Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu mpendwa, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. Pia nampongeza Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu wake na Watumishi wote wa Wizara ya Mifugo. Nami leo nimewiwa kuchangia kwenye bajeti hii ya mifugo na ninataka nimwambie tu Mheshimiwa Waziri kwamba, kwenye Wilaya ya Kahama, Halmashauri ya Msalala, Jimbo la Msalala ni wafugaji wazuri sana wa ng’ombe. Nami nijikite sana kwenye kuzungumzia leo ufugaji wa ng’ombe kwa sababu ndiyo mifugo ambayo tunaifuga katika Jimbo langu la Msalala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Msalala, utaona kabisa wananchi wangu wanafuga ng’ombe kwa wingi. Changamoto kubwa iliyopo kwenye maeneo yale ni malisho pale ambapo mifugo inaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna minada mingi ya ng’ombe kwenye maeneo yale. Tuna wafugaji wengi kwenye maeneo yale. Nampongeza sana Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, kupitia Mheshimiwa Waziri wake kwa kuweza kutupatia ng’ombe madume 50 ya ng’ombe ambayo kimsingi yanaenda kuzalisha ng’ombe wa kutosha kwenye eneo lile la Jimbo langu la Msalala. Hawa ng’ombe 560 hawataweza kusaidia, na kwa sababu ni ng’ombe wa kisasa hawataenda kuwasaidia wananchi wangu kama hatutatenga bajeti nzuri ya kuweza kwenda kujenga miundombinu rafiki kwenye mifugo hii ambayo tayari tumeshaipeleka kwenye maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunapokea ng’ombe hawa, maelekezo tuliyopewa ni kwamba, ngombe hawa wanahitaji kuoga mara kwa mara; ng’ombe hawa ni adui wakubwa wa kupe. Sasa kwenye maeneo yetu, hasa kwenye Jimbo la Msalala, utaona miundombinu ya majosho bado iko chini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana wa fedha 2021/2022 tulipokea ahadi ya kupewa majosho matano, lakini ni majosho mawili tu yaliyokuja yakakarabatiwa na yale majosho matatu mengine bado hatujayapokea. Namwomba Mheshimiwa Waziri, kama tunataka kuilinda mifugo hii ambayo ninyi wenyewe mmetuambia ni delicate sana, inahitaji kuoshwa mara kwa mara, ni adui wa kupe, basi tuhakikishe kwamba kwenye bajeti hii mtutengee majosho ya kutosha ili mifugo hii iweze kuoga, na iwezeshe sasa wananchi kuitumia vizuri na kuzalisha ng’ombe wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hapo nyuma ilizuia juu ya ugawaji wa ranch. Nami nikiri tu kwamba, kwenye maeneo yangu ukiangalia, wafugaji wengi wamekua kwa sasa. Kuna baadhi ya wafugaji wana ng’ombe kuanzia 500 mpaka 600, na hivyo kuwafanya waanze kuhamahama kwenye mapori. Wanapoenda kwenye mapori kule, matokeo yake wale ng’ombe wanakamatwa. Sasa naomwomba sana Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu wake, hebu wachukue hili, waende wakaangalie lile zoezi la kupitia zile ranch ambalo walilisimamisha kufanya uhakiki halijakamilika? Kama limekamilika, hebu mwagawie sasa wananchi wetu kule ili waweze kufuga mifugo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, hili aliandike kwamba wananchi wanahangaika kule, waende wakapitie haraka. Mkurugenzi huyu aende akafanye kazi haraka iwezekanavyo, watangaze ranch hizo wawagawie wananchi. Wanapata taabu kwenye maeneo yetu huku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hapa kuna Mheshimiwa Mbunge mwenzangu wa Ushetu, kuna mwananchi wake alikuwa na ng’ombe zaidi ya 600, ng’ombe wale waliingia kwenye hifadhi na walikamatwa na uzuri alishinda kesi, lakini mpaka sasa bado hajalipwa fedha zake. Hii yote ni kwa sababu hatuna maeneo ya kuchungia mifugo yetu. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri awe mlezi kweli kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa, Mheshimiwa Waziri, tunazungumzia habari ya wafugaji; yeye anasimamia wafugaji, lakini inapokuja kwamba mfugaji anapata changamoto, wanajitoa. Sasa naomba, hebu endeleeni kusimama na wafugaji. Mfugaji anapopata changamoto yoyote, mshikeni nendeninaye moja kwa moja kuhakikisha kwamba anatendewa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Waziri amekuja kutembelea kwenye Jimbo langu la Msalala, wakati anatukabidhi madume 50, sambamba na hilo aliahidi kutujengea bwawa la Mkoloni, Busangi. Ninaamini ahadi ile ilitolewa na Mheshimiwa Waziri ambaye alikuwa ni Mheshimiwa Mashimba Ndaki, yuko hapa; lakini Mheshimiwa Mashimba Ndaki hakutoa ahadi, aliyetoa ni Waziri, nawe umekaa hapo Mheshimiwa Waziri. Nikuombe chukua kalamu na karatasi Mheshimiwa Waziri, ahadi hii itekelezwe. Wananchi hawa tumewaahidi bwawa la kunyweshea mifugo kwenye Jimbo la Msalala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kwamba tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi kwenye maeneo yale. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri aone katika bajeti hii, atuletee watumishi wengi kwenye sekta hii ya mifugo ili waende wakawasaidie wananchi kwenye maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa la mwisho, naomba nichangie kwenye suala zima la minada. Kwenye Jimbo la Msalala tuna minada takribani zaidi ya 10, na minada hii inafanya kazi vizuri sana. Kwenye Wilaya ya Kahama Halmashauri pekee yenye mifugo mingi na yenye minada mingi ni Halmashauri ya Msalala. Sasa changamoto inakuja, hawa watu wanapoenda kuuza mifugo yao, Halmashauri inawa-charge fedha. Kwa mfano, kwenye ng’ombe wanachajiwa shilingi 7,000 kwa ng’ombe, lakini shilingi 3,500 inakatwa moja kwa moja kwenda kwenye Serikali Kuu na haiingii hata kwenu kwenye Wizara, inaenda moja kwa moja kwenye Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimwomba Waziri wa Fedha, yuko hapo, fedha ile inapokatwa muweze kuwa mnarudisha percent kwa ajili ya kwenda kufanya ukarabati wa miundombinu. Ukienda kwenye minada hii, unakuta choo hakuna, miundombinu ni mibovu, lakini wananchi wanalipa fedha. Pia Halmashauri zimeanza kuogopa kufanya uwekezaji wa kuendeleza minada hii kwa sababu fedha hawapati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unakuta Halmashauri imewekeza zaidi ya Shilingi milioni 200 kukarabati mnada, lakini hapo hapo ninyi mkiona mnada huu umependeza, mnauchukua tena moja kwa moja na fedha zote Halmashauri haipati, zinaenda Wizarani. Sasa naomba, kama Halmashauri inaenda kuwekeza fedha kwenye minada yake, hebu mtuachie tuweze kuiendesha minada hiyo, nanyi msiingilie, mtuachie wenyewe Halmashauri, ili Halmashauri ziwe na moyo wa kuendelea kuwekeza kwenye maeneo hayo. Pia fedha hii ambayo inakatwa kwenda Serikali Kuu, hasa kwenda kwenye Wizara ya Fedha, fedha ile basi iweze kukatwa asilimia kadhaa, ije irekebishe maeneo ya miundombinu kwenye maeneo yale, hasa vyoo na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, nakushukuru sana, lakini ahadi hii ya majosho matano mpaka leo hatujui yako wapi, iandike. Ahadi ya Bwawa la Mkoloni, Busangi ni muhimu sana kwa sababu ni ahadi ya kiongozi ambaye aliitoa, ni Waziri, nawe uko hapo umekalia kiti hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)