Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia sisi wote Afya njema tuko hapa kwa kuisaidia Serikali yetu chini ya Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan, mwana mama shupavu ambaye ana nia nzuri ya kuhakikisha uchumi wa nchi yetu unakimbia. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya, Naibu Waziri na Katibu Mkuu na Watendaji wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nina hoja yangu ya viwanda vilivyobinafsishwa. Mwalimu Nyerere alivitengeneza viwanda hivi kwa kanda maalum, na alihakikisha kila kanda uchumi wa kikanda unakwenda vizuri. Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani tulikuwa na viwanda vya korosho 13. Viwanda vyote vimebinafsishwa na waliobinafsishiwa wamekaa navyo kwapani, hakuna wa kuwauliza wala wa kuwahoji. Wananchi wa Mikoa hii hawana ajira, na matokeo yake sasa hivi akina mama na vijana wameamua kutafuta vijimtaji vidogo vidogo, ndiyo vinaitwa viwanda vidogo vidogo, wanabangua korosho. Hii imetokana na bei ya korosho kuwalalia vile vile wale ambao wamechukua viwanda vile, ndio wanaonunua korosho kupeleka nje. Maana yake ni kuwa, uchumi wa Tanzania unachezewa na wafanyabiashara wakubwa wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na viwanda Mkoa wa Tanga; Viwanda vya Gossage, viwanda vya chuma, viwanda vingi vya kutengeneza mpaka biscuit Tanga, leo biscuit tunaagiza kutoka nje, pipi tunaagiza kutoka nje. Halafu mnasema Tanzania tunataka tuondoke na kuendelea katika uchumi wa kimaendeleo wa viwanda, ni pagumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi inaangamia sasa hivi kwa kuletewa vyakula vibovu. Tunaona katika mitandao, chocolate inafunguliwa imewekwa dawa ndani. Hizi dawa ni za kuwaangamiza vijana wapate hormones mbaya na zile hormones zitawafanya kuwa mashoga, na wakiwa mashoga watakuwa hawawezi kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona pipi, biscuit, juice mpaka maji na mafuta ya kula, lakini leo unashangaa kibali kinapita cha kuingiza mafuta tones of tones, lakini viwanda vyetu vyote vimefungwa. Nenda Shinyanga, tulikuwa tunakula mafuta mazuri ya Okay. Tulikuwa tunakula Super Ghee Tanzania, tulikuwa tunakula Tan Bond na tumepeleka mpaka nchi za Jirani. Ziko wapi Tan Bond? Iko wapi Super Ghee? Iko wapi Okay? Matokeo yake tunaagiza mafuta kutoka nje, haiingia akilini kwa Watanzania kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanakosa ajira ya viwanda vyao, tunawaachia wafanyabiashara ambao wanasema wamewekeza, halafu vitu vyote, leo material zinapelekwa nje, wanatuletea mafuta machafu ambayo yanabadilisha afya za Watanzania. Hii haikubaliki. Kwa kweli inabidi tusage meno na tutafute mazingira magumu ya kuikwamua nchi. Pipi inatoka India, chocolate inatoka China, juice zilizoharibika viwandani, zilizo-expire wanazibadilisha dating wanazileta Tanzania. Jamani tunawahurumia watoto hawa? Tunaiuhurumia nchi? Mimi leo lazima niseme ukweli maana yake napita kujiuliza kwa miaka yote 20 tunazungumza neno hili hili, lazima lifike mwisho. Hili neno la kuagiza kila kitu kutoka nje, mpaka toothpick inatoka nje, lazima ifike mwisho. Jamani, enough is enough.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile viwanda vilivyofungwa, Wabunge ninyi nyote tuungane kwa pamoja tumsaidie Mheshimiwa Rais. Rais anafanya kazi, sisi tunafanya nini humu ndani? Kazi tuliyokuwanayo ni moja, tumuunge mkono kwa kuhakikisha tunaazimia kwa pamoja, tuiombe Serikali walete taarifa katika Kamati ya Viwanda na Biashara, wawekezaji wote ambao wamewekeza sugu na viwanda havifanyi kazi na wamekaa navyo na baadaye havifanyi kazi na kuhakikisha ajira hamna, kuwa tunawaonea aibu, aibu gani wakati wote ni matajiri. Tunashindwa kutoa ajira! Nenda Mkoa wa Lindi, aibu tupu! Hatuna kiwanda hata kimoja. Tunategemea kiwanda cha korosho, nacho kimefungwa. Aliyefunga nani? Mimi na wewe hatujui. Kwa nini tufikie hapo? Kwa nini tumwache mwananchi wa Nangaro hana kazi? Kwa nini tuwafanye akina mama na vijana hawana kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tuna vijana ndekejo ambao wanahangaika hapa wamemaliza vyuo vikuu hawana kazi, viwanda vimefungwa; na mtu aliyevifunga anakuwa na ubavu wa kusema hakuna wa kuniambia nifungue kiwanda hiki. Kweli nchi hii ya kweli ilimkomboa Mwafrika na Mtanzania kweli! Ni ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, azimio langu, au ushauri wangu, Serikali sikivu itumie TR kuhakikisha anapeleka katika Kamati taarifa yote ya viwanda vyote vilivyofungwa ili wajulikane kwa nini wanaleta kiburi hiki? Pia alipe faini, maana yake haiwezi kuacha kwa kumhoji tu, amekaa miaka mingi, miaka nenda miaka rudi hakifanyi kazi, na ametumia nafasi hiyo kuchukua mikopo benki, lakini wanachi hawana ajira. Hivi vitu lazima tukubali kwa pamoja. Tuungane Wabunge wote kwa pamoja tuwe na azimio moja la kuhakikisha viwanda vinafunguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikoa ya Pwani tunatengeneza chumvi, tuna viwanda vya chumvi. Lindi chumvi, Mtwara chumvi, Tanga Chumvi, na Pwani chumvi. Amekuja mwekezaji, anawekeza kiwanda cha chumvi, analeta chumvi kutoka India. Mheshimiwa Rais mpendwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan alikuja Lindi, akasema, ninajua kero ya Lindi ni chumvi. Naomba ufumbuzi upatikane. Mpaka leo, chumvi inaletwa kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo watu wa Lindi wamekaa na chumvi, watu wa Mtwara wamekaa na Chumvi. Uchumi wa Pwani ni chumvi. Leo chumvi inatoka India mpaka inafika Tanzania, inaachwa chumvi kutoka Kilwa tones of tones, watu wamechukua mikopo mpaka wame-paralyze, wanauziwa majumba yao, lakini chumvi zimewajalia majumbani, hakuna mahali pa kupeleka, eti kisa, mwekezaji ametafuta soko la Tanzania na kuhakikisha anatumia soko la Tanzania kupeleka chumvi Burundi, kupeleka chumvi Rwanda, kupeleka chumvi Zambia, kupeleka chumvi Uganda. Sisi wetu Watanzania masikini, watu wa chini wanahangaika na chumvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na Mkutano wa Madini, nikaenda pale, wananchi wanasema je, mikopo hii mtaifanyaje? Tumechukua mamilioni ya mikopo benki. Benki, wao wanaweka riba tu, na riba ikifizidi wanauza nyumba yako. Chumvi iko ndani. Hili siyo la kuliachia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge wa Mwanza analia, Mbunge wa Tanga analia, Mbunge wa Kagera analia, sasa tunakwenda wapi? Hatuna maamuzi. Bunge hili liwe strong, Bunge la kufanya kazi lililotuleta hapa, tumkomboe mwananchi. Mwananchi huyu ndiye aliyetufanya sisi hapa tukaitwa Wabunge. Kama tutakuja hapa hatujawasaidia wananchi wale, kwa kweli tumehangaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu la mwisho. Mimi natoka Lindi, nataka nipate majibu, Kiwanda cha Korosho cha Lindi, maana yake kwanza ndiyo eneo la kujidai, kinafunguliwa Lini? Kiwanda cha Tandahimba kinafunguliwa lini? Majibu hayo yawe na muda, siyo nikae hapa mpaka mwaka mzima, kesho tena nianze na biashara hii, siwezi nikakubali. Kwa kweli inanikirihisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dharau tunavyodharaulika watu wa kusini kuonekana masikini, hatuna viwanda. Viwanda vile vilikuwa vinaajiri watu 3,000, leo hakuna hata mtu mmoja, vimefungwa, mashine zote zimetolewa. Kama mnabisha hapa, tuondoke twende Lindi tukafungue viwanda mwone kama mtakuta mashine ndani ya vile viwanda. Wame vinyofoa na hakuna wakumwuliza chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)