Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii na kwa ridhaa yako nianze kwa aya moja ndani ya kitabu kitukufu cha Mwenyezi Mungu, inayosema, “Rabbi-rishirahii swadri, wayassirli amri, weahlul-ukudata minlisani yafqahu kauli.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana yake; nimemuomba Mwenyezi Mungu aunyooshe ulimi wangu ili niweze kuyasema yale ambayo Waheshimiwa Wabunge wameongea kwa dhamira njema kabisa ya kujenga uchumi wa Taifa hili ili niyaseme na yaeleweke, ndio maana ya aya hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru sana wewe kwa uongozi wako madhubuti, lakini pia wasaidizi wako Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Kamati zetu kwa namna ambavyo mmeongoza na kusimamia vyema majadiliano ya bajeti ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa mwaka 2023/2024.

Nawashukuru pia Waheshimiwa Wabunge wote kwa uchangiaji wenu makini mlioufanya kwa maandishi na kwa kuzungumza moja kwa moja katika Bunge hili Tukufu. Naomba niseme kuwa ninatambua na kuthamini dhamira na nia njema iliyotawala mjadala huu ambayo kimsingi ililenga kuboresha mikakati na mbinu za kisekta zitakazotumika kutekeleza malengo tuliyopanga kwa mwaka 2023/2024 na hivyo kutoa mchango unaotakiwa kwa Taifal letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee naishukuru sana Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi Kusini na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Mariam Ditopile Mzuzuri, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma na Waheshimiwa Wajumbe wote wa Kamati kwa namna ambavyo wanajenga hoja na kushauri ipasavyo kuhusu uendelezaji wa sekta ya uwekezaji, viwanda na biashara hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya viongozi wenzangu na watumishi wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na taasisi zake naomba kupokea pongezi nyingi za utendaji zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge hasa kwa Mheshimiwa Rais wetu na kwetu sisi viongozi wa Wizara. Aidha, tunaahidi kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kwa ari zaidi. Vilevile tumepokea ushauri na michango mingi ambayo ni chachu na changamoto muhimu katika kuleta maendeleo ya mipango ya uchumi yenye mchango kwa sekta ya uwekezaji, viwanda na biashara.

Mheshimiwa Spika, mawasilisho hayo yanatambua na kuzingatia pia hoja mbalimbali za sekta hii zilizojitokeza wakati wa kujadili na kupitisha bajeti za Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais na Makamu wa Rais na pia Wizara zilizonitangulia kuwasilisha bajeti zao hapa Bungeni kwani Wizara yangu ni Wizara mtambuka ambayo tunashughulika na Wizara zote.

Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa ushauri wenu na maelekezo ya Bunge hili katika kujadili bajeti ya Wizara hii tutayazingatia na kuyafanyia kazi ikiwemo kutoa mrejesho wa utekelezaji wake. Aidha, kutokana na muda mfupi nilionao katika kuhitimisha bajeti hii, maelezo na majibu ya kina ya michango mbalimbali yameandaliwa na yatawasilishwa kwa maandishi.

Mheshimiwa Spika, kabla sijajielekeza katika kujibu na kufafanua hoja mbalimbali zilizojitokeza naomba kuwatambua Waheshimiwa Wabunge 39 waliochangia katika majadiliano ya hotuba ya bajeti ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara. Kati yao Waheshimiwa Wabunge 35 wamechangia kwa kuongea hapa Bungeni na Waheshimiwa Wabunge wanne wamechangia kwa maandishi.

Mheshimiwa Spika, na kati yao, naomba uniruhusu niseme hili, kati ya Wabunge hao Wabunge 23 wamechangia kuhusu suala la Twiga Cement na Tanga Cement. Inaonesha ni kwa kiwango gani ambavyo Waheshimiwa Wabunge wanaguswa na uwekezaji na biashara ndani ya Taifa letu. Kwa shabaha ya kumbukumbu orodha hiyo itawasilishwa na kuwekwa katika Kumbukumbu Rasmi za Bunge.

Mheshimiwa Spika, naomba pia niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri wenzangu ambao wamechangia hoja hii na kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali akiwemo Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Naibu Waziri wangu, Mheshimiwa Exhaud Kigahe na Mheshimiwa Patrobas Katambi, nawashukuru sana kwa kutoa majibu kwa hoja za Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, hoja na mipango iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge katika kujadili hotuba yangu inaonesha nia thabiti ya ushirikiano wenu na Wizara hii katika kuziendeleza sekta ya uwekezaji, viwanda na biashara na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Taifa letu. Nimehamasika na jinsi mlivyonitia nguvu kwa kukubaliana nami katika mambo ya msingi na kutetea kwa nguvu zenu zote maslahi mapana na yenye maslahi makubwa ya Taifa na wananchi wetu tunaowawakilisha hapa Bungeni. Kwa ujumla wake hoja na michango mingi iliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote waliozungumza na kuchangia kwa maandishi zinashabihiana katika maeneo mengi na zimelenga maeneo mbalimbali ambayo sasa napenda kujielekeza kujibu na kutoa ufafanuzi wake.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema, hoja kubwa ilikuwa ni jambo la Twiga na Tanga Cement, nami nitajielekeza huko baada ya kuwa nimeongeza mchango kidogo kwenye majibu ya hoja za Waheshimiwa Wabunge yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri; nayo ni kuhusu suala la Liganga na Mchuchuma. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge mliotambua kwamba Serikali hii imejipanga kuleta maendeleo kwa wananchi wake, kuwafikia kulekule waliko.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wanakumbuka ni Bunge hilihili mwaka jana lilielekeza fidia hii ikalipwe. Nampongeza sana kwa dhati ya moyo wangu, Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, bila kusita ametoa bilioni 15.4 kwa ajili ya malipo ya fidia ya wananchi wetu wote kwenye mradi huu wa Liganga na Mchuchuma. Hii ni dhamira ya dhati sana. Na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge maelekezo yenu kama ilivyosema Kamati yetu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo tunayatekeleza kwa asilimia kubwa. Sasa hivi timu ile ya majadiliano inaendelea na kazi yake ya kujadiliana, kama ambavyo Serikali ilitoa maelezo yake hapa Bungeni; kwamba tunatamani kumalizana na mwekezaji yule wa mwanzo ambaye tayari tulishasainiana mikataba kwa wema na kuondokana naye ili Taifa letu lisiingie kwenye migogoro na gharama nyingine ambazo hazina msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba taarifa yetu tuliyoitoa mwezi wa 11, kwenye Bunge la mwezi wa 11 hapa Bungeni kwamba, tulipata taarifa rasmi kutoka Serikali ya China, mwekezaji yule amefilisika, ni kweli, amefilisika. Pamoja na taarifa ile ya kufilisika ile ni kampuni inayojitegemea, lazima tushughulikenayo kwa kufuata kanuni na taratibu na sheria zetu, ili kuliepusha Taifa letu kuingia katika migogoro ambayo haina maana.

Mheshimiwa Spika, aliyefilisika ni yeye, lakini bado ana mikataba na sisi; na kama ambavyo Wabunge walitahadharisha huko nyuma wakasema ni wakasema tumuite tuje tuongee naye. Huko nyuma, miaka sita iliyopita, nililieleza Bunge lako Tukufu, tulimuita hakuwahi kutokea na sasa tumemuita amekuja, yupo mezani. Tunajadiliana naye na bahati nzuri na yeye amekiri kweli amefilisika. Amefilisika, lakini bado ana mkataba na sisi lazima tuhitimishe naye vizuri, hicho ndicho ninachokisema. Kazi mliyotutuma tunaendelea kuifanya kwa kiwango cha hali ya juu kwa uharaka, lakini kwa uzalendo mkubwa wa Taifa letu ili sasa mradi huu uanze kutekelezeka, uondoke kwenye miradi ya historia, miradi ambayo ni simulizi ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maneno haya, nilimsikia Mheshimiwa Neema Mgaya alisema anataka kuleta hoja binafsi. Nilitamani sana kwamba Bunge tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuonesha njia ya kutaka jambo hili liishe sasa na kuwapelekea ujumbe wawekezaji wetu kwamba Tanzania ni salama. Ameweza kuja tumeanza mchakato huu, tumpe nguvu Mheshimiwa Rais wetu ili tulihitimishe jambo hili kwa wakati na tuweze kuona athari chanya ya mradi huu ambao umekuwa ni historia kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ambayo nilitamani niitolee maelezo inaunganishwa na hoja kubwa ambayo ningetamani nichukue muda wangu mwingi kuieleza. Nayo ni kufutwa, kuondolewa kwenye usajili kwa Kampuni ya Chalinze Cement Company Limited. Kwa nini imeondolewa? Ni jukumu letu kuzisajili, ni jukumu letu kuwawekea masharti, ili watekeleze.

Mheshimiwa Spika, msajili analo jukumu la kuhakikisha daftari linakuwa na taarifa sahihi na za uhakika na Sheria ya Kampuni imempatia mamlaka msajili kufuta kampuni yoyote ambayo wakati wa usajili iliwasilisha taarifa za uongo.

Mheshimiwa Spika, msajili anaendelea na zoezi la upekuzi wa taarifa zilizomo kwenye daftari la kampuni ambapo zoezi hili ni endelevu kwa lengo la kuhakikisha kampuni zisizokidhi vigezo zinaondolewa zote. Katika zoezi hilo msajili alibaini kuwa Chalinze Cement Company Limited iliwasilisha taarifa za uongo wakati wa usajili, kama ifuatavyo: -

Moja; anuani ya kampuni iliyosajiliwa haipo kwenye usajili popote pale ndani ya Taifa hili. Kwa hiyo, kwanza anuani ya kampuni ni ya uongo kwa hiyo, ukitaka kumfikia huwezi kumfikia, yuko wapi.

Pili; anuani za wana-hisa alizozisajili hazipo kwenye sajili zozote ndani ya Taifa letu. kwa hiyo, nayo pia hata hao wanahisa ni wa kufikirika.

Mheshimiwa Spika, mawasiliano ya simu ya mkononi yaliyosajiliwa kwetu sisi si ya mwanahisa aliyetajwa kwenye usajili huo. Aidha, kwa mujibu wa sheria msajili alitoa notice ya kusudio la kufuta Kampuni ya Chalinze Cement Company Limited ambapo wakurugenzi wake walipewa siku 30 kuanzia tarehe 19 Januari, 2023 kuwasilisha maelezo kwa nini kampuni hiyo, isiondolewe kwenye daftari la kampuni kwa kuwasilisha taarifa za uongo wakati wa usajili.

Mheshimiwa Spika, baada ya siku 30 zilizotolewa kumalizika bila ya Wakurugenzi kutoa maelezo yoyote, Msajili aliendelea na hatua inayofuata kwa mujibu wa kifungu cha 400A(3) cha Sheria ya Kampuni na kuifuta Chalinze Cement Company Limited. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, naomba waelewe dhamira njema ya Serikali yetu. Tunahitaji wawekezaji, lakini wawe wale wenye dhamira njema na Taifa letu, siyo wawekezaji wanaokuja kutuchezea Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunabaki na orodha ya makampuni mengi ambayo hayapo, makampuni hewa, lakini kibaya zaidi taarifa zote alizozisema wakati anasajili ni za uongo. Kwa hiyo, naomba hilo Watanzania wajue, mtu huyu alishughulikiwa na sheria iliyotungwa na Bunge hili hili Tukufu, hakuna sehemu yoyote ambapo Serikali ilikosea.

Mheshimiwa Spika, jambo la Tanga na Twiga Cement; nimepokea maelekezo ya Bunge lako na kama utaridhia, sisi kama Wizara tuko tayari kutoa semina kwa Wabunge wote kuhusu utendaji wa Tume ya Ushindani pamoja na Baraza la Ushindani la Taifa ili sote kwa pamoja tuwe na uelewa wa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na hoja na Waheshimiwa Wabunge kama nilivyosema 23, zaidi ya asilimia 50 ya Wabunge waliochangia hotuba ya bajeti hii kuhusu jambo hili na ilianza kuambiwa kwa nini FCC imeruhusu. FCC ndugu zangu ni Tume yetu ya Ushindani; kwa nini imeruhusu muungano wa Kampuni za Twiga Cement na Tanga Cement ambazo hapo awali ulizuiwa na Baraza la Ushindani.

Mheshimiwa Spika, jibu sahihi la hoja hii kwa Waheshimiwa Wabunge ni kwamba Tume ya Ushindani haikushughulika na ombi la muungano wa kampuni mbili ambao ulizuiwa na Baraza la Ushindani; hilo ni jibu la kwanza. Haikushughulika na ombi lile lililozuiwa na Baraza la Ushindani. Tunaheshimu sheria zote za nchi hii na hasa zile mimi Waziri wa Uwekezaji niliyebeba Katiba ya Taifa letu, nikabeba kitabu kitukufu kuapa, nimeapa kuzilinda na nitazilinda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kilichofanyika na Wizara yetu inapenda kusema na kulijulisha Bunge letu Tukufu kwamba mnamo tarehe 22 Desemba, 2022 Scancem International DA ambayo inamiliki asilimia 69 pale Twiga Cement ilileta ombi la kununua asilimia 68.33 ya hisa za AfriSam Mauritius ndani ya Kampuni ya Tanga Cement.

Mheshimiwa Spika, tarehe 22 Desemba, 2022 ndiyo tulipokea maombi hayo. Taratibu zote za kisheria zilifuatwa katika kuwasilisha na kuchambua ombi hili. Kwa mujibu wa kifungu cha 11(2) cha Sheria ya Ushindani kinachosomeka sambamba na Kanuni ya 33 ya Kanuni za Ushindani za Mwaka 2018 na Kanuni ya 2(1) ya Kizingiti cha Uwasilishaji wa Maombi ya Miungano ya Makampuni za Mwaka 2017 (The Threshold for Notification of a Merger) kinatoa wajibu kwa kampuni ambazo zinataka kuungana na zimekidhi vigezo vilivyowekwa chini ya vifungu tajwa hapo juu kuwasilisha maombi yao bila kujali kama kusudio lao la awali lilikataliwa au kukubaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vigezo hivi ni pamoja na ununuzi wa hisa au mali za kampuni inayonunuliwa, kizingiti cha mtaji wa kampuni zote mbili kama unafikia au kuzidi kiasi cha shilingi bilioni 3.5 na kubadilika kwa uwezo wa kiutawala (change of control) imebadilika?

Mheshimiwa Spika, hivyo napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, ombi hili lililoruhusiwa ni ombi jipya kutokana na vifungu nilivyovitaja kabla, ni ombi jipya ambalo tulilipokea kwa barua yenye kumbukumbu namba CDC127359/144 lililotolewa mbele ya Tume ya Ushindani kwa kuzingatia takwimu za hali ya soko la saruji kwa mwaka 2022. Kwa sababu ombi hili tulilipokea mwaka 2022 hatukuwa na sababu ya kutumia takwimu za mwaka 2020, tutatumia takwimu za mwaka 2022. Natamani sana Watanzania watuelewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi hili jipya lililoruhusiwa na Tume yetu ya Ushindani ni tofauti na lile la awali lenye kumbukumbu Na. CDC127359/136 lililowasilishwa tarehe 2 Novemba, 2021. Kwa hiyo, tuna maombi mawili; la kwanza la mwaka 2021 na ambalo lilitumia takwimu za Desemba, 2020 kwa sababu hatukuwa na takwimu nyingine katikati hapo.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya hoja za Waheshimiwa Wabunge, ombi hili lililowasilishwa tarehe 2 Novemba, 2021, liliruhusiwa kwa masharti tarehe 6 Aprili, 2022 kwa kuzingatia kigezo cha uwezo uliosimikwa. Amelieleza vizuri Mheshimiwa Naibu Waziri Patrobass Katambi, kisheria maana yake nini.

Mheshimiwa Spika, tuliruhusu kwa sababu utawala wa soko wa kampuni mbili zilizoomba kujiunga kutumia installed capacity ulikuwa unafikia asilimia 31.53 ambazo ni chini ya asilimia 35 ambayo ni threshold ya mwisho ya kuruhusiwa kwa kampuni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na sheria inavyosema, haijasema tutumie installed capacity wala sales volume, kwa sababu Sheria ya Tume ya Ushindabni is an economic act (sheria ya kiuchumi). Sheria ya kiuchumi ina-deal na behaviour za wateja wake walioko kwenye eneo lile lililopo, it’s a behavioral act, inabadilika wakati kwa wakati. Wamesema vizuri Wabunge kwamba mazingira yanabadilika na yalibadilika kweli.

Mheshimiwa Spika, kwa nini FCC waliamua ombi ambalo lilizuiwa na FCT hapo mwanzo? Nimeshalieleza wazi, ombi tuliloliamua ni jipya kabisa, wala siyo lile la zamani.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa taarifa kwamba mchakato wa kupokea, kuchambua na kutoa maamuzi ya muungano wa kampuni kama nilivyosema unaongozwa na nadharia za kiuchumi na kibiashara. Nadharia hizi na viashiria vyake, market variables, lazima viangaliwe na hivyo basi, kutokana na ukweli huu, viashiria kutoka mwaka 2020 mpaka mwaka 2022 vilibadilika na hapo tunatoa picha kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba hata huko nyuma imewahi kutokea ndani ya Taifa letu, kampuni ziliomba kuungana kwa mazingira ya kwanza wakanyimwa kwa sababu mazingira hayakuwa yanaruhusu na waliporejea mazingira yakawa yanaruhusu na wakaruhusiwa kuungana, nayo wala siyo miaka mingi iliyopita.

Mheshimiwa Spika, FCC mnamo tarehe 10 Juni, 2021 iliendelea kuzuia ombi la Kampuni ya Toyota Tshusho, zote ziko ndani ya Taifa letu kuinunua Kampuni ya CFAO Motors kama ambavyo ombi hilo lilivyozuiliwa na FCC na baadaye kuafikiwa na Baraza la Ushindani (FCT) mwaka 2013. Ya kwanza ilikuwa 2012 na sasa ni 2013, wakaruhusiwa ndani ya Taifa letu kupitia Tume ya Ushindani na Baraza la Ushindani hili hili ambalo tena leo tunasema watumishi wetu wamekwenda ndivyo sivyo na Waziri wamenisisitiza nisimamie haki na niliapa kusimamia haki na nitaisimamia.

Mheshimiwa Spika, siyo ndani ya Taifa letu tu, Nchi ya Afrika Kusini ambao wote tupo kwenye SADC, mwaka 2019 ilizuia muunganiko wa Africa Forest Fund Limited na Guka Forest Holding kwa sababu mazingira wakati huo mwaka 2019 hayakuwa yanaruhusu. Mwaka 2021 kampuni zilezile zikaomba kuungana kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya uchumi ndani ya Taifa na mwaka 2021 baada ya mamlaka za ushindani nchini Afrika ya Kusini kuridhika na mabadiliko na muundo wa soko, kampuni hizi mbili ziliruhusiwa. Kwa hiyo, siyo jambo jipya, ni jambo ambalo lipo kwa majirani zetu, ni jambo ambalo lipo ndani ya Taifa letu na kilichofanyika ni kitu cha kawaida kabisa.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja nyingi kwenye jambo hili, naomba niseme tu kidogo, maana yake imesemwa pia kwamba hakukuwa na uwazi kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii ya kutokuwa na uwazi katika ununuzi wa hisa za AfriSam Mauritius ndani ya Kampuni ya Tanga Cement, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, mara baada ya ombi hilo kuletwa Tume ya Ushindani ulifanyika mchakato wa uwazi ambapo kwa mujibu wa Kanuni ya 49 ya Kanuni za Ushindani za Mwaka 2018 tunatakiwa kutoa tangazo kwa Taifa na kwa dunia kwamba kuna mchakato huu unaendelea.

Mheshimiwa Spika, tangazo hilo tulilitoa kwenye magazeti ya Daily News na Habari Leo ya tarehe 11 Februari, 2023 ili kuutaarifu umma juu ya jambo hili tena kwamba tumeanza nalo. Hatukupokea malalamiko kwa yeyote na kikao cha wadau ambacho kilihusisha kampuni zote za uzalishaji saruji ndani ya Taifa letu, taasisi ya kuwatetea walaji ndani ya Taifa letu walikuwemo kwenye kikao, hawakupinga wakasema wameridhika mchakato uendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huyo anayekuja kinyumenyume nani? Siri yake ni ipi? Kwa nini asiiseme wazi basi tukajua? Wakati haya yote yakiendelea, nimewahi kuwaandikia barua hawa Chalinze Cement, mimi mwenyewe Waziri kwamba, nataka kwenda kuwatembelea kwenye kiwanda chenu. Mpaka leo sijawahi kupata jibu niende au nisiende. Chalinze Cement ni nani? Ni mdudu gani ndani ya Taifa letu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Chalinze Cement amesajiliwa baada ya ombi la kwanza la Twiga na Tanga kuungana, hakuwepo huko nyuma. Tumefanya kikao cha wadau, Chalinze Cement hakuwepo. Tumemaliza michakato yote anaibuka kuja kusajiliwa na sisi kama ilivyo jukumu letu la kusajili tukamsajili, si mtu ameleta documents, ametuletea tumemsajili. Sasa tumfuatilie, Waziri mwenyewe nimemwita, kama hutaki nije kwako njoo tuongee, niletee malalamiko yako. Mpaka hapa nilipo hajawahi kuja kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wenye dhamira njema ya kulinda jitihada za Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuita wawekezaji kutoka nje na kuwalinda wawekezaji wa ndani ambao tayari walishawekeza; nawashukuru sana. Wapo walioniambia na wengine wamenionesha mpaka picha ya watu hao wakizunguka kwa Wabunge kuwaeleza wasaidie kupinga jambo hili. (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Spika, naomba Waheshimiwa Wabunge tuchukue tahadhari ya hali ya juu na watu wasiolitakia mema Taifa letu. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana kui-brand Tanzania. Wawekezaji wengi wanakuja, nimesema kwa mwaka mmoja tuna wawekezaji 240, hawakuwahi kutokea katika historia ya miaka 60 ya Taifa letu, yametokea sasa, tusitumike. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Spika, kuna watu ambao wanataka kusimama mbele ya Mheshimiwa Rais kumwambia hapana Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Rais amesema hapana na mimi nimeapa kulinda sheria zote zilizopo ndani ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na nitasimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie podium hii kumwomba Chalinze Cement aje tumsaidie. Tunajua yako mengi yaliyowakwamisha wenzake, sasa aje tumsaidie kama kweli anataka kuwekeza ndani ya Taifa la Tanzania. Mimi niko tayari, wasaidizi wangu wote wako tayari, waje tuwekeze kwa pamoja na tuwahudumie Watanzania wote kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, baada ya maneno haya, naomba kuhitimisha kwa kuwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupitia kwao, nimesimama mbele yao najiamini ni mzalendo na naiamini imani yangu, nimeapa kulinda Katiba ya Taifa hili, nimeapa kulinda sheria zinazoongoza Wizara ya Uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba sana mtupitishie bajeti ya Wizara yetu kwa mwaka 2023/2024, ili tuendelee kulinda jitihada za Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuita wawekezaji, kuwawezesha wafanyabiashara wetu na hatimaye Taifa letu liweze kuhudumia Afrika kutoka hapa tulipo, liweze kuhudumia dunia kutoka hapa tulipo. Uwezo huo tunao chini ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maneno haya, naomba kutoa hoja.

WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naafiki.