Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Ramadhan Suleiman Ramadhan

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chake Chake

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia kwenye hoja iliyopo mbele yetu kuhusu Bajeti ya Wizara ya Biashara na Viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna usemi wa Kiswahili unasema, “Ngoma ikipigwa Tanga, wanademka Pemba.” Kwa geographical location baina ya Tanga na Pemba, asilimia 50 ya bidhaa tunazozitumia Pemba zinatoka Tanga. Kama hazikutoka Tanga, zitatoka Mombasa au Unguja Mjini. Kwa hiyo, bidhaa za chakula tunatoa kwa ndugu zetu wa Tanga, the same kwa bidhaa ya cement au saruji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, saruji inapoadimika Pemba, aidha tunaipata kutoka Mombasa au inaagizwa nje ya nchi kwa Zanzibar. Kwa hiyo, nimesikiliza kwa makini sana mjadala wa hoja ya ku-merge Kampuni ya Tanga Cement na Twiga Cement, vizuri sana. Wasiwasi walionao ndugu zangu Wabunge wa Tanga, Mheshimiwa Mnzava na aliposimama kaka yangu Mheshimiwa Kitandula, ndiyo wasiwasi huo huo ukaniingia baadaye mimi Mbunge wa Pemba ambaye nawawakilisha wananchi wa Pemba, hasa wa Jimbo la Chake Chake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, vile vile wanavyoogopa wao, nami ndiyo naogopa hivyo hivyo. Kwa hiyo, nilikuwa nataka kusema mengi sana kuhusiana na jambo hili kwenye how shares zilivyokwenda, vipi sheria ilivyokuwa, lakini Mheshimiwa Mnzava amezungumza kwa upana na kwa usahihi zaidi, hakuna ambaye hakumwelewa. Hakuna ubishi kwamba yapo maamuzi ya Mahakama kwenye jambo hili ya kuzuia na ku-stop ile merge isiendelee. Hiyo hakuna anayebisha kwamba yapo maamuzi ya Mahakama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mnapataje nguvu na mabavu ya kwenda kutaka kuyapindua yale maamuzi ya Mahakama? Maamuzi ya Mahakama kisheria yanapingwa kwa vitu viwili tu; aidha uka-appeal Mahakama ya juu zaidi ya hiyo ikiwa maamuzi tofauti na yale yaliyotolewa na Mahakama ya chini, jambo ambalo baada ya maamuzi yale Serikali haikufanya; au uombe review. Mahakama yenyewe ikae, iyapitie maamuzi yake, halafu iseme kwamba aidha ilikosea au itoe maamuzi otherwise. Sasa hayo yote hayapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnataka kuendelea na mchakato, jambo ambalo Mahakama walishasema hili linavunja sheria kwa mujibu wa Sheria Na. 8 ya mwaka 2003 kifungu cha 11, kwamba merging ambayo itazidi asilimia hizo za share market hairuhusiwi. Sheria hizo tumezitunga wenyewe. Kuna mtu kwenye mjadala asubuhi anasema sheria mbovu. Hii ndiyo international standards, unaitaje sheria mbovu jambo ambalo ndiyo kimataifa linakubaliwa liwe hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji akija anayatazama yote hayo ili naye awe salama, asije akawa ameanzisha biashara, katikati ya process biashara yake inakwenda watu wanakuja ku-merge, wanali-monopolize soko, yeye anakufa, anaondoka. Kwa hiyo, vitu vyote hivi tunafanya kwa sababu hizi ndiyo international standards. Kwa hiyo, tunafuata sheria kwa sababu jumuiya hizi za Kimataifa ndizo zinataka sisi tuzifuate. Kwa hiyo, tumeweka utaratibu wetu wenyewe, sheria zinatakiwa zifuatwe. Hicho ndicho nilichotaka kusisitiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari za kwamba nani alikwenda Mahakamani, sijui Chalinze Cement akaenda Mahakamani; wakati Chalinze Cement anaenda Mahakamani alikuwa na locus stand ya kwenda Mahakamani na ndiyo maana akawa part ya kesi. Kama Chalinze Cement angekuwa hayupo, maana yake Mahakama inge-determine kwamba huyu jamaa siyo part ya kesi. Hiyo kesi imemalizika, decision imetolewa, mnatakiwa mtekeleze. Hii tabia ya kuwaachia Serikali maamuzi ya Mahakama wayazingatie, wayakanyage kanyage, wayapige mateke, tutawapa mamlaka ambayo baadaye tutakuja kuyajutia sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama Bunge, tunatakiwa tusimamie kwa hali yoyote ile, Serikali waheshimu mhimili wa hizi tribunal zinapotoa maamuzi. Unaweza ukaiona ni Quasi-Judicial Body imetoa maamuzi, lakini anaye-reside pale ni Jaji wa Mahakama Kuu na ile ni binding decision yake. Unataka kuikwepaje sasa hivi? Kama kuna hoja mpya, nilikuwa nimesoma kwenye Gazeti la Citizen, hoja ya watu wa FCC ni kwamba maamuzi yalitoka 2022, sasa hivi 2023 mazingira ya soko yamebadilika. Kuna mazingira mapya, kila kitu kimebadilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa, lakini mazingira yakibadilika hayabadilishi maamuzi ya Mahakama. Maamuzi ya Mahakama hayabatilishwi na mazingira mapya. Maamuzi ya Mahakama yanabatilishwa na sheria pia. Kwa hiyo, unatakiwa ufuatwe utaratibu wa kisheria kubatilisha yale maamuzi ya tribunal. Kwa sababu maamuzi yale yanasimama, Serikali chonde chonde, heshimuni sheria kwenye jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi yale yalishatoka, mnachotakiwa ni kuyasimamia, na kama kuna jambo lingine linatakiwa kufanyika, mnatakiwa mliendee kwa busara zaidi. Hakuna anayezuia merge isifanyike, lakini ikiwa utafuatwa utaratibu wa sheria na utaratibu tuliojiwekea wa kikanuni wetu wenyewe. Kwa hiyo, hicho ndiyo nilichokuwa nataka kusema juu ya wasiwasi wetu tulionao baada ya kusikia kilio cha Wabunge wenzetu majirani zetu ambao kuathirika kwao ni moja kwa moja kunaenda kutuathiri na sisi. Kwa hiyo, hicho ndiyo nilichotaka kuchangia, na ninaomba Serikali wasikilize kilio chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)