya nchi tu na pia mabadiliko ya tabia ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nchi yetu ilikuwa ina maeneo ya watu wafugaji, maeneo ya kilimo, maeneo ya uvuvi, maeneo ya uzalishaji wa dhahau n.k. Sisi Kusini ni wazalishaji wa kilimo. Leo hii huku maeneo haya ya mifugo mvua zinachenga, leo ndio tunachukua chakula tunawapelekea lakini sasa leo hii wanatuletea mifugo sisi, leo hii mtu ana mifugo 1000, 2000, akiingia kwenye shamba la mtu lote limekwisha mara moja. Halafu, mbaya zaidi wamekuja kama wako vitani na sasa wanatuambia sisi kule sio watanzania. Wamefika wanasema kauli ninyi sio watanzania, sisi ndio Watanzania, kwenu Msumbiji, sisi tuna haki ya kuishi hapa, wanaingiza ng’ombe kwenye mashamba ya watu. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Vita, malizia mchango wako muda umekwisha.

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kero kubwa sana kwetu. Naunga mkono hoja lakini hili suala la mifugo na wakulima tunaomba Mheshimiwa Bashe, mshirikiane Serikalini muone jinsi gani ya kuacha aneo hili kilimo liweze kutumika kwa kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.