Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu sana ambayo inashikilia maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kupongeza Wizara hii na hasa Waziri na Naibu kwa kutupatia mradi mkubwa sana wa skimu ya umwagiliaji ya Bwawa la Msingi takribani bilioni 34 kwenye Mto Ndurumo ambao umekuwa ukitusumbua sana. Bado tuna bonde lingine katika Kata ya Mtambala ambalo ni Mradi wa Tatazi, bonde kubwa kabisa katika mto huu pia utume wataalamu wako; na kule Ilamoto Kata ya Mwangeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi leo nataka nijikite kwenye zao la kimkakati, zao la mkonge. Tanzania imebarikiwa kuwa na zao la asili kabisa la mkonge, zao ambalo linastawi katika Mikoa ya Tanga, Morogoro na Kanda ya Ziwa. Sisi wa Kanda ya Kati tulikuwa tunatumia zao hili kuweka mipaka tu kwenye mashamba, lakini kupitia hiyohiyo mipaka tumevuna kiasi kwamba sasa wananchi wa Kata za Kokinda, iyunda wameanza kulima zao hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka ya 1964 zao hili lilikuwa linatoa karibuni tani 230,000 na lilikuwa linachangia asilimia 65 ya fedha za kigeni. Miaka ya 1997 lilishuka mpaka kufikia tani 19,000. Mwaka 2019 Serikali iliingilia kati na kulitangaza kuwa zao la kimkakati, na uhamasishaji ulifanyika wa kutosha na angalau 2022 uzalishaji ulifikia tani 48.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takwimu za 2022 sekta ya mkonge imeajiri wafanyakazi takribani 475,302 kuanzia mashambani mpaka viwandani na hawa ni wafanyakazi rasmi wenye mikataba, achana na vibarua. Lakini pamoja na faida kubwa ya zao hili, kwa maana ya ajira katika nchi hii lakini vilevile fedha za kigeni zao hili ilakabwa koo na nyuzi za plastiki zinazoingizwa katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka ya 1970 mpaka 1990 zao hili liliuawa na nyuzi za plastiki. Serikali imeanza mkakati wa kupandisha lakini inaacha tena nuzi hizi za plastiki zinaingia nchini na sasa tunataka kwenda kulia tena zao ambalo wananchi wameshaanza kupata fedha na ajira inapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliahidi, takribani miezi nane iliyopita, kwamba itakuja na kanuni ya kuzuia matumizi ya nyuzi za plastiki kwenye vifungashio vya vyakula lakini mpaka sasa miezi nane imepita kanuni hakuna, wala katazo hakuna na nyuzi za plastiki zinaendelea kuingia katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano tu, Kiwanda cha 21 Century Holding Limited, kiwanda cha kamba kimefungwa ambacho kilikuwa na wafanyakazi 300, Kiwanda cha TPM 1998 Limited kiwanda kipo Morogoro, kimesimamisha line ya nyuzi za mkonge, kilikuwa kina wafanyakazi takribani 1,000, Highland Spinning Milling - Mdaula nacho kilifungwa, kilikuwa kina zaidi ya wafanyakazi 180, takribani wafanyakazi 1,480 wameachishwa kazi wakati tunatafuta ajira milioni nane, kwa sababu tu ya nyuzi za plastiki ambazo zinaingizwa nchini. Viwanda kama vitatu tu ndivyo vimebaki, na vinafanya kazi chini ya kiwango kwa sababu ya ukosefu wa soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, soko la ndani la kamba za mkonge ni la muhimu sana kwa sababu ambazo nimeshazitaja; kwanza ajira, lakini fedha za kigeni na hata utunzaji wa mazingira kwa kuondoa hizo nyuzi za plastiki, lakini bado halijaangaliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Serikali ije sasa na hizo kanuni kwa haraka za kupiga marufuku matumizi ya nyuzi za plastiki kwenye vifungashio vya vyakula. Aidha, nimuombe Waziri, kwa sababu Serikali inaongea, wawasiliane na mwenzake wa mazingira, watekeleze haraka agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu alilolitoa Septemba 21 na kurudia tena agizo hilo hilo Novemba, 2021 alipotembelea Kiwanda cha Kamba cha Mkonge cha Sisilana la kumtaka Mheshimiwa Waziri Jafo akamilishe andiko lake la kikanuni la kuzuia Kamba za plastiki. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ninyi ni Serikali ongeeni ili agizo hili kubwa ambalo linaokoa maslahi ya nchi litekelezwe haraka kuokoa zao hili ambalo ni la ajira, zao la mkakati na zao muhimu sana kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kulinda maslahi ya mnyororo wa zao hili naiomba Serikali ichukulie umuhimu zao hili. Halmashauri zetu zinapata cess kubwa sana kupitia zao hili kwa maeneo ambayo wanalima mkonge, lakini sasa tunaacha wenyewe kitu ambacho kinatusaidia kwa ajira, kitu kinatusaidia kwa forex halafu tunamaliza kwa nyuzi za plastiki ambazo hazina faida yeyote; na si ajabu hata kodi sizani kama inalipa kuingiza nyuzi hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nyuzi hizi zinaingia kwa ajili ya nyavu, ziende huko kwenye nyavu. Kwa hiyo, ningeomba kabisa agizo liwe kali, kamba za mkonge zitengeneze vifungashio na soko la nje liwe ziada, soko la ndani pekee yake bado linaweza kulinda zao hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimebaki kwenye eneo hili kwa nguvu sana kwa sababu nataka kuokoa ajira za vijana wa Tanzania na tuendelee kuokoa tatizo la forex katika nchi hii. Zao hili ni la asili lilikufa, limeinuliwa na sasa tunataka kuliua tena. Serikali naomba waongee ili waweze kuhakikisha kwamba wanakuja na kanuni ya kuokoa zao hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalize tena, kwa kumwomba Mheshimiwa Waziri…

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba control ya nyuzi za plastic sio tu kwa sababu ya kushindwa ku- control zinazoingia lakini hata wazalishaji wa ndani Serikali yenyewe bado haiwatambui. Mpaka tarehe 24 Aprili, ndio kwanza NEMC imetoa tangazo la kuwaambia wakajisajili.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mtinga.

MHE. FRANCIS MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, napokea taarifa hiyo. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri ametupa bwawa kubwa la skimu ya umwagiliaji, lakini kuna Bonde kubwa la Dominiki linalima vitunguu. Hatuna sehemu ya kutega maji, lakini nina hakika katika mipango yake anaweza akachimba visima vikubwa na vitunguu vikalimwa katika bonde hili, nimwombe sana Waziri katika hili. Vilevile pale Mwangeza kuna skimu nyingine ambayo ilikuwa ya ASPD II zile zilizopita, ilikufa naomba tena Waziri apeleke wataalam wake waweze kufufua.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mkalama inaweza kulisha Kanda ya Kati yote mpaka Magharibi katika zao la chakula, mahindi na mpunga na mabonde haya yapo. Namshukuru sana sasa ameamua kuwawezesha vijana wa Kitanzania kuwa matajiri hivyo na vijana wangu wa Mkalama wawe matajiri kwa kufufua mabonde haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)