Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ili nichangie Wizara yetu hii ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara. Mimi ni mmoja wa Wabunge wanaotokea Mkoa Tanga, kwenye hili suala la Kiwanda cha Tanga Cement nafikiri Mheshimiwa Tauhida ameliweka vizuri sana. Naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Tauhida kwamba Serikali inao wajibu ya kutoa ufafanuzi kwa wananchi wapate kulielewa, lakini zaidi taratibu za kisheria ni za muhimu kufuatwa kwa sababu ndio misingi tuliowekeana kama nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie kwamba, Wizara yetu hii kwenye suala zima la uwekezaji. Tunao Watanzania ambao ni wawekezaji ndani ya nchi yetu, lakini vile vile tunao wawekezaji ambao sio Watanzania ambao wamekuja kuwekeza ndani ya Tanzania. Sasa nimesoma Hotuba ya Mheshimiwa Waziri inaonyesha pana mapitio mengi ya kisera yanafanyika na pana mapitio mengi pia ya kisheria yanafanyika ili kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala hili la uwekezaji ni bahati mbaya sana kama nchi tumekuwa na mtazamo wa outward looking, yaani kila sheria na kila sera tunapojaribu kuileta ya uwekezaji inamwangalia na kumlinda zaidi mwekezaji kutoka nje na inamwangalia kidogo sana mwekezaji ambaye ni Mtanzania. Mwaka jana hapa, nitatolea mfano, tumepitisha Sheria mpya ya Uwekezaji, fikiria ni sheria mpya hii, hata miezi sita haijamaliza, lakini sheria ile ilitoa fursa kwamba ili mwekezaji aweze kupata incentives, aweze kupata vitu vyote vya misamaha ya kikodi na vivutio vya kiuwekezaji akiwa ni Mtanzania, lazima awe na mtaji wa dola laki moja. Akiwa ni mtu kutoka nje anatakiwa awe na dola laki tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaposema dola laki moja kwa Mtanzania ndio aweze kupata incentives, vivutio vya kuwekeza, unaongelea zaidi ya milioni 200 na kitu za Tanzania. Sasa unawaweka wapi Watanzania ambao wana mitaji ya milioni 150, 170, 180. Ndio kusema kwamba sheria hii wao haiwapi fursa ya kuitwa wawekezaji ndani ya nchi yao, wala ya kupata upendeleo na vivutio kama ambavyo mtu kutoka nje anapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wenzetu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji lazima sera hizo wanazozifanyia mapitio zije zikimtazama Mtanzania, mwekezaji wa ndani, mzawa, ili aweze kunufaika na uwekezaji ndani ya nchi yake. Nasema hivyo kwa sababu hata Bunge hili ambalo tumekaa hapa kesho kutwa bajeti ikija kusomwa, maeneo mengi ambayo tutakuwa tumetaja yameongeza kodi ni yale yanayoenda kuwaathiri Watanzania wawekezaji ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepambana sana hapa Bungeni kubadilisha sheria pale TIC ili kwamba mwekezaji akitoka nje akiingia ndani ya jengo mmoja apate vitu vyote ndani ya jengo hilo. Kuanzia usajili, kila kitu mpaka anatoka pale na leseni yake ya biashara, anakwenda kufanya biashara, lakini wafanyabiashara wetu wa ndani ambao ndio Watanzania, wawekezaji wa ndani, hatujawapa jicho hilo. Yeye akitaka kuanza kufanya biashara anazunguka, anazunguka mitaa yote mpaka viatu vinakwenda upande hajasajili biashara na hao ndio walio wengi na ndio Watanzania wenye nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hizi sera wanazosema wanazifanyia mapitio ambazo wamezitaja kwenye hotuba yao, ni vyema zikaja na jicho la kumwangalia Mtanzania mwekezaji wa ndani. Mwekezaji wa nje akiingia na huu mtaji wake wa laki tano kwanza kuna wakati anapewa likizo ya kodi, hata miaka mitatu wanaita grace period, lakini hata vifaa anavyonunua vinasamehewa kodi. Nitatolea mfano wa wachimbaji wadogo, mchimbaji wetu mdogo kwa mfano akisema anaagiza grader leo hapa, lazima wataligonga VAT, lakini wale wachimbaji wakubwa waliopo hapa anaagiza yale ma-grader yanaingia bure, anaagiza mpaka magari yanaingia bure na anapewa na msamaha wa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii haiwezi kuwa sawa. Hatuwezi kuwa na nchi ambayo hatuwajengi Watanzania wenyewe kuwa wawekezaji ndani ya nchi yao. Halafu mbaya zaidi mwekezaji huyu mkubwa wa nje ambaye tunamkimbilia na kuwaacha wa kwetu, sheria hii ambayo tuliitunga hapa inampa free repatriation of profit ambapo faida hii angepata mwekezaji Mtanzania ingebaki hapa hapa. Kwa hiyo ni ushauri wangu kwamba wawekezaji wazawa wa Tanzania ifike mahali kama tunavyotaka kuangalia kwa jicho la pili na kwa jicho la ukaribu wawekezaji wa nje ndio hivyo hivyo tunatakiwa tuwaangalie hawa wawekezaji waliopo ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, langu lilikuwa ni hilo, nashukuru sana kwa fursa hii, shukrani sana. (Makofi)