Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hii Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mosi, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na staff yote kwa kazi nzuri ambayo mnaifanya, kusema kweli ukiangalia mmejitahidi sana kuboresha mifugo na mmejitahidi sana kuboresha uvuvi. Mheshimiwa Waziri nakushukuru kwanza kwa namna ulivyoweza katika ile awamu ya kwanza ulivyotoa vizimba mimi kwenye Jimbo langu la Musoma Mjini tuliweza kupata vikundi saba, walipata vizimba kwa hiyo wanasubiri tu mimi na wewe tuende tukawakabidhi ili waanze maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, itoshe tu kusema kwamba pamoja na shukrani hizo baada ya kuwa wale wamesikia kwamba wenzao wamepata, sasa vikundi vingi zaidi vimehamasika na vinategemea kwamba kwenye awamu itakayofuata basi ni imani yangu kwamba watakuwa wengi watakaoomba ili waweze kufaidika na mpango huo wa vizimba katika Manisapa yetu ya Musoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nisemee tu kwa ufupi kwamba liko tatizo kidogo ambalo linatusumbua kwenye ufugaji wa samaki, tatizo hilo tunahitaji tuwe serious tuone namna ya kulitatua. Unajua watu wengi na hata wale wanaouza chakula cha samaki pamoja na wale samaki wenyewe wanatupa maelekezo kwamba samaki ndani ya miezo sita ukiwalisha hivi, watakuwa wamefika wastani wa gramu 500 na utapata biashara, lakini huwezi kuamini kwa sababu tuna watu wengi ambao ni watengenezaji wa vyakula vya samaki, wanashindwa kutupa formular kamili au kututengenezea chakula kamili kitakachoweza kuwafikisha samaki ndani ya miezi sita wapate uzito ule unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hali hiyo watu wengi wanaanza kukata tamaa kwa sababu wanafuga mpaka miezi nane lakini samaki wana gramu 200, wana gramu 300. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ninakuomba kabisa kwamba hebu hilo ulipe uzito wake kuona kwamba ni kwa namna gani tunaweza kupata watengenezaji wazuri wa chakula cha samaki. Maana leo hii ukiagiza chakula kutoka nje ndani ya miezi sita unaweza kufikisha gramu 500, kwa hiyo nadhani hilo kwetu ni tatizo kubwa kwa sababu ni watu wachache wanaoweza kuagiza chakula cha samaki kutoka nje.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo sasa hilo, ombi kwamba pale Musoma Mjini bahati nzuri wewe unapajua vizuri niko kwenye mwambao wa Ziwa Victoria na katika ule mwambao wa Ziwa Victoria ukienda pale asubuhi kuanzia Saa 12 unawakuta wakina mama wamebeba mabeseni ya dagaa vichwani na hayo mabeseni ya dagaa wakiwa wanatiririkiwa na yale maji ya dagaa, kwa maana ya kwamba wale wavuvi wa dagaa, ile kuanzia alfajiri ya Saa 11 wanafika pale hasa kwenye mwalo wangu wa Makoko, halafu wanawauzia wakina mama zile dagaa, sasa wanaanza kutembea nazo wakati mwingine mpaka kilomita tano kwa mguu. Wakifika sasa ndiyo wanaanza kuanika, tena siku hizi wamekuwa wakianika kwenye zile net, hizi net kwa maana ya chandarua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri tupate hata mashine moja au mtambo mmoja wa kukausha Samaki na dagaa pale ili samaki wakishatoka kule ziwani wanapita pale kwenye mashine wanakaushwa akina mama wetu wa Musoma Mjini waweze kufanya biashara zao kwa raha zaidi, nadhani hiyo itawasaidia kuboresha maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana watu tunaowahangaikia ndio hao wenyewe, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri uone namna tutakavyowasaidia. Jambo la pili Mheshimiwa Waziri hili linataka attention kubwa sana, ndugu zangu wale wote ambao tunaishi Kanda ya Ziwa kwa maana Mara, Mwanza na Bukoba nadhani mtakubaliana na mimi, samaki wamepungua kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kadri siku zinavyoenda ni kwamba samaki wanaendelea kupungua, kwetu sisi pale watu wa ziwani kule samaki au lile Ziwa ndiyo madini yetu, kwa hiyo watu wetu wengi wamekuwa wakipata ajira karibu zaidi ya asilimia 50 kutokana na lile Ziwa Victoria. Sasa leo pale kwangu Musoma Mjini tulikuwa na viwanda vinne, tulikuwa na Musoma Fish Park, Musoma Fish Process, tulikuwa na kiwanda cha Mzee wetu Jamaliwa lakini na Prime Catch. Leo huwezi kuamini kimebaki kiwanda kimoja cha Musoma Fish Process ambao na wao kwa sababu wanapata samaki kidogo wanalazimika kusafirisha kupeleka Mwanza katika kiwanda chao kingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaonesha nini? Kwamba kadri siku zinavyoenda yale maji yatabaki tu labda kwa ajili ya kuoga na kunywa lakini hayatakuwa maji yanayoweza kuwasaidia watu wetu kiuchumi. Kwa hiyo, mimi nilikuwa naomba kabisa tuangalie namna tunavyoweza kulisimamia hili Ziwa hasa kuondoa uvuvi haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo najiuliza hivi kama tunaweza ile Ngorongoro ndogo tukaweka Mamlaka ya Ngorongoro kwa ajili ya kuangalia Hifadhi ya Ngorongoro, tukaweka watu kama TAWA kwa ajili ya kusaidia kuangalia wanyama, hivi tunashindwa nini kuweka mamlaka ambazo zinasimsmia haya Maziwa zinasimamia mpaka na kule baharini ili suala la vile viumbe kwa maana ya samaki waweze kufugwa vizuri. Hivyo, nadhani hilo Mheshimiwa Waziri alipe uzito ili liweze kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja karibu na la mwisho ni suala la hereni. Miongoni mwa wafugaji hapa na mimi naweza nikajinafasi kwamba na mimi ni mfugaji na ninafuga vizuri. Binafsi nitofautiane tu na wenzangu kidogo pale walipoanza kukataa herein, mimi binafsi naliunga mkono sana suala la hereni kuwepo katika mifugo yetu. Kwanza litatuondolea kabisa kitu kinaitwa wizi, nadhani Mheshimiwa Waziri ni kwa sababu haujaeleza vizuri ule umuhimu wa herein. Binafsi mifugo yangu yote inazo hereni lakini ni zile hereni za plastiki, wakati nikiwa kwenye mchakato wa kuweka hizo hereni za elektroniki tayari Serikali mkasema mnaleta, kwa hiyo mpaka leo mimi nazisubiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza tu nikatumia nafasi moja ndogo tu ambayo itawa-convince watu wote wale ambao ni wafugaji wakubali zile hereni. Leo wako Wajumbe humu wamesema kwamba wafugaji hawakopesheki. Hawakopesheki kwa sababu namna ya ku-control ile mifugo yetu inakuwa shida kidogo. Leo Mheshimiwa Waziri tunao watu wa TEHAMA humu katika Wizara yako wamo, hebu waunganishe wale watu wa TEHAMA waunganishe na benki, wafanye tu kitu kimoja, mimi nina ng’ombe wangu 500 zote zina hereni maana yake ni kwamba zile ngo’mbe ili ziuzwe lazima tuuze kwa kutumia herein, kwa hiyo benki leo ukiwaambia kwamba mimi nina ng’ombe 500 hereni zake ni hizi wanaziingiza kwenye system, siruhusiwi yaani nikiuza huyo ngo’mbe hizo fedha lazima ziende wapi? Lazima ziende benki. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo kwanza itakusaidia kuhakikisha kwamba kila mmoja sasa anaona umuhimu wa zile hereni na ni kwamba maana anajua sasa tayari thamani ya zile mifugo zetu zinakuwa tayari ni dhamana kwetu hasa kwenye eneo la benki ambako ndiko wafugaji wengi wanapata taabu. Kwa hiyo, nadhani kama hilo Mheshimiwa Waziri utalipa uzito ni imani yangu kwamba linawezekana kwa sababu mimi nilishalifanyia research ni kitu ambacho kiko wazi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)