Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon Lucy John Sabu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii, nami niweze kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuletea wananchi maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa nampongeza Mheshimiwa Rais, katika kipindi hiki cha Julai, 2022 hadi Machi, 2023 miradi ya kimkakati na uwekezaji amezalisha ajira 101,353, na katika ajira hizo, ajira za vijana ni 81,082. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuleta maendeleo kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji kwa kazi nzuri anayoifanya lakini pia na watendaji wote wa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia kuhusu Kiwanda cha Vifaatiba cha Simiyu. Tarehe 11 Novemba, 2016 Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu pamoja na Mfuko wa Taifa wa Bima (NHIF), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Benki ya Uwekezaji wa Maendeleo (TIB), Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda (TIRDO), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Dawa na TMD zilisaini randama ya makubaliano ya kuanzisha Kiwanda cha Vifaatiba zinazotokana na zao la pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo mnafahamu, Mkoa wa Simiyu ni kinara katika uzalishaji wa zao la pamba na matarajio yetu katika mwaka huu tunategemea kuzalisha tani 300,000. Wananchi wamekuwa wakihamasika sana juu ya kuongeza uzalishaji wa zao la pamba kwa sababu waliahidiwa kuanzishwa kwa Kiwanda cha Vifaatiba. Jambo hili Wabunge wa Mkoa wa Simiyu tumekuwa tukilisemea mara kwa mara, lakini utekelezaji wake bado unasuasua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la idhini ya uanzishwaji wa kiwanda hicho uliwasilishwa kwa Wizara ya Fedha na Mipango tarehe 26 Juni, 2019, na gharama za utafiti pamoja na upembuzi yakinifu zilikuwa ni shilingi milioni 915 ambazo zilitumika katika utafiti na upembuzi yakinifu, lakini baadhi ya wataalamu walipelekwa hadi nje ya nchi kwenda kujifunza namna gani kiwanda hicho kitaanzishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, malengo ya kuanzishwa kiwanda hicho cha vifaatiba yalikuwa mawili, ambayo yamo katika andiko la mradi. Lengo la kwanza ilikuwa ni kukabiliana na soko la pamba ghafi ambazo zinaenda nje; na pili kuipunguzia Serikali mzigo wa kuagiza bidhaa zinazotokana na zao la pamba hususan upande wa Wizara ya Afya. Kama ambavyo tunafahamu, Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi sana katika uagizaji wa bidhaa hizi, ambapo ni zaidi ya shilingi bilioni 100 zimekuwa zikitumika katika uagizaji wa bidhaa hizi. Gharama ambazo zitatumika katika kuanzisha kiwanda hiki ni shilingi bilioni 75.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika wazo hili, tunamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye aliubeba mradi huu kipindi akiwa Makamu wa Rais na aliubeba kama mradi ambao ni mtoto wake. Sasa tunaomba Wizara itusaidie kwa sababu mradi huu umekuwa wa muda mrefu sana na wananchi walihamasika mpaka wakatoa eneo ambalo litasaidia kuanzishwa kiwanda hiki. Mradi huu tunategemea utasaidia kutoa ajira kwa vijana, na pia utasaidia wananchi wa Mkoa wa Simiyu kuweza kuhakikisha kwamba wanaongeza thamani ya pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuongeza thamani ya pamba tutapunguza pia kuagiza vifaa ambavyo vinatokana na bidhaa zitakazotengenezwa na zao la pamba. Sasa tunamwomba Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha hoja yake, aweze kutupa taarifa: Je, ni lini kiwanda hiki kitaanza rasmi? Kwa sababu wananchi wa Mkoa wa Simiyu wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu juu ya uanzishwaji wa kiwanda hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunamwomba Mheshimiwa Waziri, kwa sababu Mama alithamini mradi huu na ndiyo maana alikuwa kama champion kwenye huu mradi kipindi akiwa Makamu wa Rais, hivyo basi, tuna imani kubwa kwamba kama mtaufufua mradi huu naye atafurahi sana, na wananchi wote wa Mkoa wa Simiyu, wamekuwa wakiusubiri mradi huu kwa hamu kubwa sana, na pia tunatambua kwamba unaenda kutatua changamoto mbalimbali zinazotokana na zao hili la pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sina mengi ya kuzungumza, lakini nasisitiza juu ya jambo hili, juu ya uanzishwaji wa hiki kiwanda na Wabunge wenzangu wa Mkoa wa Simiyu tuna hamu kubwa sana ya kumsikiliza Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha hoja yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)