Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Esther Edwin Maleko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ni mimi kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Kilimo. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa awamu ya sita, Mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya, na kipekee katika kuongeza bajeti hii ya kilimo kufikia kwa kiwango cha asilimia 29.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri Bashe pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Mavunde pamoja na Wakurugenzi wote kwa kazi nzuri hii wanayoifanya kwenye Wizara kwa sababu leo tunaona mwanga bora katika kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ilani ya CCM katika ukurasa wa 33, naomba kunukuu, inasema; “35. Kilimo cha kisasa ndio msingi katika kujenga na kina nafasi ya kimkakati katika kukuza ustawi wa taifa.”

Mheshimiwa Naibu Spika, takribani Watanzania milioni 40 wako katika sekta hii ya kilimo. Kati ya wakulima hawa milioni 40 wapo wakulima wanaotoka katika mkoa wa Kilimanjaro. Niende moja kwa moja katika Mkoa wangu wa Kilimanjaro. Kama ambavyo hatuwezi kuitenganisha Kilimanjaro na mlima wa Kilimanjaro ndivyo hivyo ambavyo hatuwezi kuitenganisha kilimo cha kahawa na kilimo cha ndizi na Mkoa wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niende moja kwa moja katika kuchangia katika kilimo cha ndizi ambacho kinalimwa sana na akina mama wa Kilimanjaro. Kilimanjaro kahawa inalimwa sana na wanaume lakini ndizi ni zao la akina mama, Zao hili ni zao la kibiashara lakini pia ni zao la chakula. Nilikuwa ninaomba Wizara iangalie umuhimu wa zao hili kwa kuwapatia wakulima wa Kilimanjaro mbegu bora zinazoendana na hali ya hewa ya kulimanjaro ili akina mama wetu waache kulima zile ndizi walizokuwa wakilima zamani ambazo kwa sasa zimepitwa na wakati. Kwanza mavuno ni machache lakini zinapatwa sana na magonjwa. Wizara iangalie ni kiasi wanaweza kuwekeza katika eneo la utafiti ili tuweze kupata mbegu bora ambazo zitaenda kutuingizia kipato cha kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, katika zao hili la ndizi akina mama wetu wanahitaji pia kupata umwagiliaji ili waweze kupata mazao ya kutosha. Nilikuwa naishauri Serikali iangalie ni namna gani itaenda kuboresha ile mifereji ya asili ya zamani ili iweze kusaidia katika umwagiliaji na akina mama wetu wakilima mazao haya waweze kupata mazao yenye tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, jambo la muhimu ni namna Wizara invayoweza kutupatia masoko, si Tanzania tu na nje ya Tanzania. Tunaweza kutumia Waheshimiwa Mabalozi wetu kwa ajili ya kutangaza zao hili katika balozi za huko na sisi tukaweza kupata biashara; ikizingatiwa kwamba katika Mkoa wetu wa Kilimanjaro tunao uwanja wa ndege, na tutautumia uwanja huu vizuri kuweza kusafirisha mazao haya nje na kuwapatia akina mama wa Kilimanjaro faida kubwa katika zao hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu katia mazao ya nje, Mkoa wetu wa Kilimanjaro tuna changamoto kubwa sana kwa katika vituo vya kuuzia ndizi zetu. Akina mama hawa wanateseka sana. Ukienda kwa Sadala saa kumi na mbili kamili utakuta tayari akina mama wetu wamefika na mikungu yao ya ndizi, lakini kuna shida; kwa sababu mvua yao jua lao, hakuna soko. Si akina mama wa hapo tu, akina mama wa Mamsera wanateseka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kati ya wote, akina mama wanaoteseka zaidi ni akina mama wa Mwika. Eneo la Mwika akina mama wanauza ndizi zao barabarani kiasi kwamba kunatokea ajali nyingi na kuna msongamano mkubwa, watu hawaweze hata kupita kipindi cha soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Wizara iangalie ni namna gani inaweza kutupatia masoko ili akina mama wetu wasipate shida kwenda kuuza ndizi zao. Lakini wakienda kuuza kwenye vituo watauza ndizi zao kwa bei elekezi; kwa sababu wale wachuuzi wanapikuwa wanakwenda kuwafuata majumbani mwao wanawapa kwa bei wanayoitaka wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili sitakuwa na mchezo nitashika shilingi ya Mheshimiwa Waziri kama hatatoa maelekezo ya kutosha ni namna gani akina mama wa Kilimanjaro hawatateseka tena katika kwenda kuuza mazao yao hasa ya ndizi. Wanateseka sana kwenda kuuza mazao haya, hawajui watapeleka wapi baada ya kwamba wachuuzi wakiona kwamba jioni imefika bei inakuwa chini; na wakina mama wanaona kuliko warudi na ndizi nyumbani anawauzia kwa bei wanayoitaka. Kwa hiyo nitashika shilingi ya Mheshimiwa Waziri hapa kama hatakuwa ametoa maelekezo yanayoeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji pia teknolojia kwenye zao hili la ndizi, tunahitaji pia tupate mashine za kisasa za kuweza kuchakata na kuongeza thamani ya ndizi hata tukauza ndizi ambazo tayari zimechakatwa zikatengenezwa zikauzwa nje ya nchi kama malighafi ya aina hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo linatatiza akina mama wa mkoa wa Kilimanjaro ni mikopo. Kwa nini basi Wizara isione ni namna gani inaweza kuwakopesha akina mama wa Kilimanjaro ili nao waweze kwenda kufanya biashara yao au kuwekeza zaidi kwenye zao la ndizi? Kwa sababu wao pia ni Watanzania; ukiangalia kule katika Ziwa Victoria wavuvi wanapewa mitumbwi, ukiangalia Ziwa Tanganyika wavuvi wanapewa mitumbwi, kwani kuna shida gani na wakina mama wa Kilimanjaro nao wakaweza kupewa mikopo ili waweze kulima na kupata tija katika kilimo hiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe pongezi sana kwa Wizara kwa Serikali kwa sababu katika kipindi hiki wameweza kutupatia ruzuku ya mbolea tani 14,020. Naomba katika hilo niwapongeze sana kwa sababu katika ruzuku hii hata wakulima wa kahawa wameweza kupata mbolea hii, kwa hiyo ninawapongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa Tanzania tunazalisha kahawa tani 80,000; lakini niwapongeze sana kwa sababu huku nyuma tulikuwa kwenye tani 61,000, kwa kweli tumepiga hatua tunahitaji pongezi. Si hivyo tu fedha zinazoingia za Kimarekani katika kuuza kahawa hii ni takribani Dola za Kimarekani milioni 230. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kule Kilimanjaro, kwa sababu nimesema zao hili ni la akina baba pia akina baba wanahitaji…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante kwa mchango mzuri, kengele ya pili.

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru naunga mkono hoja. (Makofi)