Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya. Nianze kuchangia kwa kumpongeza Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya ndani ya nchi yetu. Nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri, Dada yangu, Mheshimiwa Dkt. Ashatu kwa kazi nzuri anayoifanya katika Wizara hii ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Naibu Waziri wake na watendaji wote wa Wizara hii ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusema kwamba, sera kubwa ya viwanda ni agro processing. Sisi Tanzania tunataka tuchakate malighafi zetu ili tuweze kusafirisha bidhaa nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kwa kufanya hivi tutasaidia kuongeza thamani ya tunachokizalisha, lakini vilevile sambamba na kuongeza ajira ndani ya nchi yetu. Lakini tukisema tusafirishe mazao ina maana tutakuwa tunapoteza ajira na tunapoteza mapato. Na hii ajenda tumekuwa tukiizungumza takribani miaka mitano sasa, lakini hivi sasa kama inaenda kuwa kimya. Labda ningependa Mheshimiwa Waziri aweze kuniambia akija kufanya majumuisho, ile ajenda tuliyokuwa tukiimba ya Tanzania viwanda bado ipo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulianza kutengeneza industrial park pale kurasini miaka miwili iliyopita, nafikiri kipindi kile Waziri wa Viwanda na Biashara alikuwa Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo, kama sijakosea. Tulikubaliana tuanzishe kiwanda cha chai, kiwanda cha kahawa, kiwanda cha parachichi na viwanda vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile tulikubaliana Tanzania tuwe na soko kubwa la chai kama lilivyokuwa kule Mombasa kwa majirani zetu. Hii ingeweza kusaidia wakulima wetu wa chai waache yale manung’uniko, ya kwamba tunakosa soko la chai, na hivi sasa mpaka wameamua hata kuacha uzalishaji wa chai na kung’oa baadhi ya mashamba ya chai kwa kukosa soko. Na ningependa kujua Mheshimiwa Waziri huu mchakato umefikia wapi? Ukija kuleta majumjuisho hapo utuambie kwamba, huu mchakato ambao tuliuanza pale Kurasini wa industrial park umeishia wapi?

Mheshimiwa Spika, sasa nipende kuzungumzia suala la zao la parachichi. Kama tunavyojua kwamba, Tanzania kwa East Africa ni moja ya nchi ambazo zinazalisha parachichi kwa wingi na Mkoa wa Njombe ndio unaoongoza. Paparachichi yetu tunazalisha kwa wingi na yenye ubora, lakini ni miaka mingi sana tumakuwa tukipigia kelele Wabunge wa Mkoa wa Njombe na wa Nyanda za Juu Kusini wa mikoa mingine kuhusiana na suala zima la uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata zao la parachichi ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ufike wakati sasa kama tutakuwa tunatoa ushauri haujapokelewa, basi Serikali ituambie kwamba, ushauri huu bwana, sisi hatujaupokea, ili tusiendelee kupiga makelele humu ndani ya Bunge. Maana sasa tunapiga makelele mpaka sasa tunataka kufanana na hayo maparachichi yenyewe.

Mheshimiwa Spika, katika biashara yoyote duniani kitu cha kwanza unachotakiwa kufanya katika uzalishaji wowote ni kuhakikisha kwamba una uhakika wa soko la ndani. Ili kuwa na uhakika wa soko la ndani lazima tutengeneze miundombinu ya kuwa na viwanda vya kuzalisha hili zao la parachichi. Hii fursa tuliyoiona ya kusafirisha parachichi nje ya nchi, nchi nyingi zimeona hii fursa. Hebu tukae chini tutafakari, tujiulize, je, nchi nyingine zote zilizoona fursa hii zikiamua kuzalisha kwa wingi, vipi soko huko mbele? Vipi mustakabali wa wakulima wetu wa zao la parachichi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana sisi Wabunge tunasisitiza kwamba, tuanzishe viwanda vya kuchakata zao hili, ili badaye supply ikiwa kubwa, demand ikishuka kule, huku sisi tuwe na uhakika wa soko letu ndani ya nchi. Na hii itasaidia kuwalinda wakulima wa zao la parachichi wawe na uhakika na wafurahie kile ambacho wanacho…

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Nilikuwa sijamuita, ili umalizie sentensi yako maana naona umeishia, “kwa kuwa…”. Sasa sijui ataanzia wapi kutoa Taarifa. Malizia sentensi uliyokuwa unasema, ili nimpe nafasi.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, nilitaka kusema hivi, ni kwamba, umuhimu wa zao hili la parachichi, ili liweze kuleta tija kwa wananchi ambao tunazalisha zao hili la parachichi ni kuhakikisha kwamba, tuna viwanda ambavyo vitakwenda kuchakata zao letu la parachichi, ili tuwe na uhakika wa soko la ndani endapo soko la nje likija kuharibika hapo badaye.

SPIKA: Haya, Mheshimiwa Neema Mgaya, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Halima Mdee.

TAARIFA

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nilikuwa nampa Taarifa Mheshimiwa; hotuba ya Waziri inaonesha kwamba, tunaagiza mafuta kutoka nje tani 365,000. Hoja ya Mheshimiwa Neema ni kwamba, tukiwa na viwanda vyetu vya kuchakata maana yake vilevile na mafuta yanayotokana na zao la parachichi tutaweza kutengeneza ndani. Maana yake sasa tutafidia hicho anachokisema, lakini vilevile kuzuia fedha za kigeni kwenda nje. (Makofi)

SPIKA: Haya, Mheshimiwa Neema Mgaya, unapokea Taarifa hiyo?

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naipokea Taarifa ya Mheshimiwa Halima kwa mikono miwili kwa sababu, ina tija kwa mustakabali wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nizungumzie suala la Liganga na Mchuchuma. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ametueleza taarifa njema za kulipa fidia wananchi wetu wa Mkoa wa Njombe ili kuweza kuendelea na zoezi hili la Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Spika, kulipa fidia tu haitoshi. Sisi wananchi wa Mkoa wa Njombe na Watanzania kwa ujumla kwa unyeti wa mradi huu wa Liganga na Mchuchuma tunataka kujua, ni lini chuma kitaanza kuchimbwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nilikuwa nafikiria kwa kuwa, tumeshasema faida nyingi sana za mradi huu, na tumesema hasara za kucheleweshwa kwa mradi huu, ikiwa na kupitwa kwa wakati kwa makaa ya mawe, tumezungumza sana ndani ya Bunge hili. Mimi nafikiri ni wakati sasa Bunge lako liunde Kamati Teule ya kuchunguza Mradi huu wa Liganga na Mchuchuma; na mimi nitaleta hoja binafsi ya kuunda kamati teule ya kuchunguza suala la Liganga na Mchuchuma ili kusudi suala hili liende kufanyiwa kazi kwa uharaka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nikileta hoja hiyo Mezani kwako unikubalie na uniunge mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.