Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Nianze kabisa kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na jopo lake. Hatuna mashaka na weledi wao ndio maana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaamini.

Mheshimiwa Spika, leo nitaongelea mambo mawili katika bidhaa za makundi mawili tu, bidhaa ambazo zinaingizwa ndani ya nchi yetu. Tumekuwa na kasumba ambayo imekuwa siyo nzuri sana inapokuja kwenye kuingiza bidhaa nchini. Kila kitu kwa asilimia kubwa tunaingiza. Nikawaza itafika wakati tutaingiza mpaka dhambi.

Mheshimiwa Spika, cha kwanza, nitaongelea mambo mawili. Jambo la kwanza natamani kuongelea kuhusiana na mradi wa chumvi. Wabunge wenzangu wengi wameongea vizuri kuhusiana na chumvi, wamefafanua vizuri sana. Nimwombe Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha, nilipouliza swali la msingi hapa kuhusiana na Kiwanda cha Chumvi Itumbula sikujibiwa kikamilifu. Tunaamini kiwanda kile cha chumvi hakitawasaidia tu wananchi wa Jimbo la Momba kupandisha mapato kwenye halmashauri yetu, lakini ni kiwanda ambacho chumvi inayozalishwa pale inaweza kusaidia Mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini na ambapo Wabunge wengine wametangulia kusema hapa kwamba, tuna uhitaji mkubwa sana wa chumvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bidhaa nyingine ambayo nataka kuongelea hapa ni uingizwaji wa pombe nchini kwetu. Katika imani zetu hapa, Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hatuna dini, lakini wananchi sisi ndio tuna dini. Sasa najiuliza kama wananchi tuna dini na kila mtu kwa imani yake, wapo tunaoamini pombe ni dhambi na wengine wanaamini pombe ni haramu.

Mheshimiwa Spika, kwanza niseme mimi sio mtumiaji wa pombe, lakini sina sababu ya kutokutetea maslahi ya watu ambao wanatumia pombe na kama zipo nchini kwetu zinatumika.

Mheshimiwa Spika, mara ya mwisho nilipokuja hapa nikazitetea pombe zetu za kienyeji, sikupewa majibu mazuri na Serikali na Mheshimiwa Simbachawene akaahidi vizuri sana hapa kwamba atalifanyia kazi na Mheshimiwa Waziri ni huyu huyu na Naibu Waziri ni huyu huyu.

Mheshimiwa Spika, leo nimekuja na pombe zenye thamani kubwa sana hapa, nataka Mheshimiwa Waziri aniambie hizi pombe ziko hapa nchini zinafanya nini na hizi pombe kwa namna zinavyouzwa bei ghali. Hapa nimekuja na pombe mpaka ya 270,000. Hizi pombe nimeenda kuzinunua kwenye hoteli kubwa hapa Dodoma pale Morena kwa Shabiby, ambapo naamini watu ambao wanakwenda sehemu ile ni Mawaziri wenyewe, Makatibu Wakuu wa Wizara, labda na Wabunge wenyewe na wafanyabiashara wakubwa wakubwa. Sasa swali, kama Serikali haina dini na pombe ni dhambi hizi pombe zinafanya nini hapa nchini?

(Hapa Mhe. Condester M. Sichwale aliweka juu mezani chupa za pombe mbalimbali)

MHE. CONDESTER M. SICHWALE: Mheshimiwa Spika, kuna smirnoff, nisaidie kutoa mama, green fish wanywa pombe wanajua, sijui kuna Hennessy, kuna Jack Daniels, kuna hennessy nyingine, hii inaitwa Gordonson. Haya naomba hizi za Tanzania, hizi ndio za kwetu za Tanzania zinazozalishwa hapa K-Vant na Konyagi. Swali langu hizi zote nimenunua Morena kwa Mheshimiwa Shabiby, zinagharimu zaidi ya Sh.500,000 hapa zilipo. Swali najiuliza hizi pombe zinafanya nini? Tafsiri yake wapo watu ambao wanatumia hizi.

Mheshimiwa Spika, nataka niwaulize Watanzania wenzangu walioko huko nje na Wabunge walioko huku, ni nani ambaye mtoto wake akienda kufanya kazi kwenye Kiwanda cha TBL atakataa, atasema ni dhambi. Tufanye sasa hivi awe ni Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha TBL, nani atazungumzia masuala ya dhambi hapa? Nataka kujua ni Watanzania wangapi ambao watoto wao wanafanya kazi kwenye Kiwanda cha Konyagi? Ni Watanzania wangapi ambao watoto wao wanafanya kwenye Kiwanda cha K-Vant wangapi, hawapati hiyo mishahara?

Mheshimiwa Spika, sasa najiuliza kwa nini pombe zetu mfano wa pombe ya gongo zinamwagwa, vijana wenzangu wakimbiza Mwenge kule Mtwara walimwaga pombe za Watanzania wapika gongo. Kwa nini tunadharau ubunifu wa Watanzania? Kwa nini tunadharau mawazo ambayo ni ya Watanzania. Sasa najiuliza, kwani viwanda maana yake nini? Viwanda si huwa vinaanza na wazo, mtu akipata wazo si ndio atengeneze bidhaa kwa hali ya kawaida.

Mheshimiwa Spika, hao China wanaotuletea makorokoro feki humu nchini kwetu wanafanyaje? China kila mtu hata mtoto wa miaka 10 ana kiwanda chao wanatengeneza ma-product mabovu ndio wanatuletea huku kwenye nchi zetu.” [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Spika, sasa sisi kama yupo Mtanzania ambaye anaweza akapata wazo la kutengeneza gongo mpaka watu wakalewa, jamani si Mtanzania huyu alipaswa apewe support. Sasa Serikali ubunifu ambao inautaka inataka ubunifu upi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, angalia pombe hizi zote ambazo unaziona, siku moja Mheshimiwa Waziri Bashe akiwa anaongea huko kwenye viwanda vyake vya miwa huko, anapongeza namna ambavyo wanzalisha sukari. Akawa anasema namna ambavyo wanazalisha Molasses wanauza kwenye nchi za nje ambazo wao ndio wanatuzalishia hizi wanatuletea sisi tunakunywa. Molasses inatengenezwa kwetu halafu wanasafirisha kwenda nje sisi tunarudi tukaanze kunywa pombe. Imani zetu Serikali zinasema pombe ni dhambi…

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, sasa hii dhambi inafanya nini hapa nchini kwetu?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Mtibwa mwaka huu fedha…

SPIKA: Mheshimiwa Condester.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, walizalisha molasses tani…

SPIKA: Mheshimiwa Condester.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, muda hautoshi jamani.

TAARIFA

SPIKA: Subiri kidogo kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Aida Khenani.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru napenda kumpa taarifa mzungumzaji kwamba pamoja na uzuri wa hizo chupa hizo bidhaa alizoziweka mezani, hata watumiaji wengi hawajui imetengenezwa na vitu, lakini hiyo aina ya pombe inayotengenezwa Tanzania, inafahamika kwamba material yake yanatoka shambani na yanatoka wapi. Kwa hiyo ni suala la Serikali kuongeza kuwapa motisha wanaotengeneza. Ahsante. (Makofi)

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, napokea taarifa ya Mheshimiwa Aida. Yeye Mheshimiwa Aida…

SPIKA: Mheshimiwa Sichalwe subiri kidogo inabidi uitwe ndio uanze kuzungumza. Mheshimiwa Sichalwe unapokea taarifa hiyo.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, napokea na wewe kule Ilolo, Mafyati kule Mabatini una wapiga kura wengi ambao mimi nawafahamu na nawajua wanatengeneza pombe za kienyeji. Kwa hiyo mimi na wewe tuna wapiga kura ambao wanatengeneza pombe za kienyeji. Bahati mbaya inawezekana hawatengenezi gongo lakini Kimpumu, Kindi, Komoni, Isute, zote hizo ni pombe za kienyeji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa najiuliza tunapohubiri ubunifu, ubunifu upi ambao sisi kwenye nchi yetu tunauhubiri. Kuna wachangiaji wamepita hapa aliongea Mheshimiwa Tauhida Gallos jana, akasema kuna vijana wa kitanzania ambao wanaweza kutengeneza system ambayo mtu akiwa mbali ikaweza kuzima umeme nyumbani kwake. Najiuliza hivi vijana hawa wa Kitanzania waweze kutumia akili yote hiyo kuja na utaalam wote huo washindwe kutenganisha kati ya methanol na ethanol kwenye gongo. Maana yake ambacho kinazuiliwa hapa kwenye matumizi ya gongo eti ni methanol ambayo sisi tulitegemea.

Mheshimiwa Spika, nimeenda zaidi, nimewasiliana na Profesa wa…

TAARIFA

SPIKA: Haya achilia hapo hapo kwenye kuwasiliana utaanzia hapo, Mheshimiwa Agnes Hokororo.

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nataka kumpa mzungumzaji taarifa kwamba wakati wakulima wa korosho wanalalamikia bei ndogo ya korosho ghafi, matunda ya korosho kwa maana ya mabibo yana uwezo wa kutengeneza pombe bora tena yenye virutubisho, lakini huo ubunifu haujatumika kulifanya hilo bibo litengeneze pombe bora, ambayo itatumika na Watanzania. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Sichalwe unaipokea taarifa hiyo.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, napokea.

Mheshimiwa Spika, nimewasiliana na Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam najiuliza kwenye nchi yetu kuna chuo kinachoaminika kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Profesa Kessy pamoja na watalaam wenzake Maprofesa wengine huko sijui Profesa Muhinzi, Profesa Athuman, wanasema wameshafanya utafiti kwenye suala la gongo na pombe zingine za kienyeji. Hakuna madhara makubwa ya kiafya. Serikali inachokikatalia kwenye gongo ni methanol iliyopo kwenye gongo, lakini wanasema iko mitambo ambayo wala sio shida kutenganisha…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: …methanol na ethanol kwenye gongo ili iweze kufaa…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Sasa kama watu wanasema eti gongo yetu sisi ina matatizo kwa sababu haijatenganishwa. Kwa hiyo Jack Daniel anakunywa nani? Jack Daniel kwenye nchi hii anakunwa nani? tumezikuta pale Morena. Mwananchi wa kawaida mwenye kipato cha Sh.2,500 anaenda Morena pale? Maana yake wanakunywa matajiri wa nchi hii…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, sasa gongo haifai, Watanzania tabia ya sisi kudharau vitu vya kwetu ndio hiyo sababu tuna-import mpaka dhambi. (Makofi)

SPIKA: Haya Mheshimiwa Sichalwe, subiri kidogo, Mheshimiwa Musukuma.

TAARIFA

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nampa taarifa mzungumzaji, Mbunge wa Momba, kwa uzoefu mimi natumia hivyo vitu, wala msicheke tupo wengi tu na wala sio dhambi. Natumia hivyo vitu alivyoweka mezani na watu wengi wanaovipinga wanavipinga hasa wanapokuwa makazini, lakini wanapostaafu baada ya miezi miwili, mitatu, wateja wakubwa wa hizo pombe ulizoziweka kushoto Konyagi na K-Vant ni Maprofesa na Madaktari na nina research niliyoifanya mwaka jana. (Kicheko)

SPIKA: Haya ahsante sana.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, napokea taarifa.

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, ameshapewa taarifa tatu zinamtosha, tumwache amalize hoja yake, Mheshimiwa…

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, unipendelee na muda kidogo ni ombi tu kwa faida ya Watanzania.

SPIKA: Nakupa sasa nafasi ili utulie, uchangie vizuri hoja yako.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana mama.

SPIKA: Unaipokea kwanza taarifa ya Mheshimiwa Musukuma.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nimepokea, natetea na wapigakura wako wa Jimbo la Mbeya. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimeeleza Kiwanda cha Manyara Sugar wana-export molasses tani 1,500 katika mwaka huu wa bajeti tulionao. Sasa ombi langu kwa Serikali ni hili, mimi natoka kwenye familia ya watu wenye dini, sinywi pombe, mlokole mzuri tu, lakini hizi pombe hapa zinafanya nini?

Mheshimiwa Spika, zipo Serikali duniani ambazo zenyewe zimejipambanua kwamba ni Serikali za kidini, mfano Falme za Kiarabu, ni watu ambao hatushangai, wao wanasema Serikali yao inaamini dini, lakini nawauliza watu ambao wameenda kwenye state zote za kule Falme za Kiarabu, Sharjah, Abu dhabi, Dubai hakuna mtu hakuti hizi pombe?

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, Kuhusu Utaratibu.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, kila Serikali inaamini dini, lakini hizi pombe zipo kwenye hizo nchi.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, Kuhusu Utaratibu.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, sasa sisi kwa nini…

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, Kuhusu Utaratibu.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, sasa sisi kwa nini tunakataa utaratibu…

KUHUSU UTARATIBU

SPIKA: Mheshimiwa Sichalwe kuna kanuni inavunjwa, yuko wapi anayesema kuhusu utaratibu.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Hussein.

SPIKA: Kanuni inayovunjwa Mheshimiwa.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, kwa kanuni ya 75, kanuni ambayo imevunjwa, huwa tunapita pale kwenye security, ukiwa hata una chupa moja ya maji wanaizuia. Je, hili suala linaruhusiwa kuingiza vifaa kama hivi Bungeni?

SPIKA: Sasa kuhusu utaratibu inabidi kanuni iwe inavunjwa na yule anayehusika, kwa hivyo wewe unaliza kama amevunja kanuni au hajavunja kwa kukaa na hizo pombe hapo, ndio swali lako?

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, swali langu ni hilo kwamba je amevunja kanuni au la?

SPIKA: Ahsante sana. Amefuata utaratibu kuingiza pombe humu ndani, kwa hiyo hajavunja kanuni yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Condester Sichalwe.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, mimi sitaki kutenda dhambi, kushika tu pombe inawezekana ni dhambi. Baba yangu namheshimu sana, yale aliyofanya nyuma yanatosha, busara yangu na hekima yangu asiitumie vibaya, mimi ni mtoto mdogo namheshimu kama baba yangu mzazi. Mimi sio kichaa, yaani Spika na usomi wake wote huo halafu mimi nikurupuke kufanya hivi vitu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Spika, niendelee kusema kwamba, nataka kusema nini? Nataka kusema tunapoongelea viwanda vinaanza na mawazo ya mtu wa chini, vinaanza na mtu wa kawaida, tuheshimu mawazo ambayo yanatolewa na Watanzania wenzetu, tuheshimu mawazo ambayo yanatolewa na watu wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hizi K-Vant na hizi Konyagi ni pombe za Watanzania. Sasa hivi Serikali ya South Africa itokee itangaze kwamba inatangaza ajira 100,000 kwa watu wakafanye kazi kwenye viwanda vya wine, Watanzania lukuki watamiminika kwenda pale.

Mheshimiwa Spika, tukienda huko duniani wine za South Africa ndio zinaheshimika wakati zabibu inalimwa hapa Dodoma na Dodoma wine inauzwa shilingi 10,000. Halafu Mheshimiwa Waziri wakati alikuwa anajaribu kuongelea sehemu ambazo wamepata masoko huko sijui mpaka pilipili, mbona alikuwa haongei kama K-Vant na yenyewe ni most selling pombe kwenye huko nchi za East African Community? Si ni bidhaa ya Watanzania. Kwa nini hawajivunii na hizi bidhaa, mbona hivi wanapitisha bandarini, TBS wao wanafanya kazi ya kupima hivi tu, ila TBS kwenda kukaa kushirikiana mawazo na watu wa chini kwamba huyu mtu asiyejua kusoma na kuandika anawezaje kutengeneza kindi, komoni, kimpumu watu wakalewa wanashindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naona Serikali imeweka nguvu tu kwenye kukataza gongo. Ziko baadhi ya pombe nyingi sana pia za kienyeji kwenye jamii zetu zina madhara. Kwa mfano kule kwa Profesa Mkenda, kuna hii pombe moja huku inaitwa vimolari hivyo vimolari kule Rombo inasemekana vinauwa nguvu za kiume vya wanaume wetu huko Rombo. Sasa najiuliza hayo mawazo ndio yalibidi yachukuliwe, yaani kama iko pombe ambayo Mtanzania anaweza akapata wazo, akatengeneza mpaka zikauwa nguvu za kiume za mtu huyu, si ilitakiwa ndio hiyo pombe itumike kuwafanya hawa wanaume ambao wanawaingilia watu kinyume na maumbile ili wasiteseke, kwa sababu tayari ni maarifa hayo. Sasa wanataka maarifa gani?

Mheshimiwa Spika, hizi pombe kwa sababu zimetoka Ulaya na zimepewa majina mazuri sijui smirnoff sijui kitu gani, hiyo ndio heshima, lakini ujuzi wetu wa ndani unadharauliwa.

Mheshimiwa Spika, ifike muda…

SPIKA: Dakika moja malizia.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ifike muda sisi tuache kasumba, kasumba hapa ndio inayotuponza, kasumba hapa ndio inatuletea shida. Kama soko la ndani linaonesha kuna wanywaji wa pombe wanatumia pombe. Niombe Serikali iwatumie vijana wa Kitanzania, Maprofesa na wasomi ambao wanasema wapo tayari kufanya research, kumsaidia mwananchi wa kawaida kuboresha pombe yake. Zile pombe ambazo zinakaa siku tatu hazina kazi tena haziwezi kupakiwa. Nilishakuja na vipombe vidogovidogo hapa vya Sh.3,000, tumsaidie mwananchi huyu aweze ku-pack, viweze kuuzwa kwenye nchi zetu za Jirani. Huko ndio kuinua uchumi. Tunapoongelea uchumi wa viwanda inabidi uanze na mtu mmoja mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mama Samia peke yake na matajiri hawa wachache, hawawezi wakajenga hii nchi, nchi hii itajengwa na Watanzania wenyewe kwa kuzingatia shughuli zao za kawaida ambazo wanafanya. Ni nani huko kijijini ukiacha kulima na kufuga biashara ambazo wananchi wa kawaida wanafanya ni nini, si ni pombe za kienyeji?

Mheshimiwa Spika, ninayo orodha ya Maprofesa wakubwa hapa nchini hapa, wakubwa wengine mpaka ni aibu kutaja, ukitaja watu watabaki wameshika mdomo, ambao wamesoma kwa kutumia pombe za kienyeji ukiacha gongo. Pia hizo gongo wanakunywa, tabia ya kujifanya watu ni watakatifu, wakati watenda dhambi kama watu wengine wapo hapa, kuwajaji watu ni wa kwanza, lakini laiti Mungu angeleta karatasi zao hapa, tukafunua dhambi zao, watu wangeweza kukimbia na wasingeamini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri leo aje aseme ana mkakati gani. Kama hawataki pombe, ushauri wangu basi tuseme Tanzania ni nchi ambayo haihitaji pombe ili tujue moja. Hakuna pombe nchini kwetu na pombe za kienyeji zisithaminiwe na gongo ndipo ziendelee kuitwa haramu, lakini kama pombe zitaendelea kuingia, ni lazima tutambue ubunifu wa watanzania wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)