Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami nichangie mawili, matatu kwenye hii Wizara ambayo inawagusa Watanzania walio wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nikichangia katika hii Wizara, taarifa na randama na hotuba inaeleza kwamba kilimo kimeshuka toka mwaka 2021 kuja 2022. Mwaka 2021 inaonesha kilimo kilikua kwa asilimia 4.9, leo tunaongelea asilimia 3.9. Vivyo hivyo, kilimo kimeshuka kwa namna ambavyo kimekuwa kikichangia katika Pato la Taifa, kutoka asilimia 27 kuja asilimia 26.3 hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini naongelea haya, unavyoongelea kilimo kushuka maana yake unaathiri sekta ya watu wengi ambayo ameeleza Waziri kwamba ni asilimia 65 wanategemea kilimo. Kilimo kikishuka tunaongelea umaskini, kwamba watu wengi waliokuwa wanategemea kilimo katika kujikomboa katika maisha yao ya kawaida tayari maisha yao yameshapata shaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hiyo tu, kilimo kinavyoshuka kwa sababu kilimo ni mnyororo wa thamani, kilimo kinagusa viwanda, kinagusa sekta mbalimbali za usafirishaji na kwingine, lakini unavyoona kilimo kinashuka ina maana kinakuwa na negative impact kwenye uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyoongelea kilimo, Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali amesema katika eneo dogo tu la uzalishaji wa viwanda vya alizeti, anasema kwamba kati ya viwanda 12 vilivyokuwepo, viwanda vitano vimefungwa. Katika viwanda ambavyo vimebaki kati ya hivyo 12 vinategemea ku-import product kwa asilimia 75. Kwa hiyo, unaona kwamba kilimo kushuka kinakuwa na negative impact ya kwenye uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hiyo tu, Serikali inatumia zaidi ya shilingi bilioni 450 kwa ajili ya kuagiza bidhaa za mafuta kutoka nje. Sasa hiyo tayari inakuwa na multiplier effect kwenye uchumi wa nchi yetu. Sasa ni kwa nini, tunawezaje kuendelea kuongelea changamoto ya kilimo kwa miaka zaidi ya 60 ya uhuru. Ameeleza Waziri hapa, anasema kama nchi tuna ardhi ambayo inafaa kwa kilimo zaidi ya ekari milioni 44, lakini huyohuyo akasema ni ekari milioni 10 tu ambazo zimetumika kwa ajili ya kilimo. Ni takwimu ambazo siyo tu zinakera lakini haziwatendei haki wananchi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyoeleza hapa kuna vinchi vidogovidogo kama Uganda na Rwanda ambavyo bado vinafanya vizuri, licha ya kuwa na ardhi ndogo bado wanaweza kuzalisha vizuri. Swali nauliza, je, Waheshimiwa Mawaziri tunakwama wapi? Hilo ndilo tunapaswa tujiulize. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunakuja na hoja za mbolea, lakini tunaweza kuongelea viwanda vya mbolea miaka 60 baada ya uhuru? Tunakuja na hoja za vita ya Ukraine na Russia, tunapaswa kuongelea hivyo vitu miaka 60 baada ya uhuru? Nadhani kuna kitu hakiko sawa na tukijipanga vizuri tutaweza kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia fedha tu inayotumika kwa ajili ya kuagiza bidhaa za chakula, mmeeleza ngano, sisi hatuzalishi ngano, tunazalisha ngano kidogo, mnatumia US Dollars zaidi ya milioni 221 kuagiza ngano nje badala ya kuwasaidia wakulima wetu tukiwa na ardhi ya kutosha wakazalisha ngano nchini tuka-save hizo US Dollars, tukaweza kuendeleza viwanda au maeneo mengine katika nchi yetu. Kwa hiyo, hapo ni dhahiri kwamba tunakwama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mmeeleza bayana kwamba kushuka kwa kilimo bado kumekuwa na impact katika uzalishaji. Mmeeleza hivi, katika mwaka uliopita tulizalisha tani milioni 18, kwa mwaka huu unaoisha tumezalisha tani milioni 17, ambapo hapa ukihesabu unaona surplus ni tani milioni mbili. Ukiangalia tani milioni mbili tunaweza ku-export wapi tani milioni mbili? Tunaweza kuingiza fedha za kigeni kiasi gani za kigeni kutoka kwenye kilimo tukiwa na tani milioni mbili tu? Kuna kitu hakiko sawa. Tuna ardhi ya kutosha, tuna vijana wenye nguvu, tuna masoko yametuzunguka, tuna nchi nyingi ambazo zinahitaji chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliongelea juzi kwamba sisi ni signatory wa Biashara Huru ya Bara la Afrika, tunaenda kufanya nini kama hatujajipanga vizuri kwenye kilimo na tuka- capture na ku-export tukapata fedha za kigeni? Hapo tunalo jambo la kujiuliza na tunapaswa kutoa majibu, Waheshimiwa Mawaziri mmepewa dhamana tuisaidie Serikali tuweze kufikia malengo ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mwingine. Mmeeleza kwamba kwenye maghala sasa tuna-reserve ya tani 159,000 kama sikosei, lakini ukiangalia tani hizo sisi matumizi yetu kwa mwaka kama nchi tumesema ni tani milioni 15. Ukichukua hiyo milioni 15 ukagawa kwa miezi 12 unapata kwa mwezi nchi inatumia chakula ambacho ni tani milioni moja kama na laki mbili na nusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua kwa mwezi ukagawa kwa siku unakuta ni tani 41,000 kwa siku. Kwa hiyo, ukichukua zile tani mlizoziweka kwenye reserve ambazo ni tani 159,000 unakuta tuna chakula cha siku tatu tu kuisaidia hii nchi. Yaani kukitokea kama yaliyoikuta Ukraine na Russia, Serikali kwenye National Reserve watu wa nchi hii wata- survive kwa siku tatu tu, itakuwa ni crisis! Kwa hiyo, tuna safari ya kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo kama hamnunui mazao kuna wananchi wetu wa Kagera. Niliwahi kukwambia Mheshimiwa Waziri, kwamba sisi Kagera, Kyerwa, Karagwe, tunazalisha mahindi. Mahindi kwetu ni kilimo cha biashara. Ukifika wakati wa kuuza mnatuambia tusiuze, lakini ninyi ambao mnapaswa kununua mazao tena kwa bei ya soko, hamnunui. Kwa hiyo wananchi wanabaki kuwa stranded bila kujua cha kufanya. Do you think mnatutendea haki ninyi Mawaziri vijana? Tunakwama wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninalotaka kuongelea ni kilimo cha kahawa. Bado Mkoa wa Kagera tuna changamoto licha ya kuwa leo tumeweza kufanya minada na tunamshukuru Mungu bei ilipanda, tuna changamoto ya mnyauko. Mnyauko uko kwenye kahawa zinaendelea kuharibika tunataka solution.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna changamoto ya mnyauko kwenye migomba (ndizi). Hiyo ni crisis. Leo sisi tunakula ugali kama Wasukuma, siyo sawa. Tunataka majibu ya changamoto ya mnyauko kwenye Mkoa wa Kagera. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeeleza kwamba tunahitaji mbegu za kutosha, miche mipya. Tumekuwa tukilima kwa asili ambayo ni ile miti mikubwa. Tunataka mbegu za kisasa. Nimesoma kwenye takwimu, nikaona hamjatutendea haki, sisi ni wakulima wakubwa wa robusta lakini kwa miche mliyoonesha hapa, licha ya kwamba Mkoa wetu na mikoa mingine inayozalisha robusta ina asilimia kubwa, zaidi ya 40, sisi tumepata miche michache sana, it’s not fair. Nadhani usiwe mkakati mdogo mdogo wa kupunguza nguvu ya robusta kwenye soko please! Tunaomba tupewe miche ya kutosha tuweze ku-compete.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikimaliza bila kuongelea masoko ya kibiashara ya Mrongo na Nkwenda sitawatendea haki wananchi wangu wa Kyerwa. Ninataka majibu, kwanza ni fedha kiasi gani ilitumika kujenga yale masoko ambayo mwisho yalitelekezwa, pia sababu ya kuyaanzisha yale masoko ambayo kimkakati yalikuwa mpakani kutusaidia tufanye biashara ya ndizi na kahawa. Je, walioweka huo mkakati walikosea? Kama hawakukosea, sisi tunalima ndizi, ndizi zetu leo zinakuwa smuggled kwenda Uganda, na zinajikuta ziko Marekani na kwingine, kwa nini sisi tusifanye hiyo biashara? (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Anatropia.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa soko la vanila. Tunaomba mtupe jibu la soko la vanila kwa sababu tupo stranded. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana, muda wako umeisha, nakushukuru sana Mheshimiwa Anatropia.