Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Aloyce Andrew Kwezi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini mbili nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutupa heshima kubwa sana ya kutuletea tunu ya Waziri mchapakazi, Waziri mwadilifu, Waziri mbunifu Bwana Bashe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Wizara hii, lakini nisije nikasahau naanza kujenga hoja yangu moja kwa kuhakikisha nasema naunga mkono hoja kwenye Wizara hii asilimia 100. Na pengine niwaombe Wabunge wenzangu dada yangu Mheshimiwa Esther alikwa hapa ametoka kidogo lakini Wabunge wenzangu ambao walikuwa wanawazia hata kuweka shilingi wasiweke mabadiliko ni makubwa sana. Mheshimiwa Waziri ahsante sana, tunakupongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo masuala machache tu ambayo yamenifanya nipongeze, kwanza nimeanza kwa kumpongeza, kwa sababu zao la tumbaku katika Mkoa wetu wa Tabora ndiyo siri kubwa ya uchumi. Zao la tumbaku katika nchi yetu ndiyo zao la pili ambalo linachangia fedha za kigeni baada ya kahawa na nina uhakika kuanzia mwaka huu kwa mauzo yanayondelea na baada ya Mheshimiwa Bashe kuondoa ukomo wa wakulima kuwapangia azalishe kiasi gani cha tumbaku, sasa nina uhakika tumbaku inakwenda kupikwa hata kahawa saa nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mchango wa tumbaku kwenye fedha za kigeni unakwenda kuwa mkubwa sana zaidi hata ya hizi dola ambazo tumeona hapa milioni 154. Kwenye tumbaku nilikuwa na ushauri makampuni mengi yamejitokeza kununua tumbaku na kwa mara ya kwanza nasema kabisa tumbaku kuna soko linaendelea katika Kata ya Kazarole Wi lakini tumbaku tunaongea mpaka inafika dola tatu na kampuni ambazo zimefanya vizuri lazima nizitaje hapa kwa sababu nitakuwa kama Mbunge sijawatendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni imefanya vizuri ni Kampuni ya Mkwawa, Kampuni wa Wodika ya Zimbabwe ile na kampuni ya tatu ni Kampuni ya GTI. Hawa wamejitahidi kwakweli sijaona tumbaku mpaka sasa hivi ambayo kwa kampuni hizi zinanunuliwa chini ya dola moja lakini bado kuna makampuni yananunua hata chini ya dola moja. Nilikuwa ninaomba yajitafakari kwa sababu mambo ni mazuri kwa kampuni nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri, Kaliua pale ndiyo Wilaya inayoongoza sasa hivi kwa kuzalisha tumbaku kwa wingi, kwa sababu Mkoa wa Tabora ndiyo unao zalisha nusu ya tumbaku nchi nzima, lakini katika Mkoa wa Tabora Kaliua ndiyo inayozalisha nusu ya tumbaku katika Mkoa wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna vitu ambavyo nilikuwa najiuliza na ningependa nimshauri hivi ni kwanini tunashindwa kujenga viwanda vya kuchakata eneo kama Kaliua? Nina wazee wangu nilikaa nao siku moja wakanishauri, Mzee Kisamfu lazima nifikishe salamu zake hapa. Mzee Kisamfu akaniambia mwanangu Kwezi unashindwaje kumshauri Waziri? Unashindwaje kuishauri Serikali? Sasa hawa wazee wote, nimekutana na Kachala, nimekutana na mzee Mwaisame, nimekutana na nani? Wanataka kiwanda angalau cha kuchakata kijengwe Kaliua pale ni junction tuna miundombinu, reli ziko safi kwa maana ya kwenda Mpanda, kwenda Kigoma na kuja huku Dar es salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani kila siku tukaweka center moja tu ya Morogoro. Kwa hiyo, nilikuwa naomba uongee na wawekezaji hawa ili waone namna ya kuanza kujenga huko na nimesikitika nikaona Mkwawa ameisha karabati kule, kukarabati ya nini si angekuja tu Kaliua pale maji Mama analeta, umeme unajengwa hivi shida ni nini? Kwa hiyo, nilikuwa nakushawishi hivyo hili malighafi zinatoka pale Kaliua vijana wanahitaji ajira. Wakipata ajira wananchi wa Kaliua nao ni sehemu ya Tanzania lazima tujenge tuepuke zile zana za kusafirishwa mara gari imepata ajali tumbaku imekuaje hayo yote hayatakiwi sisi utatoa pale sokoni unakwenda hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri jambo la pili ambalo ningeliongelea ni mbolea, nikushauri kwa Mwaka huu ile mbole ya kupandia huwa inawahi sana mwezi wa nane imeishafika ni kwanini mbolea ile ya mazao mengine isifike mwezi wa nane huo huo? Kwa sababu hakuna tunacho chelewa na tuna muda wa kujipanda nikuombe ujipange kwa mwaka huu tusipate ile adha ya kuchelewa mbolea na uangalie vile vituo pia vya wale mawakala wakave zile kata zote. Kata zetu ziko scattered kutoka Jimbo la Ulyankulu kule mpakani mwa Ushetu kwa Mheshimiwa Cherehani mpaka ukafika Ukumbi Kabuko ni kilometa 271 wilaya moja sasa unaweza ukangalia ukiweka hivyo kuna sehemu zina tuathiri. Kwa hiyo, nilikuwa naomba la mbolea kwanza, zije kwa wakati alafu zije kwa maana ya kutosheleza vituo vyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ningependa kushauri na hili nimefurahi ni kweli kabisa kuiweza Wizara hii ni kwa sababu wewe wamekwambia Mnyamwezi na Mgogo mtani wetu huyo anakusaidia na ni mzuri kweli kweli. Kwa hiyo, sina wasiwasi mnatosha kwa sababu mngekuwa hamtoshi kwa kweli leo ningeweza kushika shilingi lakini nashawishika kuwashawishi hata Wabunge wengine ondoeni shilingi twende kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri jambo la umwagiliaji ndiyo nilitaka nishauri kwenye hotuba yako nimeona umeandika Uyui alafu ukaandika Igwisi lile Bwawa la Igwisi liko Kaliua. Kwa hiyo, nilikuwa naomba mrekebishe hapo, alafu tulikuwa na maombi maeneo matatu kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji sisi kule mvua ni ya msimu mmoja tunataka angalau kipindi cha kiangazi yale maji tuvune kwa maana ya Zugi Mlole nilikuomba tuwe na bwawa pale pamoja na mradi wa umwagiliaji mzuri lakini nikakuomba Igwisi, nikakuomba Ugunga. Igwisi nimeiona imengia sasa haya maeneo mawili ndiyo nilikuwa naomba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, nilikuwa naomba haya maghala sasa. Kwenye maghala ningeomba muwaishe mchakato kwa sababu tenda ilishatangazwa waanze kujenga yaani nimeona ghala zuri sana kwa ndugu yangu na Mwenyekiti wangu Bwana Sillo yuko hapo. Nikajiuliza kiwanda gani? kumbe ni ghala na sisi kwetu maghala yako sehemu tatu nilikuwa naomba na ile wilaya unafahamu ndiyo wilaya inayozalisha mazao kwa wingi katika Mkoa wetu wa Tabora. Ndiyo maana unaona hata own source yetu sisi inategemea mapato ya ndani yote yanategemea mazao. Kwa hiyo, nikuombe mchakato ule wa ujenzi uende kwa kasi ili tuweze kuhakikisha wananchi wa Kiliua wananufaika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ambalo ningeweza kulisema niseme kwamba wakulima hawa, wakulima mwaka huu wamefurahi. Kwa hiyo, kwa logic ya kuwa na fedha wanajitosheleza kwa mwaka huu wanategemea mengi ila sehemu ya magunia ni shida, wanapokopeshwa magunia yanapokuja kurejeshwa yale magunia, umekopa mia yanarudi 30 sasa mnajikuta kuna mzigo unakuwa unaendelea waangalie wale watu wa bodi na wengine ili kuhakikisha tatizo hilo kwa wakulima linakwisha ili mkulima afaidi matunda mazuri sana ya Rais, matunda mazuri ya wewe Waziri wetu mchapakazi tunae kutegemea na timu nzima kwa ajili ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ningependa kuchangia ni hili la mbegu za alizeti na michikichi, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri. Kigoma jiografia yake inafanana na Kaliua ndiyo maana umeona kwanza tulipokea mbegu za michikichi, tulipokea mbegu za alizeti nikuombe sasa mwaka huu zije mapema. Sisi kazi yetu ni kulima na kazi yetu ni kuhamasisha lakini ombi moja tuendelee kuwaelimisha wananchi, kwa sababu sehemu kubwa ya Kaliua na maeneo ya Mkoa wa Tabora wamelima sana tumbaku ili kuhifadhi mazao ya chakula maana yake wanawezakana wakapendezwa na hela wasihifadhi tukarudi kwenye njaa au tukawa na dalili ya kukusumbua hilo ndiyo ningependa kuliomba tulifanye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii wakulima ambao wamekuwa ni mifano leo wamepiga simu wakanipa ushauri wakasema mfikishie salama Mheshimiwa Bashe, nisipowataja hapa nitakuwa sijatenda haki, Mzee Magola, Juma Issa, Mheshimiwa Behewa, Ndezilio, Juma Haji, Kayungilo, Moshi, Sengirunva na Samweli Nyawita hawa wameniambia fikisha salama. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umeisha.

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima zote naunga mkono hoja niwaombe Wabunge wenzangu tuiunge hii Wizara msiweke shilingi toeni shilingi zenu. (Makofi)