Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi. Naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa hii ili nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwenye Bajeti hii ya mwaka 2023/2024. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda moja kwa moja kwenye hoja mahususi kabisa inayohusu Kiwanda cha SONAMCO, kiwanda ambacho ni cha usindikaji wa tumbaku. Kiwanda hiki kimesimama kwa muda mrefu sana, toka mwaka 2010 mpaka hivi sasa kiwanda hiki hakijawahi kufanya kazi na, kiwanda hiki kiko Mkoani Ruvuma katika Wilaya ya Songea katika Manispaa ya Songea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Desemba mwaka 2022 Mheshimiwa Waziri Mkuu aliita wadau mbalimbali, wadau wa tumbaku na walikuja pale Songea na ukafanyika mkutano mkubwa sana ambao kimsingi mkutano huu umezaa matunda mazuri sana. Nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa jitihada hizi ambazo anazifanya hasa katika kuangalia ustawi wa Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkutano huo pamoja na mambo mengine, kulijadiliwa namna gani ya kuweza kufufua Kiwanda cha SONAMCO Kiwanda cha Usindikaji wa tumbaku ambacho kiwanda hiki endapo kitaanza kufanya kazi, maana yake kina uwezo wa kuajiri wananchi 3,000 ambao watakuwa wananufaika na kiwanda hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni ya Vodsen Tobacco Limited ndiyo ambayo ilionesha nia ya kuwekeza na kuweza kufufua kile Kiwanda cha SONAMCO cha Songea Mjini. Kwa hiyo, sasa kupitia Bunge lako hili Tukufu, naomba nichukue nafasi hii sasa kumwomba Waziri wa Viwanda na Biashara ili aweze kuwapa uwezeshaji kampuni hii ili waweze kuja kuwekeza katika kiwanda hiki na kiwanda hiki kiweze kufanya kazi mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, naomba nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Hussein Bashe ambaye amekuwa akifanya kazi nzuri ya kuhakikisha kwamba anainua Sekta ya Kilimo, pia Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, kaka yangu Stanley Mnozya ambaye amekuwa akifanya kazi nzuri, hata kufikia hatua hii ya kiwanda hiki sasa kuweza kuanza uwekezaji wa kuinua kiwanda hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende kwenye suala la Twiga na Tanga Cement. Nimesikiliza toka asubuhi, Wabunge wengi humu ndani wamechangia, nami nikawa najiuliza tu, hata kama ninatoka Ruvuma ambapo tunahudumiwa kwa ukaribu sana na cement ambayo inatoka katika kiwanda cha Dangote, lakini nimesikia kilio cha Wanatanga wenzetu. Kwa kuwa wana Tanga ambao wamekuwa wakililia suala hili la cement kwa maana ya Kiwanda cha Tanga Cement kuendelea kuwepo hai, nikajaribu kujiuliza, ni nini ambacho kinasababisha? Nimegundua yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Twiga Cement wanataka kununua Kiwanda cha Tanga Cement, lakini katika ununuzi wao maana yake, endapo watanunua hizo shares, tayari Twiga Cement watakuwa wanamiliki share zaidi ya 68% ambayo kimsingi sheria inakataza. Suala hili linakinzana na sheria ambayo tumeitunga wenyewe katika Bunge lako hili Tukufu. Sasa najiuliza, ni kwa nini Serikali inadhamiria kwa makusudi kuvunja sheria hii? Kwa nini Serikali isirudi nyuma na kukaa chini kuanza mchakato huu upya ili kupitia na kuhakikisha kwamba utaratibu huu unafanyika chini ya sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nichukue nafasi hii kumwambia Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, zisikilize kelele hizi za wengi. Sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Urudi tena upya kwa ajili ya mchakato huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nishauri Bunge lako Tukufu hili kwamba mchakato huu uanze upya hapa tayari mchakato haujakaa sawa sawa. Kwa sababu kama mchakato umeenda vizuri hakukuwa na sababu ya kelele nyingi ambazo zimekuwa zikipigwa humu ndani, mchakato urudi upya lakini pia sheria izingatiwe hakuna sababu ya kukanyaga sheria ambayo tuliitunga sisi wenyewe kuna sababu gani? Sioni kwanini sheria ivunjwe kwa makusudi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo jingine naomba niseme kwa kuwa jambo hili linasimamiwa chini ya Baraza la ushindani naomba baraza la ushindani liheshimiwe katika maamuzi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine la mwisho kwenye eneo hili marekebisho ya sheria kama sheria hii inakinzana na maamuzi ambayo yanataka kufanyika dhidi ya uwekezaji huu. Basi sheria hii irudi hapa tuirekebishe sheria kwanza badala ya kuikanyaga sheria na baada ya kurekebisha sheria ndiyo mchakato huu tuendelee nao. Aidha, kufanyike mapitio upya ambayo yatapelekea sasa mchakato huu kwenda vizuri na niseme tu kama kutakua kuna jambo lisiloeleweka zaidi basi nimuombe Mheshimiwa Spika aunde Tume kwa ajili kuchunguza jambo hili hatimaye jambo hili liweze kuleta majibu sahihi ambayo wananchi wa Tanzania wanamatumaini na Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie suala la Matrekta ya URSUS, haya matrekta yamekuwa yakilalamikiwa sana na matrekta haya yameletwa kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara. Hata hivyo mpaka sasa hivi wananchi ambao walinunua haya matrekta wamekuwa wakilalamika, wamekuwa wakisumbuliwa na makampuni mbali mbali ambayo yanahusiana na madalali, Takukuru. Ingawaje Takukuru sasa hivi awafanyi hiyo kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba niseme kwamba tunaomba sana mchakato huu wakufatilia jambo hili kama vile ambavyo Mheshimiwa Spika aliamua kulichukua na kulifanyia kazi kwa ukaribu nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Spika wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson Mwansansu kwa uamuzi wake aliyouchukua na kwamba sasa mchakato huo uende kwa haraka ili wananchi wawe na amani. Tumekuwa tukipigiwa simu, wengine wanakimbia majumba yao hawana amani kwenye maisha yao lakini bado wamefilisika na yale matrekta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matrekta ni mabovu, unachukua tu trekta kitendo cha kuwa jipya kabisa unaliingiza shambani, unaambiwa na fundi limekatika mgongo mara limekatika sijui kifudifudi. Kwa hiyo, haya matrekta hayana nia njema kwa wananchi wetu. Kwa hiyo, niombe Wizara pamoja na eneo ambalo Mheshimiwa Spika ameona wafanyie kazi jambo hili waharakishe huu mchakato hili wananchi waendelee kuwa na amani kwa sababu kinacho endelea huko mitaani inawezekana kabisa tukapata majibu ambayo siyo mazuri kwa wananchi yanayoendelea huko mtaani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, EPZ naomba leo nizungumze na Waziri mwenye dhamana hii. Kwenye eneo hili la Viwanda na Uwekezaji EPZ walichukua maeneo ambayo yako kwenye Kata ya Mwenge Mshindo Wilaya ya Songea Mjini Manispaa ya Songea. Maeneo haya kimsingi yana miaka karibu kumi na tano wananchi hawajalipwa fidia ninaomba Waziri atakapokuja aeleze Aidha, kama hawezi kulipa pesa zote shilingi bilioni tatu na milioni mia nane azikate pale katikati alipe kwa awamu mbili tofauti wananchi wale wanateseka wamekuwa wadumavu hawana maendeleo yeyote, hawawezi kuendeleza chochote kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana jambo hili uweze kulishughulikia na utakapo kuja hapa na niseme Mheshimiwa Waziri endapo kama jambo hili utotoa majibu yanayoeleweka ninakusudia kuondoka na shilingi yako. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)