Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Augustine Vuma Holle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia leo kwenye Bunge lako Tukufu. Nikushukuru pia wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza nimshukuru Mheshimiwa Rais na wasaidizi wake, kwa maana ya Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kuhakikisha kwamba Wilaya ya Kasulu au Mkoa wa Kigoma kwa ujumla tunapata kiwanda cha kuzalisha sukari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hapa kwa sababu kwa miaka mingi iliyopita Wabunge wa Mkoa wa Kigoma tume-push agenda hii humu humu Bungeni na hatimaye Serikali iliweza kuweka mazingira mazuri na hatimaye mwekezaji wa Mufindi Papers au Kasulu Sugar ameanza shughuli zake pale, wamepanda miwa na ujenzi wa kiwanda unaendelea. Tunaamini muda siyo mrefu Wilaya ya Kasulu kutakuwa na kiwanda kikubwa sana cha sukari katika Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapo hapo nimpongeze Mheshimiwa DC na Mkurugenzi kwa kazi nzuri waliyofanya kuhakikisha kwamba wana-manage changamoto ndogo ndogo ambazo zilikuwa pale kwenye vijiji husika, hasa wakati wa kupata ardhi na mambo mengine, na kuhakikisha kwamba muwekezaji anaendelea na shughuli zake vizuri.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nimeona kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri, anasema Benki ya Kilimo imetoa bilioni 47 kwenye mwaka wa fedha uliopita kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao na kuongeza thamani ya mazao.

Mheshimiwa Spika, Benki ya Kilimo inafanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba inawezesha viwanda kwa kuchakata mazao mbalimbali kwenye kilimo na uvuvi. Sasa tumeona kuna initiative nyingi sana za Serikali kwenye kilimo na sehemu zingine, lakini bila kuwa na viwanda ambavyo vinachakata mazao hayo ni ukweli usiopingika kwamba kilimo chetu hakiwezi kuwa na tija na mkulima hatuwezi kumsaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kamati yetu ya PIC ilipendekeza kwenye taarifa yake ya mwaka uliopita kwamba Serikali iiongezee mtaji Benki ya Kilimo, bilioni 100. Ni vizuri, tunataka kujua kama Bunge au wananchi Serikali imefikia wapi katika kutekeleza jambo hilo? Kwa sababu kwa kufanya hivyo tunaamini watu wengi watakopeshwa. Hata wa Mkoa wa Kigoma tumepata fursa ya kupewa, kuna mwekezaji amepewa mkopo tunajenga Kiwanda cha Kukamua Mawese Mkoa wa Kigoma, tulikuwa hatuna.

Mheshimiwa Spika, Dodoma hapa wamejenga Kiwanda cha Kukamua Mchuzi wa Zabibu. Kwa hiyo lazima tuimarishe, lazima Serikali iwape fedha ya kutosha Benki ya Kilimo ili iweze kuhakikisha inawezesha ujenzi wa viwanda kwenye maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, na mimi nitagusa suala hili la cement kidogo. Kwa nini nagusa; naomba Mheshimiwa Waziri anisikilize kwa makini sana. Cement kwa Dar es Salaam inauzwa mfuko mmoja shilingi 14,000. Cement Kigoma au Kasulu Vijijini mfuko mmoja unauzwa shilingi 28,000, yaani ni mara mbili ya Dar es Salaam. Sasa tumepiga makelele sana kwa maana ya kuishauri Serikali kuendelea kuongeza production, yaani uzalishaji na Serikali imechukua hatua ya kushawishi wawekezaji nje ya nchi na ndani ya nchi ili wawekeze kwenye viwanda vya cement ili cement na kule Mbeya, kule Kigoma iweze kushuka iwe kama Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, sasa amepatikana muwekezaji kwenye kiwanda ambacho kinasuasua anataka kuleta over one trillion halafu inakuja movement ya kupinga jambo lile kwa sababu kuna technicalities eti hazikufuatwa. Sasa nimefikiria unakumbuka hata wakati tunaanza ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere walikuja watu hapa wakasema tumekiuka Sheria za Mazingira. Wakati tunaanza ujenzi wa SGR walikuja watu wakasema mnakiuka moja, mbili, tatu. Nataka niseme nampongeza Mheshimiwa Waziri na FCC kwa maamuzi ya kijasiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi hii tumekwamakwama kwa sababu ya kukosa maamuzi wakati mwingine. Vitu vidogo vidogo unakuta vinamzungusha mwekezaji mpaka anaamua kurudi kwao, hatuwezi kwenda namna hiyo, no thank you. You can not reject wawekezaji wa over one trillion eti kwa sababu kuna technicalities za mwanzo hazijafuatwa. Nilidhani wakati tunachangia hapa, tulipaswa tumpongeze kwanza Waziri, halafu tutoe ushauri wa namna ya Kwenda, tuwe supportive sio ku- discourage, eti unakataa one trillion unaijua wewe vizuri, unaijua one trillion vizuri wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hela ni ngumu jamani, hatukubaliani. Lazima huyu mwekezaji atiwe moyo, lazima huyu mwekezaji apewe nguvu, apewe mwongozo wa kutosha kwa maslahi ya Watanzania, hasa wa Kasulu Vijijini ambao wananunua cement kwa shilingi 28,000 wakati Dar es Salaam wananunua kwa shilingi 14,000 we cannot accept this.

Mheshimiwa Spika, hongera Mheshimiwa Waziri anafanya kazi vizuri, lakini sasa ukiangalia hofu ya watu, nilijaribu kuongea na watu hasa wa Mkoa wa Tanga ambako ndio kuna kiwanda chenyewe. Hofu yao kubwa wanasema kwamba huyu akinunua hiki kiwanda kinaenda kufa na walitoa mfano wa baadhi ya viwanda ambavyo vimeshakufa. Wakasema viko viwanda kadha wa kadha ambavyo vimekufa pale.

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kujua, FCC kwenye mashauri yao wana ruling za aina tatu. Moja kumpa mtu yaani anunue au a-merge katika jambo hili. Jambo la pili, unampa bila masharti, unampa tu bwana tumekubali, hakuna masharti yoyote, nunua. Jambo la tatu, unampa na masharti, masharti haya ndio ambayo yanaweza kusaidia kumlazimisha ili production ya eneo lile iendelee na kiwanda kisifungwe au kumkatalia. Sasa naamini Waziri atakapokuja hapa atakuja kuwaambia vizuri, huyu mtu anakubaliwa kwa misingi gani, anapewa bila masharti au anapewa mashati. Ningeshauri apewe kwa masharti kwa maana ya kwamba tuwe na uhakika kwamba tukimpa kiwanda kile haendi kukifunga, anaenda kukiendeleza, hivyo, ajira zinaendelea kuwepo na cement ya kutosha inakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)