Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Alexander Pastory Mnyeti

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Misungwi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. ALEXANDER P. MNYETI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri anayoendelea kuifanya katika Taifa letu. Pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Serikali kwa ujumla kwa kazi na namna ambavyo wanamsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo matatu ya kuzungumza kwenye Wizara hii. Jambo la kwanza ni namna ambavyo bado tunaendelea kuagiza bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi ambazo tuna uwezo wa kuzizalisha ndani ya nchi yetu. Hili nimekuwa nikilisema sana. Kwa bahati nzuri Mheshimiwa Waziri wakati anaeleza hapa asubuhi amejaribu pia kuelezea jinsi ambavyo bado tunaagiza mafuta ya kula, bado tunaagiza ngano, tunaagiza vitunguu, na tunaagiza vitu vingi sana kutoka nje ya nchi, ambapo vitu hivi tuna uwezo wa kuvizalisha wenyewe ndani ya nchi yetu kupitia mashamba yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikishauri sana, yako mashamba makubwa ambayo walipewa wawekezaji miaka ya nyuma wayaendeleze. Wawekezaji hawa wameyatelekeza mashamba haya. Unakuta mtu amepewa shamba ekari 40,000, ekari 30,000, lakini kwenye ekari 40,000 huko anatakiwa alime ngano kwa asilimia 100, halimi hiyo ngano. Ekari 40,000, anaishia kulima ekari 3,000 au 2,000. Ekari 38,000 anatelekeza, ameacha. Unakuta kwenye shamba hilo la ekari 40,000 yeye mwenyewe anakodisha wananchi wanaozunguka maeneo hayo ekari 5,000, shamba linalobaki lote ameliacha. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, nenda kwenye mikoa mikubwa kama Morogoro, Tabora na Mwanza, mashamba yametelekezwa. Kule Misungwi kuna shamba la vitunguu, scheme ya umwagiliaji nzuri kabisa ambayo Mwisraeli alitutengenezea vizuri, sasa imetelekezwa, hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, haya mashamba Watanzania wako tayari kuyaendeleza, na hata kama sio Watanzania, wako wawekezaji wenye uwezo na vision ya kuendeleza haya mashamba, na wana nguvu, wana mtaji wanaweza kuwekeza. Hao wawekezaji ambao hawawezi kuwekeza hayo mashamba, watupishe tuweke watu wengine. Sasa hili limekuwa kama wimbo, tumekuwa tukilisema sana, lakini hatuoni Serikali ikizichukua hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Kanda ya Ziwa na Mwanza kwa ujumla tunahangaishwa sana na kitu kinachoitwa mfumuko wa bei. Bidhaa za Viwandani zimekuwa zikipandishwa bei na wafanyabiashara na zinawaumiza watumiaji wadogo wadogo kule vijijini. Unakuta kitu kama nondo, milimita kumi sasa hivi ni shilingi 18,000 mpaka 20,000, mwingine anauza shilingi 21,000 au shilingi 22,000, lakini ni kuanzia shilingi 18,000 mpaka shilingi 22,000. Nani anayedhibiti hii bei ya nondo kule kwa mtumiaji Busongo, Nunduli, Serengeja mpaka Mwaulile? Kwa sababu mtu anajiamulia kutengeneza bei yake anayoitaka mwenyewe, anakwenda kuuza sokoni, na anayeumia ni mwananchi wa mwisho kabisa kule kijijini ambaye bei hi inamuathiri moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo asubuhi tulikuwa tunazungumza hapa habari ya Tanga Cement. Sisi kanda ya ziwa hatuna kiwanda cha cement. Tunategemea sana Tanga Cement ambao ndiyo majirani wetu wa karibu kutuletea kule cement kule Tanga. Nimejitahidi kuangalia kwa nini hii kelele imetokea pale asubuhi? Nilichojifunza ni mambo matatu makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanga katika hali hiyo inayoendelea sasa hivi, ile deposit ya Tanga ambayo inachimbwa sasa hivi, inakwenda kuwa machimbo, kwa sababu watu watachimba ule mzigo, watapeleka Dar es Salaam kwa ajili ya cement. Kwa kuwa mahitaji ya Dar es Salaam ni makubwa sana, maana yake huyu mwekezaji anayetaka kununua kile kiwanda atawekeza kule nguvu zaidi ya kwenda kuchimba material na kupeleka Dar es Salaam kwa ajili ya production.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo naliona hapo, kwa nini tunashindwa kuweka wazi jambo hili? Kwa sababu viwanda hivi ni miongoni mwa viwanda ambavyo vilikuwa ni vya Serikali. Kule Tanga kuna viwanda viwili vya chuma ambavyo wawekezaji wameshindwa kuviendeleza na Serikali imevichukua. Ukienda kule Moshi kuna viwanda vya mbao na miti, wawekezaji wameshindwa kuviendeleza, Serikali imevichukua. Halikadharika Mwanza, halikadharika Arusha. Sasa najiuliza swali dogo tu, kwa nini hiki kiwanda, kwa masharti hayo hayo ambayo walipewa mwaka 1997, kwa nini hiki kiwanda kisirudi Serikalini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hawa wawekezaji ambao tuliwapa kwa nia njema wameshindwa kukiendesha kiwanda na kukiendeleza, wamefilisika, kama mlivyofanya Wizara ya Uwekezaji kuchukua vile viwanda vya wengine kupitia Msajili wa Hazina, kwa nini msifanye hivyo hivyo kwenye kiwanda hiki, mkarudisha Serikalini, halafu Serikali ikamlipa huyo mwekezaji aliyeshindwa kuendeleza, halafu ikatafuta mwekezaji mwingine ili kupunguza hizi kelele ambazo zimekuwa zikiendelea katika Taifa letu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu nililoliona, tutakaporuhusu kiwanda hiki kimilikiwe na mtu huyo huyo mmoja, kwa sababu tunafahamu viwanda vikubwa katika nchi hii viko vitatu. Kiwanda hiki cha Tanga, Twiga pamoja na Dangote, washindani wakubwa wawili sasa ukishajumlisha hicho kiwanda kikawa kitu kimoja, tafsiri yake ni kwamba, ushindani hautakuwepo, kwa sababu huyu mtu atakuwa anajipangia bei anavyotaka yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei anayoiamua yeye; leo tunanunua cement kule Mwanza shilingi 24,000 mpaka shilingi 25,000. Tutakapompa dhamana ya kumiliki na kiwanda kingine kiwe kimoja, tafsiri yake ni kwamba, akiamka akasema bei ni shilingi 40,000, hakuna wa kushindana naye kwa sababu ndiye mwenye viwanda vikubwa kwenye nchi yetu. Sasa huu ushindani tutaufanyaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba jambo hili Wizara iingilie kati, ione namna ambavyo inaweza ku-rescue situation hii ili sisi watumiaji wa mwisho kule chini kwa wananchi, tuweze kutumia gharama nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, ajitahidi sana yeye na Wizara yake kulinda wawekezaji wa ndani. Kumekuwa na changamoto nyingi sana. Wawekezaji hawa wa ndani wanapata misukosuko midogo midogo huko kwenye zile taasisi za Serikali. Shida ni kwamba, Mwafrika ukipata hela, unaulizwa maswali milioni moja kuliko angepata hela mtu mwingine ambaye sio Mwafrika. Yaani ni kwamba, kuna watu, kikundi kidogo kimejimilikisha fedha nchi hii, kiasi kwamba akija mtu mwenye hela mpya, maswali atakayoulizwa ni mengi kuliko uwekezaji alioufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mtu aliingiziwa fedha, shilingi milioni 500 kutoka kwenye akaunti ya Mheshimiwa Kingu, maswali atakayopigiwa na Benki Kuu, ni afadhali akaingiziwe hiyo milioni mia tano akiwa Uganda. Utaulizwa fedha inatoka wapi? Yaani hata wao hawajui fedha inatoka wapi. Fedha huwa inatoka benki, kwenda benki. Ukinikuta na fedha nyumbani kwangu, hapo chukua hatua, lakini kama Mheshimiwa Kingu ameingiza fedha kutoka benki kwenda benki, unauliza maswali gani, kwamba fedha inatoka wapi? Fedha huwa inatoka benki inakwenda benki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana, wawekezaji wa ndani, watu wanajitahidi sana kuwekeza ndani ya nchi yao, lakini vikwazo na ukiritimba umekuwa ni mwingi sana, kana kwamba hawana uwezo wa kuwekeza kwenye Taifa lao. Kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri hilo nalo ulitazame kadri inavyowezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)