Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ili niweze kuchangia Bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka huu 2023/2024. Naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini pia kwa maboresho makubwa sana kwenye Wizara ya Kilimo. Halikadhalika niwapongeze sana Waziri na Naibu Waziri na delegation yao yote kwa namna ambavyo wanafanya kazi kubwa ya kuinua Sekta hii ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, udhibiti wa ubora wa mbegu; naomba nizungumzie suala la udhibiti wa mbegu katika nchi yetu. Naomba kwenye eneo hili itumike teknolojia ya juu zaidi kwenye uandaaji wa mbegu. Kwa sababu tunaona mbegu ambazo tunanua nje ya nchi yetu ya Tanzania zina ubora zaidi na mimi nitakuwa shahidi kwenye mbegu aina ya Pannar 53, mbegu ya mahindi ambayo niliinunua mwezi Desemba pale Nchini Mozambique.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii mbegu inafanya vizuri sana, lakini nilipoulizia ndani ya nchi nikaambiwa kwamba hii mbegu haijathibitishwa, haitakiwi iletwe huku nchini. Sasa vitu vizuri kama hivi sisi tunachelewa kuchukua maamuzi. Mbegu hii Mheshimiwa Waziri kama atapenda twende shambani kwangu kabla sijavuna ili ashuhudie namna mbegu hii ya Pannar 53 ilivyobeba mahindi mawili mawili na yote yana afya. Kwa hiyo, naamini kabisa endapo kama mbegu hii pia itaingizwa nchini itaongeza tija kwa wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie sasa mnyororo wa thamani ya mazao. Mheshimiwa Waziri anafanya kazi nzuri sana na tunaona sasa Wizara ya Kilimo inashika kasi. Kasi ya hali ya juu yaani unaweza kufananisha na kasi ya standard gauge railway, hongera sana lakini nataka nizungumzie kwenye masuala ya mazao haya. Mheshimiwa Waziri pamoja na kazi nzuri sana anayoifanya ya uzalishaji, lakini sasa hebu twende mbele zaidi wafikirie namna ya kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kwa mfano kwenye Mkoa wetu wa Ruvuma, ni kwamba mkoa huu ndio ambao unaongoza na umeshika nafasi ya kwanza mara nne mfululizo katika uzalishaji wa mazao ya nafaka Nchini Tanzania. Pasipo shaka yoyote hata mwaka huu tutaongoza halikadhalika. Sasa hebu twende sasa tutoke hapa tulipo kwenye kuuza mazao kama mazao Waziri atuongozee tuweze kupata sasa viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atuambie kwenye mahindi sasa atapeleka viwanda vingapi vya kuchakata sembe, kwenye soya atapeleka viwanda vingapi vya kukamua mafuta na kwenye alizeti atapeleka viwanda vingapi vya kukamua alizeti ili tuweze kuuza bidhaa ambayo imekamilika. Tukifanya hivyo, itasaidia sana kumwinua mkulima, itaongeza ajira, lakini pia itasaidia kuingiza pesa za kigeni baada ya kuwa tumeuza mazao hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tumbako; Mheshimiwa Waziri naomba niseme kwamba wananchi wa Mkoa wa Ruvuma wamefurahia sana sana namna ambavyo Waziri amekuwa ukisimamia vizuri kwenye eneo hili la zao la tumbako na kwamba sasa suala la tumbako halijawa ni mzigo kwenye Mkoa wetu wa Ruvuma. Suala la tumbako limeleta ustawi katika wananchi wetu wa Mkoa wa Ruvuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapozungumza sasa hivi ni kwamba, miaka miwili iliyopita Mkoani Ruvuma tulikuwa tunazalisha tumbako tani laki tatu…

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa hivi ninapozungumza tunazalisha tumbako tani milioni tisa…

NAIBU SPIKA: Taarifa.

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba jamani taarifa mzishikilie, nina mambo ya msingi sana ya kuchangia hapa leo, tafadhali sana.

TAARIFA

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, namwambia dada yangu sio tumbako ni tumbaku. (Makofi/Kicheko)

NAIBU SPIKA: Taarifa hiyo Mheshimiwa.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, hizi taarifa nyingine saa nyingine zinakuwa zinapunguza hadhi fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirekebishe hapo kwenye tani 500 za tumbaku. Ilikuwa tani 500 ndio ambazo zinazalishwa miaka miwili iliyopita, lakini sasa hivi zinazalishwa tani milioni tisa na kwamba wawekezaji na wanunuzi wamepatikana. Nichuke nafasi hii kuwapongeza sana wale wanunuzi wanaonunua tumbaku katika Mkoa wetu wa Ruvuma. Hali kadhalika nampongeza Mheshimiwa Waziri, nampongeza Mheshimiwa Rais, nampongeza pia Mkurugenzi wa Tumbaku Tanzania kwa kutusaidia kutafuta wadau mbalimbali ambao kimsingi wameleta ushindani na hatimaye sasa tumbaku katika Mkoa wa Ruvuma inaleta tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwa tumekuwa na uzalishaji huo sasa umefika mahali Mheshimiwa Waziri atambue wazi tuna uhitaji mkubwa wa Kiwanda cha Sontop pale Songea na kwamba sasa tumbaku hii inayozalishwa katika Mkoa wa Ruvuma iende ikachakatwe pale pale. Juzi nimeongea kwenye Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, lakini nimeona uko umuhimu wa kurudia tena ili Waziri mwenye dhamana asikie. Kama kuna jambo linasubiriwa kwa hamu sana katika Mkoa wa Ruvuma, basi ni Kiwanda cha Uchakataji wa Tumbaku cha Sontop. Kiwanda hiki kinaweza kuajiri wananchi 3,000 ambao kimsingi utasaidia kukuza pato katika mkoa wetu wa Ruvuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu; ninapozungumzia suala la miundombinu nataka nizungumzie suala la Bonde la Kimbande ambalo liko pale Nyasa katika eneo la Mbaba Bay. Bonde hilo ni la muda mrefu linafanyiwa kazi lakini miundombinu yake imechakaa sana. Kwa hiyo, tunaomba kupitia Wizara hii waje waturekebishie ili vijana waweze kuendelea kuwekeza kwenye bonde lile.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Bashe, tunampongeza sana kwa sababu amefanya kazi nzuri na anastahili kupongezwa. Kuna mambo ambayo yanafanyika katika uboreshaji wa miundombinu, ujenzi wa maghala, vihenge, pikipiki kwa Maafisa Ugani, vinasaba kwa Maafisa Ugani lakini pia nataka nizungumzie kwenye eneo hilo, kwamba wakati Waziri akiwasilisha nilimsikia amezungumzia suala la kuhakikisha kwamba anawatafutia magari Maafisa Kilimo wa Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni jema sana. Naomba uboreshaji huo uende sambamba na kutafuta zana za kilimo ambazo zitamsaidia mkulima kwa sababu mpaka sasa hivi tunavyozungumza katika Mkoa wangu wa Ruvuma pamoja na kushika nafasi ya kwanza, lakini bado wamekua wakitumia jembe la mkono. Kwa hiyo ni vizuri sasa Mheshimiwa Waziri aje na mkakati mzuri badala ya kuuziwa matrekta mabovu ya URSUS…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante. Kengele ya pili hiyo.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Eeh! My Jesus Christ. Nimalizie?

NAIBU SPIKA: Ahsante, kengele ya pili.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja.