Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

hon Hassan Seleman Mtenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru na nikuombe kwa ridhaa yako nirekebishe jina. Naitwa Hassan Seleman Mtenga.

Mheshimiwa Spika, nami nianze kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anazozifanya kwenye suala la kulihudumia Taifa, hasa Jimbo la Mtwara Mjini.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumshukuru Waziri wa Viwanda na Biashara. Dada yangu kwa kweli anastahili sifa na anafanya kazi ya kumwakilisha Rais. Pia Mheshimiwa Waziri amepata msaidizi mzuri sana, Katibu Mkuu, Dkt. Hashil, naweza nikasema ni Katibu Mkuu wa mfano; moja ya Makatibu bora ambao wanapokea simu za Wabunge any time. Huyu bwana, kwa kweli anatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Liganga na Mchuchuma, tunarudi nyuma tunasema kwamba huu mfupa ambao ulimshinda fisi. Kwa ushirikiano mkubwa wa Katibu Mkuu na Waziri wa Viwanda na Biashara, nadhani mgogoro huu umefika mwisho, na Watanzania sasa watapata stahiki zao, nikizungumza Serikali kupata mafao kupitia Liganga na Mchuchuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara hii ya Viwanda na Biashara ndiyo Wizara mama ambayo inategemea uchumi mkubwa ndani ya Taifa letu. Kwa nini nazungumza hivi? Tunazungumza kwamba tuna viwanda, na tunapozungumza ajira, zipo kwenye viwanda. Sasa tukiangalia Mtwara, Lindi na Dar es Salaam, tunavyo viwanda zaidi ya 5,000 ambavyo vinazalisha chumvi. Viwanda hivi 5,000 ni viwanda vidogo vidogo ambapo huko nyuma tulipoanza ingekuwa sasa hivi, tumeshapata viwanda vikubwa zaidi ya vitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jambo ambalo kwa kweli linasikitisha sana. Chumvi yetu ya Tanzania imefika sehemu imeuawa na kukosa soko kwa sababu ya mwekezaji mmoja tu. Chumvi hii ambayo sasa hivi imekosa soko, na mara nyingi wataalam wa Kiwanda cha Neel wanasema chumvi hii ina madini ambayo siyo salama kwa binadamu.

Mheshimiwa Spika, unayeniona nimesimama hapa, nimeanza kula chumvi ya Mtwara mpaka umri huu unaoniona, sijapinda mgongo, sijapinda kichwa wala miguu. Sasa hawa wataalam wanaofika mahali wanaua soko na chumvi ya Watanzania eti kwa sababu ya chumvi ya nje, leo chumvi ya Mtwara, Lindi na Dar es Salaam ilikuwa inauzwa Afrika kwa ujumla toka tumeanza, sasa hivi hii chumvi haiendi huko, kwa sababu wataalamu wa Neel wanaagiza chumvi kutoka nje, lakini wana- export kutoka Tanzania kwenda Kongo na Malawi wakati chumvi ya Watanzania ipo.

Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Waziri, alitembelea Lindi Mtwara na Kilwa na akaona mwenyewe kwa macho yake chumvi ilivyokuwa nzuri, na chumvi ilivyojaa kwenye maghala, alitoa tamko, akaelezea umma ya Watanzania kwamba kuanzia sasa Neel wasipewe kibali cha kuagiza chumvi nje, wachukue chumvi yetu ya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yako mambo mengine yanasikitisha sana. Wakati Mheshimiwa Waziri anatoa tamko, Wizara ya Madini imefika mahali wakasema huyu tumpe kibali. Sasa ninashauri, hawa ni Mawaziri wawili, hata kama kuna mambo ya kiutaalamu, anapotoa tamko Waziri wa Madini ambalo linamhusu Waziri kwenye sekta nyingine, basi wakae wazungumze. Siyo anatoka mtumishi mmoja, anasema aah, huyu mwana mama ni mwanasiasa. Tusizungumze siasa kwenye maslahi ya watu. Tunazungumza maisha ya watu wa Lindi, Mtwara na Dar es Salaam wanaozalisha chumvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ukija Mtwara ukiwaona wananchi wa Mtwara ambao walikuwa na utajiri wa chumvi, utayemkuta ana kiatu kizuri cha shilingi 60,000, ukimkuta mwananchi mwenye shamba la chumvi ana kiatu cha kuvaa chenye thamani ya shilingi 60,000 mimi nadhani nitatafuta milioni, nikakupatia, kwa hali ilivyo mbaya na wananchi jinsi walivyoathirika na uchumi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali, hawa ni Watanzania wetu, tuna kila sababu ya kuwasaidia. Tulipofikia sasa hakuna haja ya kuagiza chumvi nje. Katika viwanda hivi nazungumza zaidi ya 5,000 wamekosa ajira watu wangapi? Yuko mzee mmoja, Mohamed Nassor pale Mtwara, alikuwa na mashamba yake ya chumvi, lakini kwenye uzalishaji alikuwa ni mzalishaji bora. Kulikuwa kuna akina mama pale zaidi ya 400 ambao wanafanya kazi na wanalipwa, wale akina mama 400 wote wamepoteza ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa unaweza ukatuona tunazungumza kwa sauti kubwa sana.

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, taarifa tena ndugu yangu?

SPIKA: Mheshimiwa Mtenga kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Stanslaus Nyongo.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, nimeipokea.

TAARIFA

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, nomba nimtaarifu mzungumzaji kuwa Tanzania ina mahitaji ya chumvi tani 250,000 kwa mwaka, na tunaingiza asilimia 70 kutoka nje, na wakati sisi tuna uwezo wa kuzalisha chumvi zaidi ya tani 300,000 kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa hiyo mchangiaji.

SPIKA: Mheshimiwa Mtenga unaipokea taarifa hiyo?

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, nimeipokea taarifa hiyo kwa mikono yote miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumze kuhusu Wizara hii. Nimeangalia bajeti ya viwanda na biashara, nadhani inafika kwenye Shilingi bilioni 109, lakini huu ndiyo uti wa mgongo wa Taifa hili. Leo tunakwenda kuweka bajeti ya Wizara fedha hii, na kwenye uhalisia hatuwezi kuwapata wawekezaji bila Ofisi ya Katibu Mkuu, Waziri mwenye dhamana, wakazunguka nje na ndani kutafuta wawekezaji, hela hii itakwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kama kuna uwezekano, safari tunayokuja, ya bajeti nyingine, Wizara hii tuiangalie kwa jicho la huruma. Fedha hii iliyotengwa ni ndogo mno. Tuna haja ya kuwa na wazawa ambao wanaweza kuwa na viwanda ndani ya nchi hii, lakini kwa mfumo uliokuwepo sasa, wa mabenki yetu, hatuwezi kuwapata wazawa kwa asilimia 70 ambao wanaweza kuwa na viwanda ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, leo wako watu walikuwa wanatafuta LCs za benki wapate dhamana ya mtaji wafungue viwanda. Wamesaga lami, wamesaga viatu zaidi ya miaka saba, nane, lakini leo anakuja mtu na briefcase hapa. Tulimsikia Mheshimiwa Rais analalamika hapa, anasema kaja mtu mmoja hapa, kaingia huku, kaingia huku, hana nyumba hana kitu gani, amechukua mabilioni ya Shilingi na ameondoka. Rais wetu analalamika.

Mheshimiwa Spika, haya inawezekana humu tukaishauri Serikali kila mkoa tuunde pale Kamati, wale wafanyabiashara waliotafuta LCs za benki na wakitaka mikopo mikubwa, vikwazo gani wamekutana navyo? Tutapata majibu humu, maana yake inawezekana...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30 Mheshimiwa malizia.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, inawezekana tunakuja humu tunajifungia, tunazungumza, lakini yaliyokuwa nyuma ya pazia hatuyajui. Kama tunataka kumsaidia Rais kwa dhati kabisa, hebu ifike mahali sasa tuwe tuna maamuzi. Nimeshauri kuhusu kiwanda cha Neel, biashara ya kuleta chumvi, nadhani ifike mahali tuseme, inatosha sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)