Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu kunipa nafasi ya kusimama tena ndani ya Bunge hili. Nikushukuru sana ingawa haupo kwenye kiti Mheshimiwa Spika kwa uongozi wako wa Bunge letu hili Tukufu. Nichukue nafasi hii kuwashukuru sana sana, pia wananchi wangu wa Buchosa ambao nipo hapa Bungeni kuwawakilisha, nafanya kazi hii waliyonituma kwa uaminifu wote ili kero zao ziweze kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza nianze kwa kusema, miezi 11 iliyopita nilisimama hapa Bungeni nikaeleza wasiwasi wangu. Ni kama nilikuwa na wasiwasi kwamba nchi yetu ingerejea ilikokuwa, kwa sababu tulikuwa tayari kwenye uchumi wa kati, pato la Mtanzania mmoja mmoja lilikuwa tayari limekwishafika dola 1,080, lakini kwa corona ilivyokuwepo, Ukraine vita na nini, nikahisi tungerudi tulikokuwa. Hata hivyo, kazi kubwa imefanyika na mtakumbuka niliwaomba hapa kwamba Watanzania tufanye kazi kubwa sana tumuunge mkono Rais wetu ili nchi yetu isirudi ilikokuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo nina furaha sana moyoni mwangu kwa sababu taarifa nilizonazo ni kwamba nchi yetu imepenyeza na imezidi kwenda mbele pamoja na changamoto ilizokuwa nazo. GDP ya Taifa letu hivi sasa ni bilioni 85, wakati ule tunazungumza zilikuwa zinakadiriwa kuwa Dola za Kimarekani bilioni 67. Leo ninapozungumza ni bilioni 85, tumekuwa na pato la Mtanzania hivi sasa kutoka 1,080 tumefika 1,232. Pamoja na yote yaliyotokea. Kwa hiyo naomba nisimame hapa kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sana tu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewahi kuzungumza hapa, nirudie tena na nitazungumza kila ninaposimama kwamba we have the most intelligent in Africa and in the world. Kuthibitisha hilo Tanzania image yake sasa hivi Kimataifa imebadilika kabisa. Sisi kukaa pamoja na dada zangu pale, kukaa pamoja, Rais amefanya image yetu imebadilika. Tanzania sasa hivi inajulikana kama one of the democratic country in the world, kwa sababu ya kuishi pamoja na ndugu zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zangu hizi ziwaelekee Wabunge wote walioko hapa kwa namna wanavyotoa michango yao hapa Bungeni. Mimi hoja yangu ipo kwenye suala la umaskini wa Taifa letu. Najua wamezungumza juu ya viwanda, wamezungumzia Twiga, naomba nisiguse kabisa habari ya Kiwanda cha Twiga na Tanga Cement. Naungana na hoja ya dada yangu Tauhida pale alichokisema ndio ninachokisema mimi ya kwamba suala hili lina utata, limeleta kelele nyingi, turejee mezani tukaangalie tatizo liko wapi. Langu ni suala zima la umaskini wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maendeleo tuliyoyapiga nchi yetu ni tajiri lakini watu wake bado ni maskini. Bado ni maskini, watu wana shida nyingi sana huko mtaani, maisha ni magumu pamoja na pato letu kuongezeka mpaka dola bilioni 85, lakini watu bado wana shida nyingi sana, maisha ni magumu. Inavyoonekana ni kwamba hii bilioni 85 iko kwenye karatasi, lakini haipo mezani mwa Mtanzania wa kawaida. Hapo ndio nataka niongelee mimi hoja yangu ya leo kwamba, umaskini bado upo na ni lazima tutafute njia yoyote ile ya kuhakikisha hii 85 bilioni inaonekana kwenye maisha ya Mtanzania wa kawaida. Hoja yangu ipo hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale wasomaji wa vitabu bila shaka wamewahi kusoma kitabu cha Marehemu Profesa Mtulya aliandika kitabu kinaitwa Growth and Development. Kwamba kuna tofauti kubwa sana kati ya growth na development. Kukua ni ku-increase in size, tume-increase in size tuna pato kubwa la Taifa lakini development in increase in activities, kuongezeka kwa activities za Taifa. Kwamba ukuaji huu unaonekanaje kwenye maisha ya Shigongo, kwenye maisha ya Kingu, kwenye maisha ya mkulima wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado ukuaji huo haujaonekana kwenye maisha yetu. Ni kama jenereta liko nje, lakini ndani ya nyumba kuna giza na jenereta inawaka. Ina maana kinachokosekana hapa ni cable ya kutoa umeme nje kuingiza ndani, hakuna connection kubwa kati ya GDP na maisha ya Mtanzania wa kawaida. Sasa niliposimama hapa leo naongea na Wizara ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo ni Wizara muhimu sana kwa Taifa letu. Wizara ya uratibu, Wizara hii ikisimama sawasawa kwenye uratibu itatuondolea umaskini wa nchi yetu. Nataka niseme mambo ambayo mimi naamini yakifanyika katika nchi yetu, umaskini wa Tanzania utaondoka au kupungua kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, naamini sana kwenye kilimo, naamini sana kwenye agriculture. Tulime na Serikali imeamua kulima kweli, Mheshimiwa Rais ameongeza fedha nyingi sana Wizara ya Kilimo ili tulime na kweli tunalima sana. Kilimo kitatutoa kwenye umaskini wetu, kimeajiri watu wengi katika nchi yetu, bahati mbaya sana kilimo chetu hiki, watu wengi wanatumia kilimo cha mkono, asilimia 70 ni jembe la mkono, asilimia 20 ni ng’ombe na asilimia 10 pekee yake ndio zimetumika zana za kilimo za kisasa kama trekta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme kitu kimoja kama Mheshimiwa Bashe analima, Mheshimiwa Ashatu ana mambo kadhaa ya kufanya. La kwanza, anatakiwa kuhakikisha mazao yetu yanatangazwa na masoko yanatafutwa, hiyo TanTrade anayo yeye kwenye Wizara yake. La pili, anatakiwa kuhakikisha mechanization ya kilimo inafanyika, zana za kisasa anayo TIRDO ofisini kwake anayo TIRDO na anayo TEMDO, lakini lingine ana CAMARTEC katika zana za kilimo ambazo zinatumika huko mashambani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba utusaidie Wizara hii ipewe pesa za kutosha kwenye hayo maeneo niliyoyasema, tofauti na hapo tutalima kweli mazao lakini post harvest loss yetu itakuwa kubwa, mazao mengi yatakuwa yanaharibika na hakuna masoko, hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ambalo unatakiwa kulifanya ni innovation, utakumbuka nilishakuja hapa nikasema juu ya innovation ya kwamba ubunifu ni kitu cha muhimu sana kwenye Taifa letu. Tuna vijana wengi wamebuni vitu vingi sana, lakini hawana mitaji amezungumza dada yangu Tauhida hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshakuja hapa nikasema, narudia kusema tena na leo kwamba, kuna mtu mmoja kule Iringa aligundua umeme anasambaza kijiji kizima. Kuna kijana mmoja pale Mabibo alikuwa na redio yake anatangazia watu pale Mabibo lakini badala ya kusaidiwa katika nchi hii ukiwa mbunifu unajikuta unaingia kwenye matatizo. Hiyo sio jambo sahihi naomba tufanye kila kinachowezekana kuwasaidia wabunifu wa nchi yetu. Vijana wetu wanatoka vyuo vikuu na shahada wana ubunifu lakini hawana mitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishamshauri Mheshimiwa Waziri aanzishe National Innovation Fund. Aanzishe Mfuko wa Ubunifu wa Taifa na huu sio lazima akusanye pesa yeye, kuna Global Innovation Fund huko ina pesa nyingi tu. Tunaandika mradi tunapewa mabilioni ya pesa, tena sio mkopo ni grant. Nilishamwambia, tulishaongea nikiwa Kamati ya Viwanda na Biashara nilisema sana. Nasema tena leo na leo nitakuwa mkali kidogo, nitataka nipate maelezo kwamba nini kinaendelea kuhusu Global Innovation Fund. Hatuwezi kuwa na vijana wenye akili kiasi hiki kwenye Taifa letu, hawana mitaji wana ubunifu wao ndani ya nyumba, lakini wanakufa bila kufanya chochote. Hatuwezi kukubali Waheshimiwa Wabunge, ni lazima National Innovation Fund ianzishwe. Kenya wanayo, South Africa wanayo, Ethiopia wanayo, kwa nini sisi hatuanzishi? Naomba sasa tuwathamini wabunifu wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kuwawezesha Watanzania. Watanzania wanahitaji kuwezeshwa, China miaka 15 iliyopita iliamua kwa nia moja kwamba tunaenda kuweka watu wetu kwenye list ya makampuni 500 duniani haikuwepo hata kampuni moja ya Kichina. Leo ninapoongea hapa nusu ya ile list ni kampuni za Kichina. Kwa sababu nchi iliamua we need a political will to change mambo. Lazima tuamue kama Taifa ya kwamba ile list tuhakikishe tunafanya jambo wenyewe, watoto wetu waweze kuwa na pesa. Tuwape Watanzania uwezo wa kuwa na kipato waweze kushikilia uchumi wa nchi yao. Tumechoka kuwa watazamaji, wageni wanakuja hapa siku mbili, tatu wameshatajirika, wanaondoka hapa na mali zetu sisi tunaendelea kubaki maskini. Nataka majina mapya ya mabilionea kwenye nchi hii, majina mengi kwa muda mrefu ni yale yale tu. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)