Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nami nitajitahidi kuwasilisha kama Mheshimiwa Prof. Muhongo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naipongeza Serikali kwa kutenga bajeti zaidi ya kilimo, lakini nisisitize kwamba, pamoja na pesa hizi, ziendane na kuongeza nguvu kazi yenye ujuzi mkubwa na uthubutu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kuamua kutenga Mabwawa 100. Kipekee bajeti hii imetaja irrigation kwenye Lake Victoria basin ikiwemo Kagera na Muleba. Kwa misingi hiyo, naunga mkono hoja. Kipekee, miradi ile midogo midogo ya visima 150 kila Halmashauri, yakiwa na matenki ya irrigation kusudi kuwasaidia wananchi wadogo wadogo, kutoka kwenye robo hekta na nusu hekta kuwapeleka kwenye hekta mbili wakilenga mazao maalum kama maharage. Kwa msingi huo, umewafikia wananchi, umewajumuisha, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi najikita kwenye Tanzania Coffee Industry na niangalie kwa namna gani inaweza kuchangia uchumi wa nchi hii kutupeleka zaidi. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, tulikuwa na kipato cha shilingi milioni 944 mwaka 2021 kama export, leo ametangaza kwamba tumefikia shilingi bilioni 1.38, ni hatua moja. Sasa kwa kuchelea, muda usitoshe, naomba katika tasnia ya kahawa na hususan Mkoa wa Kagera nitoe mapendekezo yafuatayo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa visima alivyopanga, na kwa irrigation scheme aliyopanga, tunaomba kwa Mkoa wa Kagera, Serikali iwahimize na kuwahamasisha wananchi wapande zaidi mibuni ambayo ni michanga inayoweza kuongeza kahawa. Pia sisi kahawa ilipoanguka bei tulipanda miti ya hovyo hovyo, naomba sasa Serikali tusaidiane, tuhamasishe wananchi, watumie kanuni za kiuchumi, waondoe ile miti, wapande miti rafiki, wafanye intercrossing na kahawa ili tupate kahawa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba na kuishauri Serikali kuwa kwa Mkoa wa Kagera uwepo mpango maalumu wa kugawa miche bora angalau milioni 25 mpaka miche 30 kwa mwaka. Nitaeleza kanuni zake za uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri unisikilize, unao mkakati wako wa kahawa 2021/2025, kwa heshima na taadhima wewe ni rafiki yangu, nenda kaupitie upya. Huo mkakati ukapitiwe upya na Katibu Mkuu anisikilize, kama akitaka ushauri, nitamshauri upya. Aupitie mkakati ili utuwezeshe sisi kutumia zao la kahawa kuweza kuzalisha zaidi na kuleta pesa nyingi za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naanza kuchangia tasnia ya Kahawa Tanzania. Soko la Kahawa Duniani ni dola bilioni 126.36, sisi Tanzania mazao yetu ya kahawa tunauza nje dola milioni 204. Katika soko la Shilingi bilioni 126 sisi tunachukua Dola milioni 204. Nakupongeza Mheshimiwa Waziri, nimepata habari kwamba South Korea umeingia, nimepata habari kwamba China mazao yako yameingia, nimepata taarifa kwamba Middle East umetufungulia soko, lakini kama wanavyosema watu wa Tanga, ukiona kobe juu ya mti, kuna mtu aliyempandisha. Nampongeza huyo aliyekupandisha kuweza kuingia masoko hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya Kahawa Tanzania yanaendelea kukua, kama nilivyoeleza, tumeshaingia kwenye masoko hayo. Hata hivyo, tuangalie wenzetu kama alivyofanya Mheshimiwa Prof. Muhongo. Kwa mwaka 2021/2022 Uganda waliuza Kahawa ya dola milioni 862, ndiyo maana nasema urudie mkakati wako. Mkakati wako unazungumza quantity, hauzungumzii amount of money. Ukiusoma unazungumza quantity, hatuhitaji idadi, tunahitaji pesa tunazopata. Chini ya Mamlaka ya Kahawa ya Uganda, wanaeleza mamlaka itakachofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waganda wana mkakati wao wa kuingiza sokoni dola milioni 300 kwa mwaka, na kwa miaka mitano wanapanga kuingiza dola bilioni 1.5 kwa kutumia kahawa tu. Kwa hiyo, kwa mwaka 2022 mpaka miaka mitano ijayo watakuwa na 1.5 in additional na ile dola milioni 800, yaani watafikia dola 2.362, hiyo ni Uganda.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naiona Tanzania kama kwa mfano wa Kagera niliokwambia, kama tukiweza kuzalisha miche bora milioni 25 mpaka milioni 30 kwa Kagera ambayo inazalisha asilimia 44 ya Kahawa yote ambayo yote ni Robusta, nina uhakika kwa hesabu za uwiano utaweza kuingiza karibu dola milioni 600.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa uwiano huo kama tasnia nzima ya kahawa Tanzania, ikiweza kuwekezwa kwa nguvu hizo tutaweza sisi Tanzania kuzalisha bilioni 1.56 kutokana na kahawa kwa miaka mitano mpaka kumi ijayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naishauri Serikali, hii miradi ya uwekezaji ielekezwe kwenye zao hili la Kahawa. Kwa mfano; kwetu upande wa Kyelwa, Kyelwa ni wazalishaji wazuri wa Kahawa, wapewe miche zaidi. Lakini Ngara wanasifika kwa kuzalisha Kahawa yenye ubora mkubwa sana. Waangaliwe waweze kushindana na mshindani wetu wa Burundi. Pia bora Mzee Kanyasu ulikuwa Mkuu wa Wilaya pale. Vilevile sehemu ya Biharamulo ambayo ilikuwa sehemu ya BCU ukiunganisha na Muleba ni ukanda ambao unaweza kuzalisha Kahawa kwa wingi. Umekuja na mpango wa irrigation ambako utafanya irrigation sisi kwetu hatuhitaji visima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukianzia ukanda wa ziwa kuanzia sehemu za Mayondwe, kuja sehemu za Kagoma, kuja sehemu za Izigo Kwenda Lwanganilo mpaka Kimwani, sehemu zote unaweza kuweka pump kwenye maji una irrigate kwenye ukanda wote wa ziwa na tunapata Kahawa nyingi. Ndio maana nasema Kagera tunaweza kuzalisha dola milioni 500 kwa kutumia Kagera tu. Kwa uwiano huo pato la kipato cha Mkoa wa Kagera litaweza kuendelea, wala hatuhitaji viingereza wala kitu gani, ni kwamba unazalisha zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pesa ambazo Serikali imepanga, nimeunga mkono hoja. Lakini kwa kuwekeza pesa hapa utaweka shilingi moja na utapata shilingi mbili, hili ndilo eneo la sekta ya kiuzalishaji ambalo unaweza kuzalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuzalisha, liko suala la utumiaji wa Kahawa. Sisi tunatumia 0.07 kwenye kahawa…

NAIBU SPIKA: Ahsante, ahsante.

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: …wenzetu wa Algeria wanatumia kilo tatu, tunywe kahawa, kahawa ni burudani.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante.

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)