Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii jioni ya leo. Kwanza napenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu kwenye sekta hii ya kilimo kwa kuongeza fedha katika bajeti kila mwaka, kuanzia mwaka jana. Fedha zinaongezeka kila bajeti inapokuja. Ninampongeza kwa juhudi mbalimbali anazohamasisha Wizara hii iweze kufanikisha malengo na majukumu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara; Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wake wote kwa mikakati madhubuti waliyojipangia katika kupaisha sekta hii ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona katika bajeti Wizara imejipanga na mikakati madhubuti ya kuhakikisha sasa tunaingia kwenye sekta ya kilimo, kilimo chenye tija, kwa maana ya kwamba kuwekeza katika vitendea kazi kwa Maafisa Ugani, viuatilifu, utafiti pamoja na umwagiliaji. Fedha zikiingizwa kwa wakati, na tukipata fedha nyingine zaidi, kilimo chetu kitakuwa cha hali ya juu na chenye tija kwa manufaa ya mkulima, na kuongeza pato la Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kina utashi na kina hamasa kwa kupata masoko. Masoko ndiyo yanayosababisha kuongeza utashi na hamasa kwa mwananchi na mkulima kulima zaidi, kwa maana atapata tija katika kilimo chake. Kwa hiyo, sasa kilimo kianzie sokoni halafu kije shambani kwa maana ya kwamba masoko ambayo tuna uhakika nayo tuhamasishe wakulima wetu walime zaidi pamoja na mazao mengine ya kujikimu wenyewe yaendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara ya Kilimo, inafanya jitihada kubwa kutafuta masoko ya wakulima. Jitihada hizi zikiungana na Wizara ya Biashara, masoko ya wakulima wetu yatakuwa makubwa zaidi. Masoko siyo ya nje tu, ni pamoja na masoko ya ndani kwa maana ya kuwekeza viwanda kwa ajili ya malighafi za wakulima, kusindika na kuyaongezea thamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo nataka nijikite kwenye kilimo hasa kilimo cha asili. Nimeona kwenye bajeti, kuna mpango wa kuhuisha mbegu zetu za asili na kuzifanya ziwe nyingi zaidi. Mbegu za asili tunajua, zina virutubisho vingi na havina kemikali. Kwa hiyo, kwa mbegu za asili tutapata mazao yenye uhakika pia wa afya zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nahamasisha na kuishauri Wizara iendelee na juhudi hizo za kuwahamasisha wakulima wetu kuweka mbegu zile za wakulima ambazo ni mbegu za asili, tuwaongezee utaalamu, tuwape taaluma ya kuweza kuzalisha mbegu zile zaidi. Usalama wa chakula ni pamoja na usalama wa mbegu. Tukiwa na mbegu zetu, itakapotokea zahama yoyote huko duniani, sisi tuna mbegu zetu na kilimo chetu kitaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo tukiunganisha na umwagiliaji, kilimo kile kitakuwa na tija kwa kutumia kilimo hifadhi na kilimo hai. Kilimo hai kinatumia mbolea zetu za asili kwa maana ya mbolea ya samadi, kwa hiyo, tunazuia udongo wetu na ardhi yetu kuharibiwa, na wataalamu wapo. Tuchukue wataalam hawa na utaalam wao kuongeza kwenye wakulima wetu wa kawaida namna ya kulima kilimo hifadhi na kilimo hai, pamoja na kutumia mbegu zetu za asili. Kilimo hai kinahifadhi ardhi, kinahifadhi udongo na tunapata vyakula vyenye virutubisho ambavyo havijaadhiriwa na kemikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna viwanda vya mbolea ndani ya nchi. Bado kuna haja ya kuongeza viwanda vya mbolea ndani ya nchi na viwanda ambavyo vitakuwa vinamilikiwa na wananchi wa hapa nchini kwa maana ya kudhibiti soko la mbolea kutoka nje, tutauziana hapa wenyewe, na pia mbolea hiyo wazalishe mbolea ambayo inalingana na mahitaji ya udongo wetu na mahitaji ya ndani ya kilimo chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri tuhamasishe viwanda vya mbolea na vikiwemo viwanda vya mbolea vya asili kama hii ya samadi, tuifanyie marekebisho ili iweze kutumika katika ardhi ya kilimo kwa ajili ya kuhifadhi udongo wetu na kuhifadhi ardhi yetu na kuwasaidia wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mbolea ni silaha kubwa kwenye kilimo. Chochote kikitokea duniani kama majanga, maafa, tukiwa na viwanda vyetu ndani ya nchi, vinavyotosheleza wakulima wetu, kutakuwa hatuna tatizo lolote kwa sababu tunao mtaji wetu wa mbolea na mbegu ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuwasaidia wakulima ruzuku ya mbolea. Jihada hizo ziendelee, lakini pia uhamasishaji wa viwanda vyetu vya mbolea vya ndani ya nchi, uendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, napenda kuipongeza Serikali kwa mradi wa BBT uliobuniwa na Wizara ya Kilimo, kwa kweli utakwenda kumkomboa kijana na mwanamke. Nami naongezea kwamba, Wizara ya Kilimo itafute dirisha lingine ambalo litamsaidia mkulima ambaye hana elimu kabisa, au kaishia madarasa ya chini kabisa, hana utaalamu wa kuingia kwenye mitandao, hasomi hata gazeti, hana hata kile kisimu cha tochi. Yule naye anahitaji kupata fursa kama hii ili naye aweze kumiliki ardhi na kuendesha kilimo. Wizara ibuni mbinu muafaka itakayomshirikisha mkulima mdogo yule aliyeko kijijini ambaye hana fursa nyingine yoyote ya kitaalam ili naye aweze kumiliki ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwasaidia kwa njia hiyo, tutakuwa tunaweka uwiano sawa wa kumiliki ardhi kama keki yetu ya Taifa aliotujalia Mwenyezi Mungu tuweze kuipata kwa usawa wa elimu za aina zote, rika zote na jinsia za aina zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwa kusema, nawapongeza sana Wizara, waendelee na jitihada zao hizo, tunawaunga mkono, tutaendelea kuwashauri pindi inapobidi, kwa sababu tunaona mwelekeo upo, tutatoka hapa. Dhamira ipo ya kutoka hapa, nchi imedhamiria na Wizara imedhamiria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)